Safari ya Bulicheka na mke wake katika nchi ya Wagagagigikoko.

Sehemu ya Tatu

Siku moja Bulicheka alikuwa chumbani mwake saa za usiku. Mara akasikia mlio wa ajabu. Akasikiliza zaidi, akafikiri labda mnyama wa msituni au wa porini ndiye aliyepaliza sauti yake. Kumbe, sivyo!

Mlinzi yule mwenye kazi ya kuulinda mji wakati watu wamelala, alikuwa akiipiga mbiu yake kwa nguvu zake zote.

1631989285263.png


Watu wote wakashtuka, wakazindukana katika usingizi wao, wakaruka kutoka vitandani, wakatoka nje kuangalia kuna nini? Karibu wote walichukua mikuki yao, kadhalika mishale na ngao, wakifikiri kuna vita. Kumbe haikuwako vita yoyote, bali mji wao ulikuwa ukiteketea kwa moto.

1631989255329.png


Nyumba mbili zilikuwa zimekwisha shika moto. Moshi mzito ulitoka katika mapaa, na cheche za moto zikarushwa angani, zikapeperushwa na upepo na kuangushwa katika nyumba nyingine.

Watu wote wakahangaika sana kuyaezua manyasi juu ya mapaa, na kuvitoa vyombo vyao nje, ili wasipate hasara kubwa mno.

Hata Bulicheka alikwenda, kwa haraka sana, kuwasaidia watu wake. Aliona ni jambo muhimu kwa mfalme kuwasaidia watu wa nchi yake. Akaingia katika nyumba zilizoshika moto, ili apate kuangalia kama watu wote walikuwa wamekisha kutoka, na kama vyombo vyote vimeondolewa au hapana.

Bulicheka akawa shujaa sana. akapitapita katikati ya ndimi za moto bila kuogopa hata kidogo. Moshi ukamwingia machoni, lakini hakujali. Mikono yake ikapata malengelenge, bali yeye akavumilia tu. Watu wote wakahakikisha kwamba huyu ni shujaa kweli kweli.

Mwishowe, akakutana na mtu mmoja aliyekuwa akilia machozi, anapiga yowe na kulalamika.

Akamuuliza, “Kuna nini, mama? Una uchungu gani?”

Akajibu, “Mtoto wangu amebaki ndani ya nyumba yangu, nami siwezi kuingia nimtoe sababu ya moto.”

Bulicheka akasema, “Niambie upesi yumo katika nyumba gani?”

Akajibu, “Yumo ndani ya nyumba ile inayowaka kabisa.”



Basi, Bulicheka hakusitasita. Mara ile akaingia ndani ya nyumba hiyo. Watu wote wakastaajabu. Mtu huyu haogopi kitu chochote!

1631989193207.png


Hawakuweza kumuona kwa sababu ya moshi mwingi, na ndimi za moto zikauzuia mlango. Watu wakasimama nje kumngoja Bulicheka atoke tena, lakini alikawia kuonekana.

Hatimaye, akajitokeza, uso wake umetapakaa masizi na nguo zake zimechafuka, lakini mkononi alikuwa amemshika mtoto mchanga, naye anapiga makelele kwa hofu ya moto.

1631989151641.png


Watu wote waliosimama nje walipomuona, wakapiga vigelegele kwa shangwe, wakimshangilia sana. na mama mwenyewe, akampokea mtoto wake kwa shukrani kubwa. Mwana alikuwa mzima kabisa, wala hakupata hasara yoyote ile.

Kwaajili ya ujasiri wake huo, Wagagagigikoko wakampenda sana Bulicheka.

Siku moja akawauliza, “Je, nyinyi mwaweza kuunda merikebu kubwa?”

Wakasema, “Hatujui sisi.”

Bulicheka akawaambia, “Basi, nitawafundisheni.”

Wakaiunda merikebu nzuri sana. ilipokuwa tayari wakaenda baharini ili wapate kuijaribu.

1631989087478.png

1631989109246.png




Kwanza safari yao ilikuwa nzuri sana. wakaipeleka kwanza upande wa kaskazini, halafu upande wa mashariki, halafu upande wa magharibi tena, kadiri ya upepo ulivyowafaa, na mwisho wakaipeleka upande wa kusini, wakaiona merikebu yao kuwa ni nzuri kabisa, wakafurahi.

Lakini siku ya tatu walipokuwa wanataka kurudi kwao, upepo ulianza kuvuma kwa nguvu sana. kweli, nguvu ya upepo ule, ilikuwa nguvu ya ajabu.

Siku hiyo, upepo ulivuma mchana kutwa, na hata wakati wa usiku haukutulia. Minazi ilitikiswa kama mianzi, madafu yote yakaangushwa chini, na makuti yakapeperushwa.

Hata nyumba za watu zikasukwasukwa ovyo juu ya nguzo zao, kama vile zinaelekea kuanguka na kubomoka. Usiku huo hakuna mtu aliyelala usingizi.

1631989019611.png


Bulicheka hakurudi na watu wake alivyokwenda nao katika merikebu.

Asubuhi yake Lizabeta akapanda juu ya mnara ili apate kuangalia baharini kama meli inakuja, lakini hakukiona hata kitu kimoja. Akalia machozi.

1631988966710.png


Lakini machozi yake yote yalikuwa ya bure tu.
 
Upepo ule ulipoanza kuvuma na kuikokota ile merikebu, Bulicheka na watu wake walifanya kazi kubwa sana ya kukiongoza chombo chao vizuri. Wakajaribu kwa bidii yao yao yote kuirudisha bandarini, bali hawakufaulu.

Kwanza, usukani wenyewe ulivunjika vipande vipande. Halafu, hata mlingoti ukapasuka kama kijiti kwa ajili ya upepo uliokuwa ukivuma mno. Mwishowe, wakakagongana na jabali, merikebu ikatoboka, na kuanza kuzama. Hapo, wakawa hatarini kweli kweli. Merikebu yao ikasukwasukwa huku na huku mara kwenye jabali, mara baharini. Hapakuwa tena na mtu aliyeweza kusimama wima.

1631989545057.png


Siku ya tatu, upepo ukatulia. Bulicheka na wenzake wakaondoka katika chombo chao, wakajaribu kulipanda lile jabali. Hali yao ilikuwa mbaya sana. jabali tupu, hakuna mti wala mnyama, wala mtu.

Bulicheka akasema, “Ni afadhali tujenge hema hapa. Tunavyo bado vipande vya mlingoti, na tanga ambavyo vitatufaa. Basi wakapiga hema ili kujilinda na ukungu wa bahari, wakapumzika, wakalala.

Asubuhi yake, wakatazamana, wafanye nini sasa? Kisha kuwa hawana jahazi, dau wala ngalawa au mtepe, na kuogelea ni mbali mno hadi huko kwenye nchi kavu.

Walipokuwa katika kulifikiria hili, wakakiona kisiwa kimoja ng’ambo ya bahari, na kuna namna ya ngalawa ndogo inayokuja toka kisiwani. Na ngalawa ile ilipokaribia wakaona inaongozwa kwa makasia, na mtu mmoja aliyekuwa mzee.

Mtu yule akafika, akapanda jahazi, akaja kusimama mbele ya hema, akapiga hodi. Mara Bulicheka akatoka nje, akampokea vizuri sana, akamuuliza, “Wewe ni nani?”

1631989586132.png


Mzee akamjibu, “Mimi jina langu Miraji. Nimekaa katika kisiwa changu kwa miaka kumi na mitatu, na sijawahi kumuona mtu yeyote. Leo nimekuona katika jabali hili, basi, nimekuja kukuchukua.”

Lo! Bulicheka na wenziwe wakafurahi sana kuokolewa katika taabu yao. Wakamfuata mzee Miraji katika ngalawa, naye akawapeleka mpaka nyumbani kwake.


1631989611091.png





Mzee Miraji alikuwa na nyumba nzuri. Ilikuwa kama pango katika mlima, lakini mbele yake kulikuwako kiambaza chenye mlango na dirisha moja.

1631989651357.png


Akawapokea vizuri sana, hata akawapikia chakula, akatandika meza. Kwa maana, mle ndani ya pango mlikuwa kama nyumba hasa mkiwa na meza, viti na vikombe.

Bulicheka akastaajabu, akamuuliza, “Kwa nini umetuambia ya kwamba umekaa hapa katika kisiwa peke yako kwa muda wa miaka kumi na mitatu, na kumbe kila kitu unacho?”

Mzee Miraji akamjibu, “Kweli, hasa! Bali nguo sina. Katika mavazi yangu yote, sasa nimebakiwa na gunia tu. Sikiliza bwana, sikuja kwa hiari yangu katika kisiwa hiki. Nilitupwa kwa nguvu za upepo kama ulivyofanywa wewe. Wenzangu wote walizama pamoja na merikebu yao, ila mimi nikasalimika. Basi, nilipopanda mlima huu, nikayakuta haya yote. Mtu mwingine alikuwa akiishi hapa, lakini mimi sikumkuta tena. Na juu ya meza hii, nilikuta barua moja, inayoeleza habari ya kuwako hazina, lakini sijui ni mahali gani ilipo. Nimeitafuta kila mahali, lakini mpaka sasa sijafaulu kuipata.

1631989683633.png


Alipokuwa alisimulia mambo hayo, mara wakasikia namna ya ngurumo chini ya ardhi.

Bulicheka akauliza, “Kitu gani hicho?”

Mzee Miraji akamjibu, “Ngurumo hiyo inatoka kwenye mlima ule ulioko karibu. Mlima huo ni volkeno, hutoa moshi na mara moja moja, hutoa hata moto.”

Bulicheka akashtuka kuisikia habari kama hiyo. Akasema, “Hivi kuna hatari hapa?”

Mzee Miraji akajibu, “Hatari yenyewe siyo kubwa sana, lakini sijui hapo siku za mbele.”

Wakatoka nje kwenda kuuangalia mlima huo. Kweli ulikuwa ukitoa moshi mzito sana, na hata moto ukaonekana kidogo.

1631989712919.png


Mara walipokuwa katika kuuangalia, nchi yote ikaanza kutetemeka sana, ngurumo ikawa kali mno, na moshi ukaenea juu ya kisiwa chote. Mawe yakaporomoka toka mbinguni, hata mzee Miraji na Bulicheka wakarudi mbio nyumbani mwao, ili kujilinda na mvua ya mawe iliyoanza kunyesha.

1631989745460.png


Bulicheka akaichukua nguzo moja iliyokuwa mbele ya mlango, akaiegemeza ili ipate kuuzuia mlango usifunguke. Kwa maana kulikuwa na makelele, mshindo na ngurumo ya ajabu. Nchi yote na hata mlima ukatetemeka, ukatikiswa hasa, ikawa wasiwasi tena kusimama wima.

1631989766392.png


Mara wakausikia mshindo mkubwa sana kama vile ukuta wa nyumba yao umepasuka.
 
Wakaangalia, kumbe wakaona ni kweli, upande wa kushoto, jabali lilipasuka kabisa, na kutokana na kupasuka huko, hazina yenyewe iliyofichika kwa miaka mingi, ikaonekana, sarafu za fedha na dhahabu zikatawanyika ovyo chini, zikajifiringisha huku na huku na kuijaza nyumba nzima.

1631990222842.png


Lo! Kwanza Bulicheka na mzee Miraji walipigwa na mshangao. Halafu wakakumbuka, kumbe hiyo ndiyo hazina iliyokuwako, sasa tumeipata.

Wakachukua magunia, kila mtu gunia lake, wakayajaza sarafu tele, kadiri walivyoweza.

1631990253161.png


Mzee Miraji akasema, “Kwanza, nitanunua nguo, halafu nitanunua nyumba nzuri na kitanda cha samadari.”

Bulicheka akauliza, “Kweli, nilikuwa nimesahau, kumbe, yote ni bure tu!”

Wakati huo, wakaona mlima wa volkeno umetulia sasa. Bulicheka akafungua mlango ili apate kupunga hewa, akaangalia kama nje kungali kumetanda bado au kumepambazuka vizuri.

Alipokuwa akiangalia nje hivi moyo wake ulianza kudundadunda gogogogo, kwa sababu alikuwa ameiona meli moja ikikaribia, ndiyo nafasi ya kuondoka katika kisiwa chao.

1631990287103.png


Wakawasha moto upesi, wakakipepea kitambaa kwa nguvu, hata mwisho nahodha wa meli akaona. Akawatuma watu wake katika mashua kusudi ya kuwachukua Bulicheka, mzee Miraji na Wagagagigikoko wale waliosafiri pamoja na mfalme wao.

Wakapokelewa vizuri na nahodha wa meli. Bulicheka akamuuliza, “Unasafiri kwenda mji gani?”

Nahodha akajibu, “Tunakwenda Mombasa sasa.”

Bulicheka akasema, “Vizuri sana, mimi vile vile nataka kwenda Mombasa, lakini kwanza sina budi kumchukua mwenzangu ambaye yuko katika nchi ya Wagagagigikoko. Naomba twende kwanza upande ule, mimi nitakupa nauli yoyote utakayoitaka.”

Nahodha akakubali, “Wakarudi kwanza katika bandari ya nchi ile ya Wagagagigikoko, nao wakafurahi ajabu. Hasa Lizabeta alifurahi mno, akacheka mpaka mashavu yakamwuma.

Bulicheka, akamwita waziri mkuu akamwambia, “Ama, napenda sana kuiangalia nchi yetu. Meli hiyo iliyotuleta hapa itakwenda Mombasa, nami nitakwenda pamoja nayo. Wewe chukua ushanga huu wa ufalme, utatawala hadi hapo nitakaporudi tena.”

Waziri huyu akaona ameheshimiwa sana, akashukuru akasema kwamba atafanya bidii ya kutawala vizuri kabisa, wenyeji wote wakafurahi.

Mwishowe, Bulicheka na Lizabeta wakapanda meli, wakaenda zao.

1631990315954.png
 
Kuna vitabu vya asili ya China nilisoma enzi za primary early 90's sijui vinaweza kupatikanaje.? Kuna "Hekaya za Kale za China Volume II", "Madada Saba" na "Lin Mkubwa Na Lin Mdogo"
 
Kuna vitabu vya asili ya China nilisoma enzi za primary early 90's sijui vinaweza kupatikanaje.? Kuna "Hekaya za Kale za China Volume II", "Madada Saba" na "Lin Mkubwa Na Lin Mdogo"
Sijawahi kuvisikia. Ila ntavicheki.
 
Back
Top Bottom