Serikali ina upande wake kwenye maendeleo. Je, wewe mtanzania unajua tabia zako zinarudisha nyuma juhudi za maendeleo?

buffalo44

JF-Expert Member
May 8, 2016
3,139
6,283
Kama huwezi kusoma Makala hii soma hitimisho basi.

UTANGULIZI.
Ni masikitiko makubwa kuona watanzania huku mitandaoni wakishangilia Umoja wa ulaya(EU) na Marekani kuingilia mambo ya Nchi huru ya Tanzania.
Japo ni kweli kuna mambo baadhi ambayo serikali inafanya yasiyo ya kuridhisha lakini kufikia hatua kuwaunga mkono wazungu ambao historia inawaeleza kuwa ni watu wasio na urafiki wa kweli na waafrika hasa kisiasa ni jambo la kushangaza.

Tangu lini EU na USA walisaidia kutoa serikali ya ulimwengu wa tatu madarakani na nchi ikapiga hatua?, kama ipo nitafurahi kusahihishwa. Mambo ya ndani ya nchi ni ya muhimu na akiliye na haki nayo ni Serikali ya nchi peke yake. Kuingilia mambo yake ni kutoheshimu mipaka na haki ya kujitawala.

Historia inajirudia. Libya walishangilia Ghaddafi kutolewa madarakani ila sasa matokeo yapi wanapata?, Iraq ilifurahia uvamizi wa George H.W Bush. Ila sasa nchi ikoje?
Venezuela tunayo mataifa makubwa yaliingilia ila nchi iko wapi?. Pote hakuna maendeleo chanya.

Tuachane na siasa tuongelee maendeleo kwa ujumla kwa mtu mweusi. Ni vyema kwanza tufahamu kuwa maendeleo hayaji kiujumla bali yanaanza na mtu mmoja mmoja kisha wengine kuja kuyarekebisha kidogo ili Yazidi kuwa na matokeo makubwa na yanayoendana na wakati. Maendeleo huanza na mtu mmoja mmoja.

Hata hivyo kuna upande wa serikali pia unaochukua nafasi kubwa katika hatua zote za maendeleo. Lengo la Makala hii sio kuitetea serikali wala kuwapiga dongo USA na EU bali lengo lake ni kujadili kuhusu watanzania wanaoshangilia kuingilia kwa EU na USA ili nchi ipige hatua. Nataka kujadili kwanza matatizo yao makubwa kwenye mchango wa maendeleo wanayolilia na kuomba EU na USA kuingilia ili wapate.


WATANZANIA NA MAENDELEO.
Maendeleo hayaji kimiujiza yanaletwa kwa mapambano. Watanzania wanapambana, Ndio? Wanataka maendeleo, Ndio. Maendeleo gani, jibu langu nionalo ni moja tu, Wanataka maendeleo ya kuongezeka kwa pesa mfukoni, wachache wanataka mabadiliko kwenye mifumo muhimu itakayotumiwa na vizazi vijavyo.

Kabla ya kuilaumu serikali kwa kufanya maisha magumu mtaani tungependa kujua mchango wa mwananchi mmoja mmoja kwenye maendeleo katika ngazi zote ili kupata haki ya kuilaumu Serikali.

Tuangalie unafiki wa watanzania unaotokana na tabia kwenye matatizo ya nchi hii.

1; Ukosefu wa pesa mtaani.
Ni jambo la kushangaza kuona watu wakiikomalia serikali kuwa imeshidwa kuingiza pesa mtaani. Pesa zipo ila pesa zinazolalamikiwa ni zile zinazotapanywa kwenye kila kitu na kurahisisha mambo. Niseme tu serikali nayo ina sababu yake na raia pia wanasababu zao kwenye suala zima la kupotea pesa na kuwa chache.
Waafrika kiujumla tunafahamika vizuri kwenye matumizi ya pesa kuanzia serikali hadi wananchi.
Wengi hawana nidhamu ya pesa zikiwa mkononi. Hakuna kutunza akiba kwa ajili ya kujihami mbeleni hali ikiwa mbaya kama sasa.
Kingine watanzania tuna tabia ya kulazimisha kuishi maisha ya dunia ya kwanza huku sisi bado hatuna vyanzo vya kueleweka vya pesa. Hela ikipatikana ikiwa milioni mawazo huwa gari au nyumba nzuri au kununua kitu chochote ili wajisifie uzungupori, matokeo yake mitaji ambayo ingefaa kwenye maendeleo ya kuzalisha pesa inaishia kwenye kujionyesha. Alafu baadae tunakuja kulaumu serikali hii ndio sababu bila kujiangalia kwanza.

Kwenye suala la michango kuna unafiki wa hali ya juu. Harusi michago inazidi milioni 5 hadi kufikia 50 na watu wanafurahi, harusi inakaa siku moja tu na million hizo zinatapanywa, je ni harusi ngapi zinafanyika kwa siku Tanzania nzima?. Na mtu akileta wazo la biashara kuchangiwa hata kutoa elfu 10 tu ni mbinde. Wajasiriamali wanalenga nini? Kutatua changamoto na kutengeneza faida na hakuna wa kumchangia. Unafiki huu, wajasiriamali wana mchango kufanya pesa iwe mtaani maana waweza kutoka nje ya nchi na kutengezafaida kwa kuingiza pesa za kigeni.

