Sera mbovu katika kusimamia rasilimali za taifa zinaliangamiza taifa

sammosses

JF-Expert Member
Jan 24, 2011
1,682
1,110
Katika umbaji wake Mwenyezi Mungu alitumia hekima na busara katika kuumba mbingu na nchi,lakini alimuumba binadamu akampa akili akimtofautisha na wanyama na mimea. Hakuishia hapo alizitenganisha mbingu na nchi, akazijalia nchi rasilimali za kutosha ili binadamu aweze kuyatawala mazingira na kuzitumia rasilimali katika kutekeleza matakwa ya uendeshaji maisha yake ya kila siku.

Haikuwa kosa kumilikishwa rasilimali ambazo binadamu alizojaliwa na Mwenyezi Mungu, lakini kosa lilikuwa kwa waliomilikishwa rasilimali hizo, aidha walizitumia vibaya kwa kufanya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao hakuweza kuleta tija kwa taifa au walizitumia rasilimali hizo vibaya kwa maslahi ya watu wachache kwa kujilimbikizia mali kupita kiasi na kusahau wajibu wao katika kuzisimamia rasilimali hizo kwa faida ya wote.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mfumo gani huu,mfumo wa shetani,watu wanawanyang'anya mali masikini na kuwapa matajiri, Mwalimu aliwaza mbali sana mpaka kufikia kutoa tamko hilo. Alipata sana mashaka mara baada ya kuona rasilimali ambazo aliziona ni hazina ya taifa zinabebwa kama hazina mwenye kutoka mikono ya watu masikini na kupewa matajiri ambao ni wageni kutoka nje ya nchi yetu kwa maslahi yao binafsi.

Tumeona taifa linavyopita vipindi vigumu vya mpito kutokana na taifa kuzidi kuwa masikini katika mstari wa nchi masikini duniani ilihali hazina yake inazidi kwisha na kuiacha nchi ikiwa mashimo,athari za kibailojia na kikemikali ambazo zimeathiri uchumi wa sehemu husika, mathalani ukizunguka sehemu ambazo Mungu alizijalia madini katika nchi yetu,unaweza kulia kutokana na umasikini uliowagubika wanachi wa pale, lakini mbaya zaidi wameathirika na kemikali za sumu ambazo zimesababishwa na maji yenye kemikali kumiminikia mtoni ambako binadamu wa maeneo hayo wanayatumia kwa matumizi yao ya kawaida.

Uchumi wa maeneo ya migodi ya madini ni duni kutokana na sera mbovu ambazo zimeshindwa kuwalinda wananchi wa maeneo ambayo waliyatunza ndo maana wageni hao wameyakuta. Wananchi wamejengewa chuki na uoga kutokana na wawekezaji hao kuwajengea uadui ambao mwisho wa siku ni vita kati ya wawekezaji na wenyeji.

Vijana wanapata ajira ambayo haikidhi mahitaji yao ya kila siku kutokana na nguvu kubwa wanayo tumia kufanikisha rasiliamli hizo kwenda kujenga kwenye mataifa makubwa ambayo hayakumbani na madhara ya uchimbaji wanayoyapata vijana wetu wa Kitanzania. Sera mbovu ambazo serikali imezisimamia zimeendelea kuwa mwiba kwa rasilimali watu kutokana na serikali kushindwa kusimamia haki stahiki za malipo kwa vijana wetu.

Kilio cha vijana wa Kitanzania ni kwa serikali kukosa uzalendo kutokana na viongozi ambao ni Watanzania wenzetu wameendelea kutumika kuwakandamiza Watanzania wenzao na kufanywa mamluki kwaajili ya maslahi ya wageni hao. Tumeona mwanasheria mmoja ambaye ni mzawa mwenzetu anavyotumika vibaya kuhakikisha anabana haki stahiki za wenzake kwa kuwa tu yeye ni tabaka fulani ndani ya nchi.

Leo hii Watanzania wanaamka na kujua umuhimu wa rasilimali zao, lakini serikali inashindwa kukaa na wanachi hao kama wanavyofanya wakati wa kuomba dhamana ya uongozi. rasilimali zao zinapelekea kumwaga damu isiyo na hatia bila kujali utu wa mtu.

Bunge nalo linasimamia ukandamizaji wa haki za wanyonge katika kumiliki rasilimali zao, jumba lile la limekuwa kama pango la wanyang'anyi kwa kutumia nafasi zao za kiheshimiwa kupitisha sheria kandamizi dhidi ya wananchi wake kwa kuuza utu wa Mtanzania na kunufaika posho zinazotokana na kodi ambazo wavuja jasho wa nchi wanakamuliwa.

Tumeona matumizi mabaya ya madaraka katika kusimamia hazina ya taifa, nchi inazidi kuwa masikini inayozungukwa na mahandaki lakini deni la taifa badala ya kupungua linazidi kuongezeka ilihali madini yetu, wanyama wetu wanasafirishwa siku hadi siku. Tumeona usiri wa mikataba unavyoliangamiza taifa lakini wabunge wamebaki wakigonga mabenchi, wapi taifa lina kwenda ilihali kila Mtanzania hajui kesho yake ilivyo?
 
La msingi ni watanzania bila kujali itikadi za vyama wala dini kuiondoa CCM madarakani. Tofauti na hapo tutakuwa tunajitumainisha kwa maisha bora na hivi kuendelea kuishi kwa kubahatisha mambo mithili ya wapiga ramli..
 
Ajabu hata zile fursa za ajira zinawalenga wateule wao,mtu ana staafu kutokana na umri baada ya miezi mitatu anateuliwa kuwa balozi nchi fulani,hivi hatuna vijana wenye sifa hizo mpaka wastaafu wanateuliwa tena ilihali walishamaliza muda wao wa utumishi?
 
Back
Top Bottom