Salva Rweyemamu ajikanganya kuhusu Rais Kikwete | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Salva Rweyemamu ajikanganya kuhusu Rais Kikwete

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Fidel80, Mar 6, 2009.

 1. Fidel80

  Fidel80 JF-Expert Member

  #1
  Mar 6, 2009
  Joined: May 3, 2008
  Messages: 21,976
  Likes Received: 104
  Trophy Points: 145
  MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu jana alitoa taarifa inayoonyesha kujikanganya kuhusu makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha ufuatiliaji wa utendaji baina ya Rais Jakaya Kikwete na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake.


  Akizungumza na waandishi wa habari jana, Salva alizungumzia habari iliyoandikwa na Mwananchi kuhusu makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha Rais na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake, akisema kuwa habari hiyo ilipotoshwa, huku akionyesha kuchukizwa na habari zilizowapa wapinzani haki yao ya kidemokrasia ya kutoa maoni yao kuhusu hotuba za rais wao.


  Salva, mwandishi wa zamani wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo na baadaye Dimba na Rai, alidai gazeti la Mwananchi liliandika habari inayoonyesha kuwa "Mhe. Rais Kikwete amejiingiza kwenye suala la ununuzi wa mitambo ya umeme ya Dowans".


  Sakata hilo la Dowans linahusu mvutano uliopo baina ya serikali na moja ya kamati za bunge ambayo imeishauri mitambo hiyo ya ufuaji umeme wa dharura isinunuliwa kwa vile kufanya hivyo ni kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, wakati Wizara ya Nishati na Madini ikisisitiza kuwa mitambo hiyo ya mitumba ni mizuri na inafaa kukabiliana na tatizo la upungufu wa umeme linalobashiriwa kutokea.


  "Gazeti la Mwananchi la leo, Jumatano Machi 4, 2009 limeandika habari zenye kichwa cha habari: 'Kikwete ajitosa sakata la umeme" kikifuatiwa na habari inayoonyesha kuwa Mhe. Rais Kikwete amejiingiza katika suala la ununuzi wa mitambo ya umeme ya Dowans," alisema Salva katika mkutano wake na waandishi wa habari.


  "Mwananchi limeandika habari hiyo, kama ilivyofanywa na vyombo vingine vyote vya habari, kutokana na taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais kufuatia kikao cha jana (juzi) cha tathmini ya utendaji wa serikali kati ya Rais Kikwete na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake.


  "Vyombo vingine vyote vimeripoti habari hii kwa usahihi kama ilivyotolewa," ameandika Salva katika taarifa yake. Hata hivyo, vyombo vingi vya habari havikuripoti habari hiyo zaidi ya gazeti la Mwananchi, Uhuru na televisheni ya TBC1.


  Salva, huku akikiri katika taarifa yake kuwa Mwananchi haikumuhusisha rais na suala la mitambo ya Dowans kutokana na maelezo yaliyo kwenye aya ya pili ya habari hiyo, anaendelea kudai kuwa "Mwananchi imesema uongo kwa kupindisha ukweli na kupotosha habari iliyotolewa (na kurugenzi yake)".


  Salva anasema: "Huu ni upotoshaji wa makusudi ambao shabaha yake inajulikana kwa gazeti la Mwananchi peke yake. Ni uchochezi tu wa kumwingiza Mhe. Rais katika suala ambalo hahusiki nalo kabisa. Suala la Dowans halikujadiliwa kabisa katika kikao."


  Hata hivyo, Mwananchi ilieleza kuwa taarifa ya mwandishi huyo mkongwe ilieleza bayana kuwa kikao hicho hakikuzungumzia suala la Dowans, ambalo limesababisha mtafaruku baina ya kamati za bunge za Nishati na Madini na ile ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma.


  Katika aya ya kwanza ya habari hiyo, Mwananchi iliandika "Rais Jakaya Kikwete ameondoa utata katika mjadala wa utekelezwaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma alipoeleza kuwa sheria hiyo 'isiwe kikwazo katika miradi mikubwa ya miundo mbinu ya nishati' katika kipindi ambacho suala la ununuzi wa mitambo ya ufuaji umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited limekuwa gumzo kubwa", ikibainisha kuwa rais amejitosa kwenye suala la umeme na si mjadala wa mitambo ya Dowans.


