Baraghash
JF-Expert Member
- Dec 18, 2012
- 2,713
- 1,789
Leo Bungeni, katika kipindi cha maswali na majibu, Mhe Ali Saleh,CUF katika swali lilioulizwa kwa niaba yake na mbunge kutoka chama mbadala, alitaka kujua sababu zilizoipelekesha Tanzania kuridhia kurejesha uhusiano na (madhalim)Israel.
Katika majibu Dk.Suzan Kolimba,Naibu Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki,alielezea kuhusu ukuta wa Berlin, siasa za Ujerumani magharibi/mashariki na kusambaratika kwa muungano wa kisoviet (USSR) kama shabihiano maridhawa wa kimatukio na urudishaji wa uhusiano wa kibalozi na nchi ya Israel.
Hatua inayoonekana kama Tanzania imekubali kutia ulimi puani na kukubali kufufua uhusiano huo uliovunjwa mwaka 1973 baada ya vita vya Yom Kippur na Hayati na baba wa Taifa hili Mwl. Nyerere.
Baba wa Taifa Nyerere alifikia uamuzi huo unatokana na msimamo wa Tanzania katika kugombania nchi kujitawala na haki za wapalestina kuwa na maamuzi ya kujiamulia mambo yao wenyewe kwa mustakabali ya nchi yao.
Fatwa hiyo ilifuatiwa na kuitambua Palestina kama Taifa halali chini ya PLO na kuruhusiwa kufungua ubalozi wake mjini Dar es salaam na Zanzibar.
Baada ya hatua hiyo,Tanzania ilitoa msimamo na nanukuu "Our desire for friendship with every other nation does not, however, mean that we can be unconcerned with world events, or that we should try to buy that friendship with silence on the great issues of world peace and justice" mwisho wa kunukuu. Je, sababu ziliopelekea kufutwa kwa uhusiano na Israel sasa hazipo tena,zimeyayuka,zimefunikwa kombe au zimepatiwa ufumbuzi?
Hivi amani ya dunia na haki za wapelestina zimeshapatiwa suluhisho? Hivi tunapokaa juu ya viriri na kupayuka kuwa tunadumisha fikira za baba wa Taifa kumbe tunakuwa tunahubiri unafiki! Sababu za kuvunja uhusiano na Israel bado zipo na ukweli ni kuwa zimeamirika zaidi.
Katika mwaka 2014 vita vya uonevu dhidi ya wapelestina "Operation Protective Edge" kwa mujibu wa Umoja wa mataifa ,Israel imewanakamisha kwa kuwaua wapelestina 2,104, pamoja na raia 1,462 kati yao 495 ni watoto na 253 wanawake, wakati wao majahili wamekufa askari 66 tu. Hivi taifa hili ndio la kuonea fahari kuwa rafiki na kuwa na uhusiano wa karibu wa kibalozi?
Serikali yetu sikivu mpeni heshima ya kweli na kumuenzi Baba wa Taifa kivitendo na si kinadharia tu. Haitoshi kwenda kuzuru kaburi lake kila mnapo kuwa na dhiki na kutaka kugombania wadhifa, huku nafsi zenu zikisutwa na maamuzi mnayoyatenda!