Saratani ya mlango wa kizazi inavyowatesa wanawake wengi duniani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Saratani ya mlango wa kizazi inavyowatesa wanawake wengi duniani

Discussion in 'JF Doctor' started by MziziMkavu, Jul 28, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jul 28, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  [​IMG]

  KWA mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya mwaka 2010, Tanzania kwa upande wake inao wastani wa wanawake 6,241 ambao huugua saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka, ambapo 4,355 kati yao hufa.

  WHO inakadiria kuwa asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika zaidi katika nchi zinazoendelea.
  Hali hiyo si ya kufikirika bali ni ya kweli kwani wanawake wengi wa Kitanzania wanathibitisha hilo kwa kutoa shuhuda mbalimbali.


  Mmoja wa wanawake hao, Esther Ngunangwa ambaye aliamua kufanyiwa uchunguzi baada ya kuhisi maumivu makali ya tumbo ambayo yalimsumbua kwa zaidi ya miezi sita.


  “Nilifanyiwa uchunguzi na baadaye ikaonekana nina tatizo la saratani ya mlango wa uzazi, niliamua kufanyiwa uchunguzi huo kwa sababu nilihangaika kwa zaidi ya miezi sita bila kupata ahueni,” anasema Ngunangwa.


  Naye Anitha Msigwa, anasema aligundua kwamba, anakabiliwa na ugonjwa huo baada ya ugonjwa kufikia hatua mbaya, jambo ambalo limemfanya akate tamaa ya kupona ingawa anaendelea na matibabu ya kudumu.
  Idadi ya wanawake, wanaoamua kufanyiwa uchunguzi huo, inaongezeka baada ya kuwepo kwa huduma hiyo ambayo awali haikuwahi kuwepo.

  Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Getrude Mpaka, hakuwa nyuma katika kuhamasisha wanawake kukubali kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya uzazi ili wale wanaobainika kuwa na tatizo hilo waweze kupatiwa tiba.

  “Niliamua kupima ili nihakikishe afya yangu baada ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuanza kutoa huduma ya uchunguzi na tiba ya saratani ya mlango wa kizazi, Nashukuru sina tatizo la kansa, jambo la msingi hapa nimepima na nimejijua,”


  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na hospitali nyingine za wilaya mkoani humo, inafanya uchunguzi wa tatizo hilo baada ya tafiti kuonyesha kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi hana nchini na duniani kwa ujumla.


  Mratibu wa huduma ya uchunguzi wa saratani hiyo mkoani Iringa, Dk Gwachele Faustine anasema mkoa wake ni miongoni mwa ile ambayo idadi kubwa ya wanawake wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

  “Nchini Tanzania hasa katika Mkoa wa Iringa, tatizo la saratani ya mlango wa kizazi ni kubwa na linakua kwa kasi ndio maana tumeanza kampeni hii kwa wanawake,ili wengi wachunguzwe na kutibiwa mapema,” anasema Dk Gwachele.


  Mtaalam huyo anasema tangu waanze zoezi hilo, wamewachunguza wanawake 887 kati yao 70 walionekana na mabadiliko ya awali, 20 walikuwa kwenye hatua ya awali na tisa walifanyiwa upasuaji.


  Anaongeza kuwa wanawake walio kati ya umri wa miaka 30 hadi 50, ndio walio katika hatari kubwa ya kupata maambukizi na kwamba, saratani hiyo inatibika iwapo ugunduzi utafanyika mapema.


  Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina wanawake milioni 10.97 walio na umri wa miaka 15 na kuendelea, ambao wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hiyo.


  Kwa Afrika Mashariki, asilimia 33.6 ya wanawake wote, wanasadikiwa kuwa na virusi aina ya Human Papilloma Virus (HPV)ambavyo ndivyo visababishi vya ugonjwa huu.


  Hata hivyo, RAS Mpaka anasema licha ya kwamba huduma hiyo inatolewa bure bado wanawake wengi hawajapata mwamko wa kupima afya zao, jambo ambalo ni hatari ikiwa kansa hiyo itafikia hatua za mwisho.
  Anasema ni vema wanawake wakapima ili kujua afya zao ikiwa wameathirika wapate matibabu haraka, kwa madai kuwa inawezekana kutibiwa kwa wale wanaowahi.


  Kuanza kutoa huduma


  Dk Gwachele anasema Mkoa wa Iringa umeanza kufanya uchunguzi na kutoa tiba ili kuokoa maisha ya wanawake ambao wamekuwa wakipoteza maisha yao kutokana na saratani ya mlango wa uzazi.


  Uchunguzi huo ambao unafanywa na mkoa huo ukishirikiana na Wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa msaada wa Shirika lisilo la kiserikali la Jhpiego, ulianza mnamo mwaka jana.


  Kwa sasa huduma hiyo inatolewa katika vituo saba katika Mikoa ya Iringa na Njombe.

