Sangara wachanga 900 wakamatwa kwenye gati

Njowepo

JF-Expert Member
Feb 26, 2008
9,710
2,226
Na Mwandishi wetu
2nd November 2011
Kikosi cha Doria cha Idara ya Uvuvi mkoani Mwanza, kimekamata zaidi ya samaki wachanga 900 aina ya Sangara kwenye gati la kufikishia samaki katika Kiwanda cha kusindika minofu ya samaki cha Vicfish kilichojengwa kandokando ya ufukwe wa Ziwa Viktoria, jijini Mwanza.
Samaki hao ambao uzito wao haukuweza kufahamika mara moja, walikamatwa Oktoba 28, mwaka huu saa nne usiku muda mfupi baada ya boti ya wakala anayesambazia kiwanda hicho samaki kutia nanga kwenye gati hilo.
Mkuu wa Kikosi cha Doria cha Idara ya Uvuvi mkoani Mwanza, Juma Makongoro, alithibitisha kukamatwa kwa samaki hao wachanga kwenye gati hilo, lakini alikataa kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo kwa maelezo kuwa taarifa zaidi zingetolewa na Mkuu wake wa kazi, Angelus Mahatane.
Mahatane ambaye ni Afisa Uvuvi mkoani Mwanza hakuweza kupatikana ofisini ili kuzungumzia suala hilo na alipopigiwa simu ya mkononi iliita tu bila kupokelewa kwa muda mrefu.
Mkuu wa Maabara ya Ubora wa Samaki iliyopo Nyegezi jijini Mwanza aliyejitambulisha kwa jina moja la Lukanga, alipoulizwa alithibitisha kukamatwa kwa samaki hao kwenye gati la kufikishia samaki kiwandani hapo ambao wanaaminika kuwa walikuwa ni kwa ajili ya kuchakatwa.
Lukanga alisema kuwa samaki hao walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kulikuwa na boti ambayo ilikuwa ikitoka kwenye mojawapo ya visiwa vilivyopo katika Ziwa Viktoria kwa upande wa Tanzania ambayo ilikuwa imebeba shehena ya sangara wachanga kwa ajili ya kwenda kuwauza katika Kiwanda cha Vicfish jijini Mwanza usiku.
Alisema hadi juzi, taratibu zilikuwa zikifanyika ili kupata kibali kutoka mahakamani kwa ajili ya kugawa samaki hao katika baadhi ya shule au taasisi zingine ambazo zinahitaji msaada wa chakula kwa vile samaki hao hawana madhara kiafya na kwamba hatua zingine zingechukuliwa baadaye dhidi ya wahusika.
Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Viwanda vya Kusindika Minofu ya Samaki nchini (TIFPA), Alfred Xavier, alisema kuwa amepata taarifa juu ya kukamatwa kwa samaki wachanga kwenye gati la kufikishia samaki kiwandani hapo kutoka kwa baadhi ya watu na kwamba walikuwa wakisubiri taarifa kamili kutoka kwa Mkurugenzi wa Uvuvi nchini kwa ajili ya kuchuka hatua.
Xavier alisema kuwa ikibainika kwamba kiwanda cha kusindika minofu ya samaki kimekutwa na samaki wachanga mfano sangara ambao wako chini ya ukubwa wa sentimeta 50 hupewa adhabu ya kutosafirisha minofu ya samaki nje ya nchi kwa kipindi cha wiki moja na kwamba mhusika akirudia kosa hilo, adhabu ni kutosafirisha minofu ya samaki nje ya nchi kwa kipindi cha mwezi mmoja ambapo taarifa hizo hutolewa kwa wizara husika.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Vicfish, Murtza Alloo, alithibitisha samaki hao wachanga kukamatwa, lakini alisema amaki hao bado walikuwa ni mali ya wakala kwa vile walikuwa hawajapokelewa kiwandani.
Alloo alisema ili saamaki kuwa mali ya kiwanda ni pale ambapo tayari wanakuwa wamepokelewa na wameandaliwa kwa ajili ya kusindikwa.
Uchunguzi unaonyesha kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ,viwanda vya kusindika minofu ya samaki vilivyoko eneo la Kanda ya Ziwa vimekabiliwa na uhaba wa samaki, hali ambayo imesababisha viwanda mbalimbali kupunguza wafanyakazi kutokana na kupunguza shift.
Kwa mfano kiwanda ambacho awali kilikuwa kikiendesha shift tatu kwa siku sasa kinaendesha shift moja tu kutokana na uhaba wa samaki na hivyo kupunguza maelfu wafanyakazi wao.
CHANZO: NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni
MY TAKE
Kama mpaka viwanda vinapokea Sangara wachanga sasa wakija isha si watafunga Viwanda jamani
Ivyo viwanda ndo vingekuwa mstari wa mbele kukomesha uvuaji wa sangara wadogo for their sustainability ya Viwanda vyao na ukuaji wa hao sangara kwa kiwango kinachotakiwa
 
Back
Top Bottom