Sakata la Madini: Je, Watanzania tuko tayari kunywa Sifongo?

mwankuga

JF-Expert Member
Aug 30, 2010
334
120
SAKATA LA MADINI:
JE, WATANZANIA TUKO TAYARI KUNYWA SIFONGO?

Katika makala mbili zilizopita, nilimpa kongole Mhe. Rais kwa kutambua kwamba tunaibiwa katika uvunaji wa rasilimali madini. Hili ni jambo jema sana kama uongozi wa juu kabisa unapoamua kuchukua hatua, kwani watanzania wamekuwa wakipiga kelele muda mrefu. Mbali na hizo kelele, maeneo ambayo yana madini, ni kiashiria tosha kwamba hatufaidiki na chochote.

Aidha nilimshauri Mhe. Rais na serikali yake kuwa makini kwa kila hatua watakazochukua ili kuhakikisha nchi inafaidika na uchimbaji wa madini, maana kwa kila hatua itakayochukuliwa, ina madhara yake. Nilimshauri Rais, kufanya vita hiyo ni ya kitaifa, kuliko vita ya mtu mmoja. Akubali kushaurika na kuwashirikisha watu wa aina mbalimbali, hata nje ya chama chake ambacho ni chanzo cha tatizo hili. Hakuna shaka kwamba sasa tuko vitani. Katika hii vita tumewaandaje wananchi kukubaliana na matokeo yoyote yatakayotokea?

Swali hili limenifanya nikumbuke mambo mengi sana. Safari hii nimekumbuka madhira wanayopata watu wa Zimbabwe kutokana na sakata la ardhi, na maisha waliyoishi watanzania mara baada ya vita ya Kagera. Robert Mugabe ni miongoni mwa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha rasilimali za nchi (ardhi) zinatumika kwa faida ya wananchi wake. Amepigania uhuru wa Zimbabwe na hatimaye amekuwa Rais wa “maisha” wa nchi ya Zimbabwe.

Robert Mugabe alianza vizuri sana. Zimbabwe ilikuwa miongoni mwa nchi iliyokuwa inafanya vizuri sana katika nyanja ya kilimo na uchumi kwa ujumla. Pamoja na hilo kulikuwa na tatizo la ardhi ambalo lilitengenezwa enzi za ukoloni. Kulikuwepo na mikataba kadhaa ambayo ilikuwa inaongoza ugawaji wa ardhi ndani ya Zimbabwe (Lancaster House Agreement). Mikataba hiyo ilitokana na ukweli kwamba ardhi nzuri ilikuwa inamilikiwa na watu wasiozidi 4500 (asilimia 70 ya ardhi yote) huku wakulima wadogowadogo (waafrika) wakilimiki asilimia 30 tu.

Hili lilikuwa ni tatizo kubwa katika serikali ya Mugabe. Katika mkataba wa Lancaster, kulikuwa na kipengele cha watu wenye ardhi kubwa (walowezi wa kizungu) kuuza ardhi kwa hiari, huku serikali ya Uingereza ikifadhili zoezi la ununuaji wa ardhi. Kwa kuwa zoezi hili lilitegemea zaidi hiari ya muuzaji na uwezo wa kipesa wa mnunuaji, hali ikaendelea kuwa mbaya, na kibaya zaidi umaarufu wa Mugabe ukaendelea kushuka, huku maveterani wa vita wakiwa tishio jipya kwa Mugabe. Kutokana na hilo, Mugabe alichukua hatua kadhaa ikiwemo kuja na sheria ya Land Acquisition Act, ambapo serikali ilipewa maamlaka ya kuchukua ardhi kutoka kwa walowezi wa kizungu na kuwapa wakulima wadogo wadogo.

Kwa bahati mbaya sana, serikali ikashindwa kusimamia zoezi la ugawaji wa ardhi, huku ardhi kubwa ikiangukia mikononi mwa maveterani wa vita, mawaziri na viongozi wa serikali katika ngazi tofauti, na wananchi wakibaki palepale. Mwisho wa siku Zimbabwe imeporomoka kiuchumi, na kuifanya nchi kuwa kwenye wakati mgumu sana baada ya vikwazo kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani. Pamoja na kwamba Mugabe alianza vizuri, lakini kwa sasa limebaki jina. Hakuna jipya analofanya zaidi ya kusogeza siku.

Wakati wa utawala wa kipindi cha mwisho wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Nyerere, maisha yalikuwa magumu sana. Baada ya vita ya Kagera, Mwalimu Nyerere aliwatangazia wananchi kufunga mikwiji, kwa hali ya uchumi ilivyokuwa ngumu. Nyerere aliwaandaa watanzania kuwa tayari kwa ugumu wa maisha. Sababu zilikuwa nyingi, ikiwemo madhara ya vita vya Kagera, kupanda kwa bei ya mafuta, na sera mpya za Benki ya Dunia na Shirika na Fedha ambazo Mwalimu hakukubaliana nazo.

Nimejaribu kutoa mifano kuonyesha jinsi maamuzi ya viongozi yanavyoweza kuleta madhara kwa wananchi. Kwa sasa na sisi tuko kwenye vita. Hii ni vita kubwa kama ambavyo nimeeleza kwenye makala mbili zilizopita. Kwa maamuzi yoyote ambavyo serikali yetu itafanya kuhusu uchimbaji wa madini kuna madhara ya moja kwa moja ambayo wananchi watayapata. Hiyo inatokana na ukweli usiyopingika kwamba uchumi wetu ni tegemezi sana. Kwa kiasi kikubwa tunawategemea watu ambao ndio tunapambana nao, ambao wanatuibia rasimali zetu kwa njia ya halali.

Huu ni wakati wa kufanya maamuzi magumu lakini sahihi kwa masilahi ya watanzania wote. Viongozi wetu watulize akili na kuona njia nzuri ya kutatua tatizo hili. Muhimu zaidi ni viongozi wetu, kuwaandaa watanzania kisaikolojia, wawe tayari kwa lolote litakalojitokeza. Watanzania wawe tayari kunywa sifongo, kwa ajili ya kutibu maradhi yetu.

Katika wakati ambao serikali ilioko madarakani haieleweki inafuata mfumo (kanuni) upi wa uchumi, wakati huu kukiwa na joto kali la kiuchumi huko mitaani, pengine mbeleni hali inaweza kuwa ngumu sana, ni vema watanzania wakajua kwamba, inawezekana tukakabiliana na hali ngumu zaidi siku za mbeleni, kulingana na hatua ambazo tutazichukua katika sakata la madini.

Kwa jinsi uchumi wa dunia ulivyo, ni wazi kwamba ukiwagusa tu mataifa ya Ulaya na Marekani, utegemee kupata vikwazo vya kiuchumi. Hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha Taifa linapunguza utegemezi, na kujenga uchumi imara ambao utawafaidisha wananchi.

Haipendezi, na inakera kuona viongozi wanatembea kifua wazi, wakijinasibu kwamba uchumi unakua, huku wananchi wanaoishi chini ya piramidi, wakizidi kudhoofu. Isije ikatokea kama Zimbabwe, ambapo vita ya kugawa ardhi ikageuka kuwa neema kwa viongozi wachache na kuwaacha wananchi wengi wakiwa kwenye shida zisizoisha.
 
jana PM Majaliwa katoa jibu kuwa hili swala si mchezo,mkubwa haombagi msamaha,kupitia kwa majaliwa mkubwa anaanza kuomba msamaha!!
 
wao wanaishi masaki,mikocheni,upanga, mbezi beach nk hali ikiwa mbaya watapanda ndege kukimbilia ughaibuni..

Ubinafsi ni ugonjwa mbaya sana Africa, problem creator want to solve the problem - hii ndio iliyotokea kwa Mugabe, yeye ndio aliyetengeneza tatizo kwa kuwa kibaraka wa wazungu na baada kugeuka na kujifanya mzalendo.

Watanzania tusiposimama na kuleta ujuaji tutatumbukia kwenye shimo lefu saaana ambalo wengi wanatamani tutumbukie ili wajenga mataifa yao na kuwafanya watanzania watumwa wao, Watanzania hatuna jirani mwema hapa tusimame wenyewe na tuwe kitu kimoja kwenye jibu la ukweli tuache unafiki.
 
Kwa hiyo mleta mada unashauri tuendelee na status quo kwenye hii sector ya madini?
 
jana PM Majaliwa katoa jibu kuwa hili swala si mchezo,mkubwa haombagi msamaha,kupitia kwa majaliwa mkubwa anaanza kuomba msamaha!!

Ni muhimu sana kufanya uamuzi kwa umakini na utulivu wa hali ya juu. Hakuna haja ya kukurupuka, japo tunafahamu tangu zamani kwamba tunaibiwa, japo ndani ya sheria
 
wao wanaishi masaki,mikocheni,upanga, mbezi beach nk hali ikiwa mbaya watapanda ndege kukimbilia ughaibuni..

Ubinafsi ni ugonjwa mbaya sana Africa, problem creator want to solve the problem - hii ndio iliyotokea kwa Mugabe, yeye ndio aliyetengeneza tatizo kwa kuwa kibaraka wa wazungu na baada kugeuka na kujifanya mzalendo.

Watanzania tusiposimama na kuleta ujuaji tutatumbukia kwenye shimo lefu saaana ambalo wengi wanatamani tutumbukie ili wajenga mataifa yao na kuwafanya watanzania watumwa wao, Watanzania hatuna jirani mwema hapa tusimame wenyewe na tuwe kitu kimoja kwenye jibu la ukweli tuache unafiki.

Umenena yaliyo mema
 
Kwa hiyo mleta mada unashauri tuendelee na status quo kwenye hii sector ya madini?

Hapana. Sio lengo la makala yangu. Ninachoomba ni kwamba kuwepo na utulivu sana katika kuamua suala hili, ili mwisho wa siku ufanyike uamuzi makini. Aidha wananchi wanatakiwa kuandaliwa kwa hali yoyote itakayojitokeza, maana kwa kina uamuzi utakaofanyika, kutakuwa na madhara yake.
 
Back
Top Bottom