Serikali kuchukua hatua dhidi ya wahujumu BoT
*Balozi wa Ufini ashangaa kasi ya tuhuma za rushwa
*Ahoji: Mbona taasisi za kimataifa zinatoa ripoti nzuri?
Na Mwandishi Wetu
*Balozi wa Ufini ashangaa kasi ya tuhuma za rushwa
*Ahoji: Mbona taasisi za kimataifa zinatoa ripoti nzuri?
Na Mwandishi Wetu
Source: MajiraWAZIRI Mkuu, Bw. Edward Lowassa amesema Serikali ndiyo iliyoitisha uchunguzi wa hesabu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na itachukua hatua kuhusu tuhuma za rushwa endapo ripoti ya wakaguzi wa kimataifa, waliopewa kazi ya kuikagua benki hiyo itathibitisha hivyo.
Alikuwa akizungumza na Balozi mpya wa Ufini nchini, Bw. Juhan Toivonen, aliyekwenda kumtembelea ofisini kwake mtaa wa Magogoni Dar es Salaam jana.
Bw. Lowassa alisema ni vema mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania wakajua ukweli, kwamba Serikali imeamua kwa dhati kupambana na rushwa na kwamba ndiyo iliyoitisha uchunguzi wa BoT.
"Ripoti ya ukaguzi ikikamilika, Serikali itachukua hatua zinazostahili, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Nne imedhamiria kweli kupambana na rushwa kwenye ngazi zote," alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Nne, kamwe haifanani na Serikali inayoendekeza rushwa kama zinavyoonesha taarifa zinazochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini hivi sasa.
"Kama ingekuwa ni Serikali inayoendekeza rushwa, basi ni dhahiri ingeshindwa kukusanya kodi ingeshindwa kupeleka mabilioni ya fedha za maendeleo kwa wananchi vijijini, kama ilivyofanya katika bajeti ya mwaka huu," alimwambia Balozi huyo.
Serikali ya Awamu ya Nne sasa inakusanya wastani wa sh. bilioni 250 kwa mwezi ikilinganishwa na sh. bilioni 25 za mwaka 1995/96. Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali pia ilipeleka sh. bilioni 286 kwa halmashauri za wilaya kwa ajili ya kugharimia shughuli za maendeleo.
Bajeti ya mwaka huu ambayo ni kubwa kifedha kuliko yoyote iliyowahi kupitishwa katika historia ya nchi hii, vilevile imetenga maeneo ya kipaumbele na kuyapa fedha za kutosha.
Elimu imetengewa sh. trilioni moja; Miundombinu (Barabara) sh. bilioni 777, Afya sh. bilioni 589.9; Kilimo sh. bilioni 379 na Maji, sh. bilioni 309.
Naye Balozi alisema anashangazwa na kasi ya taarifa za tuhuma za rushwa katika vyombo vya habari nchini, wakati ukweli ni kwamba taasisi za kimataifa za uchunguzi wa rushwa zinatoa ripoti nzuri kwa Tanzania.
Shirika la Kimataifa la Kupambana na Rushwa (Transparency International) katika ripoti yake ya hivi karibuni, lilieleza kuwa Tanzania inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki kwa mapambano dhidi ya rushwa. Tanzania ilikuwa nchi ya 14 katika Afrika wakati Uganda ni ya 22 na Kenya ikiwa ya 42.
Balozi Toivonen alisema nchi yake inakamilisha taratibu za kuipa Tanzania msaada wa dola milioni 36 za Marekani (kiasi cha sh. bilioni 45) katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Waziri Mkuu pia alionana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Dk. Kandeh Yumkella na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa, Balozi Keitaro Sato, ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Japani nchini.