Hussein Massanza
JF-Expert Member
- Dec 26, 2012
- 1,015
- 2,191
My take:
Rais Magufuli wakati anaongea na wafanyabiashara Ikulu alisema alikaa na Kimei na kugundua taasisi nyingi za serikali zimehifadhi pesa nyingi sana kwenye taasisi za fedha ambazo serikali inaenda kukopa kwazo hivyo serikali kufanya biashara na fedha zake yenyewe.
Sasa serikali imeagiza serikali na taasisi zake kuondoa fedha zake katika mabenki ya biashara na kufungua akaunti benki kuu ambako itazihifadhi.
Kutokana na benki kuu kutokuwa na matawi yaliyosambaa nchi nzima, serikali imetoa ruhusa kwa taasisi hizo kuwa na akaunti kwenye benki za biashara ambapo wataweka fedha zinazotosheleza kutimiza majukumu yao ya kifedha kwa kipindi cha mwezi mmoja.
==================
SERIKALI imeanza kuchukua hatua za kupunguza riba za mabenki kwa wananchi kwa kuagiza akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya biashara zifungwe na kuhamisha fedha zilizoko katika akaunti hizo kwenda akaunti zitakazofunguliwa Benki Kuu (BoT).
Agizo hilo limetolewa na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru hivi karibuni, akiwataka watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi hizo, kufuata maelekezo matano ya kufunga akaunti zao katika mabenki ya biashara na kuhamishia fedha hizo BoT.
Katika agizo la kwanza watendaji hao, wametakiwa kufungua akaunti ya mapato yao kwa aina ya fedha za mapato wanayopokea, kama ni za kigeni au Shilingi za Tanzania, katika tawi la karibu yao la BoT haraka iwezekanavyo kabla ya jana.
Baada ya kufungua akaunti hizo, watendaji hao wametakiwa kuelekeza makusanyo yote ya fedha za ofisi zao ikiwemo fedha za ruzuku zinazotoka serikalini kwenda katika akaunti mpya zilizofunguliwa katika matawi ya BoT.
Agizo la tatu la Serikali kwa watendaji hao wametakiwa kuhamisha fedha zote zilizobakia katika akaunti zao zilizoko katika mabenki hayo ya biashara na kupeleka katika akaunti mpya zilizoko BoT.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhusiano pekee kati ya mashirika hayo na mabenki ya biashara itakuwa akaunti itakayohifadhi fedha za uendeshaji ambayo imetakiwa kuwa na fedha zinazotosha uendeshaji wa shughuli za taasisi zao kwa mujibu wa matarajio ya matumizi yao ya kila mwezi.
Hata hivyo, katika agizo la tano watendaji hao wameaswa kuhakikisha fedha yoyote itakayokuwepo katika akaunti hizo kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za taasisi, ihakikishwe inapata mapato ya riba kulingana na viwango vya riba vilivyopo katika soko.
Utekelezaji Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kuhusu utekelezaji, Mafuru alisema tayari baadhi ya mashirika na taasisi hizo zimeshatoa taarifa za utekelezaji wa maagizo hayo.
Alifafanua kwamba si rahisi kwa mashirika yote kufanikisha hatua zote ndani ya muda waliopewa unaokwisha leo, kwa kuwa baadhi ya mashirika, ufunguzi wa akaunti ni lazima ufanyike kwa uamuzi wa bodi ya wakurugenzi.
Mafuru alisema akaunti zingine za mashirika na taasisi hizo, ziko katika akaunti za muda maalumu katika benki hizo za biashara, hivyo kabla ya kuzifunga na kuhamisha fedha husika, kutahitajika majadiliano kati ya shirika au taasisi husika na benki yake.
Kwa mujibu wa Mafuru, la muhimu ni kuanza utekelezaji wa agizo hilo na tayari taasisi hizo, zimeshatoa taarifa ya utekelezaji wake. Sababu Akizungumzia sababu ya hatua hiyo, Mafuru alisema fedha za mashirika na taasisi hizo ni za Serikali na baadhi ya mashirika ambayo hutumia fedha za ruzuku ya Serikali pia huweka fedha hizo katika mabenki hayo.
Akifafanua alisema wakati mwingine mashirika hayo hupelekewa fedha za ruzuku nyingi kuliko mahitaji yao ya wakati huo na Serikali ikipungukiwa na kutafuta fedha za kukopa kutoka vyanzo vya ndani, mabenki hayo huchukua fedha hizo za ruzuku na kuzikopesha kwa Serikali kupitia mnada wa hati fungani za Serikali.
Kwa mujibu wa Mafuru, katika mazingira hayo Serikali hujikuta ikikopeshwa fedha zake yenyewe na wakati wa kulipa mikopo hiyo, hulazimika kulipa na riba ambayo ni fedha ya wananchi inayotumika kulipa mabenki hayo, wakati ingeweza kufanya kazi zingine za maendeleo ya wananchi.
