Serikali kukubali Katiba kuwekewa viraka Dodoma maana yake ni hii...

bagamoyo

JF-Expert Member
Jan 14, 2010
21,245
24,108
MAKAMU MWENYEKITI WA CHADEMA TUNDU LISSU, AFICHUA UOZO WA KATIBA INAYOPENDEKEZWA NA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA, TUNAPIGWA TENA

Kufuatia taarifa ya Prof. Rwekaza S. Mukandala kubainisha kuna hoja 5 katika hoja 80 zilizoibuliwa zinazohitaji uharaka wa kufanyiwa kazi, baada ya mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi uliofanyika Desimba 2021 mjini Dodoma.
 
ALUTA CONTINUA! VUGUVUGU LA
DEMOKRASIA NA MAJUKUMU YETU KATIKA MWAKA MPYA 2022:

UJUMBE KWA WATANZANIA

Ndugu Wananchi na Watanzania Wenzangu,

Siku kama ya leo mwaka jana niliwaambieni maneno yafuatayo: “Katika siku ya mwisho ya mwaka huu, naomba niwapongeze wote kwa kufikia mwisho wa mwaka huu, … niwape pole wote ambao ndugu, jamaa, marafiki na majirani zao walimaliza mwendo wao kabla ya kufikia mwisho wa mwaka huu (na) wale wote ambao mwisho wa mwaka huu na siku ya kwanza ya mwaka ujao inawakuta wakiwa wagonjwa mahospitalini, wafungwa na mahabusu magerezani au wakiwa katika hali nyingine yoyote isiyokuwa ya neema na furaha.” Salamu hizi zina uzito wa kipekee mwaka huu kwa sababu, miongoni mwa wanaomalizia mwaka huu na kuanza mwaka ujao wakiwa ndani ya kuta za magereza ya watesi wa wananchi wetu ni pamoja na Mwenyekiti wetu wa Chama, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, na walinzi wake watatu.

Kama Albert Einstein, pengine mwanasayansi maarufu kuliko wengine wa karne iliyopita, alivyowahi kusema, Mwaka Mpya unatupatia fursa ya “kujifunza kutokana na ya jana, kuishi kwa ya leo, na kutumainia kwa ya kesho.” Kama ilivyokuwa kwa mwaka wa kabla yake, 2021 ulikuwa mwaka mrefu sana kwa nchi yetu. Ulikuwa mwaka wenye milima mingi na mabonde kadhaa. Kwa vyovyote vile, ulikuwa mwaka wenye mafundisho mengi.

MILIMA NA MABONDE YA 2021

Watanzania wenzangu,

Tuliuanza mwaka huu mwanasheria Tito Elia Magoti na mwenzake Theodory Giyani – wote wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wakiwa wafungwa wa maoni; na Mdude Nyagali wa CHADEMA akiwa mfungwa wa kisiasa. Leo tunaumalizia huku watatu hawa wakiwa huru, na Mdude Nyagali akiwa anaandika kitabu kuhusu mateso aliyokutana nayo mikononi mwa watesi wake na watesi wetu. Tuliuanza huku Masheikh wa Uamsho kutoka Zanzibar wakiingia mwaka wao wa nane kama “... wahanga wa tuhuma za uongo za ugaidi na sheria za kikandamizaji za utawala huu.” Tunaumalizia huku “... mateka (hawa) wa utawala wa Magufuli” wakiwa huru. Hata mimi mwenyewe niliuanza nikiwa na kesi sita za ‘michongo’, lakini naumalizia huku nikiambiwa kesi zote hizo zimefutwa!

Tuliuanza huku tukiwa na hofu kwamba yule aliyejiita ‘mtetezi wa wanyonge’ angebadilisha Katiba na kujiongezea muda wa kututawala ‘tutake tusitake’; tunaumalizia huku akiitwa ‘Mwendazake’, na wale ‘wanyonge’ wake aliowauzia vitambulisho bandia vya machinga wakivurumishwa kila mahali katika mitaa ya miji na majiji yetu kwa nguvu za kijeshi na kwa ukatili mkubwa. Ni mwaka ambao tuliambiwa kwamba kudai Katiba Mpya ni chokochoko; kwamba Katiba Mpya haitatuwekea chakula mezani wala kutupatia huduma za afya, elimu au maji ya kunywa. Tunaumalizia huku wale waliotuambia maneno hayo wakituahidi kwamba, sasa, watapiga kiraka kingine kwenye Katiba iliyopo ili kuondoa “mambo yanayolalamikiwa sana.” Ama kweli, kama anavyosema mwanazuoni maarufu wa Kimarekani mwenye asili ya Jordan, Nido Qubein, hali yetu ya sasa haiwezi kutuamulia tunakoweza kwenda, bali inatuamulia mahali tunakoanzia tu.

SIO BAHATI WALA HURUMA!

Ndugu wananchi,

Yote mema niliyoysema hapo juu kuhusu yaliyotutokea, na mengine mengi ambayo sijayasema, hayakutokea kwa bahati tu au kwa kuonewa huruma na mtu yeyote. Tuliyapigania na kuyadai kwa njia mbalimbali na kwa nyakati tofauti tofauti, ndani ya nchi na katika uwanda wa kimataifa na wa kidiplomasia, kama nilivyoelezea katika salamu zangu za mwaka jana. Kama ingekuwa ni huruma basi na masheikh, viongozi na wanachama wetu na watuhumiwa wengine wengi ambao bado wanateseka katika magereza na mahabusu mbalimbali za mikoa ya Arusha, Mwanza, Dar na kwingineko katika nchi yetu kwa sababu ya kesi za michongo za ugaidi au mauaji nao wangeachiliwa huru.

Kama ingekuwa ni ucha Mungu na ubinadamu tunaouambiwa ambiwa sasa hivi, basi wacha Mungu hawa wasingeendelea kuwasumbua viongozi wetu wa kidini pale wanapohubiri mambo wasiyoyapenda, kama walivyomfanyia Askofu Emmaus Mwamakula mwanzoni mwa mwaka na kama wanavyomfanyia Askofu Josephat Mwingira sasa hivi. Aidha, wangekuwa tofauti na Mwendazake, Mwenyekiti wetu wa chama na walinzi wake wasingemalizia mwaka huu, na kuanza mwaka ujao, wakiwa Ukonga na Segerea kwa kile ambacho kila mtu, adui ama rafiki, anajua ni kesi ya michongo, inayoendeshwa kimichongo, kwa ushahidi wa michongo, na kusimamiwa kimichongo na majaji wa michongo!

