Saa 10 na Mstaafu Hayati Rais Mkapa

JOYOPAPASI

JF-Expert Member
Jan 10, 2016
250
408
#RIPMzeeMkapa Ni #Mwanao Anthony Mtaka

Saa 10 na Mstaafu Hayati Rais Mkapa

Nimebahatika kupata fursa kadhaa kukaa na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa enzi za uhai wake.

Fursa ambayo sitaisahau ni ile ya masaa 10 ya mazungumzo kati yetu alipokuja shambani kwake Turiani Morogoro mwezi Novemba 2014, wakati huo nikiwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero.

Masaa 10 na Rais Mkapa, muda ambao ni nadra sana kwa yeye kumpatia mtu kwa mazungumzo yalinijenga na kunikomaza kiuongozi. Nilipata fursa ya kujifunza mengi kutoka kwake na kupata ufafanuzi juu ya maoni mengi juu yake niliyoyasoma kwenye magazeti. Tulizungumza mambo mengi sana yahusuyo uongozi na hatma ya nchi yetu.

Nilitumia wasaa huo kumuuliza ikiwa anayaona yale aliyoyazungumzia kwenye hotuba zake kabambe ikiwemo ile aliyoitoa kwenye Halmashauri Kuu ya CCM ya Agosti 2004 maarufu kama "Ushupavu wa Uongozi" (The Courage of Leadership); na ile hotuba yake aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa 2005 wa kuchagua Mgombea Urais wa CCM zitakidhi matakwa ya siasa za 2015.

Nilitaka pia kujua maoni yake kuhusu mtazamo na hisia juu ya uamuzi wa kuwaondoa wazee (Wenyeviti Wastaafu, Makamu Wenyeviti Wastaafu na Makatibu Wakuu Wastaafu) kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM. Jibu lake lilikuwa uamuzi ule ulitokana na mapendekezo yao wazee kuomba wapumzishwe kwenye vikao hivyo vya juu vya chama. Sababu zao kubwa zilikuwa mbili.

Kwanza, waliona busara kumpatia Rais na Mwenyekiti wa Chama aliyeko madarakani uhuru zaidi wa kuongoza. Pili, kuondoa dhana iliyokuwa ikijitokeza kila walipopata udhuru na kutohudhuria kuhisiwa na vyombo vya Habari kwamba wamesusia vikao vya Mwenyekiti. Ushauri wao ulikuwa ni kuundwa kwa Baraza la Wazee ili kukidhi dhima yao ya kutoa ushauri.

Aidha, uamuzi ule uliwaondoa tu kuwa wajumbe wa kudumu wa vikao vya chama lakini haukuondoa uwezekano wa wao kualikwa kwenye vikao hivyo kwa mwaliko maalum.

Udadisi wangu haukuishia hapo. Nilimuuliza pia mtazamo wake juu ya maoni ya wengi dhidi ya mafanikio ya sera yake ya ubinafsishaji. Alinifurahisha kujua kuwa, amekuwa akisoma na kuona namna ambavyo jambo hilo lilivyopokelewa na wachambuzi mbalimbali. Kilichomshangaza yeye ni namna ambavyo wapinzani wa sera hiyo ama kwa makusudi au kwa kupitiwa walijikita tu kwenye mifano ya maeneo ambayo ubinafsishaji haukwenda vizuri.

Alishangaa kwa nini watu hao hawakutoa pia mifano mizuri ya ubinafsishaji kama ile ya Benki ya NBC iliyozaa Benki ya NMB, Kiwanda cha Sigara (TCC), baadhi ya viwanda vya sukari vinavyofanya vizuri na maeneo mengine. Tukiwa bado kwenye eneo hilo, nilimuuliza kwa nini aliamua kubadili noti na sarafu alipoingia madarakani.

Jibu lake lilikuwa, uamuzi ule ulilenga kuwashawishi wale waliokuwa wamehodhi fedha majumbani mwao kuzirudisha benki. Kwa maelezo yake, uamuzi ule ulikuwa wa mafanikio kwani fedha iliyorudi benki ambayo ilikuwa nje ya mzunguko ilikuwa ni zaidi ya ile iliyokuwapo katika benki zetu.

Jambo lingine nililotaka kupata mtazamo wake ni ule utamaduni wa kukabidhi kofia ya uenyekiti wa Chama kwa Rais mpya (kuunganisha kofia mbili) kabla ya miezi 24 ya kwanza kuisha, yaani kabla ya Mkutano Mkuu wa Chama kikatiba. Maelezo yake yalikuwa kwamba kipindi hicho ndio muafaka zaidi wakati Rais mpya akiwa bado kwenye fungate ya kisiasa (political honeymoon). Baada ya muda huo, Rais huwa ameelemewa na mambo mengi.

Nikataka pia kujua kwa nini hapendi kuongea chochote kama mzee mstaafu wakati ambao CCM walipitia mambo mengi kati ya 2008-2014. Jibu lake lilikuwa kwamba silaha nzuri kwa kiongozi mstaafu duniani ni kukaa kimya maana upo mstari mwembamba sana kati ya kushauri na kutoa maoni kwa upande mmoja, na kukosoa na kuingia kwa upande mwingine.

Mazungumzo yetu yaliendelea na kwa kweli sikumpatia wasaa wa kupumzika. Nikataka kujua iweje hakuwahi kumteua Comrade Abdulrahman Kinana katika nafasi yoyote ilihali alikuwa meneja wa kampeni zake za urais mara mbili. Jibu lake lilikuwa alitamani kumteua lakini Ndugu Kinana alimkatalia. Alifanya hivyo tena ilipofufuliwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kumuomba ampendekeze kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki jambo ambalo alilikubali.

Tukaendelea, nikamuuliza, katika siku ya kwanza ya urais wake baada ya kuapishwa na kurejea Ikulu ni jambo gani la kwanza alilolifanya? Akaniambia, alimwandikia mtangulizi wake Rais Ali Hassan Mwinyi barua kwa mwandiko wa mkono wake bila kuichapa, akimshukuru sana kwa mchakato mzima wa kumpata Rais na kuahidi kuendelea kuomba ushauri wake katika kuendesha nchi.

Nilipomdadisi juu ya mtazamo wake kwenye kinyang’anyiro cha urais 2015 kilichokuwa mbele yetu wakati huo hakuwa tayari kufunguka. Pengine ni katika kuishi ile dhana ya kuwa ukistaafu unapaswa kujifunza kukaa kimya. Hata hivyo, nilimchokoza kwa kumtajia majina ya wagombea mbalimbali waliokuwa wakitajwa tajwa wakati huo. Nilimtajia majina 13. Wakati nikimtajia jina alikuwa anaitikia tu kwa kutikisa kichwa.

Yapo majina ya wagombea ambayo hakuwa akiamini kama kweli watagombea na wapo wale alioshia kutabasamu na wapo ambao waliomsisimua. Utulivu wa mzee Mkapa ulikuwa unafanya kutojua hisia zake, lakini unapogusa mahala anapopapenda uliweza ona hata mishipa ya utosi wake ikifurahi. Nililiona hilo nilipolitaja jina la Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Ni dhahiri Rais Mkapa alimpenda sana Dkt. Magufuli. Haikuhitajika tochi kuona mapenzi yake kwa Magufuli. Alichozungumza siku hiyo kilibaki funzo na darasa kwangu.

Tulizungumzia zaidi ya masuala ya siasa. Nilipenda pia kufahamu maisha yake nje ya siasa na uongozi. Mmoja wa wasaidizi wa Mzee Mkapa, wakati huo marehemu Mkude ambaye alikuwepo usiku ule hakusita kueleza hisia zake kwangu. Aliniambia kuwa mimi ni mwenye bahati kupata wasaa mrefu vile na Mzee Mkapa.

Kuonyesha furaha yangu, nikamwambia kaka Mkude fursa ile itabaki kwenye kumbukumbu za maisha yangu kama Novemba Kuu (The Great November). Marehemu Mkude ndiye aliyenipiga picha na Mzee Mkapa usiku ule Mtaka wa mwezi Novemba baada ya mazungumzo yetu yaliyoanza saa kumi jioni na kumalizika saa saba usiku.

Mbali na mazungumzo yetu, nimekuwa msomaji mzuri wa hotuba zote za Mzee Mkapa alizotoa kila mwisho wa mwezi akiwa madarakani na zile alizotoa katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa. Niliendelea kuwa mtoto na rafiki wa Mzee Mkapa hata nilipohamishiwa Wilaya ya Hai na baadae kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Bado nilipata nafasi ya kuzungumza naye kwa kirefu, japo sikuwahi kuyapata tena masaa 10 kama ilivyotokea Turiani. Mzee Mkapa aliendelea kuwa rafiki yangu, Mwalimu wangu na kila tulipoonana hatukuacha kuzungumza na kwa kweli nilimdodosa na kujifunza mengi.

Leo Mzee Mkapa hayupo nasi. Niseme nini zaidi? Nimempoteza baba, rafiki na mtu aliyependa kuniona nikifanya vizuri kwenye kazi zangu na hasa akinisisitiza kuwasaidia wananchi wanyonge kutoka kwenye umaskini na kuwatatulia shida zao.

Hakika nchi imepoteza mzee mwenye maono, msimamo na mwana mageuzi wa kweli aliyeipenda nchi yake kwa dhati ya moyo wake. Miaka 10 ya utawala wake alitufikisha mahala pazuri, alijenga taasisi ambazo zitaishi daima mioyoni mwa Watanzania, aliipenda imani ya kanisa lake na kuheshimu imani za watu wengine.

Natoa pole kwa Mama Anna, watoto wake na nampa pole Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumpoteza Kiongozi Mashuhuri kwenye nchi na mlezi wake aliyemuamini na kumpa dhamana ya unaibu waziri akiwa na umri ulio chini ya miaka 40.Nampa pole kiongozi wangu wa zamani Ndugu William Erio, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF ambaye kupitia yeye, Mzee Mkapa alinipenda na kuniamini.

Nampa pole nyingi dada yangu Dkt.Ellen Senkoro, Mtendaji Mkuu wa Mkapa Foundation ambaye wakati wote wa shughuli za Mzee Mkapa alipenda kunialika kwenye shughuli za Mzee wangu huyu.

Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele Mzee Mkapa. Hii dunia sisi ni wapitaji. Miaka yetu hakika ni ya kukopeshwa. Pumzika baba yangu, pumzika rafiki yangu, pumzika kiongozi wetu, Tutaonana kwenye ile asubuhi njema na iliyo kuu.

Mwanao
Anthony Mtaka.
IMG-20200727-WA0317.jpg
 
Mh Mtaka ,najua utapita kusoma maoni haya, nakupa pongezi nyingi sana, kwa kazi nzuri ya kubadilisha mkoa wa Simiyu, wewe ni hodari na mchapa kazi mwenye hofu ya Mungu.

Asante kwa bandiko zuri. Naomba unialike nije Simiyu kukusalimia na kujadili maendeleo ya mkoa wetu. Niko tayari kuwajibika, kuchapa kazi na kukusaidia pale utakapoona inafaa katika kukuza Mkoa wa Simiyu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom