Sababu 10 kwanini unapaswa kusoma vitabu kila siku

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,070
Siyo siri kwamba usomaji wa vitabu umeshuka sana kwa walio wengi. Watu wanatumia muda mwingi kwenye simu zao, kwenye mitandao ya kijamii na kwenye kufuatilia habari kuliko kusoma. Na hili ndiyo chanzo kikuu cha matatizo na changamoto ambazo watu wengi wanazipitia kwenye maisha yao.

Ipo kauli kwamba hakuna kitu kipya chini ya jua, kila kinachotokea sasa, kilishatokea huko nyuma, ila kwa sasa kinaweza kuwa kinatokea kwa namna tofauti.

Hata matatizo na changamoto unazopitia sasa, siyo mpya na wala wewe siyo mtu wa kwanza kuzipitia. Wapo wengi ambao walishazipitia, na uzuri ni kwamba walizitatua na wakaweka suluhisho la changamoto hizo kwenye vitabu ambavyo unaweza kuvisoma na ukaondoka kwenye matatizo na changamoto unazopitia.

soma11.jpg


Lakini cha kushangaza ni kwamba umegoma kupata suluhisho la changamoto hizo, kwa sababu hutaki kusoma vitabu. Nasema hutaki kwa sababu ndiyo sababu pekee, sababu nyingine unazojipa kwamba huna muda au huna fedha za kununua vitabu unajidanganya tu. Huo muda unaopata na fedha za kununua data za kuperuzi mitandaoni siku nzima unatoa wapi?

Hapa tunakwenda kupata sababu kumi kwa nini tunapaswa kusoma vitabu kila siku, kama sababu hizi zitakupa msukumo wa kusoma vitabu,

Karibu upate sababu hizi 10 za kusoma vitabu kila siku na uanze kusoma ili uweze kuzifaidi.

1. UNAKUWA HURU MILELE.
“Once you learn to read, you will be forever free.” - Frederick Douglas

Frederick Douglas alikuwa mtumwa ambaye alijifunza mwenyewe kusoma na kuandika, na baada ya kujua kusoma, hakubaki tena mtumwa na aliweza kupigania haki za watu na kukomesha utumwa.

Kuna utumwa wa aina nyingi unaendelea kwenye zama tunazoishi sasa, watu wasiosoma vitabu huwa wananasa kwenye utumwa huo na kushindwa kuishi maisha yao kwa uhuru.

Kuwa msomaji wa vitabu na utakuwa huru milele, hakuna anayeweza kukutishia kwa sababu unajua vizuri chochote unachopaswa kujua.

2. UNAKUWA KIONGOZI.
“Not all readers are leaders, but all leaders are readers.” - Harry Truman

Hakuna kiongozi ambaye hasomi, na kama utapata nafasi ya uongozi kwa upendeleo bila ya kuwa msomaji, hutadumu nayo kwa muda mrefu, kwa sababu utafanya mambo yasiyo sahihi.

Uongozi haimaanishi wa kisiasa au kuchaguliwa, bali chochote unachofanya, unaweza kuwa kiongozi kama utakuwa msomaji. Kwa sababu kwenye kusoma utayajua mengi, utajua kwa kina kile unachofanya, utakifanya kwa ubora wa hali ya juu na wengine watakuwa wanakuangalia wewe kama mfano katika kufanya kwao, na hapo utakuwa kiongozi.

Soma vitabu na watu watakuwa tayari kukufuata hata kama hujawaambia wakufuate. Na ukishakuwa na wafuasi, basi wewe ni kiongozi, hata kama huna cheo.

3. KUNAKUPA UELEWA MPANA WA MAMBO.
“Books allow you to fully explore a topic and immerse yourself in a deeper way than most media today.” - Mark Zuckerberg

Kuna watu huwa wanachekesha sana, wanaamini kusoma habari au makala au kufuatilia mijadala mbalimbali mitandaoni ni sawa na kusoma vitabu. Hiyo siyo kweli, unaposoma habari, makala au mijadala mbalimbali, unapata uelewa wa juu juu tu kwenye jambo husika.

