Safari ya Mei mosi na harakati za Wafanyakazi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Safari ya Mei mosi na harakati za Wafanyakazi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Consigliere, Apr 28, 2011.

 1. Consigliere

  Consigliere JF-Expert Member

  #1
  Apr 28, 2011
  Joined: Sep 9, 2010
  Messages: 8,063
  Likes Received: 7,530
  Trophy Points: 280
  Mei mosi ni siku ambayo wafanyakazi wote nchini wanaungana na wenzao wengine duniani kuazimisha siku yao ya Kimataifa na mimi nikiwa mmoja wa wanaothamini mchngo wao katika jamii napenda kuchukua fursa hii kuwatakia maadhimisho yenye mafanikio na malengo yenye kutizika.

  Mei Mosi(May Day) ni jina la sikukuu tofauti tofauti ambazo huazimishwa kila tarehe moja ya mwezi wa tano. Lakini kubwa na iliyo maarufu zaidi ni siku ya kimataifa ya wafanyakazi, ambayo ni ukumbusho wa mafananikio ya kijamii na kiuchumi yakiwa ni matokeo yaliyoletwa na vuguvugu la wafanyakazi. Tarehe moja ya mwezi Mei hutumika kwa sababu mwaka 1884 Shirikisho la muungano wa Wafanyabiashara na Wafanyakazi, lililoanzishwa na wafanyakazi mwaka1872 huko Canada, lilipigania kuwepo kwa masaa nane tu ya kufanya kazi kwa siku wakiwa wamevutiwa na hatua waliyoichukua wenzao wa Canada Wafanyakazi wa Marekani nao wakadai kuwepo na muda kama huo wa kufanya kufanyakazi nchini mwao ifikapo Mei mosi mwaka 1886. Hali hii ilisababisha hali ya vurugu na kuyumba kwa soko la marekani na hii ilikuwa mwaka 1886, pia huu ndiyo ukawa mwanzo rasmi wa utaratibu wa kufanya kazi kwa masaa nane tu kwa siku nchini Marekani.
  Marekani ni moja kati ya nchi chache duniani ambazo huwa hazina maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi. Moja ya sababu hizi ni kitendo cha wafanyakazi wa nchini humo kuamua kwa sauti moja kupigania madai yao ya msingi kabisa, katika kupigania huko kulipelekea hali ya soko na uchumi wa taifa hilo kuyumba. Pamoja na kuwa historia ya mapambano baina ya matabaka ilianza miaka mingi sana nyuma kabla hata ya zile zilizoanzia Canada na Marekani, lakini kumbu kumbu za karibuni na nzuri zaidi ambazo zilipelekea kuzitikisa hata serikali za nchi husika na ambazo zikaambukiza mataifa mengine ni hizo za nchi hizo mbili japo kwa upande wa nchi ya Canada kwenyewe ambapo ndipo harakati zilipoanzia, hawakuwa na athari kubwa ukilinganisha na nchi ya Marekani ingawa haukuripotiwa umwagaji wa damu, lakini kwa hali yoyote ile kitendo cha kufanya uchumi na soko la nchi hiyo kuyumba iliumiza vichwa vya viongozi wa taifa hilo na kuwapa hasira juu ya harakati zile. Pia sababu nyingine ambayo pia ni ya msingi kabisa iliyopelekea Marekani kuweka kinyongo au hasira juu ya madai ya wafanyakazi ni ukweli kuwa harakati zile za wafanyakazi zilianzia nje ya Marekani yenyewe na zilikuwa ni zao la watu wenye itikadi pinzani na zile za kwao yaani za Kikomunist dhidi ya Zile za Kibepari ambazo walikuwa wanazifuata wao, na kwa kuwa watetezi wakubwa wa tabaka hili la wafanyakazi walikuwa ni watu kama wakina Fredrick Engels, Karl max na wengineo ambao pia kimtazamo walikuwa ni mihimili mikubwa ya itikadi za Kikomunist. Itikadi ambazo zilikuwa zikitetea kwa nguvu zote tabaka la wafanyakazi ambalo ni la wazalishaji (nguvukazi) dhidi ya lile la mabepari ambalo lilianza kuibuka kuchukua nafasi ya ukabaila katika miaka ya 1840, na hivyo kufanya matabaka haya mawili kuwa katika uhasama mkubwa japokuwa shughuli zao za kila siku zinategemeana kama viungo vya mwili.
  Katika manifesto ya Kikomunisti mfanyakazi anashauriwa kuufahamu ubepari kwa undani kwanza, ili aweze kujihami nao, kwani kama nilivyokwisha eleza hapo juu, kuukwepa ni kitu kisichowezekana kwa jinsi matabaka haya yanavyotegemeana.
  Katika kuhakikisha kuwa haiipi heshima wala upekee wowote na kendelea kuifunika siku hii katika mipaka ya nchi yake, Serikali ya Marekani imeweka siku nyingine rasmi za kiserikali katika tarehe hii hivyo kufunika uwezekano wowote wa siku hii kuwa rasmi na ya kiserikali ndani ya nchi hiyo.
  Kwa upande wa Uingereza mitazamo ya kisiasa huicha imegawanyika katika kambi mbili. Kambi ya kwanza ni kundi kubwa la wahafidhina ambalo husherehekea May day jumatatu ya kwanza ya mwezi wa Mei ambayo kwa nchini Uingereza hujulikana kama “Spring Bank Holiday”. Siku hii huitwa hivyo kwa sababu ni siku ambayo benki zote hufungwa ( Pia kwa kawaida siku za mapumziko nchini Uingereza huitwa Bank Holiday), kwa kuwa shughuli karibu nyingi huusisha mzunguko wa pesa, hivyo siku hii huwa ni mapumziko kwasababu katika siku hii hakuna utaratibu wowote wa utoaji na uwekaji pesa katika benki nchini humo ambao hufanyika. Pia kwa kuwa uingereza nayo ni moja ya nchi za kibepari ambazo ziliathirika na harakati za wafanayakazi katika kudai haki zao, ambazo pia ni moja ya zao la itikadi za Kikomunist nayo haiipi upekee sana siku hii.Kambi ya pili ina kundi dogo ambalo hujumusisha (si moja kwa moja) vyama vya “The Labour Party, The Scottish Socialist Party,The Communist Party of Britain,The Socialist Workers Party na vyama vinginevyo vya mlengo wa kushoto, kundi hili hujumuika na wenzao wa sehemu mbali mbali katika kupongezana na kuweka mikakati mipya katika kufikia malengo ya wafanyakazi na ya kijamii kwa ujmla.
  Wakati mwingine harakati na madai ya wafanyakazi yalitumiwa na yangali yanatumiwa tuangalie ukweli huu katika kile ambacho kilpata kutokea nchini ujerumani na wanasiasa katika kufikia malengo yao katika uwanja wao wa siasa. Tunaambiwa kuwa nchini Ujerumani kulikuwa na kawaida ya kuwa na maandamano ya kila katika siku hii ya Wafanyakazi. Lakini mnapo mwaka 1929 serikali ya chama Social Democratic (SPD) iliyapiga marufuku maandamano hayo ya kuadhimisha siku ya Wafanyakazi, lakini chama cha Kikomunist cha KPD, ambacho ndiyo kilikuwa na nguvu mjini Berlin bado kiliitisha maandamano ambayo mpaka jua lilipokabidhi zamu kwa giza kushika hatamu yalikuwa, yamegharimu maisha ya waandamanaji, wafanyakazi, pamoja na watu wengine 32 waliouawa na Polisi, na ikiwaacha watu wasiopungua 80 wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Polisi wa mjini berlin chini ya maelekezo ya wataalam wa serikali ya chama SPD, walifyatua jumla ya risasi 11,000 hadharani katika kuhakikisha wanayadhibiti maandamano hayo.
