Serikali imekaa kimya...

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
...wakati wao ndiyo waliowaleta hawa "wachukuaji"

Kitimtim TRL makao makuu

2008-04-05 09:38:18
Na Raymond Kaminyoge

Zaidi ya abiria 100 wa Shirika la Reli Nchini (TRL) ambao walikata tiketi kwa ajili ya kusafiri na treni, `wamevamia` makao makuu ya ofisi hizo na kumbana Mkurugenzi Mkuu Msaidizi, Bw. Dhananjay Naik wakimshinikiza awape usafiri.

Aidha Bw. Naik alipata wakati mgumu zaidi alipokwenda katika ofisi za kukatia tiketi na kukutana na abiria wengine ambao nao walimzunguka na kutaka awaeleze hatima yao.

``Hapa huondoki tueleze tunasafiri vipi kwenda makwetu, fedha mmechukua, usafiri hatuuoni na wala hamtuelezi chochote, tuwaeleweje?`` Alihoji mmoja wa abiria hao, Bi. Magdalena David.

Mkurugenzi huyo ambaye ni raia wa India, kila alipojaribu kuwaeleza abiria hao aliishia kutukanwa matusi ya nguoni na kila alipojaribu kuchomoka katika kundi hilo la abiria wenye hasira walimzuia asiondoke.

``Tunafanya mipango ya kuwarejeshea fedha zenu,`` alisema mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, abiria hao walisema wanataka TRL ikodi mabasi ili yawapeleke kwa sababu nauli watakazorudishiwa haziwezi kutosha kusafiri kwa barabara.

Wakati hayo yakiendelea abiria wengine walipandisha jazba na kutaka kumpiga mkurugenzi huyo lakini akaokolewa na polisi wa kituo kikuu cha polisi cha mkoa ambao walimsindikiza kwenda ofisini kwake.

Hatua ya abiria kudai usafiri inafuatia wafanyakazi wa TRL kugoma kufanya kazi hadi mwajiri wao atakapowalipa nyongeza za mshahara ambapo wanataka kima cha chini kiwe Sh. 160,000 kwa mwezi badala ya Sh. 87,000.

Mwezi uliopita, baada ya wafanyakazi hao kugoma, Menejimenti ya TRL iliahidi kuwalipa wafanyakazi hao nyongeza hiyo ya mshahara mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini halikufanya hivyo hali iliyoanzisha mgomo mwingine.

Kufuatia mgomo huo, huduma za usafiri za shirika hilo zimesitishwa hadi wafanyakazi hao watakaporejea kazini.

Baadhi ya abiria hao walisema wameishiwa fedha za matumizi hali inayowafanya walale katika stesheni hiyo huku wakiombaomba chakula.

Wakati hayo yakitokea, wafanyakazi wa Shirika hilo walioanza mgomo wao tangu juzi, jana waliingia katika siku ya pili na kusisitiza kuwa hawatafanya kazi hadi kieleweke.

Habari zilizopatikana wakati tukienda mitamboni zinasema, uongozi wa shirika hilo jana ulianza kuwarudishia abiria hao nauli zao.

SOURCE: Nipashe
 
Wafanyakazi TRL waishangaa serikali

Abiria wageuka ombaomba

na Prisca Nsemwa, Dar na Rahel Chizoza, Dodoma
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Reli nchini (TRL) wamesema kuwa wanaishangaa serikali kwa kumtetea mwekezaji wa kampuni hiyo, ambaye amepuuzia mkataba ambao aliusaini yeye mwenyewe.

Wafanyakazi hao leo wanafikisha siku ya tatu ya mgomo wao kudai mshahara mpya ambao waliahidiwa kupatiwa kuanzia mwezi uliopita, lakini mwajiri huyo ameshindwa kutimiza ahadi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Sylivester Rwegasira, alisema kuwa serikali ilitakiwa imchukulie hatua za kisheria mwajiri huyo, kwa kuwa aliisaini mkataba huo na hajautekeleza.