Na kama ilivyokuwa kwa kesi nyingine za michongo nilizozitaja hapa, tutaimaliza michongo hii iliyobaki na ile itakayokuja siku za mbeleni kwa kuendeleza mapambano ya kudai Uhuru, Haki, Demokrasia na Maendeleo ya Watu. Ni mapambano ya kudai haki tu, sio kutegemea huruma za watesi wetu, ndio yatakayotuokoa! Kwa hiyo, ushauri wangu wa siku kama ya leo mwaka jana bado una nguvu: “... [H]atuna budi kushughulikia tatizo la wafungwa wa kisiasa na wa maoni, wa sasa na wajao.

“Hatuna budi kufahamu na kusambaza taarifa za kila mtu aliyekamatwa, au kushtakiwa au kufungwa kwa sababu ya msimamo wake wa kisiasa au kwa sababu ya kutoa maoni yasiyowafurahisha watawala. Tutengeneze orodha ya kila aliyekamatwa, kuwekwa mahabusu au magereza au kushtakiwa au kufungwa kwa sababu za kisiasa na kosa alilotuhumiwa nalo. Tufanye kampeni na kupaza sauti, ndani na nje ya nchi yetu, ili wafungwa hawa wa kisiasa na wa maoni waachiliwe huru. Tuwasaidie kwa michango kwa ajili ya mawakili wanaowatetea mahakamani; tuwatembelee magerezani au kwenye mahabusu za polisi, na tusaidie ndugu au familia zao. Kwa vyovyote vile, tusiwafanye wajisikie wakiwa na wapweke katika saa yao ya uhitaji.”

HALI NGUMU YA MAISHA

Ndugu wananchi,

Licha ya mahubiri kwamba nchi yetu imeingia uchumi wa kati, tulianza mwaka huu huku hali za kiuchumi na kimaisha za wananchi wetu zikiwa mbaya sana. Kwanza, mamilioni ya vijana wetu waliohitimu shule na vyuo mbalimbali nchini wamekoseshwa ajira kwa sababu uchumi huu wa kati hautengenezi ajira bali uko kwenye makaratasi na matamko ya kisiasa ya watawala tu. Watawala wetu ni mabingwa wa kuwashauri vijana wetu kujiajiri huku wao wenyewe waking’ang’ania ajira za kisiasa na wamekuwa tayari hata kuua watu ili kubakia madarakani.

Matokeo yake ni kwamba mamilioni ya vijana wetu hawa wamelazimika kujigeuza kuwa maduka yanayotembea, wamachinga, na sasa wanawindwa na kufukuzwa mitaani kama wanyama pori waharibifu wa mazao.

Pili, tuliuanza mwaka huu huku gharama za maisha na bei za bidhaa muhimu kama chakula, maji, umeme, mafuta ya taa na petroli, mbolea na pembejeo za kilimo na bidhaa za ujenzi zikiwa juu kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja kabla.

Tunaumalizia mwaka huu huku bei za bidhaa hizo zikiwa juu zaidi ya mwaka jana. Kwa mfano, bei ya kilo moja ya unga wa sembe imepanda kutoka shilingi 1,000 hadi karibu shilingi 1,200; mchele umetoka shilingi 1,000 hadi 2,400, wakati kilo ya maharage imepanda kutoka shilingi 1,200 hadi shilingi 2,400. Aidha, kilo ya sukari imepanda kutoka shilingi 1,800 hadi shilingi 3,000 sasa. Vile vile, lita ya mafua ya alizeti imepanda kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 9,000 sasa, na mafuta ya Korie yameongezeka bei kutoka shilingi 4,000 hadi 6,000 sasa.

Kwa upande wa pembejeo za kilimo, bei ya mbolea imepanda bei kutoka shilingi 50,000 hadi takriban shilingi 110,000. Kwa upande wa gharama za ujenzi, bei ya simenti imepanda kutoka takriban shilingi 12,000 kwa mfuko hadi shilingi 18,000, na bei ya tani moja ya nondo imeongezeka kutoka shilingi 2,050,000 mwezi Julai hadi shilingi 3,000,000 Disemba hii. Hili ni ongezeko la karibu 50% katika kipindi cha miezi mitano! Bei za nishati nazo zimepanda huku bei ya lita ya mafuta ya dizeli ikiruka kutoka shilingi 1,500 hadi shilingi 2,500, na petroli ikiongezeka kutoka shilingi 1,800 mpaka shilingi 2,600 sasa.

Ongezeko hili la bei za bidhaa muhimu kwa maisha ya mamilioni ya Watanzania ni matokeo ya sera mbovu za serikali hii ya CCM. Sehemu ya ongezeko hili inatokana na tozo lukuki za serikali kwa wakulima, wafanya biashara, waagizaji au wazalishaji wa mazao au bidhaa hizo. Tozo hizi kubwa na nyingi zinatokana na matumizi makubwa na ya anasa ya serikali.

Nchi yetu sasa ina Ikulu mbili, miji mikuu miwili na makao makuu ya serikali mawili na Rais, mawaziri na watendaji wa ngazi za juu wa serikali wanatumia muda mwingi na gharama kubwa wakisafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa ajili ya shughuli za serikali. Msafara wa Rais peke yake una mamia ya magari na helikopta angani. Hii ni bila kuhesabu gharama kubwa za kuhudumia vyeo lukuki vya walaji wengine katika ngazi za mikoa na wilaya na mashirika na taasisi mbalimbali za serikali.

Ndugu wananchi,

Hali hii mbaya ya maisha haijatokana na ongezeko la tozo za kinyonyaji za serikali hii peke yake. Uwekezaji katika mambo ambayo hayana tija kwa uchumi wetu nao umechangia kwa kiasi kikubwa katika hali hii mbaya. Naomba kutumia mfano wa Mradi wa Bwawa la Umeme lililopewa jina la Baba wa Taifa ili tusihoji kama ujenzi huo una tija yoyote kwa nchi yetu.

Tuliuanza mwaka huu huku tukiambiwa kwamba kazi ya ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere ulikuwa umekamilika kwa asilimia 45. Tunaumalizia huku tukisikia kwamba Mradi huo, unaokadiriwa kugharimu kati ya takriban shilingi trilioni 7.25 hadi trilioni 12.5 - kwa kutegemea unamwamini mtaalamu gani - umekamilika kwa asilimia 62.7. Hata hivyo, kwa uchambuzi wa taarifa za kitaalamu na kwa kulinganisha na uzoefu wa miradi ya aina hii kwingineko duniani, Mradi huu unaweza kugharimu kati ya takriban shilingi trilioni 17.4 hadi trilioni 25, huku ukichukua kati ya miaka nane hadi kumi kukamilika. Wakati tukiendelea kumwaga matrilioni haya katika Mradi huu, tunaendelea kukabiliwa na matatizo makubwa ya mgawo wa umeme kila mahali nchini.

Kwa upande mwingine, kama hawa wanaojiita watetezi wa wanyonge wangeamua kuwekeza matrilioni hayo katika miradi mikubwa au ya kati ya nishati mbadala za jua au upepo au gesi asilia, ambazo zina uwezekano mkubwa wa kutatua matatizo ya nishati katika nchi yetu, gharama zake zingekuwa nafuu zaidi, huku muda wa kukamilisha miradi hiyo ikiwa kati ya mwaka mmoja hadi miwili. Ukweli ni kwamba wakati wa utawala wa Rais Kikwete kulitengenezwa mpango mkakati wa nishati ambao ulilenga kuendeleza miradi ya aina mbalimbali za nishati ikiwemo maji, gesi asilia na upepo.

Lakini mtetezi wa wanyonge alipoingia madarakani mwaka 2015, miradi yote hiyo ilitelekezwa na nguvu na rasilmali zote zikaelekezwa kwenye Mradi mmoja ambao haujulikani utaisha lini, kwa gharama gani na utatoa umeme kiasi gani, kwa sababu takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali haziaminiki kwa kuwa ni takwimu za michongo kama yalivyo mambo mengi ya serikali hii. Na Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere ni mmoja tu. Hapa hatujazungumzia Mradi wa Ujenzi wa Reli ya SGR ambao nao umegharimu matrilioni hadi sasa na hauelekei kukamilika, achilia mbali manufaa yake ya mashaka kiuchumi kwa mujibu wa uchambuzi wa kina wa wataalamu huru.

Na wala hatujazungumzia manunuzi ya ndege yanayoendelea, huku tukiambiwa kwamba ATCL yenyewe haijawahi kuingiza faida tangu tuanze kumwaga matrilioni ya shilingi kwenye manunuzi ya ndege hizo, na huku tukiona biashara ya usafiri wa anga ikianguka kila mahali duniani kwa sababu ya ugonjwa wa corona. Sisi tunanunua ndege kwa mikopo, kama inavyodaiwa sasa, au kwa pesa taslimu - kama tulivyokuwa tunaambiwa wakati wa Mwendazake - huku wenzetu ambao wana uzoefu mkubwa zaidi wa biashara hiyo wakirudisha ndege walizokodi kutoka kwa watengenezaji kwa sababu ya mazingira mabaya ya biashara hiyo.

Rai yangu kwa Rais Samia na serikali yake, ndugu wananchi, ni kwamba apate ujasiri wa kisiasa wa kuiangalia miradi yote hii upya na kuamua kama kuna manufaa yoyote ya kiuchumi na kijamii kuendelea nayo kwa muundo wake wa sasa. Akijiridhisha kwamba miradi hii haitekelezeki bila kuifilisi nchi yetu, kama ushahidi huru unavyoonyesha, basi awe na ujasiri wa kuachana nayo. Asipofanya hivyo, tena kwa haraka, kuna hatari kubwa mbeleni ya miradi hii kuwa magofu ambayo hayatakamilika. Rais Samia apate ujasiri wa kuwaambia Watanzania ukweli mchungu badala ya kuendelea kutudanganya na maneno matamu kama ‘kazi iendelee’ kama ilivyokuwa ‘hapa kazi tu’ ya Mwendazake. Ni bora kupata aibu kwa kusema ukweli na kupunguza hasara, kuliko kupata laana ya kuwadanganya wananchi na kuliongezea taifa mzigo mkubwa zaidi wa madeni na hasara zinazoepukika!

Ndugu wananchi,

Kwa miaka mitano ya utawala wa Magufuli, huku Samia akiwa namba mbili wake, tulidanganywa kwamba miradi yote hii, na mingine mingi, ilikuwa inaendeshwa kwa fedha zetu wenyewe. Sasa tunajua kumbe miradi hii ilikuwa ni pesa ya mikopo, na sasa tunaambiwa kwamba katika miaka mitano ya utawala wake, Rais Magufuli alikopa pesa nyingi kutoka nje kuliko alizokopa Kikwete kwa miaka kumi ya utawala wake. Sasa tunaambiwa kwamba deni la taifa limefikia zaidi ya shilingi trilioni 70 na malipo ya riba kwa deni hilo pekee ni zaidi ya shilingi trilioni 10 kwa mwaka. Tukumbuke kwamba hizi ni pesa zinazolipwa kwa mikopo kwa ajili ya miradi ambayo bado haijakamilika na kuanza uzalishaji!

Wananchi wenzangu,

Ulevi huu wa mikopo hauelekei kwisha au kupungua, hata baada ya Mwendazake kwenda zake. Kwa taarifa zilizopo, kwa mwaka huu peke yake, serikali yetu imekopa dola milioni 875 (sawa na takriban shilingi trilioni 2.2) mwezi Mei kutoka Benki ya Dunia; dola milioni 150 (shilingi bilioni 375) kwa ajili ya Zanzibar mwezi Juni kutoka Benki ya Dunia; dola milioni 567 (takriban shilingi trilioni 1.4) mwezi Septemba kutoka IMF; dola milioni 256 (takriban shilingi bilioni 640) kati ya Mei na Septemba kutoka AfDB, na dola milioni 650 (takriban shilingi trilioni 1.6) kutoka Benki ya Dunia mwezi huu pekee.

Kwa hiyo jumla ya madeni ya mwaka huu peke yake ni takriban dola bilioni 2.5, sawa na takriban shilingi trilioni 6.245. Zaidi ya watu wachache tu serikalini, sio Bunge wala watanzania kwa ujumla wetu tunaojua masharti ya miikopo hii, ila tunajua tutailipa yote na riba juu tutake tusitake! Kwa hali hii, Spika Ndugai alikosea aliposema kuna siku nchi yetu itapigwa mnada: imeshapigwa mnada tayari, tena siku nyingi ila bado hatujajua bei yote ya mnada huo!

