Sampuli ya ubongo wa wasanii bongo kama wapigakura wa ujima

Kingjr2

JF-Expert Member
Sep 8, 2018
644
1,271
Ameandika Luqman Maloto
Nami naiwasilisha kwako


SAMPULI YA UBONGO WA WASANII BONGO KAMA WAPIGAKURA WA UJIMA

NIGERIA ilifanya Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Muhammadu Buhari wa chama cha APC, alitetea kiti chake chia urais dhidi ya Atiku Abubakar wa PDP.

Kumbukumbu; masupastaa wawili wa Nigeria, Davido na Wizkid kila mmoja alitengeneza headline yake. Davido alijipambanua waziwazi kumuunga mkono Atiku na alifanya kampeni mtandaoni. Wizkid alikataa ofa ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya kushiriki kampeni za kisiasa.

Tuanze na Davido; ni mwana wa familia ya Adeleke. Ni koo yenye uzani mzuri kifedha na mamlaka kwenye jimbo la Osun, lililopo Kusini Magharibi ya Nigeria. Anko wake, Ademola Adeleke alikuwa seneta wa jimbo la Osun kuanzia mwaka 2017.

Kabla ya Ademola kuwa seneta wa Osun, kaka yake, Isiaka Adeleke (anko mwingine wa Davido), ndiye alikuwa seneta wa jimbo la Osun kwa vipindi viwili. Isiaka alipofariki dunia Aprili 23, 2017, ulipofanyika uchaguzi mdogo,i Ademola aligombea na kushinda.

Sasa, mwaka jana, Ademola alikuwa anagombea useneta kwa awamu nyingine kupitia chama cha PDP. Davido kwa kumpa sapoti anko wake, alifanya kampeni kumuombea kura. Na kwa vile Atiku alikuwa akigombea urais kupitia PDP, ikawa sababu ya Davido kumuombea kura na yeye.

Ni tafsiri kuwa Davido aliingia kufanya kampeni sio kwa sababu ya fedha, bali kwa kumuunga mkono anko wake. Davido aliingia kwenye mapambano ya kisiasa kwa ajili ya familia yake.

Tuje kwa Wizkid; kipindi cha uchaguzi Nigeria mwaka jana, top rapper wa Azikiwe-Land, Mi Abaga, alitoboa siri kuwa Wizkid alipewa ofa ya mamilioni ya fedha ili ashiriki kampeni za mmoja wa wagombea urais lakini alikataa.

Mi alisema kuwa Wizkid alikataa ofa yoyote ya kushiriki kampeni za uchaguzi kwa kile alichosimamia kwamba hakutaka kuwa na upande wowote kipindi cha uchaguzi ili kuwapa uhuru mashabiki wake kuchagua bila presha.

Katika kujazia nyama alichokisema, Mi alimtaja supastaa mwingine wa Nigeria, Olamide, kwamba alikuwepo kwenye kikao hicho ambacho Wizkid alikataa ofa hiyo ya mamilioni ya fedha. Alisema kuwa kikao kilihudhuriwa na wanamuziki wengine lakini hakuwataja kwa majina.

Ukiachana na alichokisema Mi, yeye mwenyewe Wizkid, mara kwa mara alitoa matamko kuwataka wananchi wa Nigeria kuwa kitu kimoja na kutogawanywa na hoja za wanasiasa.

Hiyo ndio akili ya Wizkid, kukataa upande wa kisiasa kwa sababu anajfahamu yeye ni mwanamuziki, ni msanii. Anapendwa na watu wa vyama vyote. Kwa nini awagawe?

Si kosa kwa msanii kugeukia siasa; kama Arnold Schwarzenegger aliyaweka kando maisha ya Hollywood, akagombea ugavana wa California kupitia chama cha Republican. Kisha, akawa gavana kwa mihula miwili yenye jumla ya miaka nane. Kuanzia mwaka 2003 mpaka 2011.

Yupo Sugu, Joseph Mbilinyi. Rapper na mmoja wa forefathers wa Bongo Fleva. Kwa mihula miwili amekuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini. Leseni ya kugombea ubunge aliipatia Chadema.

Supastaa wa Uganda, Bobi Wine. Robert Kyagulanyi. Ni mbunge sasa. Na kwa utafiti ndiye mwanasiasa wa upinzani anayepewa nafasi kubwa ya kumtikisa Rais aliye madarakani, Yoweri Museveni.

Orodha ni ndefu. Yupo galacha wa Nollywood, Desmond Elliot. Mwaka 2015 alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Surulere. Chama kilichompa tiketi ya kugombeq ni APC.

Tuna haja ya kutaja wote? Sioni sababu. Kimsingi, msanii kugeuka mwanasiasa sio kitu kibaya. Hata msanii kufanya kampeni za kisiasa kwa sababu ya kuamini mgombea ataleta matokeo anayoona yanafaa.

P Diddy, Jay Z na mastaa wengi weusi walimpigia kampeni Barack Obama mwaka 2008 ili awe Rais kwa kwanza mweusi Marekani. Wamarekani weusi walikuwa na kiu ya kuona taifa hilo linaongozwa na mtu mweusi.

Hawakufanya kampeni kwa utumwa wa fedha. Walipigania maono yao. Hicho ndicho wasanii wanapaswa kusimamia. Sio kupanda majukwaani kupigia kampeni watu ambao hata hawawaamini.

Msanii anapanda jukwaani kuburudisha kwenye kampeni za mgombea ambaye hata yeye binafsi hamkubali, lakini anafanya hivyo kwa sababu ya pesa. Hiyo ndio sampuli ya wasanii wa Tanzania.

Huu ni mwaka wa uchaguzi, kila msanii anawaza majukwaa ya kisiasa kwa fedha. Hawazi mustakabali wa taifa. Hao ndio wasanii wetu.

Mwaka 2015, Diamond Platnumz, alipanda jukwaani Arusha, Sheikh Amri Abed Stadium, kutumbuiza wakati Edward Lowassa alipotangaza nia ya kugombea urais. Kisha, wakati wa kampeni alimpigia debe Rais John Magufuli aliyekuwa anapambana na Lowassa. Ni fedha tu.

Wasanii wa Tanzania walitia fora mwaka 2015. Walipanda jukwaani kuwapigia kura wagombea waliokuwa wanashindana na wasanii wenzao. Ilitokea Mikumi kwa Profesa Jay, vilevile Mbeya Mjini kwa Sugu.

Mwaka 2015, wasanii kama Juma Nature, Ray Kigosi, Aunty Ezekiel na wengine, walipewa hela wakawa upande wa Lowassa, yaani Chadema na Ukawa. Badaye wakapandiwa dau, wakageukia kwa Magufuli, kwa maana ya CCM. Ni kwa sababu wasanii wetu hawana misingi. Uoga na fedha ndivyo vinaendesha akili zao. Wanavyoishi utadhani ni wasanii wasio na sababu yoyote katika sanaa wanayoitumikia.

Mwaka huu, wasanii wanapaswa kujiheshimu. Wasipelekeshwe na fedha wala hofu. Wanatakiwa kutumia sanaa zao kuwaunganisha watu. Wasanii kutumika kisiasa ni matokeo ya kuwa na sanaa bila misingi. Na sanaa bila misingi ni janga.

Yupo wapi Marlaw ambaye aliigeuza hit song yake ya Pii Pii (Missing My Baby) kuwa wimbo wa kampeni Uchaguzi Mkuu 2010. Baada ya hapo alipotea mazima. Sasa hivi wasanii kila mtu yupo bize kuandika nyimbo za kampeni. Wajitazame sana. Wanazingua bigtime na hivyo vinyimbo vyao vya kampeni. Vinyimbo vya kujikomba.o

Unajua nini? Wasanii wa Bongo huu ni muda wa kutumika. Watasimama majukwaani kukata mauno, kupiga kelele kwenye majukwaa ya wanasiasa, watawakwaza mashabiki wao, watapewa pesa na kuona maisha wameyapatia. Baada ya uchaguzi watatelekezwa. Shida zao zitabaki palepale.

Mwaka 2025 ukiwadia, watatumika tena kwenye kampeni na watachekelea. Wataona maisha ni poa. Watatunga na kuimba nyimbo nyingine. Shida zao zitakuwa ni zilezile zinazowafanya wabaki maskini hadi kutegemea kampeni za uchaguzi.

Wasanii Bongo wapo kama wapiga kura enzi za ujima, baada ya uchaguzi, wanatelekezwa. Hawakumbukwi. Changamoto zao hazitatuliwi. Wanabaki maskini. Uchaguzi mwingine ukifika, wanapewa ‘vijihela’, fulana na kofia, au hata chakula. Kisha wanasahau na kupiga kura kwa walewale waliowasahau na kuwatelekeza, kisa wamepewa sahani ya wali na maharage.

Wasanii hebu jifunzeni kujiheshimu. Lindeni thamani yenu.

Ndimi Luqman MALOTO
 
Unajikanganya, at the same time unasema sio vibaya wasanii kuwa wanasiasa muda huo huo unatoa maoni wasishiriki kwenye kampeni.

Waache wasanii wapige hela, huo ndio muda pesa za kampeni zipo nje nje,pia hata wasanii wana haki na uhuru wa kumpigia mtu yeyote kampeni kama walivyokuwa watu wa sekta nyingine.

Unasema Marlaw kapotea kisa kampeni, Mbona Diamond hapotei na alianza kumpigia kampeni J.K 2010, akaja kwa J.P.M 2015?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kingjr2,

Hata sis wa mitandaon wengine hatujui hata itikadi mirengo wala sera ya vyama vyetu lkn tunashabikia kinoma noma, inabid tujitathmin bandugu.
 
Back
Top Bottom