Salamu hizi ziwafikie Shekhe Kishki, Mazinge na wahadhiri wengine wa Kiislamu

Salaam,

Kwanza nianze tu kwa kusema mimi ni Mwislamu na kama ilivyo kwenye dini kukumbushana, kutahadharishana, kunasihiana na kupendeleana mema ni sehemu ya maagizo na maamrisho tunayolazimika kuyafuata.

Mikoa ya kusini hususani vijiji vya Ruangwa (naongelea pahala nilipo na ushahidi napo zaidi) kumekuwa kuna mambo au taratibu za tofauti kabisa katika serikali na katika dini. Utofauti huo umetokana na elimu wanayomezeshwa watu kutoka kwa mashehe uchwara waliopo katika jamii.

Sasa kinachonihuzunisha zaidi watu hawa hawajawahi kupata kutembelewa hata na shekhe mmoja (nimedodosa dodosa nikagundua hilo)akaja kufanya mihadhara walau kupatiwa chakula cha nafsi. Kwa maana hiyo yote ninayoyaona wanaenda kinyume kumbe wapo sahihi kwakuwa wanafunzwa hivyo na mashekhe zao na hawajawahi kuambiwa (kuonywa) kwamba sivyo

Hali hii imenifanya nishangae sana maana hawa wahadhiri wamekuwa maarufu sana kwenye maeneo mengi mengineyo kwa kuurudisha umma kwenye mstari na sehemu zingine nimeshuhudia wakirudia kwenda kupiga kambi hata zaidi ya mara mbili je vipi kwa maeneo ya huku... kwamba;

a. Ni miongoni mwa maeneo ambayo hayakupata bahati kufikwa ila yapo kwenye mkakati (basi ndo mfanye mfike) au
b. Ni miongoni mwa maeneo yaliyoonekana yapo vizuri kidini hivyo hayakupewa kipaumbele kwahiyo hakukuwa na haraka ya kuja (basi ndo mjue kumeharibika sasa) au

c. Ni miongoni mwa maeneo yaliyosahaulika hayakuwa kwenye mkakati (basi ndo myafikirie kuyajia) au

d. Ni miongoni mwa maeneo ambayo mlifika zamani labda mkaishia baadhi ya sehemu za mjini tu mkahisi imetosha (basi sivyo! Mambo bado mabichi)

Mifano ni mingi sana lakini hapa nitatoa michache ambayo watu wa huku wanajishikamanisha nayo wakidhani ndio sheria za dini (au za serikali)

A. Kuachana (talaka) ni jambo la kawaida sana na wakiachana cha kwanza ni kugawana pasu kwa pasu. Mwanzo nilionaga kina Pembe wakiigiza nikajua muvi tu kumbe huku ndo mpango yaani unaoa halafu after mwezi mke anadai talaka na mali yako anashadadia mpaka ikatwe nusu apewe. Nimeshuhudia mtu akijenga nyumba nyingine ya pili huku akisema hii ni maandalizi siku tukigawana na mke wangu basi hatuna haja ya kuuza hii nyumba bali kila mtu apate nyumba yake (kwamaana ni salwala la kawaida talaka-pasupasu) na kweli kama mwezi mbele ikawa vilevile alivyosema

B. Uchumba, huku mtu akishatoa posa (wenyewe wanaita hela ya barua) basi huyo mke ni wake tayari na akija wazazi wa mwanamke wanampisha anajitawala bali hata kumchukua akalale naye kisha amrudishe kesho pia ruksa. Wengi sana wanaishi hata miaka 5-6 pamoja na huku hawajaoana na hata kuzaa wanazaa. Nimeshuhudia ndoa nyingi ambazo kabla yake wanandoa wamekuwa wakiishi pamoja kama mke mume (yaani hakuna tofauti na dizaini ile ya manaswara ya kubariki ndoa)

C. Swala Swaumu na Zaka, kuna kijiji 99% ni waislamu ila ni 20% tu wanafunga mwezi mtukufu huku 01% pekee (asilimia moja na wala siyo kumi) ndo wanaoswali. Ukiuliza wanakwambia sheria ya kufunga hauruhusiwi mtu wa kike ambaye hajaolewa kufunga wala mtu ambaye kula yake anaipata kwa njia za haramuharamu (mfano kuhongwa) naye haruhusiwi kufunga. Hawajaishia hapo tena wanaaminishana kwamba mwenye kula ya wasiwasi hatakiwi kufunga (tena bora ingekuwa wanamaanisha chakula hasa bali eti futari futari na matunda matunda muda wa magharibi)

Anayeishi na huyo mchumba wake ambaye bado hajamtolea mahari ndoa ipite basi wote wawili hawaswali wala hawafungi. Yaani wanaamini ni sahihi kuishi na kimada bora tu umeshatoa posa huku tena wanaamini kwamba kuishi na kimada ni dhambi (uzinifu) kwahiyo hafai hata kuswali wala kufunga swaumu kwa dhambi hiyo

D. Kuchinja, sisi tunahangaika kujielimisha juu ya kwamba kuelekea kibla au kuvua viatu kwenye kuchinja ni lazima au laa kumbe kuna jamii ambazo wao bado wapo kwenye kwamba aliyechinja apewe (nyama ya) shingo asepe nayo ( wenyewe wanaita uchinjo). Tena bora apewe tu kwa hiari ya mwenye kinachochinjwa basi... lahasha mtu anasema kabisa nipeni uchinjo wangu niondoke mie maana wa kwenda kuuliza juu ya roho ya kiumbe huyu ni mimi mchinjaji

E. Sherehe za idd sijui pasaka na nyinginezo hazina nafasi huku japokuwa waislamu ni kama wote. Ikifika Dec vile wachaga wakirudi kwao kwajili ya Christmas basi kwa kipindi cha nyuma ndo ilikuwa ikifika misimu ya korosho na ufuta wamwera wanarudi kwao kwajili ya ngoma za asili (zipo sherehe nyingi mf kiangulo, manyago).

Sasa hivi baada ya serikali kuingilia kati hizo ngoma kwajili ya wanafunzi basi ndo mpira umehamishiwa kwenye mziki. Yaani kijijini hamlali kila siku watu wanakodi mziki tena mziki mnene kwajili ya sherehe hizo basi hapo kwenye mziki ni kufuru tupu usiku kucha.

Wanaweza kuanza saa 12 jioni mpaka 12 jioni tena ndo mziki unaisha watu wakitoka hapo sauti hawana nguo ni tope mwili mzima yaani hawatamaniki. Yaani serikali ilizuia ile mikusanyiko ya kuchangishana na kufanya sherehe siku za masomo ambapo process zake ni karibu wiki 2-3 sasa wao wameamua kila mtu anafanya mwenyewe kwake lakini kitu ni kilekile.

F. Ulevi, watu wengi wanatumia bangi na/au pombe za kienyeji na ni kitu cha kawaida tu. Ubaya huku sioni viongozi wa dini wala wa serikali za vijiji wakikemea jambo baya lolote.

G. Matusi, huku matusi ni kionjo cha kawaida katika maongezi... kama ni mgeni mwanzo utapata tabu sana. Nidhamu katika utendaji hakuna unakuta kwenye mikusanyiko kiongozi anaongea (ukiacha viongozi wanaoambatana na polisi) huku watu wanapiga zao stori tena kwa nguvu tu. Mfano makabirini harusini mabaraza ya dini wachache sana mnakuwa concentrate na jambo husika lakini wengine shekhe anaongea wao ndo kwanza wanapiga kelele tu na shekhe hakemei

H. Kuna utaratibu wa kunyweshana sijui ni kitu gani hata lakini wanakunywaga watu wale wa qadiria shamsia na shazilia. Basi huku kama hukunywa hiyo unakuwa hujajinasibisha katika kundi fulani wenyewe wanadai hata ukifa mashekhe watasuasua kwenye kukusitiri

I. Mtu akizini au akifumwa na mwanafunzi au mke wa mtu au makosa mengine yoyote basi ni kitega uchumi kwani anashikwa faini kubwa sana na kesi inakuwa imekwisha. Hilo yawezekana la kawaida kwa baadhi ya makosa lakini siyo kwa mtoto wa shule na mke. huku mtu yupo radhi kuusuka mchongo kabisa na mwanawe au mkewe ili wakupige hela yaani anairuhusu zinaa ili apate kipato na hili limeenea sana.

Nimeongelea upande wa dini tu kama nilivyotangulia kusema mwanzo mimi ni Mwislamu na wengi katika wahusika ni waislamu hivyo naongelea (kuwa si sahihi) kwa kiislamu. Upande wa kiserikali napo kuna mengi mfano ni ule uzi nilileta humu kwamba watu wanaunguza sana misitu bila hatua zozote kuchukuliwa.

Hayo na mengine mengi yanakwenda kinyume mimi nimejitahidi kwa kiwango changu kuyasemea ila sina ushawishi wala elimu ya kufanikiwa kivile kama mashekhe waliobobea kwahiyo yeyote mwenye uwezo na awajibike.
Toeni vijana wakasome kisha wakirudi waje waelimishe watu wenu,sio njia pekee kutegemea watu wa sehemu fulani.

Lakini pia ni muhimu sana kusomesha mtoto elimu ya dunia inamfungua akili kuachana na baadhi ya tamaduni za kipuuzi ikiwa huyu mtoto hakusoma dini basi pengine akatumia elimu dunia kuachana na baadhi ya ujinga
 
Dini yako iliwakuta hao watu wana mila na taratibu zao,wataamua wanayoona yanafaa kuachwa na yanayofaa kuendelea nayo.
Religion does not exist in a vacuum. It exists within an environment. However much we would like to practice religion as it is in its guiding principles and holy books thereof used, we cannot void culture out of it.
 
11 Reactions
Reply
Back
Top Bottom