Neno Corona, hakika sitakuwa nimekosea nikisema linatawala vinywani mwa wanadamu kwa sasa kuliko maneno mengi tunapoongelea magonjwa ya mlipuko. Hii imetokana na uzito wa maradhi yenyewe, hasa kwa vifo vinavyotokea kila dakika ulimwengu mzima kufuatia mlipuko wa ugonjwa huu.
Kuna badhi ya watu walioichukulia kimzaha mzaha, lakini ukweli usiopingika ni kwamba ni ugonjwa hatari. Mbali kuogopesha watu, hasa matajiri na viongozi wakubwa dunia nzima, wapo waloanza kujinyonga hata kabla hawajafikiwa. Vifo vya hapa na pale, matajiri, madaktari, watu wa kila rika.
Rwanda, kama nchi ndogo, imepiga hatua kadhaa nzuri na za kufurahisha kuwalinda raia wake na madhara makubwa yatokanayo na janga hili. Mimi nimeishi hapa na nimeona kuna funzo kwa nchi nyingine jirani.
Mwanzoni, hata Rwanda makosa yalifanyika, waliruhusu watu kutoka safari za uarabuni kuingia bila kuwekwa karantini. Baada ya siku tu zisizozidi 5, wale wageni walikuwa tayari na dalili. Serikali ililazimika kufunga mipaka ya anga na ardhini.
Navyoandika hivi sasa (Aprili 11, 2020) ni wiki ya tatu sasa hakuna ndege kuruka, isipokuwa kwa sababu maalum na zisizoepukika. Magari ya abiria toka siku serikali ilipotangaza hali ya dharura, yamepigwa stop, watu wote wamelazimika kubaki majumbani kwao kasoro tu wale wanaouza vyakula, maduka ya madawa, na benki. Sekta nyingine zisizo na utoaji huduma wa haraka zimesitishwa.
Ni kweli kusitisha ghafla huduma imeathiri wananchi kwa kiasi kikubwa. Lakini, kipi bora kati ya njaa inayoweza kuzuilika na ugonjwa ambao kwa hali zetu si rahisi kutibu kwani hauna tiba wala kinga?
Hapa Rwanda tulianza na mgonjwa mmoja tu, lakini mpaka sasa idadi imefika watu 118. Hii imetokana na nini? Mtu anapokuwa na virusi na bado yuko huru kuungana na jamii, ni dhahiri kwamba atakutana na watu wengi na humo humo wengi wao wataathirika. Kwa wale ambao wana uelewa mdogo, ugonjwa huu wataufananisha na magonjwa mengine (kama mafua au malaria); wanakosea sana!
Serikali ya Rwanda iliona baadae itaelemewa na mzigo wa wagonjwa na vifo, ikaamuwa kuunda timu ya kuwasaka na kuwaweka sehemu zilizotengwa wanaohofiwa kuwa na virusi hivyo. Haikuwa kazi rahisi, lakini mpaka sasa bado serikali inakabiliana na usambaaji wa virusi hivi. Cha ajabu sasa, wale walotengwa ndo humo humo inatoka hiyo idadi niliyotaja juu, kila kukicha.
Bahati nzuri na kwa jitihada hizo, kwa sasa hapa Rwanda hatuna mauti au mgonjwa mahututi.
Jana, hapa Rwanda wamepatikana wagonjwa 5 waliokuwa uraiani na imegundulika walikutana na baadhi ya watu waliopo huko walikotengewa.
Kwenye suala la misaada kwa walioathirika, hasa wale vibarua wapatao mlo mmoja tena baada ya kutumia nguvu zao kila siku, Serikali imejitolea kuwagawia chakula cha msaada mpaka pale watakapojiridhisha kutokuwa na maambukizi mapya. Wanyarwanda wenye uwezo (raia) wamejitolea kuwasaidia majirani zao. Viongozi mbalimbali wa Serikali mishahara yao ya mwezi mmoja imetolewa kuisaidia Serikali kuwalisha wananchi.
Kwa sasa safari za mikoani ni marufuku, jambo ambalo limewapa kikwazo walalahoi, lakini kuliko kupeleka ugonjwa huko, ubinadamu umetumika na siku zinasonga.
Kubaki nyumbani, imekuwa ni amri. Polisi kuanzia wa ngazi za juu mpaka wa chini, mgambo na 'reserve force', wako mitaani kuzuia safari za hapa na pale. Jambo ambalo kwa sasa ni muhimu.
Sokoni(kumbuka, imeruhusiwa kufanya tu biashara ya vyakula),kila mlango unaopokea watu,maji safi na sabuni kwa ajili ya kunawa mikono yapo.
Wenzetu huko Tanzania, mmejipangaje kukabiliana na janga hili?
Corona unaifata wewe, haikufuati kwako - BAKI NYUMBANI, USALAMA KWANZA