Kushuka kwa riba Kuhusu athari ya hatua hiyo kwa uchumi na hasa katika mzunguko wa fedha, Mafuru alisema kumekuwa na mtazamo ambao si sahihi, kwamba mzunguko wa fedha utapungua.
Alisema wenye mtazamo huo wanasahau kwamba BoT ni benki na mabenki yanapopungukiwa fedha, hukopeshana yenyewe kwa yenyewe na kutozana riba, lakini pia yana fursa ya kwenda kukopa BoT.
Kwa mujibu wa Mafuru, kwa kuwa BoT kwa hatua hiyo itakuwa na fedha nyingi, mbali na kuikopesha Serikali wakati itakapopungukiwa fedha, lakini pia itakopesha mabenki ya biashara pale yatakapopungukiwa fedha.
Katika hatua hiyo, alisema BoT itakopesha mabenki ya biashara kwa riba ndogo kuliko inayotumika na mabenki hayo wakati wa kukopeshana yenyewe kwa yenyewe, hivyo kutumia fursa hiyo kudhibiti riba ya mabenki hayo kwa mikopo itakayotolewa kwa wananchi.
Alisema hatua hiyo ni rahisi kwa BoT kuongeza mzunguko wa fedha, kwa kuwa na yenyewe itakuwa ikikopesha mabenki hayo kwa riba ndogo, ili mabenki hayo ya biashara yakopeshe wananchi kwa riba ndogo, hivyo kuyadhibiti kibiashara kuliko kushinikiza mabenki kupunguza riba, wakati yapo katika soko la ushindani.
Matakwa ya Magufuli Itakumbukwa Rais Magufuli alipokutana na wafanyabiashara mwishoni mwa mwaka jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alisema anafahamu Tanzania ina benki kubwa karibu 54 na zote zinafanya biashara na Serikali, lakini zote hizi hazijajikita chini kwenda kwa wananchi.
Dk Magufuli alisema alijaribu kufanya uchambuzi akakuta karibu Sh bilioni 550 zinazozunguka katika benki hizo, ni fedha za umma ambazo kiukweli ni fedha za Serikali na hivyo Serikali inapouzia benki hizo hati fungani na kuzilipa na riba, inajikuta ikifanya biashara na mabenki hayo kwa kutumia fedha zake yenyewe.
Siku hiyo Dk Magufuli alisema mabenki haya ndiyo katika hesabu zao wanaonesha wana hifadhi kubwa ya fedha wakimaanisha kwamba wanazo fedha zimewekwa ambazo ni visenti vya Watanzania, lakini Watanzania wenyewe hawakopesheki, hawapati mikopo na kuhoji fedha hizo zinakopelekwa.
Kauli ya Dk Mpango Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango siku ya kuapishwa kushika wadhifa huo, aliahidi kushughulikia tatizo la riba kubwa inayotolewa kwenye benki nchini jambo linalochangia kushusha idadi ya watu wanaokwenda benki kukopa.
Alisema lazima sekta ya fedha isimamiwe vizuri ili kila mwananchi akope na kueleza dhamira yake kuwa atahakikisha riba za mikopo zinashuka ili wananchi wajipatie mikopo kwa riba nafuu.
Kwa sasa riba za mikopo katika benki mbalimbali zimekuwa kubwa zinazofikia asilimia 21, jambo ambalo limekuwa likihojiwa na wataalamu mbalimbali, kwani mfumuko wa bei ambao ndio wenye kawaida ya kusababisha gharama za mkopo kuwa juu, upo chini ya asilimia 10 kwa muda mrefu sasa.
Aidha, kumekuwepo tofauti kubwa kati ya riba ya kuweka fedha na riba ya kukopa fedha kwani mwananchi akiweka fedha zake benki, amekuwa akilipwa riba ndogo ya asilimia tatu wakati akienda kukopa fedha anatozwa riba ya asilimia mpaka 21.
Kutokana na hali hiyo, pamoja na kuwepo kwa taasisi nyingi za benki, wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kuwa mfumo wa fedha umekuwa ukishindwa kukusanya akiba kwa wingi na kuiwekeza kwa wajasiriamali wa ndani ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Aidha, wataalamu wengi wamekuwa wakionya kwamba biashara inayofanyika kati ya mabenki na Serikali, kwa mabenki hayo kukopesha Serikali kwa kununua Hati Fungani za BoT na kurejeshewa fedha zao kwa riba kubwa, imekuwa ikiwapa mabenki hayo faida kubwa na kusababisha yaache kufanya biashara na wananchi wanaokopa fedha kidogo na hivyo kuwapandishia wananchi riba.
Chanzo: Magazetini