Serikali haina mamlaka ya kutupangia cha kujadili (Mchakato wa Katiba) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali haina mamlaka ya kutupangia cha kujadili (Mchakato wa Katiba)

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Tankthinker, May 18, 2011.

 1. Tankthinker

  Tankthinker Member

  #1
  May 18, 2011
  Joined: May 1, 2011
  Messages: 58
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Serikali haina mamlaka ya kutupangia cha kujadili.
  MUSWADA wa sheria ya katiba mpya uliowasilishwa na serikali bungeni hivi karibuni na baadaye kuondolewa baada ya kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi, pamoja na mambo mengine, unakataza baadhi ya mambo kujadiliwa na wananchi wakati wa kukusanya maoni ya katiba mpya.

  Katika kipengele cha 9(2), muswada huo umeorodhesha mambo ambayo hayapaswi kujadiliwa na wananchi na unaiagiza Tume inayopendekezwa kufanya kazi ya kukusanya maoni kuhakikisha kuwa mambo hayo hayajadiliwi, kwa maelezo kuwa hizo ni tunu za taifa ambazo zinapaswa kulindwa na kudumishwa wakati wote.

  Baadhi ya mambo yanayokatazwa kujadiliwa na ambayo nitayajadili katika makala haya ni kwanza, suala la uwepo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uwepo wa mihimili mitatu ya dola ambayo ni serikali, bunge na mahakama.

  Mambo mengine ni pamoja na wadhifa wa urais na uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivi ni marufuku kuvijadili kwa mtazamo wa kuvifuta kabisa kutoka kwenye katiba yetu, na Waziri wa Sheria na Katiba wa nchi yetu mara kadhaa amezungumza na vyombo vya habari na kufafanua kuwa serikali haitaki kusikia mwananchi au wananchi wakija na mawazo ya kuvunja Muungano, kufuta mihimili mitatu ya dola, kufuta wadhifa wa urais au kufuta uwepo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

  “Hatujakataza kujadili mambo haya ila hatutaki mtu au watu waje na mawazo ya kutaka kuvunja Muungano wetu, kufuta mihimili mitatu ya dola, kufuta urais au kufuta uwepo wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hayo mawazo hatukubali”, anasema Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani.

  Mimi sikubaliani na msimamo huu wa serikali, hivi serikali imepata wapi nguvu hizi? Nani kawapa mamlaka haya? Serikali haina mamlaka ya kuwapangia wananchi mambo ya kujadili wakati wa kutoa maoni ya katiba mpya, serikali haina mamlaka ya kuamua ipi iwe tunu ya taifa na ipi isiwe, wananchi ndio wenye nchi, wananchi ndio wenye sauti ya mwisho kwa kila kitu.

  Ieleweke hapa kuwa mambo haya yanayoitwa tunu za taifa hayakuanzishwa wala kukubaliwa na wananchi, yalianzishwa na kusimikwa na viongozi wetu bila hata ridhaa yetu, hivyo leo hii hayawezi kupewa heshima ya “utakatifu” kiasi cha kukatazwa kuyajadili.

  Kwa mfano, ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wa pande zote za Muungano za Tanganyika na Zanzibar hawakuulizwa maoni yao kuhusu suala la kuziunganisha nchi zao, Muungano uliopo ulifikiwa na watu wawili tu, aliyekuwa rais wa Tanganyika wakati huo, hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

  Kwa hiyo, leo hii tunapokwenda kwenye mjadala wa katiba mpya, huwezi kuwapiga marufuku Watanzania kuja na wazo la kama tuendelee na muungano au tuuvunje na kuendelea kuishi kama majirani tukiwa mataifa mawili huru. Kuendelea au kutoendelea na muungano ni uamuzi wa wananchi, waachwe wachague njia ya kufuata.

  Halafu lazima ikumbukwe kuwa mambo haya hayakuanzishwa na Mungu, si amri za Mungu kiasi kwamba wanadamu hawawezi kufanya mabadiliko, mambo haya yanatokana na akili za watu, hivyo yanaweza kuwa na upungufu na hivyo kuhitaji kufanyiwa mabadiliko au kufutwa kabisa kulingana na mahitaji ya wakati.

  Kwa mfano, si lazima nchi yetu iongozwe na rais, tunaweza kuamua kuanzisha utawala wa kifalme, au kuwa na rais asiye na mamlaka ya utendaji kama ilivyo katika baadhi ya nchi kama vile Ujermani, Ethiopia na kwingineko, badala yake mamlaka ya utendaji tukayaweka mikononi mwa waziri mkuu, yote yanawezekana kama wananchi wakiamua na hakuna wa kuwazuia.

  Au si lazima nchi yetu kuwa na Bunge, tunaweza kuamua kulifuta Bunge na kubakiza mabaraza ya madiwani tu, halafu viongozi wa mabaraza ya madiwani watakuwa wakikutana kujadili na kuamua masuala ya kitaifa, ikiwamo kutunga sheria.

  Kwa ufupi ninachotaka kusema hapa ni kwamba wananchi ndio mwanzo wa mamlaka yote na vyombo vingine ikiwamo serikali, vitapata madaraka kutoka kwa wananchi, hivyo serikali isijipachike mamlaka yasiyo yake, iwaache Watanzania waamue wenyewe kwa hiari yao lipi wanalitaka na lipi hawalitaki kuwa katika katiba yao.

  Source; MWANANCHI.
   
Loading...