Sababu za kupata ujauzito wakati unatumia uzazi wa mpango

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,117
Uzazi wa mpango ni uamuzi wa hiari wa mtu binafsi mke/mume au mtu na mwenzi wake kuhusu lini waanze kupata watoto, wazae wangapi, wapishane kwa muda gani, lini waache kuzaa na njia gani ya uzazi wa mpango wangependa kutumia.

Matumizi ya kondomu, vipandikizi, sindano, vidonge, kitanzi na kutoshiriki ngono siku za hatari ni njia zinazotumika kupanga uzazi, japo machungu na lawama huja kwa wanaotumia njia hizo kushindwa kufikia lengo na kupata ujauzito.

Husna Hussein, mkazi wa Mbezi (sina jina halisi) anasema alitumia vidonge kuzuia mimba, lakini matokeo yake alishika ujauzito akilaumu njia hiyo ilimpatia hasara.

“Kuna ndugu yangu pia alikuwa na watoto wanne, aliamua kutumia kitanzi asipate ujauzito mwingine, jambo la kushangaza alishika mimba na alipojifungua mtoto alizaliwa akiwa na kitanzi mkononi,”anasema.

Bryson Joseph, mkazi wa Tabata anasema jukumu la kuhakikisha njia za uzazi wa mpango zinakuwa na ufanisi ni jukumu na mume na mke na si la upande mmoja.

“Ukisikia njia ya uzazi wa mpango imeshindwa kuonyesha matokeo kwa kiwango fulani mwanaume kahusika, wengi huwa tunapapara tunaposhiriki tendo la ndoa na wenzetu.

“Mfano kwa wale wanawake wanaotumia vitanzi huwa nasikia wanaume wanavitengua, hata kondomu wapo wanaume wanakataa, kwa hiyo elimu ni muhimu kwa wanaume zaidi,”anaeleza.

Dk Daniel Nkungu, mtaalamu wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala anasema ni muhimu kwa anayetaka kutumia uzazi wa mpango kufanya tathmini ya kina juu ya usalama na ufanisi wa kila njia.

“Si kila njia ya uzazi wa mpango inamfaa kila mtu, kila mtu ana njia yake kulingana na mazingira, sio unaenda hospitali tu unasema unaenda kuchoma sindano, vidonge au kondomu, wazielewe njia zote na wapime kulingana na umri na mazingira yake njia ipi itamfaa,”anaeleza.

Akifafanua sababu ya wanaotumia njia za uzazi wa mpango kushindwa kupata matokeo waliyotarajia, Dk Nkungu anasema kwenye matumizi ya njia za uzazi wa mpango wanachoangalia ni usalama na ufanisi wa dawa.

“Hatuna njia ambayo ni salama na yenye ufanisi kwa asilimia 100, kwa hiyo huwa tunachagua njia ya uzazi wa mpango kulingana na utashi wa mgonjwa (hali yake).

“Kuna njia za asili na za kisasa za kutumia dawa au kufunga na kila njia tunaongelea kuhusu usalama wake na ufanisi kiasi gani katika kuzuia mimba,”anaeleza.

Dk Nkungu anataja njia ya matumizi ya vidonge ili ziwe na ufanisi, mtumiaji atahitajika kutumia vidonge kila siku akitahadharisha kuruka dawa kunaleta shida.

Kwa watumiaji wa njia hii, Dk Nkungu anataja changamoto watakayoipata endapo wataruka kutumia dawa ni kupata mimba isiyo kwenye mipango yao.

“Kama atafuata utaratibu alioelekezwa, kuna utofauti wa dozi kwa kila kidonge kulingana na mzunguko ambao mtu yupo, kwa hiyo anatakiwa kufuata mshale ulivyoelekeza, mtu asipozingatia huo utaratibu hata kama anakunywa dawa ataishia kupata ujauzito,”anabainisha.

Dk Nkungu anataja utaratibu wa utumiaji wa dawa za uzazi wa mpango kuwa ni muhimu kwa anayetumia kuzingatia maelekezo ya daktari ya lini aanze kutumia na aina ya vidonge atakavyopaswa kuvitumia kulingana na maelekezo ya mshale kwenye boksi la dawa ambayo huonyesha mtiririko wa vidonge vitakavyopaswa kutumiwa.

Kwa mujibu wa Dk Nkungu, vidonge vya uzazi wa mpango vinapaswa kutumiwa kila siku akionya kuruka siku moja mhusika humuvuga homoni na ndio mwanzo wa kuharibu homoni.

Hata kwa wale wanaofunga mirija ya uzazi, Dk Nkungu anasema upo uwezekano wa njia hiyo nayo kufeli na mtu akapata ujauzito ingawa kutokea kwake ni kwa wastani wa chini ya asilimia moja.

“Njia ambazo ni salama, lakini hazina ufanisi ni za asili, ufanisi wake ni chini ya asilimia 70 unakuta mtu anashika mimba na alikuwa akizitumia njia hizo,”anaeleza.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Lilian Mnabwiru anabainisha mtu anapotumia vidonge kwa ajili ya kupanga uzazi, pale anaposahau kumeza kwa siku moja hutumbukia kwenye hatari ya kubeba ujauzito.

“Kuna wale wanaosema wanatumia njia za asili kwamba atamwaga nje, siku ukijisahau na mhusika yupo kwenye siku za hatari ndio mtu hupata ujauzito.

“Watu wakija kwetu wanataka uzazi wa mpango huwa tunawashauri, mtu anataka kupata mtoto baada ya muda gani, tunapenda kutumia njia za muda mrefu kwa sababu zile zina matokeo makubwa.

“Wanawake wengi wanapenda kuchoma sindano, sasa unakuta ile sindano inadumu kwa miezi mitatu baada ya muda huo anaweza kwenda hospitali asiikute dawa au akasahau siku ya kurudi hospitali, mtu akiacha ndio utasikia amepata ujauzito,”anaeleza.

Zingatia matumizi sahihi

Dk Lilian anaeleza ni muhimu kwa kila anayetumia njia za uzazi wa mpango kuhakikisha anafanya hivyo kwa maelekezo ya daktari.

“Watu wanaambizana mitaani, mimi natumiaga njia hii naye anakwenda huko huko, sasa mwili wa mtu mmoja na mwingine hutofautiana kwenye upokeaji wa dawa.

“Watu wamejizoesha wanajua kwa sababu walipata msaada baada ya kutumia dawa fulani, hivyo wanaamini hata mwenzake naye atapata msaada huo endapo akitumia dawa hiyo,”anaeleza.

Faida za uzazi wa mpango/ushauri

Kutumia uzazi wa mpango, Dk Lilian anataja faida mojawapo atakayopata mtumiaji ni kutopata mimba zisizotarajiwa.

“Utamudu kujipangilia mambo yako ya maisha ukiwa na uhakika kwamba upo salama kwa muda huo wote, hivyo mtu huzaa kwa mpangilio, hatua ambayo itamsaidia hata wakati wa kusomesha watoto,” anasema.

Kwa ambaye hatumii uzazi wa mpango hasa kwa mwanamke huchoka, hivyo ili kuepuka anashauri ni muhimu watoto kupishana miaka miwili ndipo mama abebe ujauzito mwingine.

“Malengo ya uzazi wa mpango ni kumpa mwanamke nafasi ya kujipangilia familia anayoitaka, kwa ukubwa na muda atakaouhitaji, unakuta wengine wapo vyuoni au shuleni wanasema wanasubiri kwanza, lakini maisha mengine alishayaanza huwezi kusema akae tu bila kutimiza yale malengo yake,”

Matumizi ya njia za uzazi wa mpango hazimkingi mtu kutopata magonjwa ya zinaa, ndio maana Dk Lilian anashauri mtu kutoshiriki ngono zembe akionya kutotumia kondomu mtu atakimbia mimba na kupata magonjwa ya zinaa.

Dk Lilian anashauri matumizi ya dawa za uzazi wa mpango yatumiwe pale madaktari wanaposhauri na si kwa kusikiliza maneno ya watu mitaani, akisema huduma za afya ni rafiki kwa wananchi wote.

Njia za asili uzazi wa mpango

Njia za asili anazotaja Dk Nkungu ni zile za kutokutana kimwili katika siku za hatari (siku ambazo uwezekano wa kushika mimba ni mkubwa) na njia nyingine mwanaume kutomwagia ndani wakati akijamiiana na mwanamke.

