Saikolojia: Je Nimlipizie kisasi au nimsamehe?. (Vita visivyoisha vya Afghanistan)

Education Mentor

JF-Expert Member
Oct 26, 2016
392
1,000
Je Nimlipizie kisasi au nimsamehe?. (Case study: Vita visivyoisha vya Afghanistan)
“.Kabla haujaanza safari ya kwenda kulipa kisasi anza kuchimba makaburi mawili...” Confucius
upload_2018-5-7_15-19-6.png

(Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga).

Kisasi ni kitu kinachoweka hisia ya ahueni katika mioyo ya binadamu kwa muda, lakini ili kikadiliwe sawasawa na mtendaji wanadamu wamejiekea mifumo mbalimbali ya haki na hukumu ili kusuruhisha au kutoa haki kwa jamii zao. Ili kusudi kuepusha watu kujichukulia sheria mkononi.

Lakini ndivyo ulimwengu unavyosema kuhusu kisasi ni sehemu ya maisha ya kila jamii unapotazama maigizo, tamthiliya au kusoma riwaya basi uwa na pande mbili zinazokinzana Mhusika mkuu na adui wa mhusika. Ambapo kama itaanza mhusika mkuu akipitia katika mateso mikononi mwa adui zake au jamii yake ikapitia katika mgogoro huo, basi ili tamthiliya au sinema hiyo iishie ikiwapa tulizo na kufurahisha watazamaji sharti kisasi kilipwe au kutokee kuingilia kati kwa Mungu au miungu kuonesha ikilipa kisasi kwa adui wa mhusika huyo.

Hivyo fahamu yapo mambo unaweza ukaachilia au ukayafikisha katika sehemu za sheria ili kupatiwa haki zako (muhimu sana hili), lakini hiyo huwa haitoshi hata kama aliyekutenda atatendwa adhabu kwa mujibu wa sheria za nchi yako. lakini usipojifunza kuachilia baada ya muda utaharibikiwa tu na wewe.

KISASI NA MAHUSIANO YA MTENDAJI NA MTENDWA.

Baba na kijana wake mwenye tabia ya kisasi na utukutu, baada ya kumpa adhabu mara kwa mara lakini kijana hajabadilika hivyo akampa sehemu ya ukuta awe anaipiga na nyundo na misumali kila mara anapopatwa na hasira ya kulipiza kwa namna zote katika kiwango ambacho wazazi na ndugu zake watasikia milio hiyo ya upigaji.

Baada ya muda kuona haijamsaidia kuondoa hali yake akamfuata baba yake kumuuliza. ni nini maana yake baada ya kijana kuona ukuta kashauharibu sana ukuta ule, baba yake akamwambia “hiyo ndiyo mfano wa nafsi za wale unaowaudhi kutokana na hasira na kupenda kulipiza kwa hata vitu visivyo na umuhimu, ijapokuwa nduguzo huwa hawakujibu chochote kwako hivyo ndivyo jinsi wanavyokuwa ndani ya nafsi zao”. Akaongeza na swali je? unadhani unaweza kuurudisha ukuta kama ulivyokuwa mwanzo kabisa kwa mikono yako mwenyewe?.

CASE STUDY: VITA ISIYOISHA YA AFGHANISTAN KWA MIONGO MINGI

“..Hao waiosamehe historia kwao hujirudia mpaka huruma inakapochukua nafasi ya hukumu..”—Alan Cohen
upload_2018-5-7_15-25-39.png

(Picha ya kielelezo inayomuonesha mwanamgambo wa Taliban amebeba silaha aina ya RPG nchini Afghanistan).

Labda wengi wetu tumeisikia sana Afghanistan hasa kuanzia mwaka 2001 baada ya kuangushwa kwa majengo pacha ya biashara nchini marekani (Septemba 7) hivyo navyotamka nchini hii kinachokuja kichwani kwako msomaji wangu ni Talibani, Osama bin laden, Mura Omar na vita, hivi ni baadhi tu unavyovifahamu.

