Ruzuku kwenye mbolea na mustakabali wa uchumi wa taifa letu

Kyara Atufigwe

Senior Member
Mar 29, 2015
120
68
Jitihada kadhaa zenye lengo la kuiinua sekta ya kilimo zimewahi kufanywa na serikali za awamu zilizopita lakini bado hazikufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Moja ya iliyokuwa changamoto kubwa katika sekta ya kilimo ni mfumuko wa bei za mbolea nchini. Bei ya mbolea imekuwa ikipanda maradufu na kukatisha tamaa jitihada za watanzania wengi kwenye sekta ya kilimo. Kwa mfano, mwaka huu bei ya mbolea aina ya CAN ilipanda kutoka Tsh 50,000 hadi 125,000 kwa mfuko mmoja, ongezeko la 150%!

Aidha, mbolea ya NPK ilifikia bei ya 130,000 kutoka bei ya Tsh 60,000 kwa mfuko mmoja. Wakati bei ya mbolea ya Urea nayo ilipanda maradufu hadi kufikia TSh. 130,000 kwa mfuko mmoja kutoka bei ya TSh. 50,000 mwezi Machi 2021, ikiwa ni ongezeko la 136%.

Sanjali na hiyo, mfuko mmoja wa mbolea aina ya DAP uliuzwa kwa Sh 150,000 kutoka bei ya awali ya sh. 62,000! wakati mbolea ya SA ambayo ilikuwa ikiuzwa kwa bei ya Tsh 38,000 ilipanda na kufikia Tsh 90,000 kwa mfuko mmoja. Kero hii ya mbolea ilikuwa ni kikwazo kikuu cha ukuaji wa sekta ya kilimo nchini.

Serikali ya awamu ya sita imeliona hili na kulifungia kazi. Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe ametangaza rasmi kuwa ruzuku ya Sh. bilioni 150 itatolewa na Serikali ili kudhibiti mfumuko wa bei ya mbolea nchini. Kwa ruzuku hii, hakuna mfuko wa mbolea ya aina yoyote ile utakaouzwa kwa zaidi ya Tsh 70,000/=

Serikali imewalipia wakulima Tsh 61,676 katika kila mfuko wa mbolea aina ya DAP ili kuishusha, kutoka bei ya Tsh 131,676 na kuifanya sasa iende kuuzwa kwa Tsh 70,000. Katika Urea, Serikali imewalipia Wakulima Tsh 54,724 na hivyo kuifanya mbolea hiyo ianze kuuzwa kwa Tsh 70,000 badala ya Shilingi 124,724.

CAN nayo sasa itauzwa kwa Tsh 60,000 badala ya bei ya awali ya Tsh 108,156. Hapa, Serikali imewalipia wakulima Tsh 48,156! Mbolea ya SA sasa itauzwa kwa bei ya Sh 50,000 badala ya Sh 82,852 baada ya Serikali kuwalipia wakulima Sh 32,852. NPK sasa itauzwa kwa Tsh 70,000 kutoka bei ya awali ya Tsh 122,695. Kwa bei hii, Serikali imewalipia wakulima Tsh 52,695.

Aidha, Serikali imejipanga kuvisapoti viwanda vya mbolea vilivyopo nchini (Dodoma na Minjingu) ili kuhakikisha kuwa mbolea yote itakayotumika itazalishwa hapa hapa nchini. Sambamba na hilo, hivi karibuni, Serikali itaenda kusaini miradi 21 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 80 inayohusu kilimo cha umwagiliaji. Haya yote kwa pamoja yanaenda kuipaisha sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Ruzuku na jitihada hizi za Serikali kwenye sekta ya kilimo zina maana gani kwa Uchumi wa Taifa letu?
Jitihada hizi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan zinaenda kuongeza sana uzalishaji mashambani na kukuza maradufu uchumi wa Taifa letu. Ni ukweli ulio bayana kuwa Taifa letu linazungukwa na mataifa kadhaa ambayo mara kwa mara yamekuwa yakikumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na hata baa la njaa. Mathalani, katika kipindi hiki cha mavuno, tani nyingi za mazao ya chakula zimesafirishwa kwenda baadhi ya mataifa hayo. Hii ina maana kuwa Taifa letu lina fursa kubwa sana ya kufanya biashara ya mazao hususani ya chakula katika ukanda wetu huu.