Kwa kuzingatia hali ya ukame unaoendelea kuzikabili sehemu mbalimbali za nchi yetu, taifa litakabiliwa na tishio la uhaba mkubwa wa chakula mwakani. Badala ya serikali hii kuendelea kuelekeza rasilmali za nchi yetu katika uwekezaji usiokuwa na tija kiuchumi wala maslahi yoyote kwa wananchi wetu na kuwaongezea mzigo wa maisha magumu, ni muhimu serikali ijiandae kukabiliana na janga hilo linalotunyemelea kwa kupunguza matumizi ya serikali na kusitisha uwekezaji huu usio na tija yoyote kwa uchumi wetu. Aidha, serikali hii iache kulitwisha taifa letu mikopo na madeni ambayo hayatalipika bila kulifilisi taifa.

MBOWE SIO GAIDI!

Ndugu wananchi,

Tarehe 9 Aprili 2021, takriban wiki tatu baada ya kuapishwa kuwa Rais, Mwenyekiti wetu alimwandikia Rais Samia “barua ya pole, pongezi na maombi ya kukutana na kushauriana na wewe.” Pamoja na kumpa pole kufuatia kifo cha Rais Magufuli na kumpongeza kwa ‘haiba na utulivu’ wake kipindi chote cha msiba, Mwenyekiti Mbowe alimweleza Rais Samia kwamba kwa kipindi kifupi cha kuwepo kwake madarakani, alikuwa “amelijengea matumaini chanya taifa letu ya kurejesha utengemano, haki, furaha na upendo kwa Watanzania kupitia hotuba zake zenye maelekezo, maonyo na ahadi.”

Aidha, Mwenyekiti Mbowe alimjulisha Rais Samia kwamba hotuba yake ya siku ya kiapo chake, ambako Rais alitoa rai ya maridhiano ya kisiasa, ilikuwa imegusa mioyo ya Watanzania, wakiwemo viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA ambao walikuwa na “mioyo inayovuja damu na macho yaliyojaa machozi kwa mengi magumu tuliyopitia na tunayoendelea kupitia katika kuutenda wajibu wetu….”

Mwenyekiti Mbowe alimuomba Rais Samia, ikimpendeza, “kutupatia nafasi ya kukuona siku, saa na mahali itakavyokupendeza kwa mazungumzo ya faragha yenye lengo (la kufungua ukurasa mpya kwa nchi yetu.”

Watanzania wenzangu,

Rais Samia alijibu barua ya Mwenyekiti Mbowe wiki tu moja baadae, yaani tarehe 16 Aprili. Naomba kunukuu sehemu muhimu zaidi ya majibu ya Rais: “Baada ya kusoma barua hiyo, Mheshimiwa Rais ameelekeza nikujulishe anashukuru kwa salamu za rambirambi na pongezi. Aidha, ameelekeza tarehe ya kukutana naye mtajulishwa.” Hatukujulishwa tarehe ya kukutana na Rais, na hatujajulishwa hadi leo hii.

Badala yake, mtu aliyemwandikia Rais barua ya heshima na unyenyekevu mkubwa kiasi hiki yupo gerezani tangu tarehe 21 Julai akikabiliwa na kesi ya mchongo ya kula njama na kufadhili ugaidi na, endapo Jaji aliyeteuliwa na Magufuli atamkuta na hatia, atahukumiwa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka thelathini jela! Na kama ambavyo tumeshuhudia mahakamani, kesi hii inategemea ushahidi wa michongo uliopatikana kwa kutesa watuhumiwa ili wakiri makosa ya kuchonga.

Ndugu wananchi,

Sisi wa CHADEMA tumedai, tunadai na tutaendelea kudai Mwenyeiti wetu na walinzi wake waachiliwe huru bila masharti yoyote. Mwenyekiti Mbowe hana, na hajawahi kuwa na hatia ya kosa lolote la jinai, achilia mbali kosa la ugaidi. Sababu pekee ambayo imemsababishia kuteseka gerezani muda wote huu ni yeye kuongoza harakati za kudai Katiba Mpya kwa ajili ya nchi yetu. Kama wote tunavyofahamu, Mwenyekiti alikamatwa jijini Mwanza ili kumzuia kuendesha kongamano la CHADEMA kuhusu Katiba Mpya lililokuwa limepangwa kufanyika kesho yake.

Kuongoza harakati za kudai Katiba Mpya, au kuendesha kongamano kwa ajili hiyo sio, na haijawahi kuwa kosa lolote la jinai, achilia kosa la ugaidi kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Kuwa na walinzi waliotumikia nchi yetu kama makomando wa kijeshi na wakaacha au kuachishwa kazi sio, na halijawahi kuwa, kosa lolote la jinai, achilia mbali kosa kubwa kama la ugaidi. Kwa sababu hiyo, Mwenyekiti Mbowe na walinzi wake ni wafungwa wa kisiasa.

Ndio maana tunadai na tutaendelea kudai waachiliwe huru bila masharti yoyote. Ndio maana wawakilishi wa kidiplomasia wa nchi rafiki na nchi yetu wanahudhuria mahakamani kuangalia kesi hii kila siku. Na ndio maana taasisi za kimataifa, kama Bunge la Ulaya, zimedai kwamba Jumuiya ya Ulaya iitake Serikali ya Tanzania kufuta mashaka dhidi ya Mwenyekiti Mbowe na wanachama wengine wa CHADEMA walioko kwenye magereza mbalimbali nchini. Na ndio maana, kwa mwaka wa pili mfululizo, Halmashauri Kuu ya Shirikisho la Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) imepitisha kwa kauli moja maazimio nane kuhusu hali ya demokrasia na haki za binadamu katika nchi yetu, ikiwemo kudai kuachiliwa bila masharti yooyote kwa Mwenyekiti Mbowe na wafungwa wengine wa kisiasa nchini.

HATUDANGANYIKI!

Ndugu wananchi,

Huu ndio mwaka ambao tuliambiwa kwamba kudai Katiba Mpya ni kuleta chokochoko. Lakini, pamoja na Mwenyekiti wetu kukamatwa na kushtakiwa kwa kesi ya mchongo ya ugaidi na licha ya makongamano yetu kuzuiliwa kwa mabavu ya Jeshi la Polisi, sisi wa CHADEMA tuliendeleza chokochoko hizo kwa namna na katika majukwaa mbalimbali.

Hatukukubali kutishwa wala kurubuniwa kwa vyeo au kwa fedha au kwa rushwa za aina nyingine. Hatimaye, wale waliotamka kwamba Katiba Mpya haina maslahi yoyote kwa wananchi na mamluki wao wameanza kuzungumza lugha ya kufanya mabadiliko ya Katiba.

