Kuanzia Mei 1, sera ya China ya ushuru sifuri kwa nchi za Afrika itajumuisha bidhaa nyingi kutoka nchi za Afrika, ikionyesha mabadiliko makubwa katika mienendo ya biashara ya kimataifa. Sera hii inakuja katika wakati muhimu kwa uchumi wa Afrika, ambao unakabiliana na mashinikizo ya nje yanayozidi kuongezeka.
Gharama za biashara za kimataifa kutokana na hali isiyo thabiti ya kisiasa kama vita ya Ukraine na mgogoro w Mashariki ya Kati, vimeathiri minyororo ya usambazaji na kuongeza gharama za kufanya biashara. Wakati huo huo, hatua za kujilinda kibiashara kutoka nchi za magharibi, zimefanya biashara ya masoko ya jadi ya nchi za Afrika kuwa magumu zaidi kufikika.
Hatua hii ya China inatoa njia kwa wafanyabiashara wa Afrika wanaotafuta soko kubwa na thabiti. Hata hivyo, mafanikio yake yanategemea jinsi nchi za Afrika zinavyoweza kujipanga na kushughulikia changamoto za kimuundo zilizopo kwa muda mrefu ili ziweze kunufaika na nafuu hiyo.
Katika miongo mitatu iliyopita, ushirikiano wa kibiashara kati ya China na nchi za Afrika umekuwa na mabadiliko makubwa. Kwenye miaka ya 1980, wakati uchumi wa China ulipoanza kukua kwa kasi, ushirikiano na Afrika ulijikita zaidi kwenye biashara ya raslimali. Bidhaa za Afrika kwenda China zilikuwa ni mafuta ghafi, shaba, cobalt, na chuma kutoka kwenye kundi dogo la nchi zenye raslimali nyingi. China kwa upande wake ilisafirisha bidhaa za viwanda, ikiwa ni pamoja na mitambo, magari, na bidhaa za kilimo kwa karibu nchi zote za Afrika. Mfumo huu wa biashara uliweka msingi wa uhusiano ambao ulipanuka haraka katika miongo iliyofuata.
Hata hivyo kupanuka kwa biashara kulionesha pengo kubwa la biashara kati ya China na Afrika, huku Afrika ikiwa na urali mbaya. Nchi za Afrika kwa kiasi kikubwa zilibaki kuwa wafanyabiashara wa malighafi za thamani ya chini wakati zikitegemea zaidi bidhaa zilizotengenezwa zilizoagizwa kutoka China. China ilianza kuchukua hatua mbalimbali za kurekebisha urari mbaya wa biashara na nchi za Afrika, ikiwa ni pamoja na kuanzisha baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), kupanua ushirikiano na kuwa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote, hatua hii ya kutoza ushuru sifuri, ni mwendelezo wa hatua za China kurekebisha urali huo.