Serikali kupangua madaktari bingwa, yapanga kuwatoa Dar na kuwatawanya mikoani

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
Madaktari watakaoguswa na panga pangua hiyo ni pamoja na bingwa wa kinamama, watoto, upasuaji, mionzi, dawa za usingizi na mifupa.

ummy-Mwalimu.jpg



Dar es Salaam. Wakati asilimia 60 ya madaktari bingwa wakiwa wamejikita kutoa huduma katika jiji la Dar es Salaam, Serikali imesema inakuja na panga pangua ya wataalamu hao wa afya ili kuimarisha huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa za mikoa na kanda.

Madaktari watakaoguswa na panga pangua hiyo ni pamoja na bingwa wa kinamama, watoto, upasuaji, mionzi, dawa za usingizi na mifupa.

Akizungumza katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na TBC, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema mgawanyo huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Novemba 25 katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila.

Alisema Rais aliwaagiza kuangalia namna ya kuwagawanya madaktari katika maeneo mbalimbali hasa ya pembezoni na mpaka sasa tayari wameshafanya mazungumzo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na mawaziri wenye dhamana.

“Tumepokea maelekezo ya Rais na jana tulikuwa na kikao na Makamu wa Rais, Waziri wa Elimu na Waziri wa Tamisemi, kweli kuna uhaba wa madaktari na wataalamu wengine wa kutoa huduma za afya lakini kama alivyosema Rais ni kwamba ilichangiwa na mgawanyo ambao si sawa,” alikiri Waziri Mwalimu.

Alisema kwamba wameshakusanya takwimu za awali na lengo ni kuwatoa baadhi ya madaktari hasa bingwa na kuwapeleka kwenye hospitali za mikoa ambazo tayari zipo chini ya Wizara ya Afya, hivyo wanatarajia kutoa majina ya madaktari watakaohama hivi karibuni.

“Tutaanza na fani kubwa sita kwanza ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi lakini daktari bingwa wa watoto, upasuaji, mionzi, usingizi na mifupa ni maeneo ambayo tumeshabainisha na tumesema angalau kila hospitali ya rufaa mkoa iwe na daktari bingwa wa watoto wawili na wanawake wawili.

“Kwa hivyo ndiyo tunaanza kuwapanga na naamini madaktari wapo tayari kwenda na kama alivyosema Rais tukute vifaa vipo sambamba na kuwapanga lakini pia tunazijengea uwezo hospitali za rufaa za mikoa ili kutoa huduma za matibabu ya kibingwa, badala ya watu kuja kurundikana Muhimbili na Ocean Road sasa wanatakiwa wapatiwe matibabu kwenye hospitali hizo na zile za kanda,”alisema.

Alifafanua kuwa kwa sasa bado wanaendelea kukusanya taarifa kwa ajili ya kuweka mgawanyo sahihi hasa kuhakikisha madaktari bingwa wanakuwepo katika hospitali za mikoa.

Kuhusu mafanikio katika sekta ya afya kwa mwaka 2017, Waziri Mwalimu alisema Serikali imefanikiwa kuanzisha bima ya afya kwa wajawazito ili kuwahimiza kujifungulia hospitalini na mpaka sasa bima hiyo inapatikana mikoa ya Mtwara, Lindi, Mbeya na Tanga.

Alitoa msisitizo kwa watoa huduma za afya wahakikishe wazee, wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanapata matibabu bila vikwazo vyovyote.

“Hadi sasa asilimia 40 ya wazee wameshapatiwa bima za afya kwa ajili ya matibabu ya bure na kwa mwaka huu tumeongeza vituo 100 kwa ajili ya huduma za uchunguzi na matibabu ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi na matiti, mwanzoni vilikuwa 340,” alisema.


Chanzo: Mwananchi
 
Huko mikoani kuna madaktari kwa nini wasi watrain hao badala ya kutafuta shortcut....lets wait and see....
Elimu yako ni ndogo sana ndugu, unadhani mtu kuwa daktari ni sawa na kumchukua mwalimu wa kawaida kumtrain ili apande ngazi? Na daktari kuitwa bingwa isikiage tu ndugu, siyo kila daktari ana kichwa cha kufikia level hizo.
 
Back
Top Bottom