Sababu 10 Kwanini Mwanyika ajiuzulu

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,009
Sababu 10 Kwanini Mwanyika ajiuzulu

Lula wa Ndali-Mwananzela Machi 19, 2008
Raia Mwema

KATIKA ulimwengu wa utoaji sababu kuna sababu ambazo zinakubalika na zisizokubalika.

Zinazokubalika ni zilizojikita katika ukweli, zinakubalika kimantiki, na hazijipingi zenyewe na hivyo ndani yake zinaushawishi wa akili. Sababu zinazopingwa ni zile ambazo si tu haziingii akilini lakini msingi wake hauna mantiki na ni rahisi kuonyeshwa udhaifu wake kwa sababu hazina ushawishi wenye kugusa dhamira za wale wanaozisikia na hivyo inatokea watu wakazikataa mara moja.

Kwa wiki kadhaa sasa tangu ripoti ya Kamati Teule ya Bunge itoke kumekuwa na wito wa kumkataka Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Johnson Mwanyika ajiuzulu. Baada ya ukimya wa muda mrefu hatimaye msomi huyo alizungumzia wazi suala hilo wiki iliyopita na kunukuriwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amekataa kujiuzulu. Si kwamba amekataa kujiuzulu tu bali pia alitoa sababu ambazo zimemfanya achukue msimamo huo wa kukataa kujiuzulu.

Mwanyika alipoingia kwenye ulimwengu wa watoa sababu akasema wazi (kama alivyonukuriwa na chombo kimoja cha habari) kuwa yeye hayuko tayari kujiuzulu kama baadhi ya watu wanavyotaka. Akatoa sababu kubwa tatu kwanini hatojiuzulu. Kwanza, alidai kuwa "sijiuzulu kwa sababu sijaiba", pili kuwa kama mtaalamu kama walivyo wataalamu wengine, basi kuna njia ya kumwajibisha, na tatu kuwa yeye ni "msafi milele na milele". Na katika kuonyesha usafi wake huo aliwataka watu kwenda kuwauliza watu aliowahi kufanya nao kazi na watakuwa mashahidi kuwa yeye ni msafi.

Sasa hizi hoja tatu ni rahisi kuzikataa kwa sababu haziingii akilini na zinapingana na mantiki. Ni hoja ambazo kuzikubali kwa haraka haraka ni kukebehi uwezo wa watu kufikiri. Hebu tuangalie moja baada ya nyingine na kuonyesha kuwa sababu hizi ni sababu za mtoto kujitetea na si mtu msomi kama Mwanyika.

"Mimi sijaiba" – Kwanza kabisa sijui ni nani aliyedai kuwa Mwanyika ameiba "penseli au kifutio". Katika kufuatilia sakata lote la Richmond sikumbuki kusoma mahali popote ambako Mwanyika amedaiwa kuiba. Hivyo utetezi wa "mimi sijaiba" hauhusiani hata chembe na hoja yoyote ya kutaka yeye ajiuzulu. Kama hakuna mtu aliyedai kuwa umeiba kwanini udai kuwa "hujaiba" isipokuwa kama kweli umeiba?

Mzazi anaporudi nyumbani na mtoto akamkimbilia na baada ya kumsalimia kitu cha kwanza mtoto huyo kusema ni "mama mimi sijaiba sukari" je mzazi atafikiri nini? Kuwa kweli mtoto hajaiba sukari? Sasa yawezekana ni kweli hajaiba lakini kitendo cha yeye kujitetea kuwa hajaiba kitamfanya mzazi kujaribu kumtega na kumwambia mtoto "mbona hujajipangusa mdomoni"? Yule mtoto akianza kujipangusha mdomo anathibitisha kuwa "amelamba" sukari! Sasa sisemi kuwa Mwanyika ameiba, ila utetezi wake hauhusiani na hoja zilizotolewa.

Lakini pia tunaweza kuonyesha tatizo jingine la utetezi wa "mimi sijaiba". Nitaomba mnioneshe mwizi mmoja aliyenyoosha mkono akisema kwamba "kaiba", hata kama hakuulizwa au hakukabiliwa na watu wenye hasira. Ukinionyesha mwizi mmoja aliyekubali makosa kabla ya kuulizwa nitakuonyesha elfu moja ambao walikataa kuwa hawakuiba licha ya ushahidi kuwakodolea mbele za macho yao.

Nakumbuka mmoja alijaribu kunichomolea pale stendi ya basi ya Tanga miezi michache iliyopita nilipokwenda kumuona Bibi. Tulikuwa tunapishana na huyo bwana akajaribu kuchomoa na mara moja nikamshtukia. Utetezi wake unasimama katika kumbukumbu zangu kama utetezi finyu wa mwizi katika historia ya wezi.

"Samahani kifungo cha shati langu kilikwama kwenye mfuko wako" alisema na kuomba radhi akitetemeka kabla sijamuitia "mwizi".

Sasa sisemi kuwa Mwanyika kaiba kuku au lolote lile ninalosema ni kuwa utetezi wa mimi sijaiba ni utetezi dhaifu na usio na msingi katika mjadala huu, kwa hiyo usingepaswa kutolewa isipokuwa kama kuna mtu alimtuhumu kuwa ameiba.

Utetezi wake wa pili ni kuwa "Mimi ni mtaalamu kama vile walivyo mawakili, anapokosea kuna taratibu zake za kumwajibisha kitaalamu." Utetezi huu unaweza kuwavutia "wataalamu" wenzake lakini kwa watu wenye kufikiria ni utetezi ambao nao kama ule wa "mimi sijaiba" ni hafifu.

Kwamba tuseme kuwa moja ya njia za kumwajibisha "kitaalamu" ni kwa yeye kuamua kuachia ngazi. Pili, tofauti na mawikili wengine, Mwanyika ni mteuliwa wa Rais na hivyo ana nafasi ambayo mawakili wengine hawana au wataalamu wengine hawana, hivyo kujilinganisha wahandisi, madaktari, n.k si sawa. Watu pekee ambao angepaswa kujilinganisha nao ni wateuliwa wengine wa Rais kama wakuu wa mikoa au mawaziri.

Hivyo kama mteuliwa na Rais Mwanyika anaweza kuwajibishwa aidha na Rais mwenyewe kwa kumuondoa au kwa yeye mwenyewe kujiuzulu. Hivyo si kweli kuwa anatakiwa kuwajibishwa kitaalamu (isomeke kupangiwa kazi nyingine). Kwa mujibu wa Katiba, Mwanasheria Mkuu anaweza kuondolewa na Rais, lakini Katiba haimkatazi kuwa hawezi kujiuzulu na kumuomba Rais amuondolee wadhifa huo.

Utetezi wake wa tatu wa "mimi ni msafi milele na milele" kwanza kabisa kwa haraka unapakana na kufuru kwani hakuna mwanadamu aliyemsafi "milele na milele"! Hilo nitamsamehe nikiamini alimaanisha "kwa muda mrefu". Tukiondoa hilo la tatizo la lugha, kauli yake hiyo kama ile ya "mimi sijaiba" ina matatizo ndani yake. Binafsi nilijiuliza (baada ya kusoma kauli hiyo), Mwanyika ni msafi kwa sababu amejilinda kutoka kwenye uchafu au licha ya kuwa kwenye uchafu alijihakikishia kuwa hachafuki?

Nikajiuliza pia je yawezekana ni msafi kwa sababu hataki kukaribia uchafu? Kwa kiongozi kama yeye siamini ni sifa nzuri kusema kuwa "ni msafi" kwa sababu usafi wake unaweza kabisa kuwa ni kutokana na kukaa mbali na uchafu na si kwa sababu ya kuushughulikia uchafu.

Nitatoa mfano; fundi makanika aliyevaa ‘ovaroli' na kuanza kutengeneza gari huku amevaa glovu na miwani ya kazi kwa mtu mwingine ataonekana ni mchafu. Lakini baada ya kutengeneza gari hilo na kuamua kuvua magwanda yale ya kazi basi fundi huyo ataonekana ni msafi. Sasa usafi wake si kwa sababu alikaa mbali na grisi bali ni kwa sababu alijilinda na mafuta hayo licha ya kuwa alikuwa anatengeneza chanzo cha uchafu huo.

Hofu yangu ni kuwa Mwanyika ni msafi si kwa sababu ameshughulikia uchafu bali ni kwa sababu amekataa na hayuko tayari kushughulikia uchafu. Hii ni sababu tosha ya yeye kujiuzulu. Hatutaki Mwanasheria anayeogopa uchafu kwenye mikataba, sheria, mahakama, n.k ili tu ajilinde na kuja kudai "mimi ni msafi".

