Sekta ya madini haijasaidia Tanzania

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,791
288,003
Posted Date::10/18/2007
...Watanzania tunalijua hili...ndiyo maana tunapiga kekeke mikataba hiyo iangaliwe upya ili iinufaishe Tanzania

'Sekta ya madini haijasaidia Tanzania'
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi

TANZANIA licha ya kuwa na utajiri wa madini bado imeshindwa kunufaika kwa kiwango kikubwa, kutokana na kukosekana mipango iliyowazi katika kudhibiti sekta hiyo.

Akitoa tathimini kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emanuel Ole Naiko, juu ya Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia ya mwaka 2007, Mkurugenzi wa Utafiti na Mawasiliano wa kituo hicho, John Kyaruzi, alisema ipo haja ya kufanyika kazi ya ziada kuona madini yanatumika kupunguza umasikini kwa Watanzania.

Kyaruzi alifafanua kwamba baadhi ya makampuni yanayochimba madini yamekuwa na ajenda zao za kibiashara na kwamba kazi kubwa kwa serikali ni kutokubaliana na mambo yasiyo na manufaa kwa nchi.

Alifafanua kwamba, sekta ya madini imekuwa ikitarajiwa kufungua milango zaidi ya uwekezaji wa moja kwa moja (FDI) na kusaidia nchi zenye utajiri huo kuendelea, lakini kwa Tanzania bado haijafanya vizuri hasa katika mipango.

"Uendelezaji wa maliasili unahusisha changamoto za kiuchumi, mazingira na kijamii, tungependa kuona hayo yanafanyika ili kuwe na ufanisi, urafiki na mazingira mazuri ya kibiashara na wakati huo huo zinachangie kuondoa umasikini na kuchochea maendeleo ya nchi yetu," alisema Kyaruzi.

Aliongeza kuwa utajiri huo wa madini, ulitegemewa kufungua milango na fursa kwa nchi husika kuweza kupiga hatua ya maendeleo lakini Tanzania bado haijaweza kufanya vizuri hasa katika mipango ambayo iko wazi.

"Makampuni ya madini yanakuja kuchimba madini yakiwa na ajenda zao, ambazo ni kupata faida, kwa hiyo jambo la msingi ni kutokubali ajenda ambazo hazina manufaa kwa nchi," alisisitiza Kyaruzi.

Kyaruzi aliongeza kwamba, matokeo yake ni umma kutoridhishwa na hali hiyo kutokana na matarajio yao ya kuona faida kutotimia.

Mkurugenzi huyo alisema ni vema kukawa na mikakati ya kuhakikisha usafishaji madini na kwamba ufanyike nchini ili kuzuia uwezekano wa madini kutoroshwa .

Aliongeza kwamba, ni vema pia shughuli za uchimbaji madini zikazingatia athari za kimazingira na kijamii, ili kuzifanya ziwe rafiki wa mazingira na maendeleo ya jamii.

"Wakati mwingine makampuni yanachimba madini kwenye sehemu fulani, lakin inakuwa haina kitu hivyo yanabaki mashimo, kwa hiyo ni vema athari kama hizo zikaangaliwa," alisema.

Alifafanua kuwa bado kuna swali kwamba ni vipi sekta nyingine kama utalii zitaweza kuimarishwa zaidi ili ziweze kusaidia ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wa changamoto, alisema TIC itajitahidi kuendelea kuvutia wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi waje kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Tanzania imeshindwa kuwa kati ya nchi kumi bora barani Afrika kwa kuvutia miradi ya FDI, lakini ikiwa ya kwanza katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa kupata dola za Marekani 377 milioni katika kipindi cha mwaka jana.

Nchi kumi bora zilizongoza barani Afrika kwa kuwa na miradi mingi ya FID ni Misri, Nigeria, Sudan na Tunisia ambazo zilikuwa na uwekezaji wa miradi ya dola zaidi ya 3 bilioni na Morocco kati ya dola 2 bilioni hadi 2.9 bilioni.

Nyingine ni Algeria, Libya, Guinea, Chad na Ghana miradi kati ya dola 1bilioni hadi 1.9 bilioni huku Marekani, Uingereza na Ufaransa zikiongoza duniani.

Kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa wakilalamikia makampuni ya kigeni kwamba, yanachimba madini na kutorosha nje huku Sera ya Madini ya mwaka 1997 na sheria yake ya mwaka 1998, vyote vikionekana dhaifu.

Udhaifu huo wa kisheria ndiyo ambao umekuwa ukiibua mijadala na malalamiko kutoka kwa wananchi, dhidi ya makampuni ya madini ambayo yanaonekana kunufaika kuliko nchi na watu wake.

Kwa sasa nchi iko katika mjadala mzito kuhusu utiaji saini mkataba wa uchimbaji madini wa Buzwagi, huku taarifa za kodi zinazolipwa na utaratibu unaotumika kisheria ukionekana kuyapa faida makampuni yanayochimba madini.

Ripoti hiyo ambayo imetaja maliasili kama gesi, madini na mafuta kama vyanzo vikuu vya kukua kwa miradi ya FDI, imeandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Biashara Duniani (UNCTAD).
 
serikali haioni hilo, kwa vile wamejisaidia wao mmoja mmoja
 
Back
Top Bottom