Mwakaboko King
JF-Expert Member
- Apr 22, 2015
- 1,099
- 207
Kifungu cha 11 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 16 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, vinataja mambo ambayo yanamkosesha au kumuondolea mtu sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura.
Kwanza, mtu atakosa sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura iwapo yuko chini ya kiapo cha utii wa nchi nyingine mbali ya Tanzania (yaani ana uraia wa nchi nyingine).
Kwa kuwa Tanzania haijaruhusu raia wake kuwa na uraia wa nchi mbili, itakuwa kinyume cha Sheria za Uchaguzi kumuandikisha mtu ambaye amebadili au ana uraia wa nchi nyingine isiyokuwa Tanzania.
Pili, mtu atakosa sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura iwapo imethibitishwa chini ya Sheria yoyote inayotumika Tanzania au vinginevyo ametangazwa amebainika kuwa hana akili timamu.
Tatu, mtu atakosa sifa ya kuandikishwa iwapo amewekwa kizuizini kutokana na uhalifu.Yapo makosa ya uhalifu yanayoweza kusababisha mtu kuwekwa kizuizini kwa mujibu wa Sheria, mtu anapowekwa kizuini anakosa sifa ya kuandikishwa.
Nne, mtu mwenye ugonjwa wa akili anakosa sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura kutokana na kwa kuwa ugonjwa huathiri uwezo wa mtu katika kufanya uamuzi kwa usahihi.
Sababu hii ni lazima iambatane na vithibitisho kwa kiafya kutoka taasisi au hospitali inayohusika na magonjwa ya akili kuwa mtu huyo ana ugonjwa wa akili kwa wakati huo wa uandikishwaji.
Hata hivyo, inawezekana ikatokea mtu akaugua ugonjwa wa akili na baadaye kupona, hivyo hata kama vyeti vya taasisi husika vilithibitisha kuwa aliugua ugonjwa huo, lakini atakuwa na haki ya kuandikishwa maadam kwa muda huo imethibitishwa kuwa amepona ugonjwa huo wa akili.
Tano, mtu aliyehukumiwa adhabu ya kifo hukosa sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura pamoja na mtu anayetumikia adhabu ya kifungo kinachozidi miezi sita gerezani.
Pamoja na adhabu ya kutumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita kumkosesha mtu kuandikishwa, hata hivyo mtu huyo anapomaliza kifungo chake ana haki ya kuandikishwa kuwa mpiga kura kwani yuko huru na kifungo.
Kifungu cha 16 (2) Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, kinasema kuwa kwa madhumuni ya aya C ya kifungu kidogo cha (1) (a), adhabu mbili au zaidi zinazopaswa kutumikiwa mfulululizo zitahesabika kuwa adhabu mbili tofauti iwapo hakuna inayozidi miezi sita.
Isipokuwa moja ya adhabu hizo zinazidi miezi sita, zitahesabiwa kuwani adhabu tofauti na kifungu kidogo cha (b) kinasema adhabu ya kifungo iliyotolewa kama mbadala wa kushindwa kulipa faini ya haitailiwa maanani.
Vifungu hivi vinamaanisha kuwa iwapo mtu ametumikia vifungo viwili mfululizo ambavyo kila kimoja hakizidi miezi sita gerezani basi atahesabika kuwa amefungwa kifungo kisichozidi miezi sita bila ya kujumlisha miezi aliyofungwa katika vifungo hivyo.
Kwa mantiki hiyo, mtu akifungwa vifungo viwili mfululizo ambavyo kila kimoja hakizidi miezi sita atakuwa na haki ya kuandikishwa kuwa mpiga kura iwapo tu kila kifungo hakizidi miezi sita.
Sifa nyingine inayomkesesha mtu kuandikishwa kuwa mpiga kura ni pale mtu anapopoteza sifa za kuwa Mtanzania kwa mujibu masharti ya Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge inayotumika inayohusu makosa ya uchaguzi wowote.
Endapo mtu yeyote aliyeandikishwa kuwa mpiga kura chini ya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa atapoteza sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura, jina lake litafutwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Ispokuwa kwamba hakuna jina litakalofutwa kutoka katika daftari la kudumu la wapiga kura isipokuwa kwa mujibu wa masharti ya sehemu hii au kwa taarifa ya mahakama kuwa mtu huyo ametiwa hatiani kwa vitendo vinavyomsababishia kupoteza sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura au kupiga kura.
Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 16 kifungu kidogo cha (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292.