“Wafanyakazi hawaielewi serikali, kwa kuwa walichotarajia ni serikali kumkemea mwajiri huyo na kumchukulia hatua kwa kupuuza mkataba ambao alisaini mbele ya viongozi wa serikali,” alisema Rwegasira.

Alisema kuwa wafanyakazi wataendelea na mgomo hadi pale watakapoongezewa mishahara na kuhakikishiwa kuwa nyongeza hiyo itaendelea kila mwezi.

“Miongoni mwa vitu ambavyo wafanyakazi wa TRL wanashindwa kuielewa serikali ni kwa nini ichukue uamuzi huo wa kumtetea mwekezaji ambaye moja kwa moja anaonyesha kupuuzia mkataba na kutokuja kwenye kikao walichokaa na (Profesa Juma) Kapuya (Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana), lazima kutakuwa na kitu kati ya serikali na mwekezaji,” alisema Rwegasira.

Alisema tayari wameshapeleka wajumbe wawili kushiriki katika kamati inayopitia hesabu za mwajiri huyo, anazodai kuwa zinaonyesha uwezo wake mdogo wa kifedha kuweza kumudu kulipa mishahara hiyo.

Pia wafanyakazi hao walisema kuwa wataendelea kulinda vitu vya kampuni hiyo kwa kuwa wanatambua ni mali ya nchi na kusisitiza kuwa hawatarudi hadi wapate fedha hizo.

Wakati mgomo huo unaendelea na safari za treni zikiwa zimesitishwa, abiria ambao walitarajia kusafiri kwa treni hiyo wanaendelea kupata shida, baadhi yao wakikosa sehemu za kulala na kulazimika kulala katika maeneo ya shirika hilo.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya abiria hao walisema kuwa wanalazimika kulala hapo kwa kuwa hawana fedha na walitarajia huenda wakasafiri mapema, lakini hadi hivi sasa hawaoni dalili yoyote ya wao kusafiri.

Kutoka Dodoma, inaelezwa kuwa baadhi ya abiria waliokuwa wakitarajia kusafiri na treni kabla ya kusitishwa kwa safari za treni kupitia Reli ya Kati, wamegeuka kuwa ombaomba baada ya kujikuta wakiwa hawana mahala pa kwenda.

Abiria hao ni wale waliokuwa wanatarajia kuanzia safari zao mjini Dodoma kuelekea mikoa ya Tabora, Mwanza, Shinyanga na Kigoma na ambao hawana ndugu na hawakuwa na fedha za kutosha kusafiri kwa mabasi.

Tanzania Daima ilishuhudia mmoja wa wasafiri hao aliyejitambulisha kwa jina la Mama Neema, akiwa na watoto wake wawili katika eneo la Stesheni mjini hapa akisema kuwa hajui afanye nini kutokana na kutokuwa na fedha ya kumuwezesha kusafiri kwa basi hadi nyumbani kwake.

Mama huyo aliyeonekana kukata tamaa, alisema alikuwa na nauli ya kwenda Tabora kwa njia ya treni na fedha kidogo ya kujikimu awapo njiani.

Alisema tangu kusitishwa kwa safari hizo amekuwa akiomba misaada ya fedha na chakula kwa wasamaria wema ili aweze kwenda mkoani Tabora ambako ndiko anakoishi.

Alibainisha kuwa alikwenda mkoani Dodoma akitokea Dar es Salaam kwa lengo la kuanzia safari, ndipo alipokwama baada ya kukutana na tangazo lililoonyesha kuwa hakuna safari kutokana na kuwepo kwa tetesi za mgomo.

Mtu mwingine pia aliyejitambulisha kwa jina moja la Mbaga, naye alionekana maeneo ya mjini Dodoma akiwa anaombaomba na kusema kuwa alikuwa anatarajia kusafiri na treni kwenda mkoani Shinyanga ambako hakuwa na fedha ya kumuwezesha kutumia usafiri wa basi.
 
Back
Top Bottom