Kama mnavyokumbuka, tarehe 15 had 17 mwezi huu kilifanyika kilichoitwa ‘Mkutano wa Wadau wa Kujadili Hali ya Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa Nchini Tanzania’, mjini Dodoma. Licha ya kudaiwa kuitishwa na Baraza la Vyama vya Siasa, mwaliko, maandalizi na uendeshaji wa mkutano huo ulifanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Aidha, gharama zote za mkutano zilibebwa na Ofisi ya Msajili.

Mada zilizojadiliwa, watoa mada na wajadili mada - wote wanaCCM au mamluki wao - waliteuliwa na kulipwa na Ofisi ya Msajili. Aidha, washiriki wote wa mkutano walilipiwa gharama zote za usafiri, malazi, chakula na posho za ushiriki kwa siku zote tatu na Ofisi ya
Msajili.

Hadi sasa hakuna maazimio rasmi ya mkutano yaliyochapishwa na kutolewa hadharani. Hata hivyo, wakati wa kufungwa kwa mkutano, Mwenyekiti wa mkutano huo, Profesa Rwekaza Mukandala, alitangaza kwamba mkutano uliibua hoja 81 ambazo zilijitokeza kwenye mkutano. Kwa mujibu wa Profesa Mukandala, baadhi ya hoja hizo ni:

➢ Sheria ya Vyama vya Siasa na ya Jeshi la Polisi zifanyiwe marekebisho ili kuondoa uonevu kwa kisingizio cha kutekeleza
sheria;

➢ Vyama vya siasa vina haki ya kufanya mikutano ya hadhara na suala la mikutano hiyo lishughulikiwe;

➢ Mchakato wa Katiba Mpya usiendelee badala yake yaangaliwe mambo machache yanayolalamikiwa sana na hayo ndio yashughulikiwe. Aidha, Katiba Inayopendekezwa ifanyiwe marekebisho na kupitishwa badala ya kuanza mchakato upya;

➢ Masuala ya NEC yamepokelewa na yanayoweza kufanyiwa kazi yatafanyiwa kazi.

Wananchi wenzangu,

Hadi sasa maazimio haya hayajachapishwa rasmi mahali popote pale. Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa amekwishaunda Kikosi Kazi cha kupitia hoja hizi. Kikosi Kazi kitaongozwa na Profesa Mukandala na Hamad Rashid Mohamed kama Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wake, na wajumbe wengine 21. Aidha, Kikosi Kazi kitasaidiwa na sekretarieti itakayoteuliwa na Msajili wa Vyama na kuongozwa na Katibu wa Kikosi Kazi ambaye ni Msajili Msaidizi wa Vyama. Vile vile, Hadidu za rejea za Kikosi Kazi hicho zitaandaliwa na kutolewa na Msajili wa Vyama tarehe 10 Januari 2022, siku kinapotarajiwa kuzinduliwa rasmi. Kwa mujibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya kukamilisha kazi yake ndani ya mwezi mmoja, Kikosi Kazi kitawasilisha mapendekezo yake kwa Baraza la Vyama vya Siasa “... ambalo litayapitia na kuyawasilisha
serikalini.”

Vyama vyote vya siasa, hasa vile ambavyo havijawahi kujishughulisha na mikutano ya kisiasa na kwa hiyo havijawahi kuwa na tatizo lolote na amri haramu ya kuzuia mikutano ya hadhara, na ambavyo vimekuwa vikishirikiana na CCM na serikali yake kwa kipindi chote cha utawala wa Magufuli na hata kabla, vilishiriki mkutano huo. Hata hivyo, sisi wa CHADEMA na, kwa heshima yao, NCCR-Mageuzi, tulitangaza wazi kutoshiriki kwenye mkutano huo kwa sababu hakukuwa, na bado hakuna, mazingira muafaka ya kushiriki katika mikutano au vikao vya aina hiyo. Viashiria vya kutokuwepo kwa mazingira muafaka na dhamira ya dhati ya kukaribisha mikutano ya maridhiano na maelewano yya kisiasa ni pamoja na yafuatayo:

➢ Wafungwa wa kisiasa, akiwepo Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, na wanachama wengine wa CHADEMA kuendelea kushikiliwa katika magereza mbali mbali nchini kwa tuhuma za uongo zilizosababishwa na msimamo wao
wa kisiasa;

➢ Vyama vya siasa vya upinzani kuendelea kuzuiliwa kuendesha shughuli halali za kisiasa kama mikutano ya hadhara na
maandamano kinyume na matakwa ya sheria za nchi yetu;

➢ Kuendelea kuwepo kwa kesi za kisiasa dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, zilizofunguliwa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Ndugu wananchi,

Hata tukiachia mbali ukweli kwamba mchakato wote huu unamilikiwa na kudhibitiwa na Serikali ya Rais Samia kupitia Ofiisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wajumbe wote wa Kikosi Kazi ni wanaCCM au washirika wao wa karibu. Licha ya wanaojulikana wazi kuwa wanachama wa CCM au watumishi wa serikali yake, wajumbe wengine wote waliobakia ni watu ambao, kwa nyakati mbalimbali na nafasi tofauti tofauti, wamejithibitisha kukubaliana na sera na matendo ya utawala wa CCM.

Kwa mfano, Mwenyekiti wa Kikozi Kazi, Prof. Mukandala, na wajumbe wawili, maprofesa Bernadetta Killian na Alexander Makulilo, ni wanazuoni ambao - kwa kutumia taasisi yao ya REDET - kwa muda mrefu wamehalalisha chaguzi za vyama vingi katika nchi yetu kwa kuzipatia ‘vyeti’ vya kuwa chaguzi huru na za haki. REDET iliupatia hata Uchafuzi Mkuu wa mwaka jana, ambao umethibitika kuwa wa hovyo kuliko nyingine zote, hati ya kuwa uchaguzi huru na wa haki yenye masharti! Ripoti yenyewe ya REDET inakiri kwamba waangalizi wa uchaguzi wa REDET ‘waliwezeshwa’ kwa kupewa mafunzo na NEC na
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa!

Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na mjumbe mwingine wa Kikosi Kazi, Juma Ali Khatib, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ADA-TADEA na mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar aliyeteuliwa na Rais wa Zanzibar. Vile vile, Makamu Mwenyekiti Hamad Rashid Mohamed, ni Mwenyekiti wa chama cha ADC ambaye aliwahi kuikimbia CUF ya Maalim Seif Shariff Hamad na kuzawadiwa ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na uwaziri na Rais Ali Mohamed Shein.

