Samaki wa Japan sasa ruksa kuliwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,112
WATAALAM wa Afya wa Afrika Kusini wamesema samaki walioingizwa nchini kutoka Japani na baadaye kuzuiwa wasisambazwe wa hofu ya kuwa na mionzi inayoweza kuathiri afya za watu, ni salama.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA), Hiiti Sillo, jana alithibitisha kupokea ripoti ya wataalamu hao na kwamba sasa amaki hao waendelee kusambazwa ili waliwe.

Akizungumzia sampuli ya samaki hao iliyokuwa imepelekwa nje ya nchi na serikali ili kujiridhisha kuhusu usalama wake ilisema ilipelekwa katika maabara ya Afrika Kusini ambayo ina ithibati katika uchunguzi wa mionzi ya nyuklia.

“Sampuli hizo zilipokelewa na maabara hiyo Agosti 25 mwaka huu na kufanyiwa uchunguzi.Matokeo ya uchunguzi yalipatikana Septemba 5 mwaka huu na yanaonyesha kuwa samaki hao hawajachafuliwa na mionzi ya nyuklia, kwa hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu,” alisema.

Julai 24 mwaka huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilitoa taarifa kwa umma juu ya samaki hao waliokuwa wanahisiwa kuchafuliwa kwa mionzi ya nyuklia. Kufuatia taarifa hiyo, Julai 23 mwaka huu serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, iliiagiza TFDA kufanya ukaguzi na kuhakikisha kuwa samaki hao walioingizwa nchini na Kampuni ya Alphakrust ya jijini Dar es Salaam, wanazuiliwa ili wasitumiwe.
Mpaka kufikia Agosti 2, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Idara za Afya mkoani Dar es Salaam na Morogoro na Jeshi la Polisi walikamata na kuzuia tani 123.908 za samaki hao.

Akizungumza kwa msisitizo Sillo alisema baada ya kupata taarifa hizo, mamlaka ilikagua nyaraka mbalimbali zilizoambatana na shehena ya samaki hao kwa kufanya mawasiliano na Idara ya Uvuvi, Kamisheni ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Kimataifa ya Japan.
“Tathmini hiyo ilithibitisha kwamba samaki hao waliingizwa kwa kuzingatia sheria na taratibu,” alisema Sillo. Alisema Julai 25 mamlaka ilichukua sampuli za samaki hao na kufanyiwa uchunguzi katika maabara ya Kamisheni ya Nguvu za Atomiki Tanzania.

“Matokeo yalipatikana Agosti 29 na yalionyesha kuwa samaki hawana tatizo lolote na salama kwa matumizi ya binadamu, majibu hayo yalifanana na uchunguzi wa awali wa sampuli za samaki hao uliofanywa na taasisi hii na yale yaliyotolewa na Shirika la Ukaguzi wa Vyakula la Japan,” alisema Sillo.
Alisema kuwa uchunguzi huo wa kimaabara uliofanyika Afrika Kusini umezingatia viwango vya kimataifa vinavyotolewa na taasisi ya kimataifa inayohusika na kuandaa viwango vya vyakula iliyo chini ya Shirika la Afya Duniani(WHO) na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO).

“Kwa matokeo ya uchunguzi huu tunapenda kuwafahamisha Watanzania kwamba samaki aina ya Marckerel walioingizwa nchini kutoka Japan wako salama kwa matumizi ya binadamu,” alisema Sillo. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Hosea Mbilinyi, alisema serikali haitaacha kuagiza samaki kutoka nje kwa kuwa wanaovuliwa nchini hawatoshelezi.

Alisema uvuvi haramu ndio chanzo cha kutotosha kwa samaki hao kwa kuwa aina hiyo ya uvuvi inatokomeza mazalia ya samaki na kuwaua samaki wadogo. “Takwimu zinaonyesha kwamba samaki wanaovuliwa nchini ni 350,000, lakini kuna upotevu wa asilimia 10 hadi 40 ya samaki hao kutokana na kuharibika kunakosababishwa na kuwahifadhi vibaya, pia mabadiliko ya hali ya hewa nayo ni moja ya sababu,” alisema Mbilinyi. Alisema hapa nchini kuna mahitaji makubwa ya samaki kuliko uzalishaji, huku akifafanua kuwa uhaba wa vifaa vya uvuvi ni moja ya sababu ya kutotosheleza kwa samaki nchini.

Alisema kuwa serikali itaendelea na doria katika maeneo ambayo uvuvi haramu hufanywa kwa kiwango kikubwa ili kuokoa upotevu wa samaki. Katika hatua nyingine Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Alphakrust, Ganeshan Vedagiri alisema pamoja na hasara waliyopata ya kukaa bila kufanya biashara kwa siku 49, wameisamehe serikali.

“Hii kazi ya kupima hizi samaki ingeweza kufanyika kwa dakika 30 tu, lakini imetumia muda mrefu sana, labda ilitokana na msukumo wa Wabunge, watu huko mitaani na vyombo vya habari,” alisema Vedagiri, ”Tumepata hasara kubwa lakini sitaki hata kuifikiria au kuijua, jina letu limechafuka lakini mwisho wa siku tunajua siku zote siyo Jumapili na tumesamehe tunaelewa kuwa hii ni sehemu ya biashara.”

chanzo: Gazeti la Mwananchi
 
Back
Top Bottom