“Njia nyingine ya asili ni ya kuangalia joto la mwili, mfano kuangalia joto kwenye kwapa, yapo maeneo ambayo daktari anaweza kukuelekeza kuchukua joto la mwili na hii inakuhitaji kuchukua umakini mkubwa.

“Kuna uwezekano mkubwa joto la mwili likipanda, ndio mayai yanachevushwa kwa hiyo msikutane kimwili,”anabainisha.

Unyonyeshaji hasa katika miezi mitatu hadi minne ya kwanza baada ya kujifungua pamoja na kutokutana na mwenza kimwili ni njia nyingine ya uzazi wa mpango anazotaja Dk Nkungu.

Watoto na uzazi wa mpango

Dk Nkungu anasema pale mtoto wa kike anapoanza kuvunja ungo na kujihusisha na ngono na haitaji ujauzito, lazima atumie njia za uzazi wa mpango japo kitaalamu anaonya si salama mtoto kuanza ngono mapema.

Uvimbe kwenye kizazi

Kumekuwa na dhana juu ya dawa za uzazi wa mpango kuhusishwa na uvimbe kwenye kizazi (fibroids), Dk Nkungu anasema hakuna utafiti uliofanyika kudhibitisha dawa hizo zinachangia tatizo hilo.

“Mpaka sasa hakuna uhusiano wa njia za uzazi wa mpango na kupata fibroids, watu wanaopata uvimbe kwenye kizazi si lazima awe ametumia njia za uzazi wa mpango na wapo wanaotumia dawa na hawapati tatizo hilo,”anaeleza.

Anasema uvimbe kwenye kizazi huchangiwa na kuwepo kwa historia ya ugonjwa huo kwenye familia, kukaa muda mrefu bila kushika ujauzito

Takwimu za dawa na watumiaji

Kulingana na hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya 2022/2023, huduma za afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja huduma kabla ya kujifungua, wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua imeimarika.

Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, kwa upande wa huduma kabla ya ujauzito, wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango dozi 1,755,349 sawa na asilimia 82 ya lengo, sindano za uzazi wa mpango aina ya depo-provera dozi 2,125,625 sawa na asilimia 93 ya lengo na vipandikizi 206,000 20 sawa na asilimia 78 ya lengo.

Dawa hizo zilisambazwa katika halmshauri zote nchini. Katika kipindi hicho, wateja waliotumia njia za uzazi wa mpango walikuwa 4,189,787 ukilinganisha na wateja 4,357,151 wa mwaka 2020.

Njia hizo za uzazi wa mpango zilizotolewa katika vituo vya huduma za afya nchini ni vipandikizi asilimia 57.1, sindano asilimia 18.5, vidonge asilimia 10.1, kondomu asilimia 5.3, kufunga kizazi mama asilimia 0.4, Kitanzi asilimia 7.2 na njia zingine asilimia 1.4 32.

Takwimu za UNFPA

Ripoti ya hali ya idadi ya watu Duniani mwaka 2022, iliyotolewa Machi mwaka huu na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na idadi ya watu na afya ya uzazi (UNFPA) imeonyesha karibu nusu ya mimba zote ambazo ni jumla ya milioni 121 kila mwaka duniani kote, hazikutarajiwa.

UNFPA imeonya hali hiyo ina madhara makubwa kwa jamii, wanawake na wasichana na afya ya kimataifa kwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya mimba zisizotarajiwa huishia katika utoaji mimba na inakadiriwa asilimia 45 ya mimba zote si salama, na kusababisha asilimia 5 mpaka13 ya vifo vya uzazi, hivyo kuwa na athari kubwa katika uwezo wa dunia kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Njia za uzazi wa mpango

Aina za njia za uzazi wa mpango ni zile muda mrefu, za kudumu na za muda mfupi, njia za muda mrefu ni kitanzi /lupu na kipandikizi. Njia za kudumu; kufunga na kukata mirija ya kizazi kwa mwanamke, kufunga na kukata mirija ya kupitishia mbegu za uzazi mwanaume.

Njia za muda mfupi; vidonge vya kumeza, sindano, kondomu ya kike na ya kiume, njia ya kuhesabu siku za mzunguko wa hedhi kwa kutumia shanga na kalenda.

MWANANCHI
 
south africa wanatumia sindano kwa wanaume miez 6 huwez kutungisha mimba mwanamke,je kwetu hakuna iyo kitu?
 
Back
Top Bottom