Mjumbe mwingine wa Kikosi Kazi, Abdul Mluya, ni Katibu Mkuu wa chama cha DP na mmojawapo wa viongozi wa vyama waliotumiwa sana na CCM kumwekea mgombea urais wa CHADEMA mapingamizi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana ili CHADEMA izuiliwe kuendesha kampeni zake.

Kwa upande wao, wale wanaoitwa wajumbe wa asasi za kupigania haki za wanawake, walemavu au zinazojishughulikisha na masuala ya siasa, viongozi wa kidini, waandishi habari na hata Vyama vya Mawakili vya Tanganyika na Zanzibar, sio watu waliochaguliwa na taasisi husika bali ni wateule wa Msajili wa Vyama vya Siasa. Aidha, ni watu ambao hawajawahi kujipambanua kwa lolote katika masuala ya kupigania haki za binadamu au demokrasia katika nchi yetu, huku wengine wakiwa watumishi wa serikali hii ya CCM kwa muda mrefu. Watu hawa hawawezi kutegemewa kupendekeza jambo lolote litakalohatarisha maslahi ya CCM katika suala zima la demokrasia.
Watanzania wenzangu,

Naomba sasa nizungumzie Baraza la Vyama vya Siasa. Baraza hili liliundwa kwa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2009. Kwa kuangalia sheria hii, hiki ni chombo kinachodhibitiwa moja kwa moja na Msajili wa Vyama vya Siasa, na kwa hiyo na CCM na serikali yake. Kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu ni mwanachama, kitake kisitake, na kinatakiwa kuteua viongozi wawili wa kitaifa kuwa wajumbe wa Baraza.

Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza wanatakiwa kuchaguliwa na wajumbe wa Baraza kutokana miongoni mwao.

Kiuhalisia, vyama vidogo vidogo na ambavyo havina uzito au uwezo wowote kisiasa nchini ndivyo huamua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, baadhi ya vyama hivi vilitumiwa na CCM na NEC au ZEC kuwawekea mapingamizi wagombea urais, ubunge na udiwani wa CHADEMA ili kuwazuia kuendesha au kuvuruga kampeni zao za uchaguzi.

Ofisi ya Msajili wa Vyama ndio sekretarieti ya Baraza, ikimaanisha kwamba Msajili wa Vyama au msaidizi wake ndiye Katibu wa Baraza. Fedha za kuendeshea shughuli za Baraza ni za serikali au za wafadhili lakini kwa kupitia serikali. Kazi za Baraza zimeainishwa kuwa ni pamoja na kumshauri Msajili juu ya migogoro inayoibuka miongoni mwa vyama vya siasa, na kuhusu hali ya kisiasa; kuishauri serikali kwa kupitia Msajili juu ya utungaji, urekebishaji na utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na sheria na kanuni nyingine husika; na kumjulisha Msajili juu ya jambo lolote linalohusu shughuli za chama chochote cha siasa.

Mamlaka ya kutunga kanuni za uendeshaji wa shughuli za Baraza yamekabidhiwa kwa Waziri anayesimamia masuala ya vyama vya siasa. Ndio kusema kwamba hata mamlaka ya kutunga kanuni hizo yako mikononi mwa serikali na, kwa mantiki hiyo, CCM. Baraza halina mamlaka yoyote ya kiutendaji au kimaamuzi kuhusu jambo lolote. Chombo hiki sasa ndicho tunataka kuaminishwa kuwa ndicho kitakachoongoza mchakato wa mabadiliko ya Katiba na sheria ili kurudisha na kupanua demokrasia katika nchi yetu! Tutegemee kitu gani kutokana na mchakato huu?

KIRAKA KINGINE HAPANA!

Ndugu wananchi,

Kamati Kuu ya chama chetu ilikutana kidigitali siku ya Jumanne ya tarehe 28 Disemba ili kutafakari masuala haya yote na kuweka msimamo wa CHADEMA kuhusiana nayo. Baada ya mjadala mrefu na wa kina, Kamati Kuu imeazimia kwamba CHADEMA haitashiriki katika shughuli zote za Baraza la Vyama ambazo malengo yake ya wazi ni kuua na kuzika ndoto na matamanio ya Watanzania ya kujipatia Katiba Mpya. Kamati Kuu yetu imefikia uamuzi huu kwa kuzingatia historia ya nchi yetu ya kisiasa na kikatiba, hasa tangu kurudishwa kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi mwaka 1992.

Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa, maarufu kama Tume ya Nyalali, iliyoundwa na Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1990, ndio ilikuwa ya kwanza kupendekeza kutungwa kwa Katiba Mpya kwenye ripoti yake ya mwaka 1991. Tume ya Nyalali iligundua kwamba kwa historia, misingi na maudhui yake, Katiba ya sasa ni katiba ya chama kimoja. Kwa sababu hiyo, Tume ya Nyalali ilisisitiza kwamba Katiba hii haiwezi kukidhi matawa na mahitaji ya mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi.

Hata hivyo, kwa miaka yote thelathini tangu Tume ya Nyalali itoe mapendekezo yake, CCM na serikali yake imeendelea kukataa kutungwa kwa Katiba Mpya. Badala yake, CCM na serikali yake imekuwa ikiweka ‘viraka’ kwenye Katiba ya sasa kwa kuifanyia marekebisho madogo madogo yasiyobadili misingi na maudhui yake Katiba. Kuanzia tuliporudi kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hadi sasa, Katiba hii imeshashonewa viraka nane.

Badala ya kupunguza matatizo ya mfumo wetu wa kiutawala na kisiasa, viraka hivi vimeyaongeza matatizo hayo. Miaka hii sita ya utawala wa Magufuli na mrithi wake wa sasa, ambapo nchi imeendeshwa nje kabisa ya taratibu za kikatiba na kisheria, ni uthibitisho tosha kwamba Katiba ya sasa haiwezi tena kututatulia matatizo ya mfumo wetu wa kiutawala na wa kisiasa. Vikijumlishwa pamoja na viraka nane vya wakati wa mfumo wa chama kimoja, Katiba hii ina jumla ya viraka 13 hadi sasa. Kama ingekuwa ni nguo, basi ingekuwa imechakaa kiasi kwamba mtu hawezi kujua kipi ni kitambaa chake cha awali na vipi ni vitambaa vya viraka!