  Tukio hili linalokumbukwa kwa lugha ya kijerumani kama Blutmai (Blood May), liliongeza uhasama kati ya vyama SPD na KPD. Wakati ufa wa mahusiano kati ya vyama hivi viwili vikubwa ukiwa umeshaongezeka sana, hapo ndipo Manazi walipopata njia ya kupita na hatimaye kujikuta wamefaidika na mahusiano hayo mabovu ya vyama hivyo vikubwa, ambavyo vilishindwa kukaa na kuunda nguvu ya pamoja dhidi ya manazi, ambao baadae walikuja kuunda serikali na hivyo kuwa chama tawala cha cha Ujerumani na hiyo ilikuwa ni mwaka 1933. Manazi waliitumia may day kwa malengo yao wakiita “siku ya kazi” ambayo mpaka sasa badi ni jina rasmi la sikukuu hiyo ya Kitaifa. Kwa moyo wa ajabu na macho makavu kabisa siku mojaa baada maadhimisho ya Mei mosi kufanyika na kufana sana, yaani Mei 2, 1933, Manazi walifuta (walipiga marufuku) vyama vyote huru vya wafanyakazi, pamoja na mashirikishi yote ya wafanyakazi nchini humo. Badala yake mwaka 1934 Reichsabeitsdienst (au RAD, Reich Labour Service) kikaundwa kama mbadala wa vyama vyote vilivyofutwa. Hata leo nchini Ujerumani maadhimisho ya siku ya wafanyakazi ni ya umuhimu mkubwa sana kisiasa, kwa sababu mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi na vyama vya kisiasa hutumia siku hii kufanya kampeni na majukumu mengine ya kisiasa, ila tangu mwaka 1987 maadhimsho ya Mei mosi nchini Ujerumani yamekuwa yakiambatana na vurugu kubwa zisababishwazo na wanasiasa wenye wahafidhina wa mlengo wa kushoto, (wapenda mabadiliko), pamoja na makundi ya vijana wawachukiao askari Polisi hivyo huyatumia maandamano hayo kuanzisha mapambano dhidi ya askari hao, hii kisaikolojia tunaweza tukasema wanatafuta tiba kwa kufanya kile ambacho kwa mtazamo wao ni kikwazo cha malengo yao hisia zao au hisia zao, kwa kifupi sana unaweza ukaiita saikoljia ya makundi. Ila taarifa zianonyesha kuwa maadhimsho ya siku ya wafanyakzi ya mwaka 2005 mjini Berlin ndiyo yaliyokuwa ya amani na utulivu katika miaka 23 iliyopita. Bila shaka mpaka hapo utakuwa umepata picha ya jinsi gani wanasiasa katika baadhi ya nchi wanavyowaona wafanyakazi kama nyenzo muhimu katika kufikia malengo yao na jinsi sauti ya na jamii ya wafanyakazi ilivyo na nguvu kama tu itafahamu jinsi ya kuzitumia karata zake.Pia nchi nyingine kama vile Australia Canada na NewZealand huadhimisha siku hii katika siku tofauti tofauti na kilichopelekea hali hiyo ni historia au asili ya siku yenyewe katika siku hizo.
  Mwaka 1955 Kanisa Catholic katika kuadhimisha siku hii ya wafanyakazi iliamua kuongeza siku kuu nyingine ya Mt Joseph (Mt. Joseph yule ambaye alikuwa Mchumba na baba mlishi wa Yesu Kristo, ambaye ni ndiye msingi, nguzo na muongozo wa imani ya Ki-kristo) ambayo ilipewa jina rasmi la siku kuu ya Mt. Joseph Mfanyakazi. Kulingana na historia niliyoieleza hapo juu kuhusu harakati za wafanyakazi na kiini hasa cha maadhimisho ya Mei mosi Labda inaweza ikashangaza na kufanya wadadisi wajiulize kwa nini kanisa halikuchukua hatua za kuitambua hatua hii mapema, lililo dhahiri hapa ni kuwa kanisa ilibidi iwe makini sana katika kufanya maamuzi kwa sababu kama tulivyoona kuwa harakati zenyewe zilihusisha itikadi za watu na kuwa vita kati ya tabaka na tabaka na kuharibu mahusiano ya watu katika ya jamii zao. Pia Kanisa lilikuwa likitafuta kwa makini uwezekano wa kuvuta hisia za watu kutoka katika maadhimisho ya Mei mosi ya “Kipagani” ambayo labda pia ingepunguza au kuondoa vita na chuki za kiitikadi ndani ya jamii na hatimaye kuzigeuza tofauti hizo kuwa changamoto katika kujilete maendeleo