Kwa jitihada hizi za Serikali, idadi ya Watanzania watakaojishughulisha na kilimo itaongezeka maradufu, uzalishaji katika sekta ya kilimo unakadiriwa kukua kwa zaidi ya 400%, lakini pia, sekta ya usafirishaji itakua mara nne ya ilivyo sasa. Aidha, ndani ya miaka mitatu, vijiji, miji na manispaa nyingi zinatarajiwa kukua kwa kasi, Viwanda vya kuchakata mazao vitafunguliwa katika mikoa mingi nchini, na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya ajira kwani kilimo kitaajiri zaidi ya 80% ya ajira nchini.

Aidha, kwakuwa hali ya wakulima kiuchumi itakuwa imeimarika sana, uwezo wao wa kufanya manunuzi (purchasing power) utaongezeka maradufu. Aidha, kutakuwa na uhitaji mkubwa sana wa zana na pembejeo za kilimo, viwaatilifu, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya biashara.
Sanjali na hayo, mapinduzi haya katika sekta ya kilimo yatapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi kutoka nje ya nchi wa baadhi ya bidhaa muhimu kama vile mafuta ya kula, ngano na shayiri ambayo Taifa limekuwa likipoteza fedha nyingi za kigeni kwa kuagiza kutoka nje na hivyo kuongeza akiba ya fedha za kigeni.

Pia, kwa mapinduzi haya katika sekta ya kilimo, chakula kitapatikana kwa wingi na hivyo Watanzania wengi watapata lishe bora muhimu kwa afya ya miili yao. Hali hii itaongeza na kuimarisha nguvu kazi ya Taifa.
Aidha, kutokana na yote hayo, Pato litakalotokana na Sekta ya Kilimo litakuwa kwa asilimia 400% na hivyo kuchochea ukuaji wa Uchumi wa Taifa letu. Soko la ndani litaongezeka na hivyo kuiimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.

Rai yangu ni kwa Wizara ya Kilimo isimwangushe Mhe Rais; iende ikalisimamie hili kwa uthabiti ili kuepusha 'vishoka' kuingilia kati na kuwauzia wakulima wa wilaya za pembezoni mbolea kwa bei za Ulanguzi. Vyombo vya Ulinzi na usalama pia vijipange dhidi ya watu wote wenye nia ovu ya kuhujumu jitihada hizi za serikali.

Pia, ni vema sasa wakulima, wadau wote wa kilimo kuanza maandalizi mapema ya kusapoti jitihada hizi za serikali. Wadau na taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya kilimo hai au kilimo bora zijizatiti na kuanza kutoa mafunzo yatakayowasaidia wakulima kuzalisha mazao mengi kutoka katika eneo dogo kwa kuzingatia maandalizi mazuri ya shamba, upatikanaji wa mbegu bora, kupanda kwa nafasi kati ya mche na mche na mstari na mstari, kufanya palizi kwa wakati, kutumia viwatilifu bora, kutumia kiasi cha mbolea kinachohitajika kwa hekta moja, na kufanya maandalizi mazuri ya uvunaji, usafirishaji wa mazao kwenda kwenye maghala na uhifadhi bora wa mazao hayo.
 
Leo tarehe 15.08.2022 agro dealer hawajui watauza mbolea kwa bei ipi.mawakala wakubwa wao katika maghala yao bei inaeleweka.sasa wao watasambaza to the grassroot let wait and see.muda sio rafiki.
 
Mimi angalizo langu ni kufanya yafuatayo,
Kuwe na uhakika na soko,
Kilimo kizingatie umwagiliaji,
Kuwe na kilimo Mseto Kati ya wawekezaji wakubwa na wadogo,
Wizara ya mifugo nayo ikuze sekta ya Mifugo Ili kutoa soko la Mazao ya kilimo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom