Serikali imesema maji yanayotoka katika Mto Ruvu Juu yanayodaiwa kuwa na sumu bado ni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali imesema maji yanayotoka katika Mto Ruvu Juu yanayodaiwa kuwa na sumu bado ni

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mbonea, Oct 8, 2009.

 1. Mbonea

  Mbonea JF-Expert Member

  #1
  Oct 8, 2009
  Joined: Jul 14, 2009
  Messages: 640
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  HABARI MUSIBA BLOG
  Serikali imesema maji yanayotoka katika Mto Ruvu Juu yanayodaiwa kuwa na sumu bado ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
  Wakati serikali ikiwataka wananchi kuondoa hofu na kuendelea kuyatumia maji hayo, sampuli za maji pamoja na samaki mmoja aliyekufa, zimepelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali kuchunguzwa ili kubaini sababu ya kifo chake.
  Waziri wa maji na umwagiliaji profesa mark mwandosya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam amesema uchunguzi wa awali wa sampuli za maji hayo umeonyesha kutokuwepo kwa dalili yoyote ya sumu na kwamba wameamua kulipelekea suala hilo kwa mkemia mkuu ili kujiridhisha zaidi na kwamba matokeo ya sampuli hiyo yanatarajiwa kutolewa kesho.
  Ameongeza kuwa dawa zote za kutibia maji na hasa chlorine ziliendelea kufanya kazi kama kawaida na viumbe wote hai hawakupata madhara yoyote na kuongeza kuwa sampuni za maji zinaendelea kuchukuliwa na kupimwa kila baada ya dakika 15 kabla ya kuyasafisha ili kuchunguza tofauti isiyokuwa ya kawaida katika tabia ya maji ghafi.
  Amesema serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo na iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote yanayotishia usalama wa maji wananchi watajulishwa.
  Hatua ya serikali ya kufautilia usalama wa maji ya ruvu juu unatokana na taarifa kuwa polisi wa mlandizi imewakamata watu kadhaa wakiuza samaki wanaodhaniwa kuwa wamevuliwa kutoka mto ruvu kwa kutumia sumu.
  Maji ya mto ruvu juu ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam.
  ————————————————–
  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu-LHRC, kimetuma jopo la waangalizi wake wa uchaguzi wa serikali za Mitaa kwenye wilaya 100 hapa nchini.
  Lengo la waangalizi hao ambao wengi wao ni wasomi kutoka vyuo vikuu hapa nchini, ni kutazama taratibu za uendeshaji wa zoezi zima, Haki za Binadamu, Vitendo vya Rushwa pamoja na kupata taarifa sahihi juu ya uchaguzi wa serikali za Mitaa.
  Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wakili Francis Kiwanga, hatua hiyo ya kupeleka waangalizi wa uchaguzi, inatokana na Ofisi ya waziri Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za mitaa, kukubali ombi la kituo hicho kutuma waangalizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
  Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa ngazi ya kijiji, Kitongoji na Mitaa, unatarajiwa kufanyika jumapili ya Oktoba 26 mwaka huu.
  ————————————————-
  Tanzania imekumbushwa umuhimu wa kuboresha miundombinu yake ya usafiri ikiwemo reli, ili iweze kunufaika na jiografia yake ya kuzungukwa na nchi zisizo na bahari.
  Aidha, imetakiwa kuboresha huduma zake katika bandari ya dar es salaam, kwa kuhakikisha inapunguza msongamano wa mizigo na hivyo kuvutia wateja kutoka nchi hizo zisizo na bahari.
  Mwakilishi wa washirika wa maendeleo ambaye pia ni mwakilishi mkazi wa jumuiya ya Ulaya balozi Tim Clark, amekumbusha umuhimu huo wakati akizungumza kwenye mkutano wa tatu wa majadiliano ya pamoja kati ya serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi kuhusiana na suala zima la miundombinu ya usafiri.
  Balozi Clark amesema umefika wakati kwa serikali kuangalia namna ya kusimamia uwekezaji kwenye miundombinu ya usafiri na kusimamia uendelevu wake kwani ni eneo muhimu katika maendeleo.
  Waziri wa miundombinu Dk. Shukuru Kawambwa akizungumzia mkutano huo amesema utatoa nafasi kwa wadau hao kufanya mapitio ya maendeleo ya sekta ya miundombinu kuangalia mapungufu na mafanikio katika utekelezaji wa mipango iliyopo, hatua iliyozungumziwa pia na naibu katibu mkuu wa wizara ya mawasilino na usafirishaji wa Zanzibar Dk. Vuai Lila.
  Pamoja na mambo mengine mkutano huo utatoka na tamko la pamoja juu ya maboresho na ushirikiano zaidi kwenye sekta ya miundombinu baina ya serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi.
  ——————————————–
  Upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalum katika jamii, umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kuu zinazoikabili sekta ya afya nchini, hatua inayosababishwa na kilichodaiwa kuwa ni ukiukwaji wa utekelezaji wa sera ya taifa kuhusiana na huduma kwa makundi hayo.
  Miongoni mwa makundi hayo ni pamoja na wazee, watoto chini ya umri wa miaka mitano na akina mama wajawazito.
  Mwenyekiti wa jukwaa la asasi za kiraia bi. Rose Mushi ameeleza hayo wakati akiwasilisha mada inayohusiana na wigo wa huduma za afya kwa ujumla, katika mkutano wa mapitio ya sekta ya afya kwa mwaka 2009, ulioanza leo jijini Dar es salaam na kuhusisha wadau mbalimbali.
  Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu wa namna watendaji wa sekta hiyo wanavyotekeleza sera zilizopo, ambapo pia alibainisha maeneo ya huduma za afya ambayo kimsingi jukwaa hilo linayaona yana upungufu.
  Waziri wa afya na ustawi wa jamii Prof. David Mwakyusa, akizungumza katika mkutano huo amesisitiza azma ya serikali ya kuendelea kuboresha huduma za afya ikiwemo ya mama na mtoto, ambayo ni miongoni mwa malengo ya milenia ya mwaka 2015, ambapo alizungumzia utekelezaji wa mipango iliyopo na mkutano huo kwa ujumla.
  Mkutano huo umehusisha wadau wa afya wakiwemo washirika wa maendeleo, asasi zisizo za kiraia, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na masuala ya afya.
  —————————————-
  Tanzania imebainika kuwa na watu milioni 2.4 wenye aina mbalimbali za ulemavu, sawa na asilimia nane ya watanzania wote.
  Mikoa ya Mara, Tanga, Ruvuma na Kilimanjaro imeonyesha kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye aina mbalimbali za ulemavu, huku mikoa ya Manyara, Dar es Salaam, Mbeya na eneo la tanzania visiwani likiwa na idadi ndogo ya watu hao..
  Takwimu za Ofisi ya taifa ya Takwimu zimebaini pia kuwepo kwa ongezeko la watu wenye ulemavu wa ngozi, ambapo takwimu za sasa zinabainisha kuwepo watu 8,193 wenye ulemavu wa Ngozi yaani Albino, tofauti na awali ambapo ilidhaniwa kuna watu 4,875 wa aina hiyo.
  Katika utafiti huo uliofanywa mwaka jana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, licha ya kubaini watu wengi wanakabiliwa na Ulemavu wa Macho, kundi kubwa linaloathirika kutokana na aina mbalimbali za ulemavu watu wenye umri wa miaka zaidi ya hamsini.
  Kutokana na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye watu wenye ulemavu, kundi la wataalamu la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na takwimu za watu wenye ulemavu, Liitwalo Washington Group, linakutana kwa siku tatu jijini Dar es salaam kwenye mkutano wake wa Tisa kujadili namna ya kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu duniani.
  ———————————-
  Naibu waziri wa mawasiliano sayansi na teknolojia dk.Maua daftari, amesema serikali imefikia hatua za mwisho za kukamilisha mradi wa anuani za makazi ikiwa ni sehemu ya utekelekezaji wa sera ya taifa ya posta ya mwaka 2003.
  Ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya posta duniani yaliyoandaliwa na shirika la posta nchini kwa kushirikiana na mamlaka ya mawasiliano nchini -TCRA, ambapo kauli mbiu yake ni huduma za posta zinazozingatia utunzaji wa mazingira.
  Amesema mradi huo pamoja na mambo mengine unalenga kuwawezesha watanzania wote kuwa na anuani za kudumu, itakayoonyesha mtaa pamoja na namba ya nyumba.
  Amesema mradi huo wa anuani za makazi utaongeza ufanisi,katika utawala bora kwa kutambua makazi ya kila raia,utaimarisha usalama pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kiuchumi,kijamii na hatimaye kuongeza mapato ya serikali.
  Kuhusu mazingira, amelitaka shirika la posta nchini kutumia mtandao wake katika kusaidia juhudi za serikali za utunzaji wa mazingira.
  ——————————–
  Wazazi na walezi wa wanafunzi katika wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, wametakiwa kushirikiana na mamlaka za elimu kukabiliana na tatizo la mimba linalowapata wanafunzi, hasa wale wanaojiunga na sekondari baada ya kuhitimu elimu ya msingi.
  Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Taaluma wa wilaya hiyo Bw. Damas Kimaro, kwenye matukio mawili ya kukabidhiwa vyumba vinne vya madarasa, madawati na samani za ofisi kutoka taasisi ya maendeleo ya Jamii Tanzania CDTF, kwa ajili ya shule za msingi Ruvu JKT na Msongola wilayani Kibaha.
  Akifafanua kuhusu makabidhiano hayo, Afisa Miradi Mwandamizi wa CDTF Bw. Omari Ngallawa alieleza kuwa, vyumba viwili vya madarasa kwa kila shule vilijengwa kwa utaratibu wa kuunga mkono nguvu za wananchi na serikali katika kuchangia maendeleo ya elimu.
