Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,476
- 39,993
(picha na New Zimbabwe.com)
Na. M. M. Mwanakijiji
Inawezekana zipo sababu kubwa tatu ambazo zimemfanya Rais Magufuli kuanza kutumia lugha ya Kiswahili anapokutana na wageni wa kigeni pale Ikulu au anaposafiri kwenda ng’ambo. Sababu hizo zikieleweka zinaweza kutudokeza kidogo kwanini yumkini Rais amefikia uamuzi huo. Naomba kupendekeza tu kuwa tunaweza tusizikubali sababu hizi na inawezekana zikaonekana si za msingi lakini zinaweza kuwa na maana kubwa kitaifa.
Sababu hizi tatu zaweza kuwa ni:
- Ameamua kuitangaza na kuikuza lugha Kiswahili kimataifa.
- Hajiamini kujieleza kw aufasaha katika lugha ya Kiingereza
- Sababu zote mbili za a na b.
- Ameamua kuitangaza na kuikuza lugha ya Kiswahili kimataifa.
Hivyo, Rais anapotumia lugha ya Kiswahili anakipa jukwaa kubwa zaidi kuliko huko nyuma. Tulizoea kwa muda mrefu kuwa marais wetu wanapoenda nje hata kwa majirani zetu wanalazimika kuzungumza lugha ya Kiingereza. Kwamba, sisi Waafrika hatuna lugha inayotuunganisha watu (lingua franca) wote isipokuwa zile lugha za kigeni. Kiswahili kama lugha ya Kiafrika ni rahisi kutamkika kwani misingi yake ya maneno iko karibu katika lugha zote za kibantu na kwa kiasi kikubwa lugha nyingine za Kiafrika.
Kwa kutumia lugha ya Kiswahili Rais anaipa heshima lugha yetu; heshima ambayo inastahili. Hivi majuzi wakati Rais Donald Trump wa Marekani alipoenda Japan tuliona jinsi Waziri Mkuu wa Japan Abe Shinzo akizungumza Kijapani. Hili limetokea hata kiongozi huyo wa Marekani alipokutana na Rais wa China au wa Urusi. Kibarua ilikuwa ni kwa wakalimani kutafrisi kutoka lugha moja kwenda nyingine. Hili halikuwa jambo la ajabu.
Hivyo, pamoja na kuitangaza na kuikuza lugha hii Magufuli anaipa heshima ambayo inastahili. Kwamba, wazungumzaji wa Kiswahili hata wakiwa na vyeo vya juu kabisa wasijione duni mbele ya wageni. Mmoja wa washairi wakubwa kabisa – kama siyo mkuu kabisa – katika historia ya nchi yetu marehemu mzee Shaaban Robert aliwahi kuandika utenzi wake mashuhuri wa “Titi la Mama li Tamu”. Ubeti wake wa kufungulia Shaaban Robert aliandika:
Titi la mama litamu,hata likiwa la mbwa,
Kiswahili naazimu,sifayo iliyofumbwa,
Kwa wasiokufahamu,niimbe ilivyo kubwa,
Toka kama mlizamu, funika palipozibwa
Kiswahili naazimu,sifayo iliyofumbwa,
Kwa wasiokufahamu,niimbe ilivyo kubwa,
Toka kama mlizamu, funika palipozibwa
- Hajiamini katika kujieleza katika lugha ya Kiingereza
Makosa haya ya lugha si ya kipekee kwa lugha ya Kiingereza. Kwa mtu anayejifunza lugha ya Kiswahili au lugha nyingine yeyote anaweza kujikuta akiyafanya mara kwa mara. Ama katika kutamka maneno au katika muundo na sarufi ya lugha hiyo. Kwa mfano kwa watu wengi wanaojifunza Kiswahili wanaweza kushangaa kuwa lugha yetu haina sana msisitizo katika herufi Fulani kama ilivyo katika lugha nyingine nyingi.
Sasa Magufuli inawezekana ameona watu wanamsema au anaonekana kama kituko kwa wageni pale anapovunja lugha ya Kiingereza hasa kwa vile ni msomi wa PhD. Hili linatuleta kwenye hoja nyingine ndani ya hoja hii kuwa kuwa msomi wa eneo Fulani haina maana mtu anaimudu lugha ya Kiingereza. Kiingereza cha kisomi (academic writing) mara nyingi si kigumu kama kile cha kujieleza. Hii ni kwa sababu lugha ya kisomi ina maneno yake na ni rahisi kufuata. Si kila msomi anaweza kuandika riwaya ya Kiingereza au insha ya kijamii kwa Kiingereza bila kupata shida ya maneno. Hili linatokea hata kwa wasomi kutoka nchi nyingine ambazo hawazungumzi Kiingereza kwa asili (native English speakers).
Sasa kama Magufuli anaona hajiamini kwa sababu ya makosa ya mara kwa mara – ambayo si ya ajabu sana – inawezekana kuamua kuzungumza Kiswahili ni salama na bora kwake kuliko kujionesha udhaifu wake wa lugha.
Ikumbukwe hili si tatizo la Magufuli tu. Wapo watu wetu wengi tu ambao wanaweza kuchanganya maneno ya Kiingereza kwenye Kiswahili (Kiswakinge) lakini hawawezi kuunda kauli zinazoeleweka za lugha ya Kiingereza. Na wengine hata Kiswahili kilichonyoka (kisichonganyana) na Kiingereza hawawezi kukitumia. Tumeona mambo haya Bungeni ambapo sharti mojawapo ni kuwa mgombea awe anaweza kujua lugha ya Kiingereza au Kiswahili. Tumeona watu wanaoomba kugombea Bunge la Afrika ya Mashariki wengine wakivunja maneno hadi unasikia kujing’ata ulimi! Lakini watu wale wale wanaweza kujieleza kwa Kiswakinge!
- Mchanganyiko wa Sababu 2 za Kwanza
Hii ina Maana gani kwa taifa?
Swali kubwa la msingi ni je jambo hili lina maana gani kwetu kama taifa? Je, ina maana sasa Watanzania wasijifunze Kiingereza kabisa na wote wajifunze kila kitu kwa Kiswahili? Je, ina maana lugha ya Kiingereza si muhimu tena? Naomba kupendekeza mambo yafuatayo:
- Ikumbukwe kuwa kama taifa na kama mtu mmoja mmoja hatuwezi kukwepa matumizi ya lugha ya Kiingereza. Kwanza kwa sababu mfumo wetu wa kiserikali unafuata kwa kiasi kikubwa mfumo wa Kiingereza lakini pili ni kuwa kwa vile lugha ya Kiingereza ndio lugha inayoiunganisha dunia. Sasa hivi ni vigumu kwenda mahali popote na kukosa kabisa mtu anayejua Kiingereza. Ni rahisi kupata mtu anayejua Kiingereza kuliko mtu anayejua lugha nyingine yeyote. Hivyo, Kiingereza hakikwepeki.
- Kwamba watu wetu wanapata shida kumudu lugha hii ni matokeo ya mambo mengi. Yawezekana kwa kiasi kikubwa ni suala la elimu na mfumo wetu wa elimu. Lugha ya Kiingereza nakumbuka ilianza kufundishwa toka darasa la tatu (sijui kama bado ni hivi). Sasa mtu anachukua Kiingereza toka darasa la tatu hadi la kumi na nne na bado hajamudu lugha hii ni shida. Ama walimu wetu, mitaala yetu au mfumo wetu mzima unahitai kuangaliwa. Na hili linahusu pia lugha ya Kiswahili yenyewe. Tumeona watu wanatoka Chuo Kikuu lakini wanapata shida kujieleza kwa Kiswahili hadi unaweza kuwaonea huruma!
- Lugha kama somo jingine lolote lile linahitaji mtu kujifunza zaidi na kujiendeleza. Kosa kubwa ambalo naweza kuliona ni kuwa watu wanadhaniwa “wanajua” kiingereza kwa sababu wamepata shahada Fulani. Kwamba, kwa vile mtu ameenda chuo kikuu basi anadhaniwa anajua Kiingereza. Na hasa kwa vile anaweza kuandika kwa kutumia “templates” na msaada ya program za kusaidia kuandika. Ni muhimu mtu kujiendeleza yeye mwenyewe. Ikumbukwe kuwa hata kwenye nchi za wazungumzaji wa Kiingereza wa asili pia na wao wanawafundisha watoto wao Kiingereza sahihi. Kiingereza cha kuandika na kuzungumza vina misamiati tofauti na kile cha kisomi. Tuliosoma kwenye hizi nchi za wenzetu tunajua kabisa kuwa hata Chuo Kikuu baadhi ya masomo ya kwanza kwenye kozi ni yale ya kupandisha lugha kidogo. Masomo haya yanaitwa “English 101” ambayo ni kozi ya mhula wa kwanza kwenye vyuo vikuu vingi. Sasa kama wenyewe hawa wanatoa hizi kozi na zinaenda zaidi sisi wengine ambao Kiingereza ni lugha ya tatu au ya nne kwanini tusione umuhimu wa kuhakikisha mtoto kabla ya kwenda Chuo Kikuu anasoma Kiingereza tena? Hadi awe anaonesha uhimili (proficiency) ya lugha?
- Ni muhimu kuanzia sasa kwa Wizara ya Mambo ya Nje au chombo husika kuhakikisha kuwa Rais anaenda na mkalimani wake ambaye anamudu Kiingereza. Asiwe mtu mwenye “mmh mmh, aah aah” nyingi! Isije kutokea lililotokea juzi Zimbabwe. Kwamba, Wizara na Ikulu hawakumuandaa mtu wa kufanya ukalimani ni jambo la aibu. Kwenye mambo haya ya kimataifa kuna taratibu za kuweza kumtumia mkalimani baada ya kuapa. Kwanini hakukuwa na mkalimani sielewi. Rais Magufuli na yeye asidhanie kuwa watu wataelewa Kiswahili kwa vile tu yeye anazungumza. Ni lazima atoe nafasi kwa mtu kumtafsiria. Japo atakuwa anaweza kuelewa mtu akizungumza kwa Kiingereza yeye bado anaweza kujibu kwa Kiswahili na mkalimani akatafsiri. Wapo Watanzania wengi ndani na nje ambao wanamudu lugha mbalimbali na ambao Rais anaweza kuwatumia.
Magufuli ameonesha njia tu. Tutaifuata au tunaona aibu na kujiona duni?
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com