Lakini nakupa elimu ya ndani kwa ufupi kuhusu kabila kubwa linaloitwa “Pashtun” ambalo lina utamaduni wa kipekee sana na unaojulikana kama “Pashtunwali” huu ni mfumo wa kanuni za maadili ambazo makabila mengi yamemezwa kuufuata kutokana na uwingi wa watu wa pashtun.

Tungesema leo hii unapotaja kanda ya ziwa kinachokuja kichwani mwa wengi ni kabila la wasukuma lakini yapo makabila mengi madogo madogo ambayo kwa kadili muda unavyoenda yanamezwa na utamaduni wa wasukuma. Pia Mbeya yapo makabila madogomadogo mengi lakini yanajikuta yanaathiriwa kitamaduni na kumezwa na kabila la Wanyakyusa.

Labda nianze leo katika makala hii kukupa historia ya kwa ufupi kuhusu taifa la Afghanistan kwa karne nyingi nyuma zilizopita hasa uhusiano kati ya jamii zao wenyewe pia jamii hizo na mataifa makubwa (Super powers).

MIKONONI MWA ALEXANDER MKUU 330 B.C ( KABLA YA KRISTO ).

Kwa mara ya kwanza Alexander the Great alifika eneo la Afghanistan baada ya kumshinda mfalme Dario wa tatu katika pigano liloitwa vita ya Gaugamela. Jeshi lake wakati huo akiwa ndio taifa babe ulimwenguni lilikutana na upinzani mkali sana kutoka katika makabila ya Afghanistan na Alexander alinukuliwa akisema hivi juu ya waafghanistani “si ngumu kuivamia ndani kivita lakini ni vigumu kuondoka kivita”. kutoka hivyo safari yake aikuendelea sana sababu alifariki akiwa ana miaka 30 tu. Na hivyo utawala wake ukashindwa hapo baadaye nakuiachana nchi hiyo.

Hivyo baadaye baada ya kuondoka kwa vikosi vyake kukapita vipindi vingi sana vya migogoro ya vita katika ya wao kwa wao na jamii zao.

MIKONONI MWA UINGEREZA KARNE YA 19 ( MIAKA YA 1800 ).

Katika kuelekea karne hii ndipo mfumo wa ubepari unaanza kuchipuka ambapo taifa la uingereza lipo katika kilele chake cha taifa babe duniani (kama ilivyo marekani leo). iliingia Afghanistan ikitokea Pakistani (wakati huo Pakistani ilikuwa eneo la India). Kwahiyo kuanzia mwaka 1837 ndipo uingereza ikaanza kukutana na upinzani kutoka kwa makabila ya hapo na jeshi la uingereza likawa limeshaaithiriwa vibaya. baadaye vikifuatiwa na vitendo vya upinzani na uasi mara kwa mara hivyo ikabidi uingereza iitawale kwa kuirimoti (indirect rule) kutokea india.

Kuna kisa kinachoelezewa askari wa uingereza na raia wake idadi ya watu 3000 waliamua kuondoka kutolokea India baada ya mashambulizi ya mara kwa mara kwa watu wake. Hivyo licha ya kukubali kuondoka waafghanistani waliendelea kuwashambulia waingereza na msafara wao njiani kiasi inakadiliwa walioweza kuingia Pakistani hai ni chini ya 100 tu.

Uingereza ilipoondoka nchini humo muda si mrefu waafghanistani wakageukiana wao kwa wao tena migogoro ikaendelea katika vipindi tofauti tofauti.

MIKONONI MWA UMOJA WA KISOVIETI USSR (1978 MPAKA 1989).
upload_2018-5-7_15-25-53.png

(wanamgambo wa Mujahidina wamesimama juu ya helikopta ya wasovieti walioitungua).

Sitaki kuelezea sana lakini kuna muda ulifika sovieti serikali yao ilipiga marufuku jeshi lao kutumia helikopta au ndege katika anga la Afghanistan ila mpaka kukiwa na ulazima sana kufanya hivyo kwa ajili ya kiusalama na kwa gharama hiyo.

Sababu zilikuwa zinashambuliwa na maroketi (“RPG” angalia picha ya juu kielelezo) mengi na kudondoshwa. Mwishoni sovieti waliamua kuondoka sababu walishindwa vita hiyo na makabila ya waafghanistan licha ya kuwa umoja wa kisoviet ulikuwa taifa babe sawa sawa na marekani wakati huo. Kipindi hicho kulikuwa na kundi linaloitwa Mujahidina ambalo lilikuwa mstari wa mbele kupinga walichoamini ni utawala wa kimabavu kwa kulinda uhuru wao na kulipiza kisasi dhidi ya wasovieti na udhalimu wao kwa wananchi wa afghanistani.

MIKONONI MWA KIKUNDI CHA TALIBANI.

Kundi la mujahidina likachukua utawala rasmi baada ya kumaliza uwepo wa wasovieti nchini Afghanistan lakini kutokana na sababu ntakazozitaja hapo baadaye kukatokea mgawanyiko ndani ya mujahidina, wakaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe mwisho likazaliwa kundi la Talibani. Kundi hili likaanza upinzani na baadaye uasi likachukua nchi mwaka 1996.

Kukawa na utulivu mdogo wakati huo huo kukiwa na mapigano madogo madogo kati ya jamii za pale hasa wale wenye itikadi kali na wasio na itikadi kali pia kitokana na kanuni za sheria katika tamaduni zao ambazo wanazishika na kuzifuata sana.

MIKONONI MWA MAREKANI ( 2001 HADI 2017).

Baada ya Ndege mbili zinazosadikia kutumiwa na washirika wa Osama bin laden kuangusha majengo pacha ya biashara nchini marekani. Marekani anaingia rasmi katika vita na Afghanistan iliyo chini ya kundi la talibani. Kutokana na teknolojia na ubabe kijeshi marekani anaingia ijapokuwa anapata upinzani lakini anafanikiwa kuiangusha serikali ya kundi la Talibani. lakini licha ya nguvu za kijeshi, kiuchumi, kitamaduni na kitekinolojia kuna wakati inaripotiwa marekani ilikuwa inaangusha mabomu ya tani kubwa kubwa kiasi cha kufumua milima na kuleta maangamizi makubwa na kwa mashambulizi ya silaha nzito nzito dhidi ya watalibani ambao bado waliendelea kutoa upinzani hivyo hivyo tu kila kukicha hawakuweka silaha zao chini.

Ni miaka mingi imepita tangia vita hiyo ianze inaenda kutimia miaka 18 huku makadilio yaliyofanywa mpaka 2017 vita imeigharimu taifa la marekani kiasi dola bilioni 2.4 sawa na Shilingi trilioni 5,472,360,000,000,000.00 za kitanzania.

Na hakuna matumaini ya vita kuisha ijapokuwa tayari marekani kaanza kuyaondoa majeshi yake huku upinzani wa talibani ukiendelea kuchukua hatamu wakiteka vijiji, miji hadi majimbo.
upload_2018-5-7_15-26-4.png

(Uharibifu baada ya shambulizi la kujitoa muhanga ndani ya jengo la ibada nchini Afghanistan ).

Lakini licha ya kuwa na serikali ya mtu wa kwao kwa sasa anaowaita wasuluhishe mezani vita yao. Lakini jamii bado imegawanyika yapo makundi ya makabila na mabwana wa vita ambao wanaoiunga mkono serikali yao na wale wanaoiunga mkono Talibani, ambao wanapigana kila kukicha vijijini hadi kwenye miji.

FAHAMU KANUNI ZA TAMADUNI ZINAZOWAONGOZA WATU WA AFGHANISTANI “PAKHTUNWALI”.

Kwa karne nyingi sana tamaduni hii ya kabila ya pashtun imeendelea kushikiliwa na makabila ya hapo kiasi wao huiita “njia ya maisha”. Katika tamaduni hiyo ina vitu vikuu vitatu vinavyoitwa (i).Ukarimu (mermestia), (ii).ushujaa (tora) na (iii).kisasi (badal).

Katika jamii za wanadamu hasa wafugaji wa wanyama wale waporini au nyumbani kifupi si kitu rahisi ukakuta simba,chui au duma ukawamuweka mmoja wapo katika banda moja na swala au pundamilia walau hata kwa siku moja tu ni kitu hakuna mfugaji yoyote anayeweza kukubali hilo.

Hata Mbwa tu (mfano wa kisasi) wa nyumbani kama ukiwa haumpi matunzo mazuri halafu ukamuweka banda moja na Kuku au Sungura (mfano wa ukarimu) lazima utakuta siku moja kawatafuna tu wote lakini kwa Paka (mfano wa ushujaa) wataishi kwa kuogopana na ikiwemo ugomvi mara kwa mara usioisha mpaka mmoja atakapoondoka.

Tamaduni ya kulipa kisasi kwa makabila ya Afghanistan imeenda mbali sana kiasi kwamba unapomtukana mtu kwao utendaji haki kwa kosa hilo ni huyo mtukanwaji kuhakikisha kamtoa damu mtukanaji (Peghor) au mtuhumiwa. Yoyote anayevunja sheria za tamaduni yao akatoroka basi lazima kisasi kifanyike kwa ndugu zake wa karibu kwa niaba ya mtuhumiwa hata ikiwa kwa kumwaga damu.

Hivyo kama ukitaka kupona mkimbie woote wewe na ukoo wako wote. Adhabu ya kuuliwa ni kitu cha kawaida sana katika sheria zao, kama juzi ulimshinda vitani Babu yao afghanistani weka akilini na ufahamu tu baba na baba wadogo leo wapo njiani wanakuja kulipa kisasi kwa jamii yako yote, na ukiwashinda mababa ujue tu watoto na wajukuu wameshaanza kufundishwa namna ya kutumia siraha watakuja kesho kulipa kisasi.

Hivyo wao hupigana vizazi kwa vizazi na wakikushinda wakakuondoa kabisa baada ya muda wanaanza kugeukiana na kupigana wao kwa wao wenyewe kwa visa vyao vya zamani kabla wewe hujafika hapo.

MUHIMU

Fahamu kisasi ni kitamu nafsini mwa binadamu lakini kinamaliza mtu taratibu sana hiyo inakufunza leo unapoingalia jamii ya taifa la waafghanistani na nyingi baadhi ya hapa nyumbani Tanzania.

Kwa karne na karne nyingi kisasi hakimpi mtu suluhisho la kudumu au kumpa tulizo nafsini la kudumu ila ukoleza moto na moto na kisha maangamizi kwako na jamii zenu na mnayekosana naye.

MBINU UNAWEZA KUTUMIA KUACHILIA/KUWASAMEHE WANAOKUUDHI (ILI KUONDOA KINYONGO/KISASI).
upload_2018-5-7_15-26-17.png

(..Kusamehe ni uamuzi wa kumwachilia huru mfungwa, ambaye unagundua mfungwa huyo ni wewe mwenyewe." Lewis B. Smedes)

1. Kusamehe kwa kuupuza (win-win)

Hii mbinu ya kupuuzia tunaitumia sana pasipo kujua tunaitumia unakuta unatembea labda mtaani au hupo kwenye usafiri wa umma halafu mtu anakukwaza kwa namna yoyote ikiwa kukukanyaga halafu anajifanya hana habari anapita. Basi unachofanya unamuangalia tu halafu unacheka kidogo huku unatikisa kichwa, halafu unaendelea na simu yako au kuongea na jirani yako.

Mbinu hii inasaidia pia katika mazingira na mazingira tu hasa unapomuangalia mtendaji halafu unakataa kusababisha makubwa kwa vitu vidogo vidogo, hivyo unapata ahueni flani yaani mimi mshindi hata kama yeye kajifanya mshindi, siwezi poteza muda wangu kugombana na mtu asiyejielewa. Wakati mwingine unaamua kuondoka na kwenda mbali kidogo na huyo anayekuudhi kwa wakati huo.

Athari ya mbinu hii pia

Inahitaji hekima sana namna ya kutumia mbinu hii na pia inategemea na mahusiano na mtendaji na mtendwaji kutoa matokeo ya mbinu hii Mfanyakazi na Bosi wake, Mume na mke na Mtoto na Mzazi. Si rahisi kumfanyia bosi wako hivyo wakati anakuwakia kisawasawa au mume na mke sababu utakapotumia mbinu hii ni sawa unamwaga petrol kwenye moto uwe na uhakika tu kutatokea mlipuko zaidi.

2. Kusamehe kwa kulinda afya ya akili yako

Nakumbuka tulikuwa na mazungumzo na rafiki zangu niliokuwa nasoma nao chuoni. Katika kujadiliana hili na lile, kuna mmoja wetu akatangaza msamaha kwa kiongozi mmoja mkubwa nchini kwa sababu alizoziona yeye binafsi zimemuumiza. Sasa mmoja akamuuliza vipi mkubwa! Kwani? hata ukimsamehe yeye ana habari na wewe au anakufahamu. na yeye akamjibu ‘kwani kutoa msamaha anapata faida nani? Ni mimi mwenye kubeba uchungu au yeye anayeendelea maisha yake pasipo kuwa na tatizo lolote’.

Mbinu hii inasaidia sana kama unakuwa una uelewa kukaa na kinyongo kwa muda mrefu kunakufanya uanze kuharibu afya yako mwenyewe kwa magonjwa kama vile msongo wa mawazo (depression), kichwa na shingo kuumwa, tatizo la mifupa, vidonda vya tumbo na macho kuanza sumbua kuona vizuri.

Msomaji wangu hapa sasa utapita mwenyewe gharama ya kinyongo na ya kuachilia hipi unaweza ilipia?. Tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinasema asilimia 60 ya aina za kansa zinasababishwa na mtu kuwa na uchungu.
3. Kusamehe kwa matumaini.
upload_2018-5-7_15-26-29.png

(Kusamehe kwa kutumaini kunahitaji kubeba hekima na kutumia akili pia).

Ni rahisi sana kusamehe wale tunaowapenda na kuwajari sababu ya mahusiano yetu na wao. Tunasamehe kwa haraka sababu ya tumaini pengine hao wenza wetu siku za usoni watabadilika. Safari hii huwa ndefu kutokana na kuamini mtendaji siku moja atabadilisha mtazamo hasi au kile usichokipenda siku za mbeleni.

Uvumilivu, upendo na saburi ni moja ya vile vinavyotusaidia katika safari hii kupangua kila hoja ya machukizo na yale yanayotujeruhi kutoka kwa wale tunaowapenda kwakuwa hatutaki kuona wakiharibikiwa sababu upendo una nguvu sana kushinda mauti.

Ni safari ya matumaini inayohitaji sana hekima sababu wapo ambao wameweza kwenda nayo mpaka kupata matokeo ya kile walichokiamini lakini wapo walioishia njiani katika safari hiyo kwa kutumia hekima kuhusu kesho itakuwa vipi, na pia lipo kundi ambalo lilijitoa hadi mwisho na mambo hayakuwa sawa tena walijikuta na wao wamebeba mizigo ya wenza wao na pengine hivi sasa wanajutia kwanini wasingeishia njiani wakafanya mengine tu.

Kifupi kusamehe kwa matumaini kuna matokeo ya aina mbili hapo baadae yale tulioyatarajia na yale hatutayatarajia. Kama umebeba uvumilivu, saburi na upendo katika safari hiyo usiache pia hekima na akili nyuma.

4. Kusamehe kwa imani.

“..Dini kubwa ulimwenguni zina mapokeo yanayobeba ujumbe wa msingi kuhusu Upendo, huruma na msamaha. vitu muhimu kuwa sehemu ya maisha yetu kila siku..” Dalai Lama

Kila imani ilumwenguni ina jambo la kueleza kuhusu msamaha na kuachilia pasipo kinyongo ili uweze kupokea thawabu kwa Mungu muumba mbingu na nchi. mfano

Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.

Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana

Hivyo unapokuza katika sababu moja wapo ya kusamehe waliokukosea unaweza kufanya hivyo ka kuangazia hasa maandiko ya imani na ukapata stamina ya kusamehe bure bila kutazamia chochote kwa binadamu mwenzako, ili uweze kupokea thawabu kwa Mungu.

Na kwa kutumia sababu au kigezo hiki kunaifanya ulimwengu wako wa ndani kusonga mbele.

5. Kusamehe kutokana na upana wa uelewa wako juu ya maisha. (Hekima)
upload_2018-5-7_15-26-48.png

(“..Mimi siyo mtakatifu, labda ufikirie ni mtakatifu mwenye dhambi anayejaribu tu...” Nelson Madiba Mandela )

Napenda kuanza kwa kumnukuu waziri mkuu wa kwanza wa India bwana Mohandas Gandhi ambaye wengi tunamfahamu kwa jina la Mahatma Gandhi aliwahi kunukuliwa akisema

“..The weak can never forgive. Forgiveness is the attribute of the strong…” Kwa tafsiri nyepesi ni kwamba watu dhaifu kamwe hawawezi kusamehe, kusamehe ni kwaajili ya watu wenye nguvu. Na nguvu aliyoizungumzia bwana Mahatma Gandhi ni ile hekima ya mtu kwenye fikra zake. Nianze kwa kutafsiri msamiati “hekima” maana yake

Tafsiri ya msamiati Hekima
Ni akili inayomwezesha mtu kufikiri na kuweza kutoa uamuzi unaofaa.busara au maarifa ya kufikiri na kuamua jambo linalofaa ambayo mtu huyapata kutokana na uzoefu wa muda mrefu. (Kamusi ya Kiswahili ya karne ya 21)


Kusamehe mtu na kutoa kinyongo ndani yako sio udhaifu ila inataka sana upana na uelewa wa fikra zako katika maisha. Pale unapoelewa madhaifu yako kama mwanadamu na kukubali kila mwanadamu ana mapungufu yake na kuhitimisha hakuna mkamilifu chini ya jua.

Pia unapofikiri kusamehe hakuwezi kubadili yaliyopita lakini kunatoa ongezeko katika kutazamia kesho yako kiafya, kifikra na kimaendeleo.

*Mwisho*

Pia ili huweze kufuatilia vizuri mafundisho haya kuhusu Saikolojia na maisha ni vizuri kama utaanza ni follow katika akaunti yangu “Education mentor” niombe radhi tu kwa wale walioniomba kuwatag hinaniwia vigumu kukumbuka majina yote.

Na pia kuhusu Maswali yoyote ya kisaikolojia na maisha unaweza niuliza PM na mimi ntayajibu kwa mfumo wa makala au “mada”.

KUHUSU MWANDISHI,

Education Mentor ana shahada ya Saikolojia, ni mwanasaikolojia anayeegemea kutambua uwepo na asili ya Mwanadamu inatokana na Mungu (Creation Theory).

Pia ni Msomaji wa Vitabu vinavyohusu Falsafa, Nyurolojia, Historia, Maandiko pamoja na Vitabu vinavyooelezea maisha ya watu mashuhuri (Biography book).

Makala nyingine alizoandika Education Mentor..
Saikolojia: Fahamu tabia ya hasira, madhara yake na namna za kuishinda

Saikolojia: Sababu zinazosababisha magonjwa ya akili ambazo wengi hawafahamu. (psychological disorder)

Saikolojia:Jifunze mambo yakayokusaidia kuwa na maisha yenye furaha (Case study Finland)

Saikolojia: Jifunze mambo yatakayokusaidia kuwa na maisha yenye furaha (sehemu ya pili)

Saikolojia: Fahamu magonjwa ya kisaikolojia, dalili,tabia na mifano.(Case study Tanzania) 

Wervemarcel

JF-Expert Member
Apr 10, 2015
2,395
2,000
Worth Reading.
Nimeifungua Asubuhi Baada Ya Kujitafakari Nimesamehe Ninaowachukia Hasa Viongozi Kama Huyu JPM. Nipo Mwepesi.
 

MZEE MKUBWA

JF-Expert Member
Jun 24, 2017
4,106
2,000
Kweli kuna nguvu kubwa ya kusamehe niliishi maisha ya kinyonge kutokana na chuki ndani yangu.

Nilipoweza kutoa msamaha siku hiyo hiyo nilihisi kitu kizito kimetoka moyoni mwangu

Ila lazima uwe na nguvu ya kusamehe ambayo mahatma Gandhi anaiita hekima ya kuweza kufikiri
 

bwii

JF-Expert Member
May 24, 2014
1,226
2,000
Kilipa kisasi inaonyesha wewe ni dhaifu,,ila kusamehe inaonuesha jinsi ulivyo strong!
 

KENZY

JF-Expert Member
Dec 27, 2015
19,143
2,000
ninamtindo wa kupuuza!

lkn mkuu kuwa na hizo hali (hasira,kisasi n.k) sini tabia za kimakundi..? mfano melancolin kuwa na uwezo mkubwa kiakili,vivyohivyo kuna watu wa kundi fulani wanakuwa na tabia fulani(kisasi) au ni tofauti na ninavyodhani..?
 

Education Mentor

JF-Expert Member
Oct 26, 2016
392
1,000
ninamtindo wa kupuuza!

lkn mkuu kuwa na hizo hali (hasira,kisasi n.k) sini tabia za kimakundi..? mfano melancolin kuwa na uwezo mkubwa kiakili,vivyohivyo kuna watu wa kundi fulani wanakuwa na tabia fulani(kisasi) au ni tofauti na ninavyodhani..?

Unapozungumzia nadharia za makundi ya personality fahamu cha kwanza sio lazima uwe na tabia hizo zoote sababu tuna malezi na mazingira tofautitofauti kila mwanadamu

lakini kuna viwango tu vinavyoweza kukujumuisha kundi la personality

mfano mtu mwenye max 75 na mwenye 90 wote wanajumuishwa viwango vya kundi "A" lakini yupo aliefanya vzr zaidi na Yule aliepata kawaida.

Vivyo hivyo unaweza ukawa melancholic 70% lkn unavitu umeviokotaokota kwengine Phlegmatic 10% sanguine 15% Na choleric 5%......hvyo hutajumuishwa kule umeangukia sana
 
Jan 25, 2018
49
95
Kweli msamaha unahitaji hekima,upendo na akili ukijumlisha nguvu ya ujasiri na uwepo wa kupuuzia, mkuu kila siku napata jipya kupitia kwako.
 
Jan 25, 2018
49
95
Hakika mkuu unatufundisha kitu uchao,nitasamehe wote kwa kwa kutumia kupuuzia,hekima,nguvu,imani pamoja na upeo wa akili yangu amayo leo umeipa muongozo mpya juu ya msamaha.
 

Education Mentor

JF-Expert Member
Oct 26, 2016
392
1,000
asanteni na karibuni wasomaji wapya wa Makala nazoandika.......nafurahia kuwafikia kila leo napoandika makala mpya changamoto kuwakumbuka woote ndio maana nawaomba kunifollow ili iwe rahisi kwangu.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom