Salome Binti aliyehatarisha maisha yangu, baada ya miaka 8 nimekutana naye tena

Jokajeusi

JF-Expert Member
Jun 1, 2018
6,305
10,580
Habari wakuu!

Wiki hii imebadilisha mpangilio mzima wa ratiba yangu kwa kuumaliza mwaka huu. Kisa na Mkasa ni kama ninavyoendelea kueleza hapo chini.

Mwaka 2012 nilikutana na Binti mmoja ambaye alijitambulisha kwa Jina la Salome, tulikutana Dar es salaam pale Mlimani City, kwenye ATM ya CRDB.
Alikuwa binti mzuri sana, sura yake haifanani na jamii ya binadamu labda kwa karibu ilikuwa inaukaribia uzuri wa malaika.

Macho yake yenye utukufu wa mahaba yaliyolegea kiasi yalinifanya nizidi kuamini yeye sio binadamu wa kawaida; nakiri, sijawahi kuona mwanamke mzuri kama yeye tangu kuzaliwa, sio kwenye magazeti, luninga au mitandao ya kijamii kote huko sijawahi kuona wala kuota ndoto kuwa kuna mwanamke mrembo kama alivyo Salome. Umbo lake refu kiasi, lililogawanyika lilizidisha hadhi na kiwango cha uzuri wake, sifikirii kama namtendea haki kwa maneno yoyote yale ya utukufu wa uzuri wake nitakayosema hivi leo, itoshe kusema, Salome ndiye mwanamke mzuri zaidi kuwahi tokea katika dunia hii.

Nilikuwa ni kijana mdogo tuu, kijana ambaye hata ndevu zilikuwa hazijaota, nikiwa ndio niko mwaka wa tatu pale UDSM, Kama mnavyojua, chuoni wapo warembo wa kila aina, na hakika kwa wakati nasoma, sifikirii kama kulikuwa na chuo chenye wanawake warembo kama kilivyokuwa chuo chetu. Jamani chuo chetu kilibarikiwa. Lakini licha ya kubarikiwa warembo wengi wa kila namna bado hakuna hata mmoja aliyeukaribia uzuri wa Salome. Natamani mdau wangu wa JF uimagine mwanamke mzuri uliyewahi kumuona alafu uzidishe mara kumi ya uzuri wake ndio angalau atafikia uzuri wa Salome, sasa nadhani utakuwa umepata mwanga hafifu kuhusiana na uzuri wa Salome.

Basi Bhana, kama walivyo vijana wengine, nikafikiri kuwa lazima nijitetee, lazima nitetee moyo wangu. Baada ya mrembo huyo kutoa pesa zake kwenye ATM, nikasema ngoja nimsemeshe walau kwa salamu, nikamsalimu, yeye hakuitikia hiyo ikauumiza moyo wangu, akanipita kwa kunikumba kidogo kwenye bega langu, kisha akaenda kwa hatua kama tano mimi nikiwa nimegeuka kumtazama, yeye akiwa amenipa mgongo; niseme tuu akili yangu ilikimbia kwa kasi sana mawazo mengi yakifukuzana na kuzunguka mithili ya vikaragosi vinavyozungushwaa na kimbunga. Kwa bahati, yule mrembo ambaye muda huo sifahamu jina lake, akageuka kunitazama, hiyo niliiona kama hisani nisiyoweza kuibeba.

Jambo la hatari likatokea, sijui niliwaza nini, nasemaa, sikufanya makusudi, sikukusudia mimi jamani Jokajeusi. Paaap! nikaenda na kumshika mkono kwa nguvu, huku nikitaka kupiga magoti, sikujua nilitaka kusemaje kama ningefanikiwa kupiga magoti, lakini haitasaidia kitu hata ningekuwa na chakusema kwani kwa upesi sana nilikamatwa kwa nguvu nyingi sana na watu nisiojua wametoka wapi.

Bila amri wala maelekezo yoyote watu wale walinipiga mitama ya haja, hapo nilishawatambua ni kina nani, kwani walikuwa wamevalia nguo za kijeshi na Dirii vifuani mwao za kuzuia risasi. Nikawa napiga kelele nikisemaa; mimi sio mwizi, sio mwizi jamani. Lakini hawakuwa na muda wa kunisikiliza, walichokuwa wakisema ni kuwa nilikuwa nataka nimuibie yule binti.Yule Binti alikuwa ameshaenda umbali kidogo wa hatua thelasini hivi mbele yake ilikuwa imesimama Cruiser V8 nyeusi yenye tinted, nikakokotwa kwa kuburuzwa huku nikipigwa mateke ya tumbo na kichwa. Sifahamu niliwezaje kuhimili mkong'oto ule kwani ulikuwa heavy sana. Watu walijaa wachukua habari, wapenda kushangaa, na wapita njia wasio na kazi.

Nikafikishwa mbele ya ile V8 tayari yule binti alikuwa keshaingia ndani ya gari mlango wa nyuma. Mlango wa gari ukafunguliwa kwani uilikuwa umefungwa, yule binti akawaambia wale watu waniache, na kweli wakaniacha. Hapo nikawa napumua kwa tabu damu zikitoka puani na mdomoni, nilikuwa kwenye hali mbaya sana. Nikiwa nimeangalia chini ya sakafu huku damu zitokazo puani na mdoni zikivuja na kudondoka pale chini.

Yule Mrembo akaniambia, "ulikuwa unataka nini wewe chokoraa"
Kama kuna kitu kilichoondoa maumivu ya vipigo vile basi ilikuwa sauti ya yule mrembo. Sauti yake ilikuwa kama sindano ya ganzi. Hapo nikiwa uso nimeuangaliza chini nikauionua polepole mpaka nilipogongana macho na yule Mrembo.

Tukatazamana kwa kitambo kama sekunde ishirini, akaniuliza kwa ukali ulikuwa unataka nini, kabla sijajibu nikasikia sauti za watu kutoka nyuma zikipiga kelele, achomwe! Achomwe! hawa ndio wezi wanaorudisha maendeleo ya watu.

Kusikia hivyo nikasema basii! Leo ndio siku yangu ya mwisho, nilijuta kwa kumshobokea mrembo yule. Tayari niliona muda mchache ujao nitakuwa moja ya wafu waliokufa kwa kuchomwa motoo! Masikini Jokajeusi.

Kusema nilikuwa nataka kumtongoza niliona ni jau na ingeonekana ni sababu ya uongo kwani kutongoza gani kule kwa kumvuta mtu mkono. Sasa nitajiteteaje, hapo nilikuwa nikifikiri.

Niliishia kusema mimi sio mwizi, basi akaniuliza kama sio mwizi ulikuwa unataka kufanya nini au kusema nini. Mrembo bado alikuwa ananisemesha kikamanda zaidi ya kikauzu. Nikamwambia ni jambo la siri, hivyo nisingeweza kusema mbele za watu wote wale. Baadaye nikatoa kitambulisho cha uanafunzi cha DARUSO, Yule mrembo akakichukua, akakisoma soma, kisha akampa mtu aliye mbele ya gari ambaye mimi sikumuona kwani vioo vilikuwa tinted.

Yule mrembo akanionea imani, akaagiza wale watu wanipakize kwenye gari ya nyuma, nikabebwa msobe msobe na kuingizwa kwenye gari aina ya Harrier tolea jipya, wengi huliita tako la Nyani. Hapo tukaondoka tukiwaacha watu wakilaani kitendo cha mimi kuondolewa pale kwani walikuwa washanunua na mafuta kabisa ya kunichoma.

Mwendo wa dakika kumi na tano tuliingia maeneo ya Mikocheni, gari niliyopandishwa ikiifuata ile V8 nyeusi. Tukaingia kwenye Geti kubwa ambapo ndani yake ilikuwepo nyumba ya ghorofa mbili, Nikashushwa kama kiroba, hapo nikiwa na wasiwasi sana, sikumbuki ni lini nilikuwa na woga kama ule. Kwwa mara ya kwanza nikamuona aliyekuwa siti ya mbele kwenye ile V8 nyeusi, alikuwa Baba wa makamo mwenye sura nyeusi isiyo na mzaha hata chembe, macho yake makavu yaliyoficha hila na ukatili wa siku nyingi yalinitazama kwa udadisi, huku yule mrembo akimtazama huyo Baba wa makamo. Wale watu wanne walionipiga kule Mlimani City nao walikuwa kimya nafikiri walikuwa wakisubiri amri. Mimi nilikuwa nimeshikwa kwa nguvu na vijana wawili wenye misuli nikiwa nimesimamishwa nikiwa nimetepeta, kama wasingekuwa wamenishikilia basi nisingeweza kusimama peke yangu.

Yule Baba akanisogelea uso wake ukiwa sentimeti chache kutoka ulipo uso wake, hapo nikayaona macho yake yakiwa yananikumbusha ukatili, ushenzi, na unyama wa mtu yule ambaye sikuwa namfahamu. Yule mrembo akamjia yule Baba, akamuita "Dady, let me speak at once with you" hapo nikajua yule ni Baba yake. Wakasogea pembeni wakaongea kama sekunde arobaini hivi kisha yule Baba akaagiza nipelekwe sehemu maalumu.

Basi nikachukuliwa mkukumkuku, huku nikigeuka nyuma mara kwa mara kumtazama yule mrembo ambaye hata hivyo naye alikuwa akinitazama, niliiona huruma machoni mwake nikasema angalau amenitazama kwa huruma. Basi nikaingizwa kwenye chumba kimoja hivi ambacho kipo katika nyumba nyingine iliyo nyuma ya ile ghorofa. Huko nikapewa mkong'oto raundi hii nikapoteza fahamu.

Sitaki kuhadithia sana nisije kuwachosha, mapenzi yetu yalizuka kama uyoga tuu shambani. Yule binti baadaye nikaja kumtambua anaitwa Salome, ni siku aliyonirudishia kitambulisho changu cha chuo ndipo alipojitambulisha. Ni siku hiyo hiyo ambayo aliniambia nimwambie nilichotaka kumwambia siku ile tulipokuwa pale ATM ya CRDB ya Mlimani City.
Hapo nipo ndani ya chumba cha mateka ikiwa ni siku ya pili, nikiwa napewa adhabu na msoto wa maana.

Nikamueleza kila kitu, nikamueleza namna ninavyojihisi moyoni mwangu, nikamueleza ninavyompenda, nikamueleza matamanio na matarajio yangu kwake endapo atanikubalia, muda nikisema hayo machozi yalikuwa yananitoka yakitiririka kwenye mashavu yenye damu zilizoganda tangu juzi. Salome akanionea huruma, naye machozi yakawa yanamtoka, tangu hapo penzi letu lilichipua kama majani wakati wa kiangazi. Alinikumbatia nikiwa nimeshakata tamaa ya kuishi, uhai ukanijia tena, akanibusu niliyekuwa na njaa ya siku mbili tumbo likashiba mapenzi yake.

Sasa salome akafanya mpango hatari wa kunitorosha usiku ule, nilishajua salome ni mtoto wa nani, na hata leo najua ni mtoto wa nani, simtaji jina kwani najua anaweza kuwa humu ndani.
Ilifika mida ya mchana kama saa nane hivi, salome kwa kuvizia akaniletea chakula na juisi ya kutengeneza, nikala kwa kufakamia kidogo nipaliwe. Baadaye Salome akaniambia nijiandae usiku atanitorosha, ashaniandalia namna ya kuondoka eneo lile yaani nyumbani kwao. Basi hofu niliyokuwa nayo nashindwa kuieleza, jina la Baba salome ni kubwa sana hapa nchini, nafasi yake ni kubwa mno, lakini maneno aliyonambia Salome ndio yalinifanya niwe na chaguo la kutoroshwa tuu, alinambia kuwa Baba yake hana huruma hata kidogo, hivyo iwe iwavyo lazima niuawe.

Basi Salome akaniaga akanambia kuwa anaenda kuweka mipango sawa, mimi nisiwe na hofu kila kitu kitakuwa sawa. Basi akaniacha mimi nikiwa mwingi wa mawazo. Hapo nikafikiri muda ule ningekuwa zangu Chuo kwenye discussion, nikakumbuka kuwa siku ya jana tulikuwa na test chuoni, hayo yote yalinifanya nijute sana, sasa niliona nimeingia kwenye mkondo mbaya wa majanga katika maisha yangu.

Mida ya saa kumi na nusu Baba yake Salome alikuja akiwa na wanaume wawili wapya kabisa tofauti na wale wa ile siku, Baba Salome alikuwa amefaa kinyumbani kabisa, alikuwa kavaa bukta nyepesi na sinlendi juu, wale watu wawili wao walivalia kaunda suti za dark bluu na miwani.

Baba Salome, akaniambia kuwa, nimejiingiza kwenye shimo la mashetani yenye kiu ya damu, hafikirii kama nitatoka salama. Aliongea sauti kujiamini iliyotulia sana, hii iliniambia kuwa yeye ni mtu mtulivu anayefanya mambo yake kwa umakini mkubwa yenye uhakika. Aliongea uongea kisha akaondoka, huku akinipa ujumbe kuwa kesho atanisafirisha mpaka Tanga, huko ndipo roho yangu itakapochukuliwa. Aliondoka akiniacha mwingi wa fikara

Giza liliingia nuru ikakimbia, hapo nikihesabu masaa machache ambayo nitakuwa natoroshwa na Salome. Mawazo mengi yalinipitia hata mengine sikuwezaa kuyakumbuka, haukuwa mtiririko wa mawazo bali Maandamano ya mawazo, yaani kichwa kilivurugwa na maandamano hayo. Muda ulienda lakini salome hakutokea, nilijua bado mapema hivyo nikatarajia kuwa Salome angefika pale saa nne usiku, lakini saa nne usiku ilifika Salome hakutokea, nilikuwa nikisimama na kuchungulia mara dirishani mara mlangoni lakini hakukuwa na dalili ya mtu kuwepo, zaidi ya taa tuu zikimulika eneo lile. Nilisimama dirishani nikitazama nje nikiwa mwingi wa mawazo, hapo nikashtushwa na kitu, alaaah! kumbe ni Kirungu yeye, mnyama fulani jamii ya panya lakini anamiiba.
Nikachoka, nikarudi kukaa, ikafika saa sita na nusu salamo hatokei, saa saba salome wapi, nikakata tamaa, hapo mwili ukiwa umedhoofika kwa usingizi.
Polepole usingizi ukanipitia, nikalala usingizi ambao pengine ulikuwa usingizi wa mwisho. Punde nikashtuka, sikumbuki nilishtuka kwa sababu gani, nikacheki saa yangu ya mkononi ilikuwa saa tisa na dakika arobaini na mbili yaani saa kumi kasoro. Doooh! Asubuhi ndio inafika ikinikuta pale pale ambapo nitapelekwa Tanga kutolewa Roho yangu kama alivyosema Baba salome. Hapo kitete cha kifo kikanikaba, wasiwaasi na mashaka ya mauti vikanishika. Nikaenda mlangoni nikagonga wapi, mwishowe ikanibidi nirudi kwenye konda na ujikunyata kama kinda la ndege huku mara kwa mara nikiicheki saa yangu.

Nikakumbuka maneno ya Salome kuhusu kunitorosha, nikahisi huenda alikuwa ananidanganya tuu. Nikaanza kumlaumu kwa kunipa ahadi za uongo, lakini punde kwa sekunde Mlango uliguswa na kwa haraka ukafunguliwa, alikuwa ni salome akiwa na Tochi, nilimfuata na kumkumbatia kwa nguvu nyingi sana. Aliniomba radhi kwa kuchelewa na kunielezea sababu ya yeye kuchelewa. Basitulivyotoka kwenye kile chumba majibwa makubwa mawili ya kijerumani yalikuwa yakinirukia rukia huku Salome akiyaambia kwa kingereza yaache, basi yakaacha huku yakitingisha mkia mara kwa mara na kumdandia dandia Salome

Basi nikatoroshwa kwa njia ya handaki lilikuwa pale nje ya ile ghorofa ambapo kulikuwa na chemba yenye mfuniko ambao juu yake kuliwekwa chungu kikubwa chenye ua juu yake. Tukapita chini kwa chini Salome akiwa anamulika na tochi yake. Tukasimama na kunyonyana denda kwa dakika tano, lakini akili yangu ikanitahadharisha kuwa bado nipo eneo hatari. Ingawa nilifurahi kunyonyana ndimi na Salome lakini haikunifanya nisahau usalama wangu. Tulitokea upande wa nyuma kumbe ilikuwepo Gari aina ya Alphard ya kijibu iliyokuwa inatusubiri. Bila kupoteza muda nikazama na kuondoshwa eneo lile nikiwaambia wanipeleke Sinza kwanza magetoni, basi safari ya kutoka Mikocheni kwenda Sinza ikaanza, tukiwa ndani ya gari mimi bado nikiwa nanuka damu za siku mbili na nusu Salome alikuwa akijibebisha huku mara kwa mara akitaka nimkumbatie na kumnyonya ndimi.

Akili moja ikaniambia, wasipajue nyumbani kwako, badi nikawaambia wanishushe Sinza Lego, wakati huo mimi nakaa Sinza Kwaremi ndani ndani kidogo. Tukafika wakanishusha, tukaagana na Salome huku akiniachia mawasiliano yake, lakini kabla sijaondoka kuna gari yenye mwanga mkali ilikuwa inakuja kwa kasi ikitokea Makumbusho kule kule tulipokuwa tumetoka barabara ya Shekilango, kwa upesi nikaanza kukimbia huku milio ya risasi ikiyaandama masikio yangu. Sikulaza damu niliingia vichochoro na kupotea mitaani.

Kilichotokea ni kikubwa, sitaki hata kukumbuka, kwani ni zaidi ya nilivyokamatwa mara ya kwanza.

Stori hii nimeikumbuka baada ya kukutana na Salome wiki iliyopita maeneo ya uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Hii ni baada ya kupotezana naye zaidi ya miaka nane hivi.

Haya maisha haya, nimepoteza kiungo kimoja kwa sababu yake, sitakaa nisahau. Lakini yote kwa yote bado ni mzima, namshukuru Mungu.

Jokajeusi
 
Boss hujanipatia kitafunwa hapa meza ya pili kutoka nyuma nimevaa jezi ya manyuu ya pundamilia
Screenshot_20200428-224513~2.jpg
 
Uzi wenyewe nimeandika machozi yakinitoka, keyboard yote tepetepe kwa jasho.

Kasie mama wa Haja
Mama wa shughuli
Kasie mzinga wa asali

Pole kwa yaliyokusibu.

Kila la kheri kwenye kusherehekea sikukuu za krismasi na mwaka mpya.
 
Back
Top Bottom