Sakata la Bosi TANROADS sasa latupwa kwa Mwanasheria Mkuu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Sakata la Bosi TANROADS sasa latupwa kwa Mwanasheria Mkuu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Jul 1, 2010.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jul 1, 2010
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,597
  Likes Received: 82,153
  Trophy Points: 280
  Thursday, 01 July 2010
  Na Yusuph Katimba, Dodoma
  Majira


  SERIKALI imesema inachunguza tuhuma zinazomwandama Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Bw. Ephraem Mrema yakiwemo madai ya kuendelea kubaki kwenye nafasi hiyo baada ya mkataba wake kumalizika Juni 4 mwaka huu na kuahidi kuweka mambo bayana mara uchunguzi huo utakapokamilika.

  Akizungumza bungeni juzi, Waziri wa Miundombinu, Dkt. Shukuru Kawambwa, alisema suala hilo ni zito linalogusa hoja za kisheria, hivyo wizara yake itamhusisha pia Mwanasheria Mkuu kulipatia ufumbuzi.
  Hatua hiyo ilikuja baada ya wabunge kuhoji malumbano yanayoendelea kwa muda mrefu sasa kuhusu mkataba wa mtendaji huyo na kutaka kupata msimamo wa serikali.

  "Mheshimiwa Spika, kuhusu muda wa utendaji kazi wa Mtendaji Mkuu wa TANROADS Serikali bado inalifanyia kazi suala hili na muda muafaka ukifikia basi tutalitolea maelekezo. Ni kweli kwamba kuna utata kati ya barua ambazo mikataba ambayo Mtendaji Mkuu yule anayo na hili ni suala la kisheria na ushauri wa kisheria lazima upatikane na Mwanasheria Mkuu wa Serikali lazima alitolee maelekezo suala kama hili.

  "Kwa hivyo si suala lile ambalo Serikali inaweza kukurupuka tu na kufanya maamuzi ambayo hayana ushauri wa kisheria kutokana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Itakapofikia mwisho wa ufafanuzi wa jambo hili, Serikali haitakuwa na kigugumizi cha kuweza kulitolea kauli na kuchukua hatua zile muafaka" alisema Waziri Kawambwa.

  Kuhusu mikataba ya baadhi ya mameneja wa TANROADS Dkt. Kawambwa alisema "Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS. Wizara ilikutana na Bodi ya TANROADS na Mtendaji Mkuu kama vile Kamati ilivyoagiza.

  "Katika kikao hicho ilielekezwa ifuatavyo kwamba wafanyakazi waliokuwa na mikataba waendelee na kazi zao hii iliwahusu mameneja wa TANROADS wa mikoa 10 ambayo ni Ruvuma, Dodoma, Iringa, Morogoro, Arusha, Kagera, Shinyanga, Dar es Salaam, Mwanza na Tabora ambao wote walitakiwa kuachishwa kazi.

  "Aidha, Wakurugenzi waliokuwepo TANROADS ambao wote aliowateua Mkurugenzi Mtendaji kabla ya muundo mpya wa TANROADS wabakie badala ya kuwaondosha ikiwa ni mchakato wa kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa taratibu za kujaza nafasi hizo kwa Wakala wa Serikali.

  "Suala hili linaendelea kusimamiwa na Bodi ya TANROADS na sisi Wizarani tunalipa umuhimu mkubwa kwa sababu ufanisi wa TANROADS ndio ufanisi wa Wizara ya Miundombinu na suala hili la ujenzi wa miundombinu wa barabara Tanzania ni kero kubwa kama ambavyo Mheshimiwa Spika ulivyoliona limeleta joto kubwa katika Bunge lako hili Tukufu."

  Katika kikao hicho, Waziri Kawambwa alikabiliwa na wakati mgumu wa hoja za wabunge kuhusu TANROADS huku wengine wakieleza kutoridhishwa na ujenzi wa barabara katika majimbo yao.

  Katika mjadala huo, wabunge kutoka Mkoa wa Tabora Bw. Lucas Selelii, Nzega (CCM) na Bw. Samuel Sitta Urambo Magharibi(CCM), Bw. Siraju Kaboyonga Tabora mjini(CCM) walioneshwa kukerwa na hali ya barabara za mkoa huo. Bw. Kaboyonga aliweka wazi msimamo wake kuwa kama hatapatiwa majibu ya kuridhisha hataunga mkono hoja.

  Barabara zilizoonekana kutawala hoja ni barabara ya Tabora, Urambo hadi Kigoma, Nzega hadi Tabora, Ipole Mbeya na Ipole Mpanda, barabara ya Tabora hadi Mpanda, Nzega hadi Urambo, na Uvinza Ilunde.

  Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilazimika kumwokoa Dkt.Kawambwa baada ya kusimama na kutolea maelezo upungufu wa fedha katika sekta ya miundombinu.

  Waziri Pinda alisema, “Hata tulipomaliza kuandaa bajeti yetu ya miundombinu, tulijua kuwa bado kuna matatizo, katika eneo lote la Tanzania, eneo ambalo bado halijafunguka ni eneo la Tabora, mimi mwenyewe nilidhamiria kuzifungua zionekane na kilichobaki ni kuwekeana saini ujenzi uanze.”

  Kutokana na kauli hiyo, wabunge wa Tabora walionekana kutulia kidogo, hata hivyo, Bw.Sitta alimwomba Waziri Mkuu, waziri wa Miundombinu pamoja na Katibu wake kukutana faragha kuzungumzia hilo kitu ambacho kilikubaliwa na Bw. Pinda.
   
Loading...