Serikali ina matumizi gani na wanafunzi walionaliza kidato cha 4 kabla ya 2020?

Oct 5, 2015
87
400
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE) NA MKANGANYIKO WA UDAHILI WA WANAFUNZI WA MKUPUO WA MACHI, 2021. JE, WATENDAJI WAKE WANAPINGANA NA MAONO YA RAIS WA NCHI ?

Kwako Waziri Pro. Joyce Ndalichako!
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge, Sura Namba 129 ili kusimamia na kuratibu utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi katika Vyuo ambavyo si Vyuo Vikuu ama Vyuo Vikuu Vishiriki nchini. Jukumu mojawapo la Baraza ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa katika Vyuo vya Ufundi nchini yanakidhi vigezo na ubora unaohitajika katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Katika kutekeleza majukumu yake, mnamo tarehe 8/1/2021, Baraza kupitia kwa Katibu Mtendaji, lilitoa taarifa kwa umma kupitia tovuti yake ya (www . nacte. go . tz) juu ya kuanza kwa udahili wa Machi 2021 kwa waombaji wa astashahada na stashahada na kwamba udahili utaanza tarehe 15 Januari, 2021 hadi tarehe 20 Februari, 2021 kwa Vyuo vyote vinavyotoa mafunzo katika ngazi hizo na kuelekeza kuwa maombi ya udahili yatumwe moja kwa moja kwenye Vyuo husika.
Taarifa husika ilisisitiza kuwa , Vyuo vitapokea maombi na kufanya chaguzi kwa wanafunzi wenye sifa na kuwasilisha NACTE majina yao kuanzia tarehe 21 mpaka 26 Februari, 2021 kwa ajili ya uhakiki.

Waombaji watakaochaguliwa na kuhakikiwa na Baraza watatangazwa na Vyuo husika kuanzia tarehe 5 Machi, 2021. Muhula wa masomo utaanza tarehe 1 Aprili, 2021. Aidha, Baraza lilawashauri waombaji na wazazi kuhakikisha kuwa wanaomba kwenye Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali ambavyo vimeorodheshwa kwenye Kitabu cha Mwongozo wa Udahili kwa mwaka wa Masomo 2020/2021 (Admission Guidebook for 2020/2021 Academic Year) ambao unapatikana katika tovuti ya NACTE.

Wakati muda wa kufanya uhakiki wa wanafunzi wenye sifa , zoezi ambalo linafanywa kwa kutumia taratibu za ndani ya Chuo na kupitia mfumo wa udahili wa NACTE, Mfumo ulizuiwa (restricted) kuhakiki baadhi ya wanafunzi wenye sifa ambao wamehitimu kidato cha Nne kwa mwaka 2020. Aidha zuio hili liliwaathiri wanafunzi ambao walimaliza kidato cha nne miaka ya nyuma na kufanikiwa kupata credit zao kwa mwaka 2020.

Kutokana na changamoto hii baadhi ya vyuo vilitoa taarifa kwa mamlaka na kwa bahati mbaya hakukuwa na majibu yanayotoa suluhu ya tatizo husika, hivyo kupelekea wanafunzi hao wenye sifa kuendelea na masomo katika vyuo vyao huku suala lao la kuingizwa katika mfumo wa udahili wa NACTE likiendelea kufuatiliwa, ikizingatia kwamba wanafunzi hao walikidhi vigezo vyote vya udahili katika kozi husika. (Isipokuwa walihitimu kidato cha nne miaka ya nyuma lakini walikosa credit, wakazitafuta na kuzipata 2020).