  “shirika hili (Jhpiego) linasaidia kutoa ushauri katika ngazi ya kitaifa juu ya mbinu mbali mbali za kupambana na saratani ya Mlango wa uzazi ili tatizo hili hatari, litokomeze,” anasema

  Hata hivyo, anasema huduma ya uchunguzi wa tiba ya saratani haipatikani kiurahisi jambo ambalo limekuwa likiwafanya wanawake wengi kwenda kutibiwa katika hospitali ya Saratani ya Ocean Road wakiwa katika hatua mbaya.

  “Hali ni mbaya kwa sababu uchunguzi wa tatizo hili haufanyiki mara kwa mara, ndio maana wale wanaoenda ocean roard hufika wakati wakiwa katika hatua ya mwisho jambo linalowafanya waanze kupata tiba endelevu,” anasema Dk Gwachele


  Anasema ugonjwa huo unaweza kuchukua miaka 10 hadi 20 toka maambukizi hadi kujitokeza jambo ambalo limewafanya waanze kuwachunguza wanawake mapema.
  Nini husababisha saratani hii?


  Mtaalamu wa magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk Scholastica Malangalila anasema, saratani ya mlango wa kizazi husababishwa na Maambukizi ya Virusi viitwavyo HPV.


  Anasema kuwa virusi hivi huambukizwa kwa njia ya kujamIiana au kugusana kwa ngozi ya mtu mmoja na mwengine, na huambukiza wanaume na wanawake.


  Vihatarishi vya saratani ya shingo ya kizazi


  Dk Malangalila anataja vihatarishi vya kansa ya kizazi kuwa ni kuanza kufanya ngono mapema, kati ya umri wa miaka 16 wako kwenye hatari kupata saratani ya shingo ya kizazi siku za baadaye.

  Mwanamke mwenye wapenzi wengi au mwenye mwanamume mwenye wapenzi wengi pia yupo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo.

  Anasema utumiaji wa mipira ya kiume au ya kike hupunguza hatari ya kupata saratani hii, lakini ikumbukwe ya kwamba kondomu siyo kinga ya ugonjwa huu.


  Sababu nyingine ni uvutaji sigara kutokana na kemikali zilizopo kwenye sigara ambazo zikichanganyika na seli au chembechembe za shingo ya kizazi, huleta mabadiliko katika shingo ya kizazi hatimaye kusababisha saratani.
  Utumiaji wa vidonge vya kupanga uzazi kwa muda mrefu hasa wale wanaotumia kwa zaidi ya miaka mitano, lishe duni au utapia mlo, kuzaa watoto wengi pamoja na umri mkubwa.


  Dk Malangalila anasema wapo ambao wanapata maambukizi ya saratani huyo kutokana na uasili wa mtu kwa madai kuwa saratani ya shingo ya kizazi huonekana zaidi kwa watu weusi kuliko watu weupe.

  Zipo sababu nyingine kama upungufu wa kinga mwilini, Historia ya saratani ya shingo ya kizazi katika familia na Kujamiana na mwanaume ambaye hajatahiriwa.

  Dalili na viashiria vyake


  Mtaalamu huyo anasema saratani ya shingo ya kizazi katika hatua za awali haina dalili au viashiria vyovyote jambo ambalo limewafanya kuanza kutoa huduma ya uchunguzi katika mjkoa huo ili wanawake,waweze kupima mapema, na kujua hali zao.


  Anasema dalili nyingine za ugonjwa huo ni pamoja na kutokwa na damu, Kutokwa na damu mara baada ya kujamiana na maumivu makali wakati wa kujamiana.


  Dalili za saratani iliyosambaa ni kupungua kwa hamu ya kula, kupungua uzito, kuhisi uchovu, maumivu ya nyonga, maumivu kwenye mgongo, maumivu ya mguu, mguu mmoja kuvimba, kuvunjika mifupa na kutokwa na mkojo au kinyesi kwenye sehemu ya uke wa mwanamke.


  Anasema matibabu ya ugonjwa wa saratani hiyo hutolewa kulingana na hatua za ugonjwa na hali ya mgonjwa.
  “Matibabu ya ugonjwa huu yanatolewa kulingana na hatua ya mgonjwa mwenyewe na njia za kutoa matibabu ni pamoja na upasuaji katika hatua za mwanzo, mionzi na dawa za saratani,” anasema.


  Hata hivyo anaongeza kuwa, ipo huduma endelevu kwa wagonjwa wa saratani ambayo hutolewa kwa lengo la kupunguza makali na kuboresha afya kwa watu wenye magonjwa sugu, ikiwemo saratani.


  Aidha, anashauri wanawake kujenga tabia ya kupima mara kwa mara ili kubaini mapema endapo wana saratani na kuanza matibabu mapema kabla maradhi hayo hayajafikia hatua mbaya.
  Mwisho.Saratani ya mlango wa kizazi inavyowatesa wanawake wengi duniani


   
 2. Maarko

  Maarko JF-Expert Member

  #2
  Jul 28, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 1,030
  Likes Received: 189
  Trophy Points: 160
  Darasa lako zuri,endelea kutuelimsha. kwa mwanaume ambaye hajatahiriwa inakua vipi hadi kusababisha saratani hii,kwa uchafu au maumbile tu?
   
Loading...