Serikali inapoficha habari ijue inajikomoa yenyewe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali inapoficha habari ijue inajikomoa yenyewe

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by kilimasera, May 11, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  May 11, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  ALIPOKUWA akifungua Semina Elekezi kwa viongozi na watendaji wakuu wa serikali yake mjini Dodoma juzi, Rais Jakaya Kikwete alizungumzia jambo ambalo limekuwa likiikwaza serikali hiyo kwa muda mrefu na kuutaja urasimu mkubwa katika kutoa habari za serikali kuwa ndio hasa jambo linalosababisha wananchi kuendelea kuamini zaidi habari zinazotolewa na vyama vya upinzani. Kwa tafsiri yoyote ile, alichotaka kuwaambia viongozi na watendaji hao ni kwamba mchawi wa serikali yake ni viongozi na watendaji wa serikali hiyo.

  Rais alisema bila kutafuna maneno kuwa, urasimu huo unafanywa na viongozi wanaopenda kukumbatia kila jambo badala ya kuwatumia watendaji wenye taaluma, na kuongeza kuwa vitendo hivyo vinaigharimu serikali yake na kwamba iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa, wananchi wataendelea kuamini habari zinazotolewa na upande wa pili.

  Aliwaambia wajumbe wa semina hiyo, wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao kuwa, anashangaa kuona serikali yake inashindwa kuzungumzia mafanikio yake yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kusema kuwa kuna udhaifu wa kujipanga miongoni mwa wasemaji, jambo alilosema linachelewesha kutolewa kwa taarifa ama kukanusha habari ambazo zimekuwa zikitolewa na upinzani.

  Tunaungana na Rais Kikwete kusema kuwa mafanikio ya serikali hayawezi kutangazwa na mtu yeyote isipokuwa serikali yenyewe na kwamba, viongozi na watendaji wa serikali yake wameonyesha udhaifu mkubwa kwa kukaa kimya na kuuacha upande wa upinzani ukitangaza habari na sera zake na kuzifanya ajenda kuu katika vyombo vya habari.

  Tunamshukuru Rais kwa kuwa na ujasiri wa kusema ukweli alipokanusha uongo na dhana iliyojengeka miongoni mwa viongozi na watendaji wa serikali yake kuwa, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika habari za upinzani na kuacha habari nzuri za serikali. Tunapata faraja pale Rais anapokiri kuwa uwoga na urasimu miongoni mwa wasemaji wa serikali ndilo hasa tatizo na kwamba hiyo inatokana na upande wa serikali kutojua kuwa vyombo vya habari vinatafuta habari na kama serikali haitoi habari, lazima vyombo hivyo viandike habari zitakazotolewa na upande wa pili.

  Na hivi ndivyo ilivyokuwa. Kwamba vyombo vya habari – hasa vya binafsi – vinafuatilia habari za serikali mchana kutwa lakini vinanyimwa habari hizo kwa visingizio dhaifu ni sababu za kutosha kwa vyombo hivyo kukosa ari na msukumo wa kuandika habari za serikali. Tulitegemea kuwa kuajiriwa kwa wasemaji wa serikali katika kila wizara kungeboresha mfumo na kasi ya upatikanaji wa habari za serikali, hasa zile zinazotangaza mafanikio ya programu na sera zake.

  Kama alivyosema Rais, vyombo vya habari havina ubaya wala kinyongo na serikali mbali na kukwazwa na watendaji wake. Sio siri kwamba hata vyombo vya serikali vilivyopo kwa ajili ya kushughulikia masuala ya habari, ikiwamo Maelezo, vimekaa mbali na vimekuwa vikivinyanyapaa vyombo vya habari, hasa vya binafsi.

  Tunakubaliana na Rais Kikwete kwamba hali hiyo lazima ibadilike sasa kwa kuwapa wasemaji wa wizara zote uwezo na nyenzo za kuwawezesha kuisemea serikali. Lazima wasemaji hao kweli wawe wasemaji walio na weredi, sio wabeba mikoba ya watendaji wa serikali. Kama alivyosema Rais, wasemaji hao lazima wahusishwe katika vikao katika ngazi zote za serikali ili waweze kuisemea kwa kujiamini. Pia lazima vyombo vya habari vya serikali vibadilike na vitangaze sera na mafanikio ya serikali badala ya kujikita katika propaganda za chama tawala, kwani hiyo ni kazi ya vyombo vya habari vya chama hicho.

  Tunapendekeza kwamba Maelezo ifumuliwe ili isukwe upya, kwa maana ya kuwa kitovu cha upatikanaji wa habari na picha zinazotoa taswira ya mafanikio ya programu na kazi za serikali. Sisi tunampongeza Rais kwa kuweka rekodi ya kazi ya vyombo vya habari vizuri na kwa kutambua kuwa serikali inapoficha habari inajikomoa yenyewe.
   
Loading...