Serikali itazame upya mfumo wake wa utumishi wa umma | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali itazame upya mfumo wake wa utumishi wa umma

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Nov 23, 2011.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Nov 23, 2011
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Maoni ya katuni


  Serikali ilipata kuanzisha mpango wa kurekebisha mfumo wa malipo kwa watumishi wake na mojawapo ya taratibu zilizoanza kutumika ni ule wa kila posho iliyokuwa ikilipwa kukatwa kodi.
  Kwa wale wanaokumbuka miaka ya mwanzoni ya tisini, mashirika ya umma, makampuni binafsi na hata serikali yenyewe, kulikuwa na utaratibu wa watu kulipana mshahara kidogo ambao ulikuwa unakatwa kodi ya mapato (PAYE) na makato ya akiba ya uzeeni, lakini posho zilikuwa hazikatwi kodi.

  Serikali ya awamu ya tatu, iligundua kwamba yenyewe ilikuwa inashiriki kukwepa kodi, kwa hiyo maamuzi mazito yalifikiwa, kwamba mbali ya posho ya nyumba, malipo mengine yote yanayolipwa kwa mafanyakazi ni lazima yakatwe kodi. Hatua zilichukuliwa na serikali ikawa inakusanya mapato mengi zaidi.


  Hatua hizi zilikuwa ni sehemu ya urekebishaji wa mfumo wa utumishi serikalini, ambao kwa kawaida huathiri pia yanayotokea katika sekta binafsi.


  Katika programu ya kuboresha utumishi wa sekta ya umma kuna eneo ambalo lilikuwa lifanyiwe kazi sawa sawa ili kubainisha kwa mfano malipo halisi ya watumishi wa umma ni kiasi gani, nani analipwa nini na kwa nini. Kwa bahati mbaya pamoja na juhudi zote zilizofanywa na serikali katika kuifanyia marekebisho sekta ya utumishi wa umma, hadi leo suala la malipo kwa watumishi wa umma limebakia kuwa eneo lililojaa giza nene.


  Kimsingi serikali inafahamu kuwa ujira inaoutoa kwa watumishi wake kuanzia wa ngazi ya chini kabisa hadi wale wa juu, haufanani na maisha wanayoishi; serikali pia inajua pamoja na mshahara kijungu jiko wa watumishi wake, hakuna anayewaza kuacha kazi kwa sababu ya mshahara mdogo; kwa nini hali hii? Ni kwa sababu watumishi wa umma hawaishi kwa mshahara!


  Jumamosi iliyopita Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Katibu Mkuu wa Nishati na Madini kuchangisha fedha taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kufanikisha kupitishwa kwa bajeti, iliwasilisha taarifa yake ya uchunguzi bungeni, na mambo mengi ya aibu, ukosefu wa uaminifu na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali yalidhihirika.


  Yote yalifanyika kuhalalisha uchotaji wa fedha za umma. Ni taarifa yenye kuamsha mchanganyo wa mawazo na hisia, hasira na huzuni, kwamba watumishi wa umma waandamizi wa ngazi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu na hata Mdhibiti na Mkaguzi na Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wanaweza kujitumbukiza katika mambo ya kufedhehesha kwa kiwango cha kutisha.


  Ukiitafakari ripoti hiyo unapata majibu ya haraka kwa nini nchi hii inahangaika sana kupiga hatua za maendeleo ya kweli kwa watu wake; maji shida, umeme hivyo hivyo, shule ziko hoi, barabara kujengwa ni kwa mbinde huduma za afya ndiyo usiseme; kwamba fedha za kutosha kufanya kazi hizo hazipo kwa sababu baadhi ya watumishi na viongozi waandamizi serikalini wameamua kujinufaisha na kodi za wananchi. Hawajali na hawana uchungu asilimia!


  Tunajua watumishi hawa wanasaka fedha kwa kuwa ujira wao kisheria hauwawezeshi kuishi hata wiki moja tu achilia mbali mwezi, kutokana na ujira kijungujiko, wameishia kuanzisha miradi ndani ya ofisi zao kama huu wa kuchangisha fedha za kupitisha bejeti! Mlolongo wa madudu haya unaelezwa umetapakaa serikalini kote. Kila wizara ina njia na mbinu zake za kuwawezesha watumishi wake; posho ya

  vikao, mikutano, safari na kila aina ya njia ya kuwezeshana kupata malipo nje ya ujira wa kijungu jiko.

  Kwa hali ilivyo, serikali inapoteza mabilioni ya fedha mwaka baada ya mwaka ambayo yanalipwa kwa mtindo huo huo wa aliyofanya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini; serikali inalijua hili, lakini inalea maradhi haya na ndiyo maana hatuwezi kujikwamua hapa tulipo kama taifa.

  Ni katika kutafakari hali hii tunashindwa kujua nini hasa kinaikwamisha serikali kufanya marekebisho ya utumishi wa umma, ili iwe wazi nani analipwa nini na kwa nini; tunataka marekebisho ya kweli yafanywe ili watumishi wa umma walipwe ujira unaolingana na gharama

  halisi za maisha. Suala la kusema kuwa fedha hazipo halina nguvu yoyote kwa kuwa hizi zinazolipwa kila mwezi kwa njia ya uficho zingetosheleza, ambacho hakifanyiki ni uwazi wa malipo haya, basi.

  Tunafikiri wakati sasa umefika kwa serikali kufanya mambo yake kwenye mwanga, ili kujenga uwajibikaji, vinginevyo itaendekea kulea uporaji na kuvuna aibu kama hii iliyopatikana juzi bungeni.

  CHANZO: NIPASHE


   
Loading...