Samia aagiza kuundwa kamati za mazingira

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wananchi katika ngazi zote kuunda kamati ndogo za mazingira zitakazosimamia sheria ndogo za mazingira na utunzaji wa misitu ili kulinda na kuokoa vyanzo ya maji.

Amewataka wananchi kwa utashi wao kuhakikisha katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani wanashiriki kikamilifu katika kusimamia na kuhakikisha vyanzo vya maji vinahifadhiwa ili binadamu na wanyamapori waishi.

“Nielekeze kuwa, kamati za mazingira katika ngazi za vijiji, vitongoji, mitaa, kata na wilaya ambazo sheria ya mazingira imeelekeza ziwepo, zianzishwe au zifufuliwe na zichukue nafasi ya kutambua na kusimamia vyanzo vya maji vilivyopo,” alisisitiza Samia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika duniani kote jana, alisema kazi nyingine ya kamati hizo ndogo ni kuhakikisha pia inafufua vyanzo vya maji vilivyoharibiwa kwa kuvihifadhi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika kuadhimisha siku hiyo nchini kaulimbiu ya Tanzania ni ‘tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu’. “Maji ni uhai wa viumbe vyote akiwemo binadamu, wanyamapori, mimea na ni uhai wa uchumi wa taifa.”

Kutokana na ukweli huo, Tanzania imeamua kuwa na kaulimbiu hiyo kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira hususan vyanzo vya maji kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, uchimbaji wa madini na matumizi ya nishati.

Alisema hali hiyo imesababisha kuwepo na upungufu wa mtitiriko wa maji katika mito mingi nchini takribani kwa kipindi cha miongo mitano iliyopita na baadhi ya mito imebadilika na kuwa ya msimu, kuchafuliwa sana na mingine kukauka.

“Tukiendelea na mwenendo huu wa uharibifu wa vyanzo vya maji, mito yetu mikuu hapa nchini kama vile Rufiji, Pangani, Ruaha na mingineyo inayotegemewa sana kwa uhai na ustawi wa Watanzania wengi, itakauka ndani ya miaka 15 ijayo,” alisisitiza.

Akizungumzia maadhimisho ya siku hiyo duniani, alisema kimataifa yanaadhimishwa nchini Angola yakiwa yamebeba kaulimbiu ‘go wild for life save the environment’ inayokumbusha umuhimu wa kuchukua hatua za makusudi kulinda maisha ya wanyamapori.

Kihistoria siku ya mazingira ilianzia mwaka 1972 wakati Baraza la Umoja wa Mataifa lilipopitisha maamuzi ya kuanzishwa kwake kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo Endelevu uliofanyika jijini Stockholm nchini Sweden.
 
Back
Top Bottom