Serikali kutoa leseni kwa hospitali na vituo vya afya

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,557
21,497
Dkt.-Ndugulile-750x375.jpg

Serikali inatarajia kutoa leseni kwa hospitali na vituo vya afya vya Umma vitakavyokidhi vigezo vya ubora wa kutoa huduma za afya ili mwananchi wajue kituo atakachoenda kina ubora gani wa huduma hivyo nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akiongea na Viongozi na Watendaji wa afya wa Mkoa na Wilaya zake kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara wakati wa zoezi la kutoa ngao kwa wilaya iliyofanya vizuri na vituo vya afya vilivyofanya vizuri wakati wa zoezi la tathimini ya kutoa nyota kwa vituo vya kutolea huduma za afya.

Dkt. Ndugulile alisema hivi sasa serikali inasisitiza kuweka ubora wa huduma za afya katika vituo vyote vya afya vya umma ili kukidhi ubora unaotakiwa wa kutoa huduma kwa wananchi, ”tunakwenda mbali zaidi usipokuwa na vigezo hospitali yako na kituo chako hutopewa leseni”

Hata hivyo amewataka wale wote waliopewa maelekezo ya nini wafanye basi viongozi wawajibike kwa kurekebisha changamoto zilizopo na wasingoje idara ya uhakiki ubora kutoka wizarani waje kukagua kwani Lengo liliowekwa na wizara ni kila kituo cha afya kupata nyota tatu hadi kufikia mwezi juni mwakani.

“Nyinyi wengine wote hamkustahili kupata cheti hata kimoja hapa,Mkoa wa Mtwara asilimia 3 za vituo vyenu vina nyota mbili na asilimia 51 vina nyota moja na zaidi ya nusu mna nyota 1 na asilimia 46 mna nyota sifuri hali ya utoa huduma bado, nimetoka hapo zahanati ya Ziwani, kwakweli hapana, ubora wa kutoa huduma pale hapana wakati mpo mjini,” alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande mwingine amewataka kamati za afya ngazi ya Mkoa na Wilaya kufanya kazi na kusimamia katika kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopatiwa kwani maboresho mengine hayahitaji fedha hivyo kamati hizo zitimize wajibu wao.

”Niwaombe mbadilike kwani mambo madogo madogo yatakuja kuwagharimu hivyo msimamie hali ya utoaji wa ubora na huduma za afya kwa mkoa wa mtwara ni mbaya, nikirudi wakati mwingine sitoongea kirafiki hivi,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka watendaji hao kubadilika katika utendaji wao na hivyo kusimamia upatikanaji wa dawa katika vituo vyao vya afya ili kusiwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba wamekosa dawa.

“Dhama imebadilika, hivyo kila mmoja awajibike, awamu hii ni nyingine, hatutaki kusikia dawa hakuna na mwananchi analalamika amekosa dawa kwenye kituo cha afya, Mhe. Rais anaipenda sekta ya afya na ameongeza bajeti ya dawa na anatoa pesa zote, sitaki kusikia dawa hakuna na wilaya itakayoshindwa basi viongozi wake nao hawatoshi,” aliongeza Naibu Waziri wa Afya.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora toka Wizara ya afya Dkt. Mohamed Mohamed alisema wizara ilingia kwenye mpango wa kuboresha huduma kwenye vituo vinavyotoa huduma za afya ya Msingi mwaka 2014 kwa kuhusisha kufanya tathimini vituo vyote vya afya nchini na kuvipa kategoria ya nyota moja hadi tano ikiwemo wa kuandaa mipango ya kuimarisha ubora katika vituo hivyo.

Alitaja maeneo yaliyoangaliwa na kufanyiwa tathimini ni uendeshaji wa vituo, utendaji wa wafanyakazi,u wajibikaji, miundombinu ya kituo, mkataba kwa mteja pamoja na mazingira salama ya kutolea huduma na ubora wa huduma wenyewe.

Jumla ya vituo 6997 vilifanyiwa tathimini nchini na katika Mkoa wa Mtwara tathimini ya awali ilifanyika mwezi mei 2016 na vituo 221 vilifanyiwa tathimini na matokeo ya awali yalikua vituo 6 vilipata nyota 2(3%),vituo 112 vilipata nyota 1(51%) na vituo 103 vilipata nyota 0 (47%).

Katika zoezi hilo Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu iliibuka mshindi kwa kupata ngao na kituo cha afya Nanyumbu kilipata cheti. Kituo kingine cha afya kilichopaya cheti ni kituo cha Nagaga cha Masasi pamoja na za zahanati ya Nanjota na Nambaya zote za Halmashauri ya Masasi zilifanya vizuri. Pia zahanati ya Shangani ya halmashauri ya Manispaa ya Mtwara ilipata cheti.


Mo Dewji
 
Back
Top Bottom