Kama unataka kupata uelewa wa ndani wa jambo, ili kuweza kuchukua hatua sahihi, nenda kwenye vitabu. Vitabu vinakuwa na utafiti na uchambuzi wa kina wa jambo lililoandikwa kwenye kitabu hicho, hivyo unapata uelewa mpana kwenye jambo husika.

Soma vitabu, utajifunza mengi na kwa kina kuliko kufuatilia habari au kusoma makala.

4. KUNAKUFUNGULIA DUNIA.
“Reading is important. If you know how to read, then the whole world opens up to you.” - Barack Obama

Usomaji wa vitabu una nguvu ya kuifungua dunia nzima kwako. Kupitia usomaji unajifunza na kuelewa jinsi dunia inavyokwenda, lakini pia unaziona fursa mbalimbali za wewe kupiga hatua zaidi.

Mtu asiyesoma kuna vitu vingi anavikosa, anaenda maisha yake kama kipofu anayehangaika kutafuta kitu wakati kipo karibu yake.

Popote pale ulipo na kwa chochote ulichonacho, una fursa nyingi zaidi za kupiga hatua. Lakini huzioni fursa hizo na hivyo huzitumii. Unaposoma vitabu, fursa hizi zinaanza kuwa wazi mbele yako na hilo linakupa nafasi ya kupiga hatua zaidi.

Soma vitabu na dunia nzima itafunguka mbele yako.

5. UTAIENDESHA DUNIA.
“Show me a family of readers, and I will show you the people who move the world.” - Napoléon Bonaparte

Napoléon Bonaparte alikuwa mbabe wa kivita ambaye aliweza kushinda vita nyingi na kubwa. Aliweza hili siyo kwa sababu ya kuwa na nguvu sana, bali kwa kujua zaidi ya maadui zake.

Ndiyo maana anatuambia ukiona familia ya wasomaji, jua hapo kuwa watu watakaoiendesha dunia. Wanaoiendesha dunia siyo wanaoshinda instagram na facebook siku nzima, siyo wanaofuatilia kila aina ya habari na udaku.

Wanaoiendesha dunia ni wale wanaosoma vitabu, wanasoma tafiti, wanakuja na njia bora za kufanya vitu, ambazo zinawasaidia watu na wao zinawanufaisha sana.

Mmiliki wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram, Whatsapp na mingineyo, Mark Zuckerberg, ni msomaji mzuri sana. Kila mwaka huwa anasoma vitabu vingi vinavyompa maarifa ya jinsi ya kuiendesha dunia. Na hakuna ubishi kwamba mtu huyu mmoja, ana nguvu kubwa ya kuiendesha dunia kuliko hata raisi wa nchi yoyote duniani.

Soma vitabu na utaiendesha dunia, kwa namna yako.

6. NDIYO HAZINA ISIYOKAUKA.
“There is more treasure in books than in all the pirate’s loot on Treasure Island.” - Walt Disney

Kama unataka kuiba na usikamatwe, kama unataka kuiba na unachoiba kidumu na wewe milele, basi soma vitabu.

Kwa nini? Kwa sababu unaposoma, unapata kwa urahisi kile ambacho kimemchukua mtu mwingine miaka mingi kukipata. Mfano mtu amejaribu biashara 10 zikashindwa, ila ya 11 ndiyo ikafanikiwa. Akaandika kitabu kinachoeleza makosa aliyofanya kwenye biashara 10 zilizoshindwa, na wewe ukakisoma, unakuwa umeiba, unakuwa umeepuka kurudia makosa yake na hivyo utapiga hatua kubwa.

Vitabu ndiyo hazina pekee isiyokauka, hazina ambayo ukiweza kuiiba hakuna atakayekukamata na hakuna anayeweza kukuibia na hazina ambayo inapatikana kwa urahisi popote pale ulipo.

7. UNAWAJUA MARAFIKI WA KWELI.
“My best friend is a person who will give me a book I have not read.” - Abraham Lincoln

Watu huwa wanalalamika kwamba hakuna marafiki wa kweli au ni vigumu kuwajua marafiki wa kweli. Hii ni kwa sababu mtu anapokuwa na mafanikio anazungukwa na watu wengi, lakini akishindwa hawaoni tena wale marafiki aliokuwa nao.