Usafi wa namna hii unanikumbusha kiongozi mwingine ambaye alishuhudiwa na Baba wa Taifa kuwa ni "msafi" na tukaambiwa tumchague kuwa ni "msafi"; kiongozi huyo alipoingia madarakani na kukutana na "uchafu" si tu alichafuka bali na yeye mwenyewe alichafua wengine.

Tanzania inahitaji viongozi ambao usafi wao unatokana na wao kushughulikia uchafu bila kuacha uchafu huo "kuwashughulikia" wao. Mwanyika si mtu wa namna hiyo. Ndiyo maana leo napendekeza sababu za kwanini Mwanyika ajiuzulu kwa kumuomba Rais amuondoe kwenye wadhifa huo; wenyewe wanasema "atengue" uteuzi wake.

Kwanini basi ajiuzulu? Tuanze na sababu ya 10 : Mwanyika amehusishwa na mojawapo ya mikataba mibaya kabisa katika historia ya Tanzania huru. Ripoti ya Kamati ya Bunge inasema hivi kuhusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo Mwanyika anaiongoza "Kamati Teule imesikitishwa na kushangazwa kwa kiwango cha chini cha umakini kilichoonyeshwa na wataalam wetu hususan Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kushughulikia suala hili."

Na zaidi ya hilo Kamati hiyo Teule iliongeza kama vile kukomelea msumari na kusema "Ubebwaji wa Richmond Development Company LLC na Wizara ya Nishati na Madini ulichangiwa na kurahisishwa zaidi na ukosefu wa umakini wa maafisa ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao, badala ya kuwa washauri wa sheria wa Serikali, wanageuka kuwa wasindikazaji!"

Kwa uthabiti wa hoja inahitimisha kuhusika kwa ofisi ya Mwanyika na kusema "Katika suala hili la Richmond Development Company LLC, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilichangia sana kulea ubabaishaji kwa kutohudhuria vikao vya majadiliano na kufumbia macho dosari bayana au pengine kutojali."

Hivyo ni wazi kabisa kuwa kwa mtu "msafi" kama Mwanyika kushughulikia suala la Richmond hakukuwa kipaumbele kwani "kungemchafua". Ningeweza kumfananisha na "bishoo" mmoja enzi zetu, lakini sitofanya hivyo.

Hivyo hiyo ni sababu ya kumi; ni uzembe wa kwake na ofisi yake hadi kusababisha nchi kuingia mkataba mbovu wa Richmond.

Sababu ya tisa : Mwanyika ameshindwa kuisimamia ofisi yake, na kama Mwanasheria Mkuu aliyemtangulia, amezidiwa na majukumu yaliyolundikwa kwenye ofisi hiyo kiasi kwamba usimamizi wa ofisi hiyo ni mgumu na ni wazi licha ya utaalamu na usomi alionao jukumu la kusimamia ofisi hiyo limemzidi.

Sababu ya nane : Mwanyika ameshindwa kutumia madaraka yake aliyopewa kisheria kusimamia wanasheria wa Serikali, hususan, katika masuala ya mikataba. Ni wazi kuwa kushindwa kwake kuwa karibu nao au kuwafuatilia kumesababisha hadi Rais kuutangazia ulimwengu kuwa tuna matatizo ya wataalamu wa mikataba. Mwanasheria Mkuu alishindwa kusimama na kueleza kama ni kweli tuna tatizo hilo na kama tunalo ni hatua gani zimechukuliwa kulikabili. Mwanyika ananguvu hiyo kwa mujibu wa sheria inayosimamia ofisi yake hiyo.

Sababu ya saba: Mwanyika kama Mwanasheria Mkuu na kama ripoti ya Kamati Teule ya Bunge inavyoonyesha ameshindwa kutoa ushauri ufaao katika masuala ya mikataba kama Sheria ya Mwanasheria Mkuu ya 2005 Ibara ya 8(1)d ambayo inampa uwezo wa kutoa ushauri huo. Mara kadhaa imeonyeshwa kwenye ripoti hiyo si tu Mwanasheria Mkuu hakuwapo bali hata mwakilishi wake hakuwapo na hakuna mahali panapoonyesha jitihada za mwanasheria mkuu kufuatilia maamuzi ya vikao hivyo, kuyapinga, kuyasahihisha au kuyakataa moja kwa moja.