  Baada ya kuona au kusikia harakati na mafanikio ya wafanyakazi wenzao, wafanyakazi wa nchi nyingine nao wakaona ni jambo jema kama watakuwa na chombo cha kuwaongoza katika kutetea maslahi yao katika maeneo yao ya kazi, na katika kubadilishana mawazo vyama kutoka nchi nyingi vikakubaliana kuwa na maadhimsho rasmi katika tarehe na siku moja ya kila mwaka japo baadhi ya nchi zikaenda na utaratibu wao katika kuadhimisha siku hii. Kadirimiaka ilivyokuwa inakwenda ndivyo vyama vingi vya kutetea maslahi ya wafanyakazi vikaanzishwa na vyote vilijipatia nguvu katika nchi zao kwa sababu mvuto wake ulikuwa ni mkubwa, kutokana na ukweli kwamba tabaka la wafanyakazi ni kubwa, na nyuma yake siku zote kuna jamii inayowategemea kutokana na kazi zao hizo hivyo unavyzungumzia wafanyakazi unakuwa unaigusa sehemu kubwa sna ya jamii. Wakati katika nchi kama Ujerumani na Uingereza na kwingineko vyama hivi vilisaidia au vilijiingiza moja kwa moja katika siasa, kwa nchi kama Tanzania vilidhibitiwa na kupewa mipaka ya shughuli na msisitizo zaidi ukiwa vyama hivi kutojihusisha na siasa, kwani walishaiona nguvu ya tabaka hili la wafanyakazi jinsi ilivyokubwa na inavyoweza kuanzisha harakati na kufikia malengo kwa muda mfupi, na hakika katika hili viongozi wa serikali za nchi zetu zilikuwa zimefanikiwa kulinda maslahi yao. Pia ikumbukwe kuwa suala la maadhimisho ya Mei mosi katika nchi nyingi halikuja kirahisi kama wengi wanavyoweza wakafikiri bali huko pia ilibidi yawekwe mashinikizo au kujengwa hoja za kuifanya siku hiyo iingizwe katika siku kuu rasmi za serikali, japo kuna nchi nyingine zilipewa kama zawadi ili kuweza kuwafumba mdomo kuhusiana na madai mengine ya kimsingi.

  Hali ya wafanyakazi katika Tanzania na nini kifanyike

  Hali ya wafanyakazi nchini Tanzania ni ya kusikitisha sana. Na hii inachangiwa na ukweli kuwa katika dunia hii ya utandawazi waajiri (Mabepari) wameendelea kutafuta faida zaidi, kuliko kujali maslahi na hali za wazalishaji, hakika hali imebadilisha kabisa, ni aina ya mfumo ambao umeondoa kabisa heshima na mahusiano mazuri katika jamii. Mimi nikiwa ni mmoja wa watu ambao wamewahi ajiriwa pia nimepitia katika nyakati hizi ngumu na za zenye makwazo mengi, kwasababu katika kampuni nyingi za kigeni na hata zile za ndani ambazo utendaji wake ni wa kutegemea “kuungiwa line” zaidi kuliko uwajibikaji huko hali huwa ngumu sana, inafikia wakati baadhi ya watu kwa kutumia nafasi walizopewa kuwasumbua na kuwaweka wenzao chini ya mashinikizo, wanajiona ni watu wa kipekee wanasahau kuwa hata kama wote tungekuwa na sifa za aina moja bado ni mmoja au namba fulani tu miongoni mwetu ambao wangepewa nafasi ya kuongoza,
  Wengine hupenda waonekane miungu watu, na kama anatokea mtu mwenye msimamo usioyumba na anayefahamu wajibu na mipaka ya kazi yake , basi huyo watamchukia na kuanza kumfanyia vituko, kuna wakati niliwahi hisi kuwa kama wangekuwa na uwezo na ili kuendelea kukusumbua basi wangeamuru mshahara wako uhamishwe ili uwe unakwenda kuuchukulia katika mifuk ya hifadhi ya kijamii au BIMA, kwakweli maudhi yanakuwa ni ya hali ya juu sana na wafanyao mambo haya si waajiri bali ni “marafiki zao” wafanyakazi ambao wamepewa nafasi za kuwaongoza wenzao hivyo hutumia ukaribu wa kikazi na waajiri kudidimiza juhudi za wenzao, na hata pale ambapo utakuta kuna matawi ya mashirisho au vyama vya kutetea haki za wafanyakazi, hali imekuwa ni ile ile, viongozi ambao wafanyakazi wamekuwa wakitegemea wangesimama kuwatetea nao wamekuwa wakiziba midomo wasije wakaharibu uhusiano wao na waajiri.
  Pamoja na kuwa na vyama vya wafanyakazi bado matumaini ya mfanyakazi katika Tanzania yanaendelea kudidimia nafahamu fika kuwa katika vita hii ya kimatabaka pia wafanyakazi wana mapungufu yao tena makubwa tu na mengine ni ya aibu, lakini bado ukweli unabaki kuwa hakuna ulinganifu wowote wa kitakwimu katika hili. Ni kweli aina ya mfumo unaohodhi uchumi kwa sasa umeweza sana tena sana kumudu soko la la mahitaji na ushindani katika uzalishaji wa bidhaa na ni aina hii ya mfumo ambao imethibitisha uwezo mkubwa wa binaadam katika kupambana na mazingira yamzungukayo, hakika ni mfumo ambao unastahili heshima ya kipekee, lakini unahitaji kuilinda heshima na mafanikio yake hayo kwa kulijali na tabaka la wafanyakazi, na kutambua kwamba ni tabaka muhimu (tabaka wezeshaji)katika kutimiza malengo yako. Kwasababu hapa hata tukiyaweka kwenye mizani matabaka haya mawili utona mchanganuo wake ni rahisi tu, angalia ..mfanyakazi ana ujuzi pia nguvu , upande wapili muwekezaji/mfanyabiashara au tumuite muajiri, yeye ana mtaji. Hapa kundi moja linhitaji ujuzi na nguvu kazi katika kufikia malengo yake na kundi jingine linhitaji pesa ili nali litimize malengo yake pia, hivyo nadhani kwa mchanganuo huu naweza nikaeleweka zaidi kuwa ninaongelea kitu gani. Waajiri wanatakiwa wajirekebisha haraka sana kadri mitaji yao inavyokua kwa sababu mtaji unapokua waajiri watahitaji kupanua miradi yao, na ikibidi kufungua mingine kwa kufanya hivyo ni dhahiri watahitaji nguvukazi (wafanyakazi) zaidi, sasa kama wataendelea kuwafanyanyia ukandamizaji je si watakuwa wamejilimbikizia mabomu chini ya vitanda walaliavyo au katika ardhi wailimayo? Hapa wafanyakazi ni sawa na mabomu yanayosubiri kulipuka wakati wowote ule mara tu watakapotoka nje ya mstari wa subira na uvumilivu,(pia ieleweke kuwa Mfanyakazi anayekandamizwa na kunyimwa haki zake ni sawa na silaha inayosubiri kutumika dhidi ya muajiri) ninatoa usia tena kwa waajiri wapendeni wafanyakazi wenu na muwafanye waione kazi yao kama sehemu ya familia zao, kwani watazipenda sana kazi zao na kuzitumikia kwa mioyo yao yote na kuwajibika kama wafanyavyo kwa jamaa wa familia zao. Baadhi ya haki za wafanyakazi ambazo inawapasa waajiri waziangalie kwa makini ni kama vile; wakuu wa vitengo kuwa na sifa ili waweze kuwa msaada kwa wafanyakazi mara tu utakiwapo, wawe pia ni watu wenye kujali na sio watu wanaosubiri kosa litendeke ili wapate nafasi ya kuonekana miungu watu, makato ya wafanyakazi kuwasilishwa katika vyombo vinavyostahili ndani ya muda , malamiko yao kusikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi haraka ili kuruhusu shughuli nyingine ziendelee katika kiwango kilichokusudiwa,
  Napenda kumaliza makala hii kwa kuhimiza tena mahusiano mazuri ya kimatabaka katika jamii, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanya jambo la manufaa kwetu sote, na hakutakuwa na majuto na kila tabaka kwa nafasi yake litafanikiwa katika malengo yake bila ya kuwa na hisia wala vivuli vya lawama.
  Na hapa serikalikali inabidi iwe mfano hai, kwa sababu mbali ya kutakiwa kuwa katika nafasi ya kuangalia na kuzilinda haki za matabaka yote mawili, pia inahusika moja kwa moja na kujikuta ikiwa na kofia mbili ya kwanza kama waangalizi wa haki, la pili inabaki katika kundi la waajiri, na waajiri walipo serikalini nao matatizo ya kwao ni mengi na serikali inashindwa kuwatimizia ndani ya muda muafaka kwa visingizio ambavyo haviingii akilini kama vile ina majukumu mengi, na kusahau kuwa matatizo au mafanikio ya wafanyakazi wao yanaihusu moja kwa moja,
  Ahsante kwa kufuatilia makala hii na ninawatakia tafakari njema

  Kwa hisani ya

  Thaddeus Musembi
   
Loading...