Unapokuwa msomaji, ni rahisi sana kuwajua na kuwapata marafiki wa kweli, kwa sababu wanakuwa ni wale ambao wanakupa vitabu ambavyo hujasoma.

Kama una marafiki ambao ukiwaambia unasoma vitabu wanakushangaa na kukuambia unapoteza muda, jua hao siyo marafiki wa kweli, wako na wewe kwa sababu kuna kitu wanapata. Siku watakosa kitu hicho, hutowaona tena.

Kuwa msomaji na wafanye watu wajue wewe ni msomaji na hapo utaweza kuwajua marafiki wako wa kweli kwa vitabu watakavyokuwa wanakupa au wanakuambia usome.

8. UNASAFIRI BILA KUTOKA HAPO ULIPO.
“Reading gives us someplace to go when we have to stay where we are.” — Mason Cooley

Moja ya njia za kuijua vizuri dunia ni kusafiri sehemu mbalimbali duniani. Lakini siyo wote wenye uwezo au wanaopenda kusafiri. Kusoma ni njia rahisi ya wewe kusafiri bila kuondoka hapo ulipo sasa.

Unaposoma vitabu unajenga taswira mbalimbali, kama ni riwaya unatengeneza picha ya matukio kwenye akili yako. Kama ni historia ya mtu unapata picha ya maisha ambayo mtu huyo aliishi, ni kama unakuwa umeishi maisha hayo pamoja na yeye.

Unaposoma kitu chochote, akili yako haitabaki kama ilivyokuwa mwanzo, ambapo ni sawa na unaposafiri kwenda sehemu yoyote. Hivyo kuwa msomaji, utafika maeneo mengi bila hata ya kusafiri.

9. NI ZOEZI KWA AKILI YAKO.
“Reading is to the mind what exercise is to the body.” — Richard Steele

Moja kati ya sheria za mageuzi inasema kwamba kitu kinapotumiwa kinakuwa imara na kisipotumiwa kinakuwa dhaifu.

Mfano mzuri ni mikono yako, kama huwa unatumia zaidi mkono wa kulia kufanya vitu, unakuwa na nguvu kuliko mkono wa kushoto. Kadhalika kama unatumia zaidi mkono wa kushoto.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa akili yako, kama unaitumia inakuwa imara, kama huitumii inakuwa dhaifu. Njia pekee ya kuitumia akili, kuipa zoezi ni kusoma vitabu. Unaposoma vitabu unaipa akili yako kazi ya kufikiria na kutengeneza taswira mbalimbali na hilo linaifanya akili yako kuwa bora zaidi.

Unapokuwa msomaji, akili yako inakuwa imara na yenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu kwa urahisi, kwa sababu imeshazoea kufikri vitu vigumu na vikubwa.

Usikubali akili yako iwe dhaifu, ifanye kuwa imara kwa kuwa msomaji.

10. UNAJITOFAUTISHA NA WASIOJUA KUSOMA.
“The man who doesn’t read has no advantage over the man who can’t read.” — Unknown

Kama unajua kusoma lakini husomi kitabu, huna tofauti na mtu asiyejua kusoma. Wote mtasumbuka kwa jambo linalofanana wakati majibu ya jambo hilo yapo kwenye vitabu.

Kuwa msomaji na utaweza kujitofautisha sana na wengine ambao hawajui kusoma au hawataki kusoma.

Rafiki, hizo ndizo sababu 10 kwa nini unapaswa kusoma vitabu kila siku. Karibu twende pamoja kwenye safari hii ya usomaji, ambapo utapata vitabu vizuri pamoja na chambuzi zake,

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
 
Uzi maridhawa Sana huu umenigusa mno. Ila wachangiaji watakuwa wachache kusoma ni utamaduni.

Wana JF wengi hasa vijana wanapenda Nyuzi za Ngono,Ulevi na kupata pesa kwa haraka.
 
9 Reactions
Reply
Back
Top Bottom