Salum Mwalimu: Leo nimetimiza miaka miwili tokea nichaguliwe kuwa Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Zanzibar

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Leo nimetimiza miaka miwili tangu nichaguliwe kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar.

Ni tarahe kama ya leo Septemba 15, 2014 katika ukumbi wa Mlimani City jijijini Dar salaam sauti ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama chetu cha Chadema Freeman Mbowe ilipotangaza jina langu mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu kama mteule wa kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Ilikuwa ni jambo la kushtukiza mno miongoni mwa wengi kwani hawakuweza kubashiri jina langu kwani sikuwa kiongozi wa ngazi yoyote na wala sikuwa maarufu katika siasa za Zanzibar na duru za Chadema visiwani humo.

Jina la Salum Mwalim liliwasilishwa mbele ya wajumbe kwa lengo la kukubali au kukataa, kama ilivyokuwa kwa pacha wangu John Mnyika yeye akiwa mteule wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara.

Punde mara baada ya kuwasilishwa kwa jina hilo na Mwenyekiti Mbowe kuelezea wasifu wangu nilipewa fursa ya kujieleza mbele ya wajumbe kwa lengo la kuomba kura. Nilifanya hivyo na muda mchache baadae kura zikapigwa na pendekezo kuungwa mkono kwa kura zote za wajumbe waliokuwepo ukumbini. Hapo safari ya maisha mapya ikaanza (from corporate to politics)

Sina sababu ya kuzungumza kwa kina juu ya namna nilivyopokea pendekezo la kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, ila itoshe kusema haikuwa rahisi kwangu hata kidogo sio kwamba sikuwa nakipenda chama changu bali nilijihisi kutotosha katika nafasi hiyo nikitambua ukubwa wa chama chetu na unyeti wa nafasi hiyo, wachache niliowashirikisha katika jambo hilo wanaweza kuelezea hali ilivyokuwa, ilinibidi kuongeza sala na maombi nikimwomba Mungu aniongoze katika kulipokea jambo hilo, mwisho wa yote nilijikuta nikiwa Naibu Katibu Mkuu na historia mpya maisha yangu kisiasa kuanza.

Uamuzi huo umeacha kumbukumbu kubwa katika maisha yangu kwamba uamuzi huo ambao baadae ulifuatiwa na maamuzi mengine ikiwemo kuacha kazi katika kampuni ya Vodam kuwa ndio uamuzi mgumu zaidi kuwahi kuchukua katika maisha yangu na sitarajii kama litatokea jambo kubwa zaidi litakalonipa wakati mgumu kuliamulia maishani kwangu kuzidi hilo.

Nitumie siku hii ya kumbukumbu kuzungumzia angalau kwa uchache safari ya miaka miwili, iliyojaa changamoto za kila aina, furaha na mafanikio. Aidha nitumie pia fursa hii kutoa shukrani zangu.

Nimshukuru sana Mwenyekiti Mbowe kwa imani kubwa aliyokuwa nayo juu yangu hadi kuniamini kuwa chaguo lake katika nafasi hiyo kubwa ya kiutendaji katika chama chetu. Imani hiyo ya Mwenyekiti ilibadili mahusiano yetu kutoka marafiki, kaka na sasa kuwa mtu na "boss" wake. Naamini haikuwa kazi rahisi kwake kuniona mimi miongoni mwa vijana wengi wenye uwezo na sifa za kunizidi mimi ndani ya chama hiki kutosha kushika nafasi hiyo, hivyo sina budi kumshukuru kwa heshima na imani hiyo. Nakushukuru sana.

Aidha, nimshukuru kipekee aliyekuwa Katibu Mkuu kwa wakati huo Dk. Willibrod Slaa kwa kukubali mimi niwe msaidizi wake, siamini kama angekuwa hanifahamu na asingekuwa na imani kwangu kama angekubali niwe msaidizi wake, kukubali kwake ni kielezo na uthibitisho tosha kwamba hakuwa na chembe ya mashaka ya kiwango cha kuwa na hofu na mimi kuwa msaidizi wake.

Hili limethibitishwa pia na imani yake kwangu kwa wakati wote tulipofanyakazi kwa pamoja kabla ya uamuzi wake wa kujiuzulu na kustaafu siasa, na utayari wake wa kunibeba,kunilea, kunifunza na kuniamini kunipa majukumu mbalimbali ya kiofisi na fursa ya kumshauri na kuamini mawazo na uwezo wangu ndio iliyonijengea nguzo imara ya mimi kujiamini na kujituma. Alinishika mkono na kunitia moyo kila wakati, Hata kama hauko nasi kwa sasa ila nakumbuka sana tulivyoishi kwa upendo kama familia ukitufunza na kutujenga mimi na pacha wangu Mnyika, katika hili kamwe sitokuwa mpofu wa fadhila kusahau mema yako kwangu. Popote ulipo, pokea shukran zangu za dhati baba.

Nimshukuru sana pacha wangu Mnyika kwa ushauri na mawazo wakati nikitafakari ombi la Mwenyekiti, nakushukuru pacha, Mungu azidi kukubariki na kutuweka wamoja kusukuma mbele chama chetu kwa masilahi mapana ya wananchi wanyonge na masikini wanaotutegema sisi kuwasemea,kuwapigania na kuwasimamia katika kupata haki zao.Upacha wetu, umri wetu, ujasiri na uthubutu wetu ni hazina kubwa kwa chama chetu na nchi yetu.

Nawashukuru wazazi wangu na ndugu zangu kwa miongozo yenu na kunitia moyo.Mlinikubalia kubeba dhamana hii ngumu ya uongozi, mlijua ugumu wake na hatari zake lakini hamkukubali kufungwa na uwoga, uchoyo na ubinafsi mliniruhusu niwatumikie wananchi na nchi yangu.

Nawashukuru marafiki zangu wa karibu walionitia moyo na kuniondolea hofu kwa kunieleza kwamba naweza nijaribu, ingawa haikuwa rahisi kwenu mwanzoni kukubali lakini baada ya tafakuri mlikuja kuwa chachu ya kipekee ya kunitia moyo na kunisukuma kwamba nisonge mbele, ninaweza. Nawashukuru sana tena sana, mmeendelea kuwa nguzo yangu muhimu, nazidi kuwaombea afya njema na mafanikio tele ili mzidi kuniombea na kunishauri vema.

Kamwe siwezi kuacha kuwashukuru kwa namna ya kipekee kabisa viongozi na wananchama wa Chadema Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Said Issa Mohammed kwa mahaba,imani na heshima kubwa waliyonayo juu yangu, wamekuwa watu wenye imani nami tangu siku ya kwanza, sitosahau walivyopokea kwa shangwe na bashasha uteuzi wangu, waliweka imani yao kubwa kwangu pasi na hofu yoyote, walinikubali na kunipokea kwa mikono miwili. Ikumbukwe wakati nateuliwa na kisha kuchaguliwa sikuwa nimewahi kushika nafasi yoyote ya kiuongozi ndani ya chama, wangeweza kukataa na kuwa na hoja lakini hawakufanya hivyo, waliniamini na kukubali kunipa heshima ya kuwaongoza, hii ni heshima kubwa. Ahsanteni sana.

Shukran hizi zimfiikie pia aliyekuwa akiishikilia nafasi hii kaka yangu Hamad Yusuf ambae kuletwa kwa jina langu na hatimae kuchaguliwa hakukumkera alinitakia heri na kunipa ushirikiano. Namshukuru yeye na iliyokuwa sekretarieti yake na watumishi wote wa ofisi ya Makao Makuu Zanzibar kwa wakati huo pamoja na waliokuwa wabunge wetu wa viti maalum kwa wakati huo kwa upande wa Zanzibar,kwa kunipokea na kunikaribisha vizuri ofisini.

Sina namna ya kuwalipa, kwani mwanzo mzuri mlionijengea ndio imekuwa nguzo imara ya utendaji wangu wa kazi, na umoja wetu, mnajua ninavyowapenda na kuwaheshimu, kamwe sitobadilika.

Sio rahisi kuwataja wote hapa ila ninawashukuru wote walioonesha imani yao kwangu wakati huo kunipokea,kuniamini,kunishauri,kuniongoza,kunisimamia kabla,wakati na baada ya kikao cha Baraza Kuu kwa wakati huo, nawashukuru wote.

Ni miaka miwili iliyojaa changamoto ambazo kwangu wakati wote napigana kuzigeuza kuwa fursa za kunifanya kuwa kiongozi bora zaidi.

Natambua ugumu wa majukumu,lakini wakati wote nimefanya kila lililondani ya uwezo wangu kutimiza majukumu yangu wakati wote na kuwa tayari kutumika mahali popote wakati wowote.

Aidha nimekuwa nikichukua hatua binafsi na kujiongeza kadiri Mungu anavyonijaalia katika kukitumikia chama chetu.

Ni kwa utamaduni huo wa kuheshimu majukumu yangu, maelekezo ninayopatiwa na chama na kwa kujiongeza binafsi leo ninapotimiza miaka miwili najiona mwenye uwezo zaidi, kujiamini zaidi, mzoefu zaidi, bora zaidi, jasiri zaidi kulinganisha miaka miwili iliyopita.

Ni imani yangu kwamba ni kutokana na utamaduni huo huo, nimejenga imani na upendo zaidi kwa kila mmoja ndani ya chama chetu na nje ya chama.

Mapenzi, heshima na imani ya wanachama wa chama hiki na viongozi wenzangu wa kila ngazi kuanzia siku ya ushindi wa kishindo katika Baraza Kuu ndio imekuwa chachu kubwa ya kujituma na kujitoa kwangu kwa hali na mali kukitumikia chama chetu, haikuwa rahisi hata kidogo kwangu kutumia muda mfupi wa takribani miezi sita tu ya kwanza ya uongozi wangu ndani ya chama kufanikiwa kufika takribani mikoa yote kwa kazi za ujenzi wa chama.

Nilisafiri usiku na mchana, kwenye mvua na jua wakati mwengine katika mazingira hatarishi ili kufika mijini na vijijini kushirikiana na viongozi wenzangu kukijenga chama, tulifungua misingi, kukaa vikao vya ndani,kufanya mikutano ya hadhara nk. Hii ilikuwa ni ahadi yangu wakati nikishukuru mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu baada ya kuchaguliwa rasmi kuwa sitokuwa mtu wa kukaa ofisini na badala yake tutakutana field kujenga chama, nimekuwa nikiishi kwa ahadi yangu hiyo.

Nawashukuru sana viongozi wenzangu wa ngazi mbalimbali kwa heshima yenu na ushirikiano wenu ulionifanya kuzoea majukumu yangu ndani ya muda mfupi na kufanikisha kazi za kukitumikia chama chetu kwa ufanisi.

Ni miaka miwili iliyonifikisha maeneo mbalimbali ikiwemo ya pembezoni kabisa mwa nchi yetu kufikisha ujumbe wa chama. Maeneo mengine nililazimika kujifunza ama kuzoe kwa haraka sana mila,desturi na tamaduni za wenyeji ili kazi ya uwasilishaji ujumbe wa chama ifanikiwe. Yapo maeneo kadhaa ambapo nimeacha kumbukumbu ya kuwa kiongozi wa kwanza wa kitaifa wa chama kufika maeneo hayo tangu kuanzishwa kwa chama chetu.

Ni hali hiyo ndio iliyokuwa ikinipa ari na nguvu ya kutowaza kulala na badala yake kuwa nanyi vijijini na mjini kukijenga chama chetu, wapo walionialika na kwengine nikifika kwa utaratibu wa kawaida wa ziara za viongozi, wote mlinipokea nilipofika katika maeneo yenu ya kazi na kunipa fursa ya kushiriki nanyi kukijenga chama.Ni kwa upendo na heshima yenu hiyo kwangu leo naweza kusimama mahali popote na nikajivunia kuwa nimewekeza nguvu na jasho langu katika chama, mngeninyima fursa na ushirikiano huo pengine hakuna mahali leo jina la Salum Mwalim lingefahamika katika medani za siasa, nawapenda sana na ahadi yangu kwenu ni kuzidisha ari na nguvu katika kuwatumikia bila woga.

Ni miaka miwili iliyonikutanisha na makundi mbalimbali ya watu wa sifa tofauti wenye hulka,ufahamu na mitazamo tofauti, lakini tumebakia wamoja tukiheshimiana, hatujatengana wala kuvunjiana heshima kutokana na nafasi zetu ama tofauti zetu, nimekuwa mnyenyekevu kwenu nanyi mmekuwa wenye kuniheshimu, rabsha za hapa na pale hazikukosekana kikubwa cha kujivunia tumebaki wamoja, tukiheshimiana na kushauriana, hii kwangu ni hatua nzuri ninapofikisha miaka miwili ya safari yangu kama kiongozi wa kisiasa.

Kama nilivyoshukuru, pia nichukue nafasi hii kuwaomba radhi wale wote ambao kwa namna moja ama nyengine huenda nimewakwaza, wanisamehe, wajue kama niliwahi kumkwaza mtu basi ni katika kutimiza wajibu kwa masilahi ya chama na si vinginevyo.

Ni miaka miwili ambayo nimeshuhudia nikibaki kuwa mwenye kuheshimu wakubwa na wadogo bila kujali vyeo, umri au vipato, nikikubali kukosolewa na kuheshimu mawazo na ushauri wa kila mmoja.

Miaka miwili licha ya changamoto na mazingira magumu ya kazi ya siasa , bado imenibakiza katika kuheshimu na kuthamini utu wa watu,kupenda watu,ushirikiano,heshima na nidhamu ya kazi zikinijengea marafiki wengi wanachama na viongozi wenzangu pamoja na wananchi kwa ujumla.

Ni miaka miwili iliyonipa fursa pana ya kutoa mchango wangu wa mawazo katika maendeleo ya chama chetu na watanzania kwa ujumla.

Ni miaka miwili iliyonipa fursa ya kukitumikia chama changu katika nafasi ya juu kabisa ya kiutendaji kwa zaidi ya miezi minane kama Kaimu Katibu Mkuu tena katika kipindi kigumu cha uchaguzi mkuu uliokuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa ndani na nje ya chama, hii ilikuwa ni bahati na fursa ya kipekee maishani mwangu, nimeingia katika vitabu vya historia ya chama.

Najua yapo niliyoyosimamia vema na yapo ambayo sikuyasimamia kwa kiwango cha kukidhi matarajio ya kila mmoja, lakini angalau ndani ya moyo wangu na hata mbele ya Muumba wangu naweza kujielezea kwa kujiamini kwamba nilitekeleza majukumu yangu kwa uaminifu na uadilifu mkubwa sana.

Namshukuru Mwenyekiti wa Taifa,Kamati Kuu ya Chama na hata Baraza Kuu kwa kuonesha imani yao tena kwangu kuniamini na kunipa fursa ya kukaimu nafasi hiyo hadi pale tulipoijaza rasmi.

Kamwe sitokuja kuisahau miezi hii minane katika maisha yangu, nilijifunza mengi katika siasa, nilikomazwa na "dhoruba" kali za kisiasa na nilifarijiwa na kutiwa moyo pia. Niliyavumilia na kuyapokea yote na kubaki nayo rohoni mwangu. Nilijipima na sina neno la shukrani kumpatia Mola wangu kwa namna alivyoniumba, alinipitisha katika kipindi kigumu lakini hakuniacha akanijaalia busara,hekima na ustahamilivu wa kisiasa kuniwezesha kukivuka salama kipindi hicho kigumu.
Ewe Mwenyezi Mungu nazidi kukushukuru.

Ni miaka miwili iliyonipeleka nami kusimama mbele ya majukwaa kuomba kura za utumushi wa watu katika jimbo la Kikwajuni Zanzibar wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, sikufanikiwa kuingia Bungeni, ila ni ukweli ulio wazi kuwa nimefanikiwa kuingia katika mioyo ya wakazi wa Kikwajuni na Zanzibar kwa ujumla na kubakia kuwa mtumishi wao. Nimefarijika sana kwa hatua hii, nawashukuru wanaKikwajuni wenzangu, mlinipokea mimi na chama changu mkapigana kufa na kupona tukishirikiana kwa hali na mali.

Mara baada ya uchaguzi ilikuwa ni miaka mitano kufikia uchaguzi mwengine, lakini tayari imekaribia kubakia minne,tutaimaliza na tutakutana tena na kwa mapenzi yake Mungu tutafika 2020 tukiwa na nguvu na afya njema, hatutorudi nyuma.

Ni miaka miwili ambayo bado imeniacha na deni kubwa sana la kukijenga chama chetu Zanzibar, najua kazi iliyombele yangu na viongozi wenzangu bado ni kubwa sana kufikia matarajio ya wengi, ila kwa kuwa sina tabia ya kukata tamaa nina imani tutafanikiwa.

Tumaini la mafanikio lililoanza kuchomoka Zanzibar kwa chama chetu, sina shaka taratibu litasambaa, nilianza na kazi ya kuimarisha umoja,mshikamano, upendo na kujenga mazingira ya kuaminiana miongini mwa wana Chadema na viongozi, kazi hii imeanza kutoa mafanikio makubwa, tumefanyakazi na wenzangu kupitia uchaguzi mkuu kukitangaza chama Zanzibar, hii nayo imezaa matunda na kututia moyo, tutaendelea na kazi ya kuboresha miundombinu ya chama, kujenga safu imara za uongozi ngazi zote kumudu kubuni na kusimamia programu mbalimbali za chama kwa lengo la kukiandaa chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu 2020, sina chembe ya hofu kwamba kwa kushirikiana na Makamu Mwenyekiti Zanzibar na wenzangu Makao Makuu Madogo Zanzibar,ofisi zetu za Kanda Unguja na Pemba, viongozi wenzangu wa mikoa,wilaya,majimbo,mabaraza na wadau wetu kazi hii tutaifanikisha, na kama ikitokea tukishindwa kuikamilisha kwa 100% ndani ya muda wetu wa uongozi basi angalau tuikamilishe kwa kiwango ambacho watakaotupokea vijiti vya uongozi wawe na kazi nyepesi ya kuikamilisha na kukifanya chama Zanzibar kuwa imara na bora.

Tutazidisha ushirikiano na wenzetu chini ya mwamvuli wa Ukawa hususan CUF kujenga upinzani wenye nguvu Zanzibar kusimamia haki,usawa na ustawi bora na endelevu wa jamii.

Ni miaka miwili niliyoihitimisha kwa kukaa gerezani kwa takribani wiki mbili sio kwa kosa la kubaka,kuiba au kuua bali kwa kosa la kuwa jasiri kudai haki,usawa na demokrasia katika nchi yangu. Nimekaa ndani kwa sababu niliamua kuitendea haki dhamana ya uongozi niliyoaminiwa na wanachama wenzangu, nilikataa uoga na hofu nikaamua kusimama imara kulinda heshima na haki ya wanachama na viongozi wenzangu na chama kwa ujumla.

Ni miaka miwili niliyoshuhudia nikikimbiwa na kuogopwa na baadhi ya marafiki na ndugu zangu wa karibu wengine wa muda mrefu kwa kuogopa kuonekana wapo karibu na kiongozi wa chama cha upinzani na hivyo kuhofia masilahi yao. Hili sikuliogopa na wala halikunirudisha nyuma,badala yake limeniongezea ari ya kufanya kazi ili kufikia ukombozi tunaoupigania, naamini ipo siku watakomboka kifikra na watatambua thamani ya kazi ninayoifanya.

Nawashukuru wote, ninapoangalia mbele yangu naona jambo moja tu, kuongeza juhudi na maarifa katika kupigania mabadiliko katika nchi yangu bila woga, kuendeleza upendo na heshima kwa kila mmoja ili kuweza kuitumikia vema dhamana ya uongozi niliyonayo, kuongeza uvumilivu na subira ya kisiasa ili kushinda lolote lenye lengo la kunikatisha tamaa na kunirudisha nyuma, kuongeza ushirikiano na kuendelea kuwa tayari kujifunza kwa wengine.

Mwisho wa yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunilinda,kunisimamia na kuniongoza katika shughuli zangu. Amenijaalia pumzi nguvu na afya njema kutimiza majukumu yangu.

Mimi si lolote si chochote bila yeye, ninayoyasema na kuyatenda iwe katika siasa na nje ya siasa ni kwa sababu yake, ninapoendelea na hii safari nakuomba unijaalie hekima,busara, uvumilivu na roho ya kupenda, kuheshimu na kuthamini watu.

Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie.

Nawapenda sana!

Salum Mwalim
Naibu Katibu Mkuu
Chadema Zanzibar
Alhamis Septemba 15, 2016
 
Safi sana kamanda Nina uhakika waziri WA propaganda hawezi andika hivi.
 
We mambo ya chadema hayakuhusu. Mandela alifungwa Peke yake . CCM mnakazi kweli mpaka mnafoji ID za Kijitonyama. Aibu kumbe namba haibagui kila moja anaisoma ahaaa ahaaa.

Huyo ndo aliyetelekezwa kule kijijini lumande na mjanja mbowe au nimwalimu mwingine...tanzania kuna vituko sana mtu ulitelekezwa peke yako ufe lumande afu leo bado unamsifia huyohuyo dah
 
Tamko koko reefu,halielezi kafanya kazi iliotukuka huko zanzibar
Kutoa pongezi kwa Dr Slaa,anaonesha anamkubali kuliko Mashinji
 
Huyo ndo aliyetelekezwa kule kijijini lumande na mjanja mbowe au nimwalimu mwingine...tanzania kuna vituko sana mtu ulitelekezwa peke yako ufe lumande afu leo bado unamsifia huyohuyo dah
Lumande ni kijiji gani huko kwenu.
 
Mapungufu yako,kwanza umeng'ang'ana Bara wakati assignment yako sana ni Zanzibar, pili hujielekezi katika kuinua na kuhamasisha watu kujiinua kiuchumi...kama wenzako umejielekeza kwenye ahadi za mabadiliko tuuuu...,Tatu inaonesha unaheshima ya woga kwa Mbowe na sidhani Kama akikosea unaweza kumkosoa ipasavyo. Jitahidi kuona hayopia otherwise uko nasiasa za kawaida So hongera! Nakutakia kheri ustaadhi
 
Ha ha ha katibu Zanzibar lakini harakati bara

Ni sawa umeoa halafu unalala kwa mchepuko
 
Salim mwalimu umerogwa wewe jitambue wenzio wanalipwa na mafisadi mapesa wewe unafungwa. Achana na Chama cha walaghai.
 
Nakupongeza kwa uandishi mzuri, hakika taaluma yako ya uandishi wa habari umeitendea haki. Nakupongeza kwa kuweza kusema ambayo watu wengine, wenye mioyo ya unafiki hawawezi kuyasema katika kipindi hiki; kumshukuru Dr. Slaa, aliyekuwa katibu mkuu wetu. Nakushukuru kwa kutojikweza, maana mara zote umeonyesha unyenyekevu na arifu katika katika kuonyesha uungwana, wa kutowadunisha wenzako ili upate sifa kuu. Tabia hii inatafsiriwa kama uungwana. Hogera sana.

Mwisho, nikuombe uongezee mafanikio yako na mafanikio ya chama chetu angalau kwa takwimu kidogo. Kwa mfano; 1. ulipata kura ngapi kutokana na wapiga kura wangani katika harakati zako za kutafuta ubunge huko Zanzibar;
2. Wakati unateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, wanachama wa CHADEMA Zanzibar walikuwa wangapi na sasa ni wangapi?
3. Kwa Tanzania nzima, tunao wanachama wangapi ukulinganisha na wakati ule unateliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu?

Ninakuomba kwa moyo mkujufu na wala hakuna chembe ya dhihaka katika moyo wangu. Ninajua thamani ya kazi yako na thamani yako mwneyewe, hivyo naamini hili ninaloliomba linawezekana.

Nawashauri viongozi wote wa CHADEMA kuanza sasa matumizi ya takwimu zaidi katika kufikia maamuzi makuu; iwe katika kuelezea mafanikio au matarajio.

Naomba ombi langu ulipe tafsiri chanya. Peoplesssssssssssssssss.
 
Hongera sana! Wote tulistuka tuliposikia jina lako! Tulishinda wote mtaani hatukuelewa kuwa tuna kiongozi mtaani kwetu tena mkubwa tu mwenye moyo w aujasiri! Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya mafanikio! Ila sijaona kumtaja mwenzi wako au sababu ni wa chama kilee? Tena Mbunge? Angalia wasije wakakuteka mawazo ukahama kambi! Pole kwa msuko suko wa UKUTA! Yatapita tu hayo ni kawaida kwenye siasa
 
Back
Top Bottom