Sakata la Kinana, Makamba ladhihirisha Ukatibu CCM ‘Kaa La Moto’

Alexander The Great

JF-Expert Member
Aug 28, 2018
4,502
23,581
Sakata la kuitwa kwa makada watatu wa CCM kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Usalama limeendelea kudhihirisha ule msemo kuwa wadhifa wa katibu mkuu wa chama hicho ni sawa na kushika kaa la moto.

Hali hiyo inatokana na Halmashuri Kuu ya CCM iliyokutana wiki iliyopita jijini Mwanza kuagiza makatibu wa zamani wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yussuf Makamba waitwe kuhojiwa na kamati ya maadili. Kada mwingine aliyeitwa ni Benard Membe.

Makada hao watatu wanatuhumiwa kutokana na sauti zao zilizorekodiwa kusambaa katika mitandao ya kijamii zikizungumzia kupasuka kwa CCM.

Kutokana na tukio hilo kuhusisha makada waliowahi kuwa makatibu wakuu, limewafanya wachambuzi wa masuala ya siasa kuelezea ugumu wa kutekeleza majukumu ya ukatibu mkuu wa chama hicho.

Historia na rekodi za CCM zinaonyesha kuwa makatibu wake wengi wamejikuta wakiingia matatani wanapokuwa madarakani na hata pale wanapoondoka.

Tangu kuasisiwa kwa chama hicho, makada tisa (9) ndio wamewahi kushika wadhifa wa ukatibu mkuu.

Hata hivyo, makatibu wakuu wawili; Pius Msekwa na Rashid Kawawa ndio hawajawahi kukumbwa na doa.

Msekwa ana historia ya kuwa katibu wa kwanza chama hicho wakati kilipozaliwa Februari 5, 1977 ingawa wakati huo nafasi hiyo ilikuwa akijulikana kama katibu mtendaji. Alishika nafasi hiyo kuanzia 1977 hadi 1982 na kisha nafasi hiyo kupewa Rashid Kawawa aliyedumu hadi mwaka 1990.

Waliofuata walikuwa ni Horace Kolimba (1990-1995), Lawrence Gama (1995-1997), Philip Mangula (1997-2007), Yussuf Makamba (2007-2011), Wilson Mukama (2011-2012), Abdulrahman Kinana (2012-2018) na sasa Dk Bashiru Ally.

Akizungumzia suala la ugumu wa nafasi ya katibu mkuu, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha Iringa, Profesa Gaudence Mpangala anaeleza unyeti wa nafasi hiyo unafanya wahusika mara nyingi wapate misukosuko.

“Katibu Mkuu anajua siri nyingi za chama kwa hiyo hata akiona kuna dosari mahali ni rahisi kwake kukosoa,” alisema Profesa Mpangala.

Hata hivyo, mchambuzi mwingine Deus Kibamba alisema nafasi ya katibu mkuu wa chama imekuwa ngumu kutokana na vyama vikongwe kuwa na tabia ya kuikuza nafasi hiyo.

“Vyama kama CCM, Zanu PF na Kanu vimewafanya watu hawa kuwa wakubwa sana, sasa matokeo yake ndio maana wanapata wakati mgumu,” aliongeza Kibamba.

Pius Msekwa (1997-1982)
Pius Msekwa hakupata misukosuko katika kipindi chake na kazi yake kubwa ilikuwa kukijenga chama ambacho wakati huo nchi ilikuwa katika mfumo wa chama kimoja.

Rashid Kawawa (1982-1990)
Rashid Kawawa alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa chama hicho baada ya wadhifa huo kubadilishwa kutoka kuwa Katibu Mtendaji na hakukuwa na tatizo katika kipindi chake cha uongozi hadi alipong’atuka mwaka 1990.

Horace Kolimba (1990-1995)
Balaa la makatibu wakuu wa CCM kukumbwa na misukosuko lilianza kwa Horace Kolimba ambaye alipata misukosuko kwa nyakati mbili tofauti, alipokuwa katibu mkuu na hata alipoachia madaraka hayo.

Kolimba alitikiswa kwa mara ya kwanza mwaka 1993 kutokana na hatua ya wabunge 55 maarufu kwa jina la G55 kudai Serikali ya Tanganyika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hoja hiyo ilifikishwa bungeni, lakini ilikwama baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuingilia kati na hadi kufikia hatua ya kuchapisha kitabu cha `Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania’ kushinikiza kujiuzulu kwa Kolimba na Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wakati huo, John Malecela kwa kushindwa kumshauri Rais Ali Hassan Mwinyi kuhusu suala hilo la kuwa na muungano wa serikali tatu.

Malecela na Kolimba ilibidi waondolewe kwenye nyadhifa zao mwaka 1994, ambapo nafasi ya Kolimba ilichukuliwa na Gama wakati nafasi ya Malecela ilizibwa na Cleopa Msuya.

Hata hivyo, misukosuko ya Kolimba haikushia hapo kwani wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 baada ya CCM kumpitisha Benjamin Mkapa kama mgombea wa chama alitoa kauli iliyomletea matatizo.

Kolimba alikaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa CCM ilikuwa imepoteza dira na mwelekeo. Kauli hiyo haikupokelewa vizuri, hivyo aliitwa kujieleza kwenye kamati ya maadili ya CCM.

Hata hivyo alipofika kwenye kikao hicho, aliugua ghafla na baadaye kufariki dunia.

Lawrence Gama (1995-1997)
Lawrence Gama alipewa wadhifa huo mwaka 1995 kutokana na kusifika kwa uchapakazi hasa kazi nzuri aliyofanya katika mikoa ya Dodoma, Ruvuma na Tabora akiwa mkuu wa mkoa.

Alipata tatizo baada ya kutuhumiwa na mmoja wa waliokuwa wawania urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete kuwa hakumtendea haki wakati wa mchakato huo.

Alipatanishwa na Kikwete na mwenyekiti wa CCM wakati huo, Ali Hassan Mwinyi na suala hilo likaisha na akawa katibu mkuu hadi mwaka 1997.

Philip Mangula (1997-2007)
Philip Mangula ni miongoni mwa makada wa CCM aliyeshika wadhifa wa katibu mkuu kwa muda mrefu. Alisifika kwa kufuata kanuni na kuongoza kwa maadili.

Aliondoka baada ya kusemekana kuwa mwenyekiti wa CCM wa wakati huo, Kikwete kutofurahishwa na sekretarieti ya chama ilivyoendesha mchakato wa kuwania kugombea urais mwaka 2005. Inadaiwa kulikuwa na taarifa hasi dhidi yake ingawa alikuja kushinda mchakato huo.

Yusuph Makamba (2007-2011)
Uongozi wa Yussuf Makamba kwenye chama hicho ulilaumiwa zaidi kwa kukizamisha chama kwenye uchaguzi mkuu 2010.

Rais Kikwete alipata ushindi wa asilimia 61 tofauti na mwaka 2005, ambapo alipata ushindi wa asilimia 80.

Makamba licha ya kuondoka kwenye wadhifa sasa amejikuta matatani.

Wilson Mukama (2011-2012)
Sera ya kujivua gamba ilimuweka Wilson Mukama katika wakati mgumu baada ya kuteuliwa kuwa katibu mkuu mwaka 2011.

Mukama aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya kuongoza kamati maalum ya kuangalia mwenendo wa chama hicho baada ya kupungua kwa kura za urais na chama kupoteza majimbo mengi kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2010.

Mukama alikuja na pendekezo la chama kujivua gamba kwa maana ya kuwaondoa watu waliokuwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, ili kurudisha mvuto wa chama kwa wananchi.

Hata hivyo, operesheni hiyo ilichafua hali ya hewa ndani ya chama na kufanya mwenyekiti Kikwete kuunda kamati ya watu watatu chini ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Pius Msekwa na Abdulrahman Kinana kushughulikia suala hilo.

Kamati hiyo ilikuja na mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangia Mukama kutolewa baada ya mwaka mmoja na nafasi yake kuchukuliwa na Kinana.

Abdulrahman Kinana (2012-2018)
Kinana alishika uongozi katika kipindi ambacho CCM umaarufu ulikuwa unazidi kuporomoka. Masuala mbalimbali yalikuwa yamechangia kukivuruga chama hicho.

Kwanza, vita dhidi ya ufisadi, ambayo ilikuwa imeleta mgawanyiko.

Jambo jingine lililoleta mpasuko ndani ya chama hicho ni kampeni za urais za mwaka 2015, kwani wanachama wengi walikuwa wameanza harakati za kutaka kumrithi Kikwete.

Hata hivyo, hali ya sintofahamu ilianza kujitokeza baada ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli kuingia madarakani na Kinana aliomba kuachia ngazi ingawa alikataliwa.

Baadae alikuwa akikosekana kwenye vikao vya chama kwa kile kilichodaiwa kuwa matatizo ya kiafya hadi alipoteuliwa Dk Bashiru Ally.

Dk Bashiru alipewa nafasi hiyo baada ya kuongoza kamati maalum ya kufuatilia mali za chama na kukabidhi ripoti kwa mwenyekiti Magufuli.

Magufuli alimteua katika nafasi hiyo, huku akimtaka kufanyia kazi kasoro alizoona wakati akifuatilia mali za chama hicho.

Hata hivyo, baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanadai staili ya uongozi wa Dk Bashiru imeanza kuleta shida kutokana na kuwakosoa waziwazi watendaji wa chama na wa Serikali.

- Nakaribisha Hoja Na Mitazamo Yenu Wadau.
 
Hichi chama ni chakavu, kimepoteza mvuto. Hata kama kinatumia Jeshi la polisi. Chama hichi kinaongozwa na mwangi wa uongozi uliopita.
Kwa maana nyingine hiki chama kilishajifia. Wakati wa mwisho wa mwaka nilienda kijijini, watu wako hoi. Usiombe watu kupoteza imani na chama ambao ni masikini wakati watu hao ndo walikuwa mtaji wa chama hicho ndo maana ili kukwepa aibu ya matokeo ya serikali za mitaa, waliamua kucheza rafu kukwepa aibu. Kwa ajili ya check and balance hembu ufanyike uchaguzi huru uone CCM itavyoaibika. Pamoja na takwimu feki za Uchumi kukua bado wananchi hawawakubali ndo maana kunanguvu kubwa ya kuzuia "free of expression".
 
Hichi chama ni chakavu, kimepoteza mvuto. Hata kama kinatumia Jeshi la polisi. Chama hichi kinaongozwa na mwangi wa uongozi uliopita.
Kwa maana nyingine hiki chama kilishajifia. Wakati wa mwisho wa mwaka nilienda kijijini, watu wako hoi. Usiombe watu kupoteza imani na chama ambao ni masikini wakati watu hao ndo walikuwa mtaji wa chama hicho ndo maana ili kukwepa aibu ya matokeo ya serikali za mitaa, waliamua kucheza rafu kukwepa aibu. Kwa ajili ya check and balance hembu ufanyike uchaguzi huru uone CCM itavyoaibika. Pamoja na takwimu feki za Uchumi kukua bado wananchi hawawakubali ndo maana kunanguvu kubwa ya kuzuia "free of expression".
Mh Rais Mstaafu Kikwete alisema tarehe 13/11/2012, pindi wakati yeye ni mwenyekiti wa chama (baada ya wana CCM kulalamika wapinzani wanakosoa sana bungeni na kwenye mihadhara)

Nukuu ya alichosema;
tapatalk_1578155980234.jpeg
 
Hichi chama ni chakavu, kimepoteza mvuto. Hata kama kinatumia Jeshi la polisi. Chama hichi kinaongozwa na mwangi wa uongozi uliopita.
Kwa maana nyingine hiki chama kilishajifia. Wakati wa mwisho wa mwaka nilienda kijijini, watu wako hoi. Usiombe watu kupoteza imani na chama ambao ni masikini wakati watu hao ndo walikuwa mtaji wa chama hicho ndo maana ili kukwepa aibu ya matokeo ya serikali za mitaa, waliamua kucheza rafu kukwepa aibu. Kwa ajili ya check and balance hembu ufanyike uchaguzi huru uone CCM itavyoaibika. Pamoja na takwimu feki za Uchumi kukua bado wananchi hawawakubali ndo maana kunanguvu kubwa ya kuzuia "free of expression".
Kwa kuwa watawala lazima watokane na chama cha siasa, je raia huko kijijini wanatamani mbadala wao chama gani ambacho angalao kinaweza kuwatoa walipo na kuwaweka sehemu iliyo bora?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kwa kuwa watawala lazima watokane na chama cha siasa, je raia huko kijijini wanatamani mbadala wao chama gani ambacho angalao kinaweza kuwatoa walipo na kuwaweka sehemu iliyo bora?

Sent using Jamii Forums mobile app
Binafsi yangu naona afadhali ya ACT-Wazalendo, japokua hawana wabunge wakutosha kuweka baraza la mawaziri kamili, lazima wafanye serikali ya maridhiano na maungano ili kukamilisha baraza la mawaziri.
 
Back
Top Bottom