Mnamo tarehe 25 na 26 Januari 2021 Baraza liliitisha kikao cha Wakuu wa vyuo na maofisa udahili , kikao kilichofanyika jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine lilitoa maelezo kuwa Serikali imezuia kudahili wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2020 kwa kuwa ina matumizi nao, kauli ambayo inakiuka Mwongozo/Kanuni za udahili.
Maelekezo hayo yasio rasmi ( kwa njia ya mdomo) yaliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha Udahili Bw. Twaha. A. Twaha yalipelekea baadhi ya wanafunzi na wazazi kuwa katika hali ya sintofahamu kwa kusababisha baadhi ya wanafunzi kupoteza haki yao ya kujiendeleza kielimu katika fani walizochagua licha ya kwamba wanafunzi husika walifanya maombi katika vyuo hivyo kwa kufuata muongozo wa udahili wa NACTE.
Kutokana na kadhia hii, Vyuo kupitia wawakilishi wao waliendelea kufuatilia katika mamlaka mbalimbali ilkiwemo baraza , ambapo ilipelekea Baraza kupitia kwa Katibu Mtendaji Bw. Adolf B. Rutayuga kuviandikia Vyuo barua za kutakiwa kujieleza sababu ya kudahili wanafunzi bila kufuata Mwongozo wa Baraza.

Baada ya ufuatiliaji na uchambuzi wa muda mrefu, Vyuo wamejiridhisha kuwa maelekezo ya kuzuia udahili wa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne, 2020 yana dosari kadhaa;

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, TAMISEMI na Wizara ya Afya zimekana kutoa maelekezo kwa Baraza kuzuia udahili wa wanafunzi hao.
Hakuna uthibitisho wa nyaraka kutoka katika mamlaka yeyote ya Serikali kwenda katika Vyuo kueleza maamuzi ya kusitisha udahili wa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne, 2020, na hata NACTE wameshindwa kuthibitisha mbele ya vyuo juu ya msingi wa maamuzi hayo.

(Kwanini walidhibiti mfumo wa udahili kwa wanafunzi hawa?)

Hata kama maelekezo husika yangekuwa na uthibitisho wa nyaraka, bado yanakwenda kinyume na taratibu za udahili za Baraza ambazo zimekuwa zikitumika miaka yote, na wanafunzi husika wamekuwa wakidahiliwa bila tatizo lolote.
Dirisha la udahili lilifunguliwa mnamo tarehe 15/01/2021, na kauli ya mdomo ya zuio la udahili wa wanafunzi hao ilikuja baadae, tarehe 25-26 Januari 2021, kitendo ambacho kinakinzana na namna bora ya utekelezaji wa sheria (retrospective approach).

Aidha , Kitabu cha Mwongozo wa udahili (Admission guide book) kimetaja sifa/vigezo mahsusi vya kujiunga na fani husika ambapo mwaka wa kumaliza kidato cha nne 2020 haiwezi / haikuwahi kuwa sehemu ya kigezo/sifa ya udahili kwa wanafunzi.
Baraza kupitia Mkuu wa Idara ya Udahili kuzuia uhakiki na udahili wa wanafunzi kupitia mfumo wake bila kujulisha Wateja, kitendo ambacho ni kinyume na Mkataba wa Huduma kwa Wateja, toleo la Februari 2018 kipengele cha 5.17 cha Mawasiliano kwa Wateja, ambapo pamoja na mambo mengine inasisitiza NACTE kuwasiliana na Wateja wao ( Vyuo, n.k) kwa njia ya barua ngumu, barua pepe na simu.

Kutokana na dosara hizi, napendekeza Mhe. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kuhakikisha anafanya yafuatayo;
Kufanya mabadiliko ya kiuongozi katika Baraza hili ili kuchochea uwazi, uwajibikaji na maamuzi shirikishi miongoni mwa wadau.

Kuhakikisha wanafunzi husika wanapewa fursa ya kudahiliwa kwenye mfumo huo mara moja.

Kuanzisha uchunguzi huru kwa watendaji wa Baraza kwa kuanzia na Katibu Mtendaji Bw. Adolp Rutayuga na Mkuu wa kitengo cha Udahili Bw. Twaha A. Twaha kuhusu ushiriki wao katika kadhia hii na pengine kujiridhisha endapo hakuna viashiria vya mgongano wa kimaslai katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kutoa fursa ya majadiliano kati ya wadau wa vyuo ili kuboresha mfumo wa udahili wa wanafunzi katika vyuo vilivyo chini ya NACTE.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom