SADC CHINI YA TANZANIA TUPIGANIE KUONDOA VIKWAZO VYA KIBIASHARA

Jul 9, 2019
9
12
Tanzania tumekabidhiwa kuongoza SADC kwa mwaka mmoja ambapo Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC,huku Prof Palamagamba Kabudi akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Dkt Faraji Kasidi akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu wa nchi za SADC.(Mwenyekiti wa Kamati ya wataalamu,ndio wenye kupika mambo).

Hakuna shaka wanachama wa SADC wanatambua uwezo wetu wa kazi kutokana na mambo yaliyofanyika katika kipindi kifupi tu cha uongozi wa Awamu ya tano katika kutekeleza miradi mikubwa,sitaitaja kwa kuwa hakuna asiyeifahamu.Tumekabidhiwa SADC huku kukiwa na vikwazo mbalimbali vinavyopunguza kasi ya biashara kati ya nchi wanachama wa SADC.

Bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na nchi wanachama wa SADC zinaweza kupata soko la ndani ya SADC bila ya kutegemea soko la nje mfano nchi za Ulaya,Marekani au Asia.

SADC ikifanikiwa kurekebisha viwango vya ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazozalishwa na nchi wanachama kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine ya SADC kwa kuweka viwango vya chini vitasaidia kuchochea biashara ndani ya SADC.

South Africa anazalisha magari ya aina tofauti (under licence).Gari hili lililozalishwa S.A likiagizwa na nchi yeyote mwanachama wa SADC basi viwango vyake vya ushuru viwe ni vya chini tofauti na gari lililotengenezwa nje ya SADC mfano Japan,China,Ujerumani,Uingereza au Marekani.

Nchi nyingi za SADC zinazalisha bidhaa nyingi ambazo zinaweza kuuziana ukiacha magari ya S.A.Mfano Tanzania tunavyo viwanda vingi vya kuzalisha nondo,malumalu,bati,simenti,kusindika nafaka km unga wa sembe,unga wa ngano,mchele,n.k.Zipo nchi nyingine zinazalisha mifugo kwa kiasi kikubwa,madini ya aina mbalimbali,compyuta,transformers,n.k

Bidhaa hizi zikishushiwa ushuru bei yake itakuwa ndogo kulinganisha na bidhaa zitokazo nje ya SADC hivyo kuvutia wateja wengi na kukuza biashara kati ya nchi na nchi.Aidha zitachochea uzalishaji zaidi kwa kuanzisha viwanda vingi kwa kuwa soko la uhakika la bidhaa zao litakuwepo ndani ya SADC yenyewe.

Hivyo,tuliangalie suala la ushuru wa forodha ndani ya nchi za SADC katika kipindi chetu cha uongozi ili tuondoe vikwazo vyote vya kibiashara kwa kuweka viwango vidogo kabisa.
 
Back
Top Bottom