Sayansi inasema wazazi wenye watoto waliofanikiwa wana mambo haya 10 ya kufanana

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Mzazi yeyote mwema hupenda watoto wake wasiingie kwenye matatizo, wafanye vizuri masomoni na kufanya kazi za maana utu uzimani. Kwakuwa hakuna muongozo maalumu wa kukuza watoto wenye mafanikio, saikolojia imeweka bayana sababu lukuki za kumtabiria mtoto mafanikio na si ajabu kuona kwamba nyingi ya sababu hizo hutokana na wazazi. Yafuatayo ni mambo ya kufanana kwa wazazi wenye watoto waliofanikiwa.

Moja. Huwafanya watoto wao wajishughulishe
"Kama mtoto haoshi vyombo, hafui nguo zake wala kufanya usafi wowote ndani ya nyumba ina maana kuna mtu anafanya kwa niaba yake” anasema Julie Lythcott-Haims mtaalamu wa malezi. Watoto wanaojishughulisha katika kazi hizi siyo tu wanafahamu kuhusu kazi bali pia wanajifunza kwamba kila mtu anatakiwa kuwajibika ili kuchangia maendeleo ya familia, jamii na hata taifa."

Mbili. Huwafundisha watoto Stadi za jamii
Watafiti wa vyuo vikuu vya Marekani wameona uhusiano mkubwa kati ya stadi za maisha walizozipata watoto wakiwa elimu ya awali / msingi na mafanikio yao kama watu wazima baada ya miongo miwili. Imebainika kwamba watoto wenye kujiamini, kushiriki kazi za jamii, wenye stadi za maisha na wenye kushirikiana vizuri na wenzao bila msukumo na wenye kuweza kutatua matatizo na kuwa msaada kwa wengine wana nafasi kubwa ya kufikia malengo ya elimu ya juu na kupata kazi / ajira ukilinganishwa na wale amabao hawakufunzwa stadi za maisha katika umri mdogo.

Tatu. Wanayo matarajio makubwa
Tafiti zinaonesha kwamba, matarajio ambayo wazazi huwa nayo juu ya watoto wao yana mchango mkubwa katika mafanikio ya watoto, hii ni kwa sababu wazazi hushiriki kikamilifu kuhakikisha wanawaongoza watoto kufikia malengo. Wazazi wenye maono ya elimu ya juu kwa watoto wao huhakikisha wanaweka jitihada kuwasaidia watoto kufikia ndoto hiyo bila kujali kipato wala miliki walizonazo.

Nne. Wana mahusiano mazuri baina yao – ni viongozi na si watawala.
Watoto waishio kwenye familia zenye migogoro, iwe wazazi wamepeana talaka au wako pamoja, nk. huwa na matatizo ya kisaikolojia yanayopelekea kukosa maarifa ya kushirikiana vyema na wenzao katika nyanja mbalimbali ukilinganisha na wale wanaoishi kaitika familia zenye upendo, amani na ushirikiano baina yao.

Wazazi hawa huwa na malengo endelevu kwa watoto wao na kufanya jitihada kuwekeza muda wao mwingi katika kutoa muongozo na kufuatilia muenendo wa maisha ya watoto wao. Mtoto hukua akijua kuna uongozi lakini wenye kumpa nafasi ya kukosea kama binadamu na kupatiwa fursa ya kujifunza kutokana na makosa na matokeo ya maamuzi yao

Tano. Wazazi wao wamepata elimu ya juu na / au wanayo hali nzuri kiuchumi.
Tafiti zinaonesha kwamba wanawake waliohitimu elimu ya juu wana uwezekano mkubwa wa kukuza watoto wenye kufikia kiwango hicho cha elimu na zaidi. Utafiti unaendelea kuonesha kuwa kiwango cha elimu cha mzazi wa mtoto kinachagiza uwezekano wa mtoto kupata maendeleo katika nyaja lukuki maishani hususani masomoni.

Kutokana na utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Stanford, utofauti wa mafanikio kati ya wenye nacho na wasionacho unakadiriwa kufikia asilimia 30 mpaka 40. Anaandika mtaalamu kwamba, “ukosefu wa afua jumuishi na za ghali, hali ya kijamii na kiuchumi hupelekea mafanikio na ufaulu kielimu.”

Sita. Huwafundisha watoto hesabu katika umri mdogo
Hivi karibuni imegundulika kwamba kuendeleza stadi na maarifa ya hisabati kwa mtoto katika umri mdogo kuna faida kubwa. Kujifunza mpangilio wa namba, kuzitambua na kuzitamka katika umri mdgo, siyo tu inaashiria mafanikio katika hisabati baadae, bali hata katika maarifa na kusoma.

Saba. Hujenga urafiki na watoto wao
Tafiti zilizofanyika kwa watoto waliozaliwa katika familia maskini zinaonesha kuwa watoto waliopatiwa malezi yenye upendo katika kipindi cha umri wa miaka mitatu ya mwanzo, licha ya kuazaliwa katika familia zenye hali duni, walifanya vizuri katika kipimo cha taaluma utotoni lakini vilevile walikuwa na mahusiano mazuri na mafanikio makubwa kitaaluma miaka 30 baadae.

Nane. Wana kiwango kidogo cha msongo wa mawazo.
Mzazi akiwa na msongo wa mawazo huathiri mahusiano yake na mtoto na hupelekea kuhamishia hisia hizo kwa mtoto. Kiufupi ni kwamba mzazi aliye na msongo wa mawazo atakuza mtoto mwenye msongo wa mawazo na mwenye matatizo ya umakini. Sayansi inatueleza kama rafiki yako ana furaha basi hisia hiyo itakuathiri, na vivyo hivyo kwa mwenye huzuni.

Tisa. Wanathamini jitihada kuliko mapungufu ama kufeli na kuhimiza uthubutu.
Watoto wakifahamu chanzo cha mafanikio basi huweza kutabiri ndoto zao na kupambana kuzifikia. Tafiti zinasema kuwa, ubongo uliojifunga na usio fikiri nje ya boksi, hudhani kwamba tabia, akili na uwezo wa ubunifu wa mtu siyo endelevu, yaani umejifunga.

Wazazi wa wanaothamini jitihada na kuhimiza uthubutu licha ya changamoto wanakuwa ni mifano ya kuigwa kwa watoto wao hasa katika kuyafikia malengo na ndoto zao. Wazazi wanatakiwa kuhakikisha wanawaweka wazi watoto wao juu ya mapambano na vikwazo wanavyopitia ili kufanikiwa na hivyo watoto kukua na dhana hiyo ya kutokata tamaa katika kufanikisha jambo.

Kumi. Kazi ya mama.
Tafiti zinaonesha kuwa kuna faida kubwa kwa watoto wanaokuzwa na mama wanaofanya kazi nyingine nje ya nyumbani. Kwamba, mabinti wenye mama wafanyakazi na waliofikia elimu ya juu wana uwezekano mkubwa kupata kazi za majukumu ya usimamizi na kupata kipato zaidi ikilinganishwa na wenzao waliokuzwa na mama wa nyumbani.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Back
Top Bottom