Sababu ya sita: Mwanyika ameshindwa kuanzisha uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama wa vitendo vya uhalifu wa kiuchumi kwa mujibu wa sheria ya kuhujumu uchumi ya mwaka 1984. Kama mtaalamu anajua sheria hiyo inampa nguvu kadhaa ambazo kama angeweza kuzitumia leo hii wasingekuwa wanafanya mchezo wa "kioo kioo, alikivunja nani" kutafuta ni nani hasa alikwapua fedha kutoka Benki Kuu.

Sababu ya tano: Katika kujilinda asionekane mchafu Mwanyika amekuwa akisubiri kupata maelekezo ya kufanya kazi kutoka juu hata kwa mambo ambayo ana nguvu ya kufanya kisheria. Kama Rais Kikwete asingemuweka kwenye hiyo kamati ya EPA Mwanyika asingeamua yeye mwenyewe kuanzisha uchunguzi huo wakati nguvu za kufanya hivyo anazo.

Sababu ya nne: Mwanyika kama Mwanasheria Mkuu hadi leo ameshindwa kuanzisha uchunguzi wa kufuatilia makampuni ya Meremeta, Mwananchi, Deep Green na Tangold ambayo nayo yanatuhumiwa kuchota toka Benki Kuu, na siwezi kushangaa kuwa anasubiri Kamati nyingine teule au maelekezo ya kufanya hivyo toka Ikulu. Kwa mtindo huu, Watanzania wataendelea kusubiri kashfa nyingine juu ya kashfa.

Sababu ya tatu: Mwanyika kama Mwanasheria Mkuu wakati anafanya uchunguzi wa mambo ya EPA, Taifa limeingia mkataba mwingine ambao na wenyewe una matatizo yake. Hajachukua hatua yoyote ile kusahahihisha. Shirika letu la ndege limeingia mkataba wa kukodisha dege kubwa la Airbus toka kampuni ya Wallis Trading ya Liberia. Ndege hiyo ambayo ilikuwa ni ya Air Jamaica hadi leo inafanyiwa matengenezo huko El Salvador.

Hata hivyo ndege hiyo iliyotakiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka jana imechelewa kufika kwa sababu ya kutowajibika kwa ofisi za Wizara ya Miundo Mbinu. Wizara hiyo inaongozwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge.

Kwa vile serikali imeshindwa kutoa udhamini kama ilivyotakiwa ndani ya mkataba huo, ATC inaendelea kulipia ndege hiyo zaidi ya dola laki nne za kukodisha na faini ya dola sitini elfu kwa kila mwezi ambao udhamini huo haujapatikana. Mwanasheria wetu Mkuu sijui kama aliuangalia mkataba huu au ni yale yale ya Richmond.

Sababu ya pili: Mwanyika ameliangusha Taifa kutokana na kushindwa kwake kutelekeza majukumu yake kama Mwanasheria Mkuu na hivyo kwa kiasi kikubwa kuchangia katika matatizo ya mikataba tuliyonayo sasa. Hili halina ubishi wa kusema "sijaiba" na "mimi ni msafi" si utetezi wa kutosha. Ametuangusha na ameliangusha Taifa hili na ushahidi upo mwingi.

Sababu ya kwanza ni kuwa afuate mkumbo wa wenzake walioawajibika licha ya kudai kuwa wao ni "bangusilo". Kama aliyekuwaWaziri Mkuu Edward Lowassa alikubali kuwajibika kwa makosa ya "walio chini yake", na kama Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walikubali kuwajibika makosa ya "walio chini yao" vivyo hivyo Mwanyika naye awajibike kutokana na uzembe wa kwake na wa wale walio chini yake.

Kama Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano aliweza kujiuzulu na Taifa linaendelea bila yeye, vivyo hivyo ofisi ya Mwanasheria Mkuu itapata mtu mwingine na inaweza kufanya kazi bila Mwanyika.

Kimsingi nilichotaka kusema kwa maneno yangu mengi ni kuwa Mwanasheria Mkuu hafai kuwa Mwanasheria Mkuu na kuendelea kwake kuongoza mambo ya EPA au uchunguzi mwingine wowote ule akiwa amezungukwa na wingu la kashfa hizi zote ni kutojali utawala bora, na kukebehi utawala wa watu wanaowajibika.

Naomba nitoe pendekezo la bure na la wazi kwa Mwanyika kwamba amuombe Rais ampangie kazi nyingine au Serikali impeleke kwenda kusomea mambo ya mikataba ili aje kuwa wa thamani kwa Taifa huko mbele kwani sasa hivi amekuwa ni wa hasara.

Kwa Mwanyika; jiuzulu sasa angalau wewe uondoke na usafi wako, kabla hujaambiwa umeiba au kuitwa fisadi. Hadi hivi sasa hujaiba lakini kutokana na kutokuwa mwangalifu na makini umeacha wengine waibe; ni kweli unataka uwajibishwe kitaalamu lakini kutokana na utaalamu wa wengine tumeibiwa; na mwenzetu umesema kuwa wewe ni msafi lakini katika kulinda usafi wako umewaacha wengine waichafue nchi! Hili halikubaliki na halina udhuru, jiuzulu sasa ulinde heshima yako.

Msomaji unasemaje, aende asiende?
 
Ajiuzulu ili kiwe nini hasa, wakati keshasema hajiuzulu? nimewahi kusikia kumpigia mbuzi gitaa.. sikuelewa maana yake.
 
Mwanyika nalindwa na MH Kikwete na wakati huo huo Mwanyika analinda siri zinazo mwngiza kikwete katika Ufisadi wa RDC.

Ki msingi Mwanyika na MH Kikwete wote wanatakiwa kufagiliwa kwa pamoja.
 
WATUMISHI WA SERIKALI:

..watumishi wa serikali wana wakati mgumu sana ktk ku-deal na wanasiasa mafisadi.

..mtumishi wa umma akipinga ufisadi mara nyingi huishia kufutwa kazi, au kupewa transfer kwenda kitendo chenye ukata. kwa ujumla anakuwa anahatarisha career yake, na familia yake.

..mbunge anapopinga ufisadi the worst thing that can happen to him ni kuachwa hapo alipo, wakati the "best" ni kupewa ulaji na kushirikishwa ufisadi, au kama yuko upinzani umaarufu wake huongezeka..

..tutawalinda vipi watumishi wanaotaka kupinga ufisadi? what is the reward for them? kusema wapinge ufisadi kwa sababu ya mapenzi na uzalendo kwa nchi yao haitoshi. hawa ni wananchi au regular people,wana familia, na ndugu wanaowategemea.

..Sijui kama kuna anayemkumbuka marehemu Dr.Fupi aliyepata kuwa Mkemia Mkuu wa serikali. Kifo chake inasemekana kilitokana na hujuma za mafisadi kutokana na msimamo wake wa kupinga mchele mbovu kuingizwa nchini.

WANANCHI KWA UJUMLA:

..Watanzania wananchi wa kawaida tunaolalamika kwenye mitandao na magazeti pia tunahusika na huu ufisadi.

..Hivi kuna ambaye hakuwa akijua kwamba Kikwete na wenzake wametumia rushwa na kashfa kujipatia uongozi?

..Yeyote yule aliyempigia kura Kikwete na CCM basi moja kwa moja ajue kura yake ilikuwa kuhalalisha ufisadi unaoendelea sasa hivi.

TUME YA MWAKYEMBE:

..Baada ya Dr.Mwakyembe kugundua kwamba Waziri Mkuu alikuwa akikiuka maagizo ya vikao vya baraza la Mawaziri kwanini hakumuita na kumhoji ni mamlaka ipi iliyompa maelekezo hayo?

..Hivi kati yetu hakuna mwenye interest ya kujua kwanini Waziri Mkuu alikuwa akikiuka maagizo ya baraza la mawaziri?

..Hakuna mwenye interest ya kujua ni nani alimuagiza Lowassa kuchukua mkondo ule? Je, Lowassa alikurupuka tu na kujichukulia madaraka asiyokuwa nayo?

..Dr.Mwakyembe ni msomi mwanasheria aliyebobea. Lakini nasikitika kwamba ripoti yake imetoa nusu-ukweli na siyo ukweli kamili.

MWISHO:

..Kuondokana na uozo huu tunapaswa kuikataa serikali ya CCM 2010. At worst hao watakaokuja wataleta uozo tofauti na huu wa miaka 40 ya TANU/CCM.
 
Back
Top Bottom