Hii ndio tafsiri sahihi ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete wakati anaanzisha mchakato wa Katiba Mpya siku kama ya leo miaka kumi iliyopita, pale aliposema kidiplomasia: “Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali ya maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki (cha miaka 50 ya Uhuru). Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa ya hali ya sasa. Katiba itakayolipeleka taifa letu miaka 50 ijayo kwa salama, amani, umoja na kuwepo maendeleo makubwa zaidi.”

Katika mazingira haya, mapendekezo ya wanaCCM na washirika wao waliokutana Dodoma chini ya mwavuli wa Baraza la Vyama vya Siasa, kwamba yaangaliwe mambo machache yanayolalamikiwa sana na hayo ndio yashughulikiwe, yana taafsiri moja tu: kuongeza viraka vingine katika hii nguo ambayo kila mwenye nia njema na nchi anajua imechakaa na haifai kuendelea kuvaliwa tena. Sisi wa CHADEMA hatutakubali kuwasaliti Watanzania kwa kushiriki katika mchakato huo. Swali nii je, tutafanya nini ili kuipata Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa ya hali ya sasa?

NI RASIMU YA WARIOBA TU!

Ndugu wananchi,

Tayari kuna msingi wa Katiba ya Wananchi: Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya mchakato ulioshirikisha wananchi wa Tanzania kwa namna ambayo haijawahi kufanyika katika historia yetu yote. Kazi ya Tume ya Warioba haikukamilika kwa sababu mchakato wake ulitekwa nyara na CCM na kunyongwa hadi kufa kwa kutumia Bunge Maalum lililopitisha Katiba Inayopendekezwa. Misingi ya Rasimu ya Warioba iko vizuri lakini inahitaji kuboreshwa zaidi.

Sisi wa CHADEMA tunapendekeza kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba ya Wananchi ambao utaunganisha nguvu za vyama vya siasa, makundi mbalimbali ya kijamii, taasisi za kidini, taasisi za kitaaluma na asasi zisizo za kiserikali ambazo zinaunga mkono madai ya Katiba Mpya na Rasimu ya Warioba.

Tunapendekeza hivyo kwa sababu huu ndio utaratibu ambao CCM na washirika wake wameamua kuutumia ili kushona kiraka kingine katika Katiba ya sasa. Kama ni sahihi kwa CCM na washirika wake kufanya mikutano na makongamano yanayohusu kushona viraka vingine kwenye Katiba ya sasa, haiwezi kuwa haramu kwa CHADEMA na washirika wake kufanya mikutano na makongamano ya aina hiyo kwa ajili ya Katiba Mpya.

Kuna sababu nyingine. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa Dodoma, Rais Samia alikiri kile ambacho sisi wa CHADEMA tumekisisitiza miaka yote ambayo serikali ya Magufuli na ya Rais Samia mwenyewe imetuzuia kufanya mikutano ya hadhara: kwamba vyama vya siasa vina haki ya kufanya mikutano ya hadhara na maandamano kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Vyama vya Siasa. Msimamo huu sahihi wa kisheria umerudiwa na wajumbe wa mkutano wa Dodoma.

Kwa vile sasa serikali na wadau wote wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa wanakubaliana kwamba vyama vya siasa vya upinzani vina haki sawa na CCM ya kufanya mikutano ya hadhara na maandamano kwa mujibu wa sheria zilizopo, CHADEMA itapendekeza kwa wale wote watakaoungana nasi kudai Katiba Mpya kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi juu ya Rasimu ya Warioba kwa njia ya mikutano ya hadhara na makongamano yatakayofanyika katika sehemu mbalimbali za nchi yetu.

Tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo, wananchi watapata uelewa mkubwa zaidi wa masuala mbalimbali yanayohusu Katiba Mpya na umuhimu wake katika maisha yao ya kila siku.

NITARUDI NYUMBANI!

Ndugu wananchi,

Kazi hii ya kuunganisha nguvu za wananchi ili kupata Katiba Mpya inayotokana na maoni yao kama yalivyofanyiwa uchambuzi na Tume ya Warioba inahitaji nguvu na mchango wa kila mmoja wetu anayeamini kwamba Tanzania haistahili tena katiba ya viraka bali inahitaji Katiba Mpya “inayoendana na mabadiliko na matakwa ya hali ya sasa.” Hao ni pamoja na mimi mwenyewe ambae, kama mnavyofahamu, nililazimika kukimbia nchi yetu ili kuokoa maisha yangu kutokana na jaribio la mauaji la tarehe 7 Septemba, 2017, na kutokana na vitisho vya mauaji mara baada ya Uchafuzi Mkuu wa mwaka jana. Na hii inamhusu Mheshimiwa Godbless Lema ambaye nae alilazimika kuukimbilia uhamishoni Canada kwa sababu hiyo hiyo.

Kama chama tulitarajia kwamba baada ya usiku wa giza nene wa utawala wa Rais Magufuli kufikia mwisho mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia na serikali yake ingefungua ukurasa mpya wa maridhiano na mapatano ya kitaifa kwa kutuhakikishia usalama wa maisha yetu na uhuru wetu. Licha ya jitihada zetu binafsi na rasmi za kutaka maridhiano ili tuweze kurudi nyumbani na kuendelea na shughuli zetu kama wananchi wengine, serikali ya Rais Samia haijachukua hatua yoyote kutuhakikishia usalama na uhuru wetu, na wala haijachukua hatua zozote kuchunguza jaribio la mauaji dhidi yangu. Badala yake, kumekuwa na kauli nyingi za kejeli ambazo zimetolewa katika nyakati tofauti na Jeshi la Polisi na viongozi wake wa kisiasa.

Pamoja na serikali kushindwa kutuhakikishia usalama na uhuru wetu, hatuwezi kuendelea kuishi uhamishoni bila ukomo. Hivyo, katika kikao chake cha tarehe 28 Disemba, Kamati Kuu ilijadili suala la kurudi kwetu kwa kina na kuazimia kwamba mimi na Mheshimiwa Lema tuanze kufanya maandalizi ya kurudi nyumbani kati ya mwezi Machi na Aprili ya Mwaka Mpya 2022. Kamati Kuu iliazimia kwamba, kwa upande wake, chama kianze kufanya maandalizi yote ya ujio wetu kwa upande wa Tanzania. Baada ya maandalizi yote kukamilika, tarehe kamili ya kurudi kwetu itatangazwa rasmi kwa wanachama, wafuasi na wapenzi wa CHADEMA na kwa wananchi wote.

Kwa hiyo, ndugu zangu Watanzania, siku hii ya leo inaleta mwisho na vile vile inaleta mwanzo, kama Cicero - mwanafalsafa na seneta wa Kirumi - alivyosema wakati anavunja ukimya wake mbele ya baraza la seneti la Roma ya kale. Inaleta mwisho wa sintofahamu juu msimamo wa chama chetu kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na juu ya mchakato wa katiba viraka ya CCM na washirika wake. Inaleta mwisho wa vyama vya siasa vya upinzani wa kweli kuwa kwenye kifungo haramu cha kutofanya mikutano ya hadhara na maandamano ambayo, kwa kauli ya Rais Samia mwenyewe, ni haki ya vyama vyote vya siasa. Na inaleta mwisho wa mimi, Mheshimiwa Lema na wakimbizi wengine wa utawala wa Magufuli kuendelea kuishi uhamishoni.

Siku ya leo inaleta mwanzo vile vile. Inaleta mwanzo wa harakati mpya za Katiba Mpya ya wananchi kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba. Inaleta mwanzo mpya kwa siasa za vyama vingi nchini kwetu, baada ya miaka sita ya giza nene lililotokana na amri haramu ya kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani. Na inaleta mwanzo mpya kwetu sisi wakimbizi wa utawala wa Magufuli kurudi nyumbani kuja kushiriki kuijenga nchi yetu na demokrasia yetu.

Watanzania wenzangu,

Ninafahamu kwamba siku zijazo hazitakuwa rahisi. Ninajua kuwa tutakabiliwa na majaribu ya kila aina na tutapitishwa katika tanuru kubwa la matatizo na magumu mengi. Lakini licha ya mazingira hayo magumu, na mbele ya changamoto kubwa na nyingi zitakazotukabili, hatutainamisha vichwa vyetu na kukata tamaa. Tunaamini, kama Kitabu cha Yeremia kinavyosema kwenye Biblia, kwamba Mwenyezi Mungu anatuwazia sisi Watanzania “mawazo ya kutustawisha na wala sio ya kutuumiza, mawazo ya kutupa tumaini kwa siku zetu zijazo.”

Brad Douglas Paisley, mwanamuziki wa Kimarekani, amewahi kusema yafuatayo kuhusu Mwaka Mpya: “Kesho ni ukurasa wa kwanza mpya wa kitabu chenye kurasa 365. Nenda kaandike kitabu kizuri”! Basi naomba mniruhusu na mimi niwaambieni Watanzania wenzangu, kwamba kuanzia kesho kila mmoja wetu, kwa kadri ya uwezo na nafasi yake, aanze kuandika kitabu hiki chenye kurasa 365. Kila mkulima aliyenyang’anywa au kukopwa mazao yake; kila mfugaji aliyeporwa mifugo yake au maeneo ya kuichungia; kila mfanyakazi ambaye hajapata nyongeza yake ya mshahara au kunyimwa stahili zake nyingine; kila mwanafunzi aliyenyimwa haki yake ya kupata elimu bora na kila mhitimu aliyenyimwa ajira aandike sehemu yake kwenye kitabu hicho.

Kila Machinga aliyeuziwa kitambulisho feki na sasa anafukuzwa kila mahali kama mhalifu na kuporwa bidhaa zake; kila mvuvi aliyechomewa moto nyavu zake au kupigwa na kuumizwa kwa kutafuta riziki yake baharini au ziwani; kila mfanyabiashara aliyebambikizwa kesi ya utakatishaji fedha ili aporwe mali zake na kufilisiwa; kila kiongozi wa kidini aliiyetishwa au kuonewa kwa kuhubiri yasiyowapendeza watawala na kila kiongozi au mwanachama wa chama cha siasa au asasi ya kiraia aliyeonewa na watawala hawa kwa miaka yote hii.

Wote hawa, na wengine ambao sijawataja, tushirikiane ili tuandike kitabu chetu kipya, kitabu cha Katiba Mpya na ya kidemokrasia itakayotuhakikishia ulinzi wa haki na utu wetu, kutuondolea ukandamizaji na kesi za michongo, kutuletea Tume Huru ya Uchaguzi na kutuwezesha kujiletea maendeleo yetu wenyewe na ya nchi yetu.

Nawatakieni Heri ya Mwaka Mpya wenye furaha, baraka na mafanikio katika maisha ya kila mmoja wenu!!!

Tundu A.M. Lissu
Tienen, Ubelgiji
31 Disemba 2021
 
Attachments

  • Waraka wa Mwaka Mpya (2).pdf
    148.1 KB · Views: 10
Hayo yamebainishwa leo baada ya Hotuba kabambe iliyotolewa na Mh Tundu Lissu kwa Taifa .

Inatarajiwa Lissu na Lema watawasili nchini Tanzania kati ya mwezi wa 3 na wa 4 2022 , huku Juhudi za kuhakikisha watu wote waliokimbilia Nje ya Tanzania kukwepa kutekwa ama kuuawa katika utawala wa awamu ya 5 wanarudi nyumbani
 
Ndio maana tunadai na tutaendelea kudai waachiliwe huru bila masharti yoyote. Ndio maana wawakilishi wa kidiplomasia wa nchi rafiki na nchi yetu wanahudhuria mahakamani kuangalia kesi hii kila siku. Na ndio maana taasisi za kimataifa, kama Bunge la Ulaya, zimedai kwamba
Jumuiya ya Ulaya iitake Serikali ya Tanzania kufuta mashaka dhidi ya Mwenyekiti Mbowe na wanachama wengine wa CHADEMA walioko kwenye magereza mbalimbali nchini. Na ndio maana, kwa mwaka wa pili mfululizo, Halmashauri Kuu ya Shirikisho la Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) imepitisha kwa kauli moja maazimio nane kuhusu hali ya demokrasia na haki za binadamu katika nchi yetu, ikiwemo kudai kuachiliwa bila masharti yooyote kwa Mwenyekiti Mbowe na wafungwa wengine wa kisiasa nchini.

Hotuba imetulia sana.

Karibu nyumbani makamanda.
 
Lissu awe makini sana, sidhan Kama nchi hii ni salama sana kwake!!

Amshukur Mungu kumpa uhai mpaka leo hi, ila asifanye haraka!!

2022-kazi iendelee
Unamaanisha asijaribu kuonja sumu kwa ulimi, yani asithubutu kumchallenge mwenyekiti ili yasije mkuta ya Chacha Wangwe, Zito, Mwigamba, Kubenea nk? Mbona yeye ashasema hatothubutu kugombea uenyekiti wa chama ili yasije mkuta yaliowakuta wenzake?
 
Back
Top Bottom