  Kwa upande wa walimu wa shule hizo wameomba asasi nyingine kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya elimu ya shule za msingi, hasa changamoto ya nyumba za kuishi walimu.
  Mchango wa CDTF kwa shule hizo katika kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa mawili kwa kila shule, madawati na samani, vimegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 16.
  ————————————-
  KIMATAIFA.
  Rais Barrack Obama wa Marekani, anatarajiwa kukutana na kundi la washauri wake wa usalama wa taifa, kwa ajili ya kupanga mikakati kuhusu hali ya vita nchini Afghanistan, ikiwa ni miaka minane ya vita nchini humo.
  Rais huyo anaangalia jinsi Marekani inavyoweza kuendelea kukabiliana na hali ya vita inayoongezeka nchini humo, ambapo wanajeshi mia nane wa Marekani wamepoteza maisha, hatua inayolalamikiwa na raia wa Marekani, ambao wanataka majeshi ya nchi yao kuondoka Afghanistan.
  Hata hivyo habari kutoka nchini humo zinasema, viongozi wa mabaraza ya wawakilishi na seneti kutoka vyama vya republican na demokrats wanatofautiana kimsimamo kwa kundi la republican, kutaka rais Obama kuwasikiliza makamanda wa kijeshi, huku wenzao wa democrats wakimtaka asikubali kushinikizwa katika kutoa maamuzi.
  Vita nchini Afghanistan vilianza baada ya shambulio la kigaidi la Septemba 11, mwaka 2001, ingawa vimeendelea kwa kipindi kirefu tofauti na ilivyotarajiwa.
  ———————————–
  Umoja wa mataifa umeahidi kutoa dola za kimarekani milioni 74 kusaidia waathirika wa mafuriko nchini Ufilipino, ambako maelfu ya watu hawana makazi na wengine wengi wakiwa hawajulikani walipo.
  Jitihada za uokoaji zinaendelea nchini humo,, kwa watu waliozingirwa na maji kujaribu kuondoshwa katika makazi yao, huku wakifikishiwa pia misaada ya vyakula na matibabu.
  Licha ya makazi ,miundombinu ya barabara na umeme imeathiriwa vibaya na mafuriko hayo.
  Mkuu wa kitengo cha misaada ya kibinadamu wa umoja wa mataifa John Holmes, amesema watu nchini humo wanahitaji chakula, maji, makazi ya dharura na huduma za afya.
  ————————————-
  Nako nchini India, zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya milioni moja hawajulikani walipo, kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini humo.
  Habari kutoka nchini humo zinasema, misaada ya kibinadamu inahitajika kusaidia watu walioathiriwa na mafuriko hayo.
  ——————————————
  Taasisi ya Sekta Binafsi, imesema ukosefu wa umeme wa uhakika nchini, ni mojawapo ya vikwazo vya ufanyaji biashara hapa nchini.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dk Evans Rweikiza amesema umeme umechangia kuifanya sekta binafsi ya Tanzania kushindwa kufanya kazi ipasavyo, na hivyo kutoa mchango hafifu kwa maendeleo ya taifa.
  Hata hivyo serikali imeahidi kuzungumza na sekta binafsi ili kurekebisha mapungufu ambayo yameainishwa kuwa vikwazo kwa maendeleo ya Sekta binafsi.
  Katika mkutano mkuu maalum wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Dar es salaam, Prof Paramagamba Kabudi ameitahadharisha sekta binafsi kuwa makini na soko la Pamoja la Jumuia Afrika Mashariki.
  ——————————————-
  Shirika la viwango nchini -TBS limefanya ukaguzi wa bidhaa aina ya vipodozi katika maduka mbalimbali katika eneo la Kariakoo jijini Dar es salaam, ambapo wamebaini kuwepo kwa bidhaa zinazouzwa bila kuwa na nembo ya ubora inayotolewa na shirika hilo.
  Nyingi ya bidhaa hizo ni zile zilizotengenezwa hapahapa nchini ambapo mbali na kutokuwa na nembo ya ubora ya shirika la viwango, bidhaa hizo pia hazionyeshi jina la mtengenezaji.
  Akizungumza wakati wa zoezi hilo la kushtukiza, Mary Meela ambaye afisa viwango mwandamizi na mkaguzi wa TBS amebainisha kupatikana kwa bidhaa hizo katika baadhi ya maduka katika eneo hilo.
  Kufuatia hali hiyo Bi Meela amewataka wafanyabiashara nchini kuwa makini na kuzingatia kuwa bidhaa wanazouza ziwe zimethibitishwa na shirika hilo kwa lengo la kulinda afya za walaji.
  Mara kadhaa TBS imekuwa ikifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa bidhaa zinazouzwa hapa nchini zinakidhi viwango vinavyohitajika.
   
 2. B

  Bulesi JF-Expert Member

  #2
  Oct 8, 2009
  Joined: May 14, 2008
  Messages: 6,447
  Likes Received: 414
  Trophy Points: 180
  Serikali itasemaje MAJI ni salama conclusively wakati mkemia mkuu bado hajatudhihilishia kuwa sumu iliyoua samaki haiwezi kutudhulu? Acheni kuchezea maisha ya watu kwa kupeleka siasa mbele!
   
Loading...