Sekretarieti CCM kuwaweka mawaziri kitanzini

sir.JAPHET

JF-Expert Member
May 18, 2012
699
133
Mwandishi Wetu
SEKRETARIETI mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeapa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya chama hicho tawala kwa kufuatilia mienendo ya watendaji wakuu wa Serikali wakiwamo mawaziri.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mpango huo wenye lengo la kuongeza ufanisi wa Serikali, utawabana pia wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wengine wanaosimamia utekelezaji wa Ilani hiyo.

Alisema ikibainika mtendaji yeyote wa Serikali anabaronga katika uwajibikaji wake, sekretarieti hiyo itamjulisha Rais Jakaya Kikwete na kumshauri awafukuze kazi.

“Lengo ni kuhakikisha kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake na endapo itabainika watendaji wanaboronga, sekretarieti haitasita kumfahamisha Rais ili awatimue ama kuwaondoa katika majukumu yao,” alisema.

Kauli ya Nape imekuja wakati kukiwa na taarifa kwamba moja ya majukumu makubwa ya Sekretariti mpya ya CCM ni kurejea katika mwongozo wa chama hicho wa 1982 unaoelekeza chama kuisimamia Serikali ipasavyo.

Hata hivyo, kumekuwapo na wasiwasi kwamba utekelezaji wa azma hiyo unaweza kukwama kutokana na mawaziri na wabunge kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Kada wa siku nyingi wa chama hicho, Steven Mashishanga mwishoni mwa wiki iliyopita aliliambia gazeti hili kwamba, ikiwa CCM kinataka kufanikiwa lazima kirejee kwenye mwongozo wake wa 1982 ambao unakielekeza kusimamia Serikali.

“Hofu yangu ni moja tu kwamba, ikiwa wabunge na mawaziri ni wajumbe wa NEC, basi hapo itakuwa vigumu kuikosoa Serikali. Mimi ninapendekeza Serikali ibaki kuwa Serikali na chama kibaki kuwa chama,”alisema Mashishanga na kuongeza: “Huwezi kuwa chama na hapohapo kuwa Serikali.”

Kadhalika, kauli ya Nape imekuja baada ya karibu miaka 30 ya kampeni zilizowahi kuanzishwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliyetaka kila mmoja awajibike, vinginevyo atakumbwa na fagio la chuma.

Rais Mwinyi aliyekuwa madarakani tangu mwaka 1985 hadi 1995, alitoa agizo kwamba kila Mtanzania anapaswa kuwajibika mahala pake pa kazi ili kuleta ufanisi.

Lakini jana Nape alisema: “Tunaweka utaratibu. Tunataka watu wawajibike katika chama na Serikali na watakaobainika kuzembea, watachukuliwa hatua mara moja badala ya kusubiri uamuzi wa Bunge,” alisema Nape.

"Kwa sasa tumeamua kwamba hatutasubiri wabunge ndiyo wawafichue mawaziri wanaoboronga kazi zao. Sisi (chama), tutahakikisha tunawafuatilia kwa karibu kwani kufanya hivyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuipa ridhaa ya kuendelea kushika dola.

"Chama kimeingia mkataba na wananchi, hatuwezi kuwaacha waendelee kuboronga kwa sababu wakati wa uchaguzi chama ndiyo kinaumizwa," alisema Nape.

Ziara mikoani
Nape alieleza kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na sekretarieti yake, wanatarajiwa kufanya ziara ya kichama mikoani kuzungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo.

Alisema katika ziara hizo, Kinana ambaye atakuwa akiambatana na baadhi ya mawaziri anapanga kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM tangu mwaka 2010.

“Ziara hiyo itaanza kesho mkoani Mtwara. Watazungumza na wakulima wa korosho na bandari. Watakwenda pia Sumbawanga na Geita ambako watakutana na wachimbaji wadogo wadogo na kumalizia mkoani Arusha,” alisema.

Elimu ya sekondari
Katika hatua nyingine, Nape alisema suala la kutaka elimu ya sekondari itolewe bure nchini si la Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, bali ni maazimio yaliyopitishwa kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.

Juzi Lowassa alikaririwa akisema kuwa wakati umefika kwa elimu ya sekondari nchini kutolewa bure na kumwondolea mwananchi wa kawaida mzigo wa kubeba gharama za elimu.

Lowassa alisema mjadala kuhusu elimu kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu kuanza kujadili suala hilo na kwamba CCM inapaswa kulifanya kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Nape jana alisema: "Hilo siyo wazo lake (Lowassa) binafsi. Suala hilo lilijadiliwa kwenye mkutano huo na tulikubaliana kwamba ni vyema kufanya hivyo ili kumshushia mwananchi gharama.”

Aliendelea: “Suala la utoaji wa elimu bure mwanzilishi wake alikuwa ni Mwalimu Julius Nyerere, labda tatizo ni kwamba watu wengi hawajui historia ya mambo. Elimu bure ilianzishwa tangu enzi za TANU, hadi wao wamesoma bure.”

Nape aliendelea kueleza kuwa “Kadri Serikali inavyoongeza uwezo wake kiuchumi, ndivyo suala hili litakavyotekelezwa ingawa tayari tumeshashusha gharama za ada kwa shule za sekondari. Pia hii inalenga kukuza hali ya kiwango cha elimu, ada ni ndogo sasa ukifuatilia unaweza kulibaini hilo," alisema.
 
CCM ni kama kinyonga, 2010 almanusura mishipa ya shingo iwapusuke kwa kumbishia DR Slaa kuwa elimu bure haiwezekani, sasa kiko wapi mbona wenyewe wameona inawezekana.
 
Huyu nae huwa anaongea mengi na hakuna linalotekelezwa. Ni porojo zake tu. Baadae wenzie watamkataa
 
Pepo anaanza mtoa pepo mwenzie, utawala wa shetani unafitinika.CCM inaelekea kuzimu.sasa inakuweje waziri akishindwa kitu kilishoshindikana kwa serikali?
 
Back
Top Bottom