Serikali Ina Wachumi wa Vyeti, Imekosa Wachumi Halisia?

Msambichaka Mkinga

JF-Expert Member
Oct 22, 2015
1,649
2,911
Katika ujenzi wa uchumi, ili uweze kufanikiwa na kusonga mbele kwa haraka ni lazima uzitambue:

Sekta wezeshi
Sekta muhimu
Sekta kipaumbele

Ukikosa uelewa huo, unaweza ukawa unapanga mipango yako, ukiamini umepanga ili kusonga mbele kumbe umepanga ili kurudi nyuma, kubakia mahali ulipo, au kwenda mbele kwa mwendo wa kinyonga.

Mawasiliano ni sekta wezeshi, ni sekta inayosaidia kukua na kufanikiwa kwa sekta nyingine, yaani sekta za uchumi na sekta za huduma. Mipango ya ovyo na ugumu kwenye sekta ya mawasiliano inaenda kuathiri sekta nyingine. Sekta wezeshi inatakiwa iwe na gharama nafuu kuliko zote ili watu waitumie vizuri katika kukuza sekta za uchumi kama vile viwanda, kilimo, madini, uvuvi, n.k.

Pamoja na sekta ya mawasiliano, kuna sekta ya nishati. Zote hizi ni sekta wezeshi. Hizi sekta ukizijazia kodi za ovyo ovyo, unadumaza sekta nyingine pia.

Sheria zetu za kodi ni mbaya sana, tumekosa watu wabunifu, tumekosa watengenezaji wazuri wa sera rafiki katika kukuza uwekezaji kiasi kwamba vyanzo vyetu vya kodi ni vichache sana. Matokeo yake, watunga sera, fikra zao zimebakia kwenye kuongeza kodi kwenye vyanzo vile vile.

Adui mkubwa wa uwekezaji ni kodi. Hakuna nchi maskini iliyowahi kuendelea kwa kasi kwa kuongeza uwingi na ukubwa wa kodi. Bali mataifa mengi yaliyokuwa maskini, yaliweza kuendelea kwa kasi sana kwa kupunguza sana ukubwa na uwingi wa kodi. Dubai (UAE), maendeleo yake makubwa yalipatikana ndani ya miaka 15 tu. Sisi zaidi ya miaka 60 ya uhuru, tunaendelea kuimba wimbo wa eti Taifa letu changa!!

Leo hii kwenye huduma nyingi kumekuwa na kodi mrundikano. Mfanyakazi anayelipwa mshahara wake kupitia benki, kabla ya pesa kupelekwa bank, anakatwa PAYEE, akitaka kutoa pesa kupitia ATM, anakatwa kodi. Anaenda kuweka pesa ile ile kwenye simu ili amtumie mama yake kijijini, wakati wa kutuma, anakatwa kodi, mama yake akitaka kuichukua ile pesa kwa wakala, anakatwa kodi, anatoa ile pesa, anaenda kununua kitenge, anakatwa kodi. Pesa ile ile inakatwa kodi hata mara 10. Huu ni wizi. Ni Serikali inamwibia mwananchi wake.

Kati ya bajeti mbaya, mojawapo ni hii ya mwaka huu, maana imejaza kodi kwenye sekta wezeshi. Na kwa bahati mbaya, kwa bunge hili ambalo, mara nyingi wanaishia kusema NDIYOOO kwa kila kinacholetwa na Serikali, sidhani kama kutakuwa na matokeo tofauti na kile kilichopelekwa bungeni na Waziri Mwigulu.

Tanzania tuna safari ndefu. Na kwa fikra hizi za kuangalia zaidi kupandisha na kuongeza kodi kwenye vyanzo vile vile badala ya kuwa na msukumo mkubwa wa kuongeza uwekezaji ili tuwe na vyanzo vingi vya kodi, tutaendelea kuwa watazamaji wa maendeleo ya Dunia.

Kwenye nchi ambazo Bunge ni imara, mategemeo ya wananchi, kunapokuwa na kodi hizi za kuwaumiza wananchi na kuumiza maendeleo ya ichumo wa Taifa, tegemeo mojawapo kubwa huwa ni Bunge, lakini hapa kwetu, Bunge letu ndiyo hili tulilo nalo! Sijui tutaegemea wapi.
 
Back
Top Bottom