  Katika aya hiyo ya pili, Mwananchi iliandika kwa umakini ikisema kuwa "taarifa kuhusu makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha ufuatiliaji baina ya Rais Kikwete na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake, haikutaja mitambo ya Dowans kuwa sehemu ya mambo yaliyojadiliwa", jambo ambalo Salva amelipindisha kwa kudai kuwa Mwananchi ilimuhusisha Rais Kikwete.


  Salva, ambaye kampuni yao ya ubia ya G&S Media Consult ilikuwa mshauri wa masuala ya habari wa kampuni tata ya Richmond Development Company iliyorithisha mkataba wa ufuaji umeme wa dharura kwa Dowans, alihoji katika taarifa yake ya jana kuwa kama Mwananchi linajua ukweli kuwa suala la Dowans halikujadiliwa katika kikao hicho, "limepata wapi habari za kumuhusisha rais na suala zima la mitambo ya umeme ya Dowans".


  Hata hivyo, kipengele D cha taarifa hiyo ya juzi ya Salva aliyoituma gazeti la Mwananchi baada ya kikao hicho cha Rais Kikwete na Wizara ya Nishati na Madini inasema: ""Kwamba ziongezwe juhudi katika uzalishaji wa umeme nchini kwa sababu programu ya taifa ya uzalishaji umeme bado iko nyuma na bado liko pengo kubwa kati ya mahitaji halisi ya umeme nchini na umeme unaozalishwa kwa sasa.


  Pia, kipengele E cha taarifa hiyo ya Salva kuhusu makubaliano hayo kinaeleza: "Kwamba dhana ya tenda na sheria ya manunuzi isiruhusiwe kuwa kikwazo katika miradi mikubwa mikubwa ya miundo mbinu ya nishati, hasa ile ambako wawekezaji wanajitokeza wenyewe kuwekeza katika maeneo ambako taifa linahitaji uwekezaji mkubwa na wa haraka na ambako nchi inaonekana imechelewa kuwekeza."


  Mwananchi iliripoti kuwa kauli ya Rais Kikwete kutaka Sheria ya Manunuzi ya Umma isiwe kikwazo katika miradi mikubwa ya miundo mbinu, imekuja wakati kukiwa na mjadala mkubwa kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans, ambayo imekataliwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria hiyo, jambo ambalo Salva amelitafsiri kuwa ni kumuhusisha rais na sakata la Dowans.


  Salva pia amerejea habari nne ambazo anadai kuwa zinathibitisha kitu alichokiita ukweli kuwa Mwananchi imebobea kupotosha kwa makusudi kwa sababu ambazo inazijua.


  Miongoni mwa habari hizo ni ile aliyoiandika Salva mwenyewe na kuituma Mwananchi wakati Rais Kikwete alipohutubia kisiwani Pemba, ambako aliwaambia wananchi kuwa wabunge hawajashika madaraka hivyo hawawezi kuwasaidia kutatua matatizo yao kwa kuwa wapinzani watachelewa na pengine hawataweza kushika madaraka, habari ambayo Mwananchi iliipa kichwa cha habari kisemacho: "Kikwete achafua hali ya siasa Zanzibar."


  Pia Salva amenukuu habari ya Januari 24, 2009 iliyokariri maoni ya viongozi wa upinzani kuhusu kauli hiyo ya Kikwete, mmoja wao wakisema kuwa "Kikwete anamaanisha serikali itaendelea kuwekwa na wao... Wazanzibari hawana haki ya kujichagulia rais wanayemtaka, bali CCM na serikali ndiyo itawachagulia rais wa kuwaongoza... basi sasa tusubiri tuone".


  Salva pia amechukizwa na habari ya Mwananchi iliyokariri viongozi wa upinzani baada ya hotuba ya Rais Kikwete ya Mwaka Mpya alipozungumzia umuhimu wa kulinda amani na utulivu waliposema tahadhari hiyo ilikuwa tishio.


  Dowans imekuwa ni suala tete ambalo linagonga vichwa vya vyombo vya habari nchini, kutokana na mvutano miongoni mwa wabunge wa kamati mbili pia kati ya bunge na serikali.


  Tayari Kamati ya Nishati na Madini chini ya mbunge wa Bumbuli William Shelukindo imepinga ununuzi wa mitambo hiyo huku Kamati ya Mashirika ya Umma, chini ya mbunge wa Kigoma kaskazini Zitto Kabwe, ikipigia debe ununuzi wa mitambo ya mitumba ya Dowans.
  source;mwananchi
   
 2. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #2
  Mar 6, 2009
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 24,566
  Likes Received: 18,527
  Trophy Points: 280
  Salva ni mwanahabari mahiri na ana uzoefu wa muda mrefu katika medani za habari. Nadhani msingi wa teuzi yake kuongoza Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ilitokana na kazi 'nzuri' iliyofanywa na gazeti lake la Mtanzania wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM.

  Kufuatia kazi hiyo, na ile ya PR ya Richmond, Mkulu akaamini jamaa ni bingwa wa PR hivyo akamleta jikoni. Nimetokea kuona akiitisha press conference ni kulalamikia magazeti ambayo hayamripoti vizuri Mkulu. Kwa wanaojua newsroom politics ni kuwa 'Kichaa Kapewa Rungu'.

  Hata ile issue ya Mwanahalisi, ni Mkulu alikasirika, Salva akapiga Tarumbeta, Mkuchika aweweseka na kupiga jaramba. Ilikuwa ni issue ndogo tuu ya Salva kumweleza Mkulu kuwa kwa mujibu wa katiba ya nchi na ya chama chake inaeleza wazi mwisho wa utawala wake ni 2010. Kueleza Kikwete mwisho wake 2010 kuna kosa gani?. Katiba ya CCM pia inatamka wazi 2010 ni mwisho wake ila atalazimika kuomba tena na chama kimpitishe. Pamoja na utaratibu wa CCM, rais aliyemaliza kipindi kimoja atapewa upendeleo, huu ni utaratibu tuu na sio katiba, hivyo hakuna kosa mwanaCCM yoyote kumpinga. Kubenea kusema kuna mpango wa kumpinga, kuna kosa gani?. Kwenye hili Salva ameonyesha udhaifu na hili la mwananchi pia ni udhaifu mwingine.

  Sisi tumetawaliwa na Wakoloni Waingereza mpaka waandishi wetu wanaandika kukloni mwingereza. Wakitakiwa kuripoti kile tuu kilichosemwa bila analysis wala opinion.

  Wamarekani wameenda mbali zaidi kwa mwandishi zaidi ya kuzisema zile 5 Ws and H, za Who, What, When, Where, Why and How, Mmarekani anazama zaidi 'So what, what does that mean and with what effect'.

  Hiyo kauli ya Rais 'tusifungwe na sheria ya manunuzi katika miradi mikubwa ya umeme na vipindi vya dharura ilitolewa wakati huu wa mjadala wa Dowans ili iweje?. mwananchi wameenda deep zaidi kwa kuelezea kauli hiyo what does it means and with what effects.

  Alichotakiwa kufanya Salva sio tuu kuiblast Mwananchi, bali alitakiwa afafanue hiyo kauli ya rais iliyonukuliwa ilikuwa na maana gani.

  Waandishi wetu wengi ni 'parrot journalist' ambao hawana uwezo wa kunyambua kauli za viongozi, wao ni kuripoti tuu kilichosemwa kama kasuku.

  Hata hivyo sio kosa la Salva, ndio majournalist wetu wengi walivyo, tena Salva ana bahati, kuna kichwa Premi Kibanga kiko chini yake. Premi akiwa BBC, alikuwa moto wa kuotea mbali, kaingia Ikulu, kamwagiwa maji, amepoa na kuwa baridi.

  Tuangalie na upande wa pili, tusije mlaumu bure Salva, kumbe anaamrishwa tuu na kutekeleza amri, kumbe hivyo ndivyo anavyotaka Mkulu mwenyewe.
   
 3. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #3
  Mar 6, 2009
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,633
  Trophy Points: 280

  Mkuu Pasco heshima mbele.
  Kwa kweli hata mimi nimeshindwa kabisa kumwelewa Salva alichokuwa anakikataa.Nadhani Salva bado anafikiri watanzania ni wavivu wa kupambanua mambo.Akubali mkulu kachemka kukimbilia kubwabwaja bila kufanya utafiti wa kutosha.
   
 4. k

  kela72 Senior Member

  #4
  Mar 7, 2009
  Joined: May 5, 2008
  Messages: 168
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Jamani.. JK + Rostam= Richmond & Dowans
  Salva anajaribu kutuzuga tu, JK nae yumo, baasi tu kina Mwakyembe wanatibua.
   
Loading...