Tunawanyima mchango alafu tunachangia harusi kama mazuzu. Hivyo hivyo tunataka urahisi wa maisha. Haaaaaa!.Watu gani hawa wanapoteza hela wenyewe alafu wanalalamikia utawala?

2. Miundombinu mibovu.
Hosipital za kijijini ni mbovu serikali inafanya nini? Malalamiko kwenye miundombinu ni mengi, ila tuje upande wenu walalamikaji huwa mnapokeaje miundombinu? Kuna wengine wanaponda miundombinu inayojengwa sehemu moja kuwa itamsaidiaje bibi yake aliye kijijini? Kuna wengine wanatembea vifua mbele. Ila yote siko hapa kudhihaki mtu yoyote awe anayeogelea nyanyake wa kijijini au anayetembea kifua mbele kama amepigwa ngumi ya mgongoni. Nipo hapa kuogelea matunzo ya miundombinu inayojengwa na serikali au kwa msaada.

Nimeona na kusikia mara nyingi wananchi wakiharibu na kutoitunza vizuri hali inayofanya serikali ichukue tena hela ambazo zingeenda kumhudumia bibi yako wa kijijini au ambazo zingefanya mtembee vifua mbele Zaidi kama umeshindiliwa na mguu mgongoni na kuzipeleka kukarabati hiyo miundombinu msiyotunza na mnayoharibu.

Juzijuzi bodaboda waliporomosha mawe kwenye mwendokasi. Siku za nyuma kulikuwa na habari ya wizi wa nati daraja moja huko morogoro daraja jipya. Habari ya kuchafua majengo ya shule na ofsi si mpya. Wizi wa vyuma vya reli unaogeleka na shughuli ya kuburuza STL,STK, SU imezidi.

Kuhusu bombardier na Boeing Dreamliner kuna watu wanataka zipate michirizi wachonge kwenye vigroup uchwara vya WhatsApp na kushare mara millioni wakisindikiza na vijembe kwa serikali, ajabu hii.
Hayo yote yamegharimu serikali mabilioni ila wananchi hawajali. Tukija kwenye maji karaha tupu, kuna watu wanakata mabomba makusudi na wengine kuiba. Nina kijiji kimoja huko Mbeya kama mfano ambacho kiliharibu mabomba ya maji ya kijiji kingine hadi Mkuu wa Mkoa kuamuru kiswekwe ndani.
Inatisha, Watanzania elimu ndogo inahitajika hata kwa wasomi wenye madgree yao maana hata vyuo vya mzumbe na UDSM kuna majengo chakavu. Ni vyema kila mtu atambue kuwa miundombinu inapoharibika serikali inachukua fedha zilizopangiwa kazi nyingine kukarabati au kujenga upya hayo majengo, huku shughuli ambazo pesa hizo zilipangiwa zikidumaa. Hali inayopelekea maendeleo kuwa taratibu na ikumbukwe kuwa wawekezaji wanapenda kuwekeza eneo lenye miundombinu ya kurahisisha uwekezaji.

Miundombinu ikishajengwa na serikali ni jukumu lenu kuilinda na kuitunza maana nyie ndio watumiaji wakuu na ina manufaa kwenu, chuki dhidi ya mjenzi usizipe nafasi.

3; Haki za binadamu.
Hadi wazungu wameingiz. Wananchi wanashangilia na kuona serikali inavunja haki za binadamu, sikatai ni kweli, ila hii mada ni kuangalia upande wa wananchi. Serikali imekataa kusomesha wasichana wenye mimba na watu wanavimba mishipa, ndio wanatunisha vena cava, ateri, ventriko ya kulia na kushoto hadi unashangaa. Kwanza nani wasababishi wa hizo mimba, kuna bodaboda, vijana wenyeakili timamu, wahuni na wazee kabisa aka mafataki.

Mtandaoni wanajisifia kutembea na vitoto vya shule na Zaidi wanarubuni wanafunzi wakiwapa mimba wanahama kwenda mbali kisha mkono mrefu wa serikali unatua kwa wasichana, hakuna kusoma tena. Hao hao wasababishi wa mimba wanaizomea serikali na kushangilia EU, na USA kuingilia, inasikitisha.

Tuna mila ambazo ni ngumu na zinabinya haki nyingi za binadamu hasa za wanawake na watanzania wanaona poa na ni kawaida tu. Lakini serikali ikifanya maamuzi ambayo yanaonekana ni sahihi kwa sababu mimba hazilazimishwi bali wanakubaliana uchochoroni, hivyo maamuzi ya serikali ni sahihi kabisa kwa maoni yangu.

Ushoga umekuwa kelele kuna wasomi wetu wanasema ni haki yao. Duh! Na kuna watu wanashangilia na kuipinga serikali, japo ni kweli serikali ilichukua hatua mbovu kushughulikia, lakini mkumbuke kipimo mnachopimia ndicho mtakachopimiwa. Mnaiponda serikali alafu mitandaoni mnatoa matusi kwa mashoga na kuona hawakubaliki kuna tofauti gani kati yenu na serikali?
Hata Raisi ni binadamu hata yeye anahitaji haki zake ziheshimiwe unapomtukana na kumdhihaki unamkosea adabu na kushindwa kujua kuwa nae ni binadamu. Hili zinatieni wote.

4. Demokrasia na uhuru wa kuongea.
Hapa nikiri kuwa serikali yetu inafeli sana. Ila niseme kweli sioni kama demokrasia ni mfumo unaoifaa Afrika na Tanzania, sababu tulizoea mfumo wetu ule wa machifu na kutegemea maamuzi kufanywa na baraza la wazee (mfumo huu naamini ungetufaa sana kama ungeimarishwa vizuri) naamini kuwa demokrasia ina vitu bora pia ambavyo vingesimama upande wa madhaifu ya mfumo wa Afrika hivyo kutengeneza mfumo wenye nguvu. Ndio tunatambua serikali inashindwa kubeba demokrasia vizuri, ila tujiulize walioasisi demokrasia hiyo, wakoje na mfumo wao.
Tunajua kuwa malezi na utamaduni wa jamii unavutia tabia ya mtu, hata akiwa kiongozi. Tuangalie tamaduni zetu, nyingi hazina demokrasia. Mtoto kuhoji hoji vitu ni marufuku, wanawake hawana uhuru wa kufanya maamuzi, mila zingine zinangilia faragha za watu. Uhuru wa kuongea kwenye familia ni mdogo Afrika ukilinganisha na walioasisi demokrasia, ambao wana uhuru hadi mtoto anabishana na mzee na kuomba haki nyingi nyingine za ajabu.
Lengo la kuelezea hapa ni kuweka sawa kuwa kabla hatujaanza kulalamika kuhusu ukosefu wa demokrasia serikalini hebu tufikirie mazingira ya jamii yanayofanya mtu awe mgumu kusikiliza wadogo au waliochini yake. Kama mada yangu ilivyo ni kuhusu upande wa wananchi kwenye maendeleo yoyote yale.

Mkitaka demokrasia bora inayoheshimu misingi ya haki za binadamu anza na mila zinazotengeneza fikira isiyoheshimu waliochini yake kabla ya kulazimisha mzee aliyetengenezwa na mila na utamaduni wa Afrika kukubali ujana wako.


HITIMISHO.
Mada hii ni ndefu, haimaanishi nipo natetea serikali hapa. Nipo hapa kutoa yangu ya moyoni kwa jinsi ninavyoona unafiki uliopitiliza wa watanzania kuikomalia serikali kila tatizo. Kumbuka hamtaridhika na chochote serikali itakachofanya. Ila kabla ya yote ningependa kuwaweka sawa kuwa wananchi mna mchango mkubwa kwenye kuimarisha sera za serikali za maendeleo au kudunisha kwa tabia zenu. Watanzania kwa umoja chukua hatua kwanza kwa sababu zinazosababisha matatizo ambazo ziko miongoni mwenu kabla matatizo hayajawa makubwa kiasi cha serikali kuchukua jukumu au kiasi cha mfumo wa serikali kuathiriwa, kama vile kupambana kwa nguvu zote na wanaowarubuni wasichana wa shule na kuwapa mimba hadi serikali kuingilia kati, kupambana na mila zinazoweka fikira zisizo za kidemokrasia akilini mwa watu, kumbuka mbegu ya leo itazalisha mavuno ya kesho, kupambana na waharibifu wa miundombinu ili serikali ielekeze nguvu kwenye kuimarisha maisha ya wakazi wa hali ya chini. Zaidi ya yote sisi wenyewe kutumia pesa kulingana na uwezo wetu sio kutumia pesa kama tajiri wakati mfuko wako ni mdogo kama priton.

MAAENDELEO HAYALETWI NA SERIKALI BALI YANALETWA NA WANANCHI KWA KIASI KIKUBWA IKIWA WATATUNZA NA KUHESHIMU KILE SERIKALI INACHOWAPA PIA SERIKALI INA FANYA WANANCHI WACHANGIE MAENDELEO KWA KUWAPA MAZINGIRA SAFI.

Ahsante sana kwa kusoma nawashukuru sana, ukiwa na ushauri au maoni tafadhali weka hapa. Chuki hazikusaidii kutatua tatizo.
 
Kazi za serikali zinajulikana dunia nzima .kinachotakiwa kwa serikali hii ya awamu ya tano ni kutimiza wajibu wake ,vile vile kupanga vipaumbele kwa ufasaha kwa manufaa ya nchi siyo dili na teni pasenti kwenye ndege na standard gauge n.k.
 
Kazi za serikali zinajulikana dunia nzima .kinachotakiwa kwa serikali hii ya awamu ya tano ni kutimiza wajibu wake ,vile vile kupanga vipaumbele kwa ufasaha kwa manufaa ya nchi siyo dili na teni pasenti kwenye ndege na standard gauge n.k.

Vipi kuhusu wewe? Mchango wako ni upi?
 
Back
Top Bottom