Serikali kutoa upendeleo kwa wazawa kwenye gesi!

Luqash

JF-Expert Member
Oct 18, 2012
916
195
SERIKALI kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetangaza kuyaalika rasmi makampuni ya wazawa yenye uwezo wa kifedha na kitaalamu kushiriki katika zabuni ya kutafuta wawekezaji wa vitalu vya utafiti wa gesi asilia sambamba na makampuni ya nje, huku gharama zake zikionekana kuwa `mlima mrefu’.

Kwa mujibu wa taarifa ya TPDC kwa umma, kuingia kwenye mchakato wa zabuni ya nne ya vitalu vya utafiti uliozinduliwa Oktoba 25 mwaka huu, kila kampuni inayoomba itapaswa kulipa dola za Kimarekani 50,000 (Sh milioni 81.5 za Kitanzania) ambazo hazitarudishwa.

Zabuni za safari hii zinahusisha vitalu saba vilivyoko bahari kuu na kitalu cha Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika na kwamba waombaji wanapaswa kuwasilisha maombi kati ya sasa na Mei 15 mwaka kesho.

Vitalu vya bahari kuu vipo katika kina cha maji kati ya mita 2000 na 3000 wakati kitalu cha Ziwa Tanganyika kinafikia kina cha mita 1,500.

Aidha, kwa mwombaji wa vitalu vya baharini atalazimika pia kununua kifurushi cha lazima cha zabuni za vitalu vya bahari kuu kinachogharimu Dola 750,000 (Sh bilioni 1.2) kwa kila kifurushi, wakati kwa waombaji wa kitalu cha kaskazini ya Ziwa Tanganyika watalazimika kununua kifurushi cha dola 350,000 (Sh milioni 570).

Makampuni yatakayobahatika kuingia katika mchakato na kupata vitalu, yatalazimika kuwa na mtaji wa dola za Kimarekani bilioni 2.4 (Sh trilioni 4 za Kitanzania) kwa ajili ya gharama za awali za shughuli za utafutaji mafuta na gesi asilia.

“Makadirio haya hayahusishi gharama za kuweka miundombinu ya kuwezesha uzalishaji, usafishaji, uchakataji, uuzaji na gharama zinginezo. Gharama za uendelezaji kuweka miundombinu hadi kufikisha gesi kwa mtumiaji huweza kufikia hadi Dola za Marekani bilioni 15 (Sh trilioni 24.45),” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TPDC, gharama ya tathimini za kijiofizikia na kijiolojia ni dola milioni 10 (Sh bilioni 16), ukusanyaji wa takwimu za 2D na 3D 5 (dola milioni 25, sawa na Sh bilioni 40).

Gharama za tathmini zote za kimazingira zinaonesha kufikia dola milioni 12 (Sh bilioni 19.5) na uchimbaji wa visima vitatu vya awali vya utafiti ni dola milioni 510 (Sh bilioni 831), kila kimoja kikigharimu dola 170,000 (Sh bilioni 277).

Aidha, gharama nyingine kuelekea upatikanaji wa mafuta na gesi asilia ni dola milioni 900 (Sh trilioni 1.46) kwa ajili ya visima sita vya tathmini, huku visima vingine kumi vya uendelezaji vikigharimu dola bilioni 1 (Sh trilioni 1.63).

Pamoja ya ukubwa wa gharama hizo, taarifa hiyo imeeleza licha ya zabuni kuwa wazi kwa makampuni ya ndani na ya nje ya nchi, utaratibu umewekwa ili kutoa upendeleo kwa makampuni ya ndani yaliyosajiliwa kwa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumilikiwa na wazawa kwa asilimia zisizopungua 50 ikiwa yatatimiza vigezo vilivyowekwa.

Source; Habari Leo, 28/12/2013
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom