Safari ya Pompeo Russia: Jitihada zilizofeli za kupunguza hitilafu baina ya Washington na Moscow

kimsboy

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
8,991
17,887
Safari ya Pompeo Russia: Jitihada zilizofeli za kupunguza hitilafu baina ya Washington na Moscow
Mei 16, 2019 02:34 UTC
Uhusiano wa Marekani na Russia katika zama za baada ya vita baridi umekumbwa na pandashuka nyingi sana. Pamoja na hayo mgogoro wa Ukraine mwaka 2014, na baada ya hapo, yaani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uhusiano wa Moscow na Washington umechukua mkondo wa kuzorota na hali imekuwa mbaya zaidi baada ya Marekani kuiwekea Russia vikwazo.
Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani siku ya Jumanne 14 Mei alifika mjini Sochi ulio katika pwani ya Bahari Nyeusi nchini Russia na kukutana na wakuu wa ngazi za juu wa Russia yaani Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov na Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo.
Lengo la safari ya Pompeo lilikuwa ni kujaribu kupunguza hitilafu baina ya Russia na Marekani katika mambo ambayo nchi mbili zinahitilafiana.
Kuhusiana na hilo, Pompeo alisema: "Si sawa inaposemwa kuwa sisi ni washindani katika sekta zote. Natumai kuwa tunaweza kupata nyuga ambazo tutakuwa na maslahi ya pamoja. Nadhani kuwa tunaweza kufikia maelewano katika maudhui za kudhibiti silaha, kuzuia uenezwaji silaha za nyuklia, migogoro ya kieneo na ugaidi."
Lakini licha ya matamshi hayo ya Pompeo, ukweli ni kuwa sera za Marekani kuhusu Russia katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa za uhasama na mashinikizo ya pande zote.
Maslahi ya madola hayo mawili makubwa duniani yanakinzana katika masuala kama vile uwezo wa kinyuklia, nishati, ushawishi katika maeneo ya Ulaya Mashariki, Asia Magharibi na Amerika ya Latini. Hitilafu hizo zimepelekea hata Marekani itangaze katika mipango yake Stratijia ya Usalama wa Taifa, Stratijia ya Ulinzi wa Kitaifa na Sera Mpya za Nyuklia kuwa, Russia ni tishio kubwa zaidi kwa Marekani na pia ni tishio nambari moja la nyuklia. Uhasama huo wa Marekani dhidi ya Russia nao haujabakia bila jibu kutoka kwa wakuu wa Moscow.
Hali kadhalika Russia imekuwa ikituhumiwa kuwa iliingilia uchaguzi wa Rais wa Marekani mwaka 2016 jambo ambalo lilipelekea wakuu wa Washington waiwekee vikwazo vipya katika fremu ya Sheria ya Caatsa. Serikali ya Trump imetumia kisingizo hicho kuweka vizingiti katika uhusiano wa kiuchumi wa Russia na Ulaya hasa kujaribu kuzuia ujenzi wa bomba la mafuta la Nord Stream 2 la gesi kutoka Russia hadi Ujerumani.
Katika mkutano wake na Pompeo, Rais Vladimir Putin ameashiria vikwazo ambavyo Marekani imeiwekea kwa kisingizio cha Sheria ya Caatsa na kusema: "Ripoti ya Robert Mueller (mchunguzi wa faili la madai ya Russia kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016) imebaini kuwa hakukuwa na njama yoyote baina ya serikali ya Trump na Russia."
Pamoja na kuwepo hitilafu nyingi baina ya pande mbili, lakini Russia imesema inaunga mkono kuboreshwa uhusiano na Marekani. Kuhusiana na hilo, Sergei Lavrov katika mkutano wake na Pompeo mjini Sochi ametangaza kuwa, umewadia wakati wa kuanzishwa muundo mpya katika uhusiano wa Marekani na Russia huku akisema nchi yake iko tayari kwa ajili ya kadhia hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani naye amedai kuwa Donald Trump anafungamna na uimarishwaji uhusiano na Russia pamoja na kuwa kuna hitilafu baina ya pande mbili.
Lakini wakuu wa Russia wamesisitiza kuwa hadi sasa hakuna hatua zozote zilizipigwa katika uimarishwaji wa uhusiano wa pande mbili. Kimsingi ni kuwa wakati hakuna nukta za pamoja ambazo pande mbili zinaafikia ili kusogeza mbele mazungumzo, basi mazungumzo kama hayo hayatakuwa na natija.
Kama alivosema Yuri Viktorovich Ushakov mshauri wa Rais wa Russia: "Katika mazungumzo ya Vladimir Putin na Mike Pompeo hakuna mafanikio yoyote yaliyopatikana lakini Marekani imeyatathmini mazungumzo hayo kuwa mazuri."
Kwa maelezo hayo tunapapaswa kutaraji kuendelea kuwepo hitilafu na msuguano baina ya Marekani katika masuala kama vile mapatano ya nyuklia ya Iran, maarufu kama JCPOA, na masuala mengine ya kimataifa.
Russia inaamini kuwa, Marekani ndiye mhusika mkuu wa hali ya hivi sasa ya kuvurugika mapatano ya JCPOA hasa baada ya Iran kutangaza kuwa inasitisha kwa muda utekelezwaji wa baadhi ya ahadi zake katika JCPOA.
Lavrov ameasiria kadhia ya JCPOA na kusema: "Russia na Marekani zina hitilafu nyingi sana kuhusu kadhia hii. Aidha ameashiria hatua za Marekani dhidi ya Iran ambazo zimepelekea kuibuka mgogoro katika eneo na kusema: "Kujiondoa katika Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na vikwazo vipya vya ununuzi wa mafuta ya Iran ni mambo ambayo yatapelekea kuongezeka mgogoro katika eneo."
 
Back
Top Bottom