Serikali inachangia wanafunzi kutojua kusoma na kuhesabu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali inachangia wanafunzi kutojua kusoma na kuhesabu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ujengelele, Sep 28, 2010.

 1. U

  Ujengelele JF-Expert Member

  #1
  Sep 28, 2010
  Joined: Jan 14, 2008
  Messages: 1,256
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Na Fredy Azzah
  WIKI iliyopita,Tanzania ilipewa tuzo ya kimataifa, kwa kutekeleza vizuri malengo ya elimu ambayo ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya (MDGs), yanayotakiwa kukamilika mwaka 2015.Tuzo hiyo ilipokewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye sherehe ya tuzo ya utekelezaji wa malengo ya milenia 2010, iliyofanyika nchini Marekani.

  Akipokea tuzo hiyo, Pinda alisema imeipa moyo Tanzania iongeze bidii ili ifanikiwe katika malengo yote ya milenia ifikapo mwaka 2015.

  kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari kuhusu tuzo hiyo, Tanzania imefanya vizuri katika lengo la elimu kwa kuhakikisha watoto wote wanaandikishwa shuleni na kufikia asilimia 95 mpaka sasa.

  Hata hivyo, wakati serikali ikiwa imefanikiwa katika kuandikisha wanafunzi wengi katika shule za msingi, utafiti uliofanywa na asasi ya kiraia iitwayo Twaweza, umeonyesha kuwepo kwa kasoro kubwa katika mchakato wa ujifunzaji kwa wanafunzi wengi wa elimu ya msingi..

  Utafiti huo uliopewa jina la 'Are Our Children Learning', ulibainisha zaidi kwamba, si tu wahitimu wengi hawawezi kufikiri, kujitegemea, kujiamini, kuchambua mambo, kuuliza na kuwa wadadisi, lakini pia baadhi yao wanapigwa chenga na stadi za msingi za kusoma na kuhesabu.

  Ripoti ya matokeo ya utafiti huo iliyosomwa kwa wanahabari inaonyesha kuwa nusu ya wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi hawawezi kusoma lugha ya Kiingereza.

  Si Kiingereza tu, ripoti hiyo iliyoshirikisha wanafunzi zaidi ya 40,000 katika wilaya 38 nchi nzima inabainisha kuwa wanafunzi wengi wanakosa stadi za msingi za kusoma katika lugha ya Kiswahili ambayo kwa wengi ni lugha maarufu wanayoitumia kila siku.

  Matokeo haya yanatupa picha halisi kuwa licha ya nchi kufanikiwa katika uandikishaji mkubwa wa wanafunzi shuleni, bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango vinavyokubalika katika dunia ya sasa.
  Hakutakuwa na maana kujisifu kwa takwimu za wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza, huku tukijua kabisa hakuna wanachokipata shuleni.

  Mzazi yeyote anapompeleka mwanaye shule, anataraji kuwa atapata elimu iliyo bora kwa ajili ya ustawi binafsi na maendeleo ya taifa.

  Kinyume na matarajio hayo, wanafunzi hawa ambao serikali inaringia takwimu za wingi wao, ndiyo hao hao wanaomaliza miaka saba darasani wakitoka kapa kichwani.

  Serikali lazima itambue kuwa, matokeo ya kuwajaza wanafunzi shuleni bila ya kujiandaa kuwasaidia kitaaluma ni jambo la hatari kwa mustakbali wa nchi hii iliyo bado change kimaendeleo. Ni vigumu kuendelea kwa kuwa na taifa la watu ambao hata stadi za msingi za katika maisha kama kusoma na kuhesabu zinawapiga chenga.

  Bila shaka utafiti huu uliwashirikisha watoto wanaosoma katika shule za serikali ambazo nyingi hupokea watoto maskini. Hawa ndiyo watakaoendelea kuburuzwa na wenzao wanaosoma katika shule za wazazi wenye uwezo.

  Kwa mtazamo wangu zipo sababu kadhaa zinazochangia hali hii katika shule za serikali ikiwemo uhaba wa walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Na pale penye walimu kuna tatizo la walimu kutokuwa mahiri katika masomo wanayofundisha.

  Lakini kubwa zaidi ni kuendelea kukumbatia mfumo mbovu wa elimu ambao nao kwa kiwango kikubwa umeathiriwa na maamuzi ya kisiasa yasiyo na tija katika elimu. Sote tunajua namna wanasiasa walivyoharibu mfumo wa elimu kwa kupiga marufuku mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili.

  Mtihani wa darasa la nne, ulikuwa kigezo kizuri cha kupima uelewa wa mtoto kama kweli ameelewa ipasavyo yale aliyofundishwa kuanzia darasa la kwanza hadi la tatu ikiwa ni pamoja na stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

  Lakini ili iweze kupata takwimu za juu kwa lengo la kuwafurahisha wale wanaotufadhili, serikali ikaamua kuruhusu hata wale wanafunzi wanaoshindwa katika mitihani ili wajaze tu idadi ya wanafunzi wanaomaliza shule.

  Mtihani wa darasa la nne ungekuwa chujio muhimu la kubaini wanafunzi wenye uwezo na wasio na uwezo kitaaluma. Tusingekuwa na taarifa ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kama mtihani huu ungekuwepo.

  Hali hii inajitokeza pia upande wa sekondari.Tumepiga marufuku mtihani wa kidato cha pili kwa lengo lile lile la kuongeza idadi ya takwimu za wanaomaliza elimu ya sekondari. Kwa wanaofuatilia matokeo ya mitihani ya taifa wanakumbuka matokeo mabaya ya wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2009.

  Kwa nini wanafunzi waliopata daraja sifuri walikuwa wengi? Jibu ni rahisi, wengi ni wale waliokuwa hawajitumi shuleni kwa kuwa waliamini hakuna mtihani wa kuwapima hadi wanafika kidato cha nne.

  Sitetei utaratibu wa kuwachuja wanafunzi kama inavyofanyika katika baadhi ya shule binafsi ambazo hatimaye hufanya vizuri katika mitihani ya mwisho, ninachokisema kufuta mitihani ya darasa na nne na kidato cha pili kumewapa mwanya wanafunzi kuzembea zaidi kimasomo wakiamini hakuna wa kuwazuia kumaliza shule.

  Siasa imeharibu elimu na nina kila sababu ya kuwalaumu wanasiasa wanaoendesha serikali yetu kwa sasa. Serikali ilaumiwe kwa haya yanayojiri sasa shuleni.
  O754224336
   
 2. JOYCE PAUL

  JOYCE PAUL JF-Expert Member

  #2
  Sep 28, 2010
  Joined: Jan 8, 2010
  Messages: 1,007
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 135
  Kidumu chama cha mapinduzi na serikali yake iliyofanya kazi nzuri ya kutimiza maazimio ya mdgs.
   
Loading...