Rushwa: Ni wakati wa kubadili mtazamo na kuikataa!


K

KAUMZA

JF-Expert Member
Joined
Aug 31, 2010
Messages
685
Likes
35
Points
45
K

KAUMZA

JF-Expert Member
Joined Aug 31, 2010
685 35 45
Rushwa umekuwa ni mzigo mzito sana kwa jamii ya watanzania. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika juu ya ubadhirifu mkubwa wa mali ya umma na hata ujenzi na usimamizi duni wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia vyombo mbalimbali vya habari vikionesha baadhi ya miradi ya maendeleo iliyojengwa kwa kiwango cha chini sana.


Mingi ya miradi hiyo, kama ni majengo ya madarasa au zahanati au hata nyumba za watumishi imejaa nyufa ambazo zinatishia uhai wa majengo hayo.


Nimekuwa nikijiuliza sana kwa nini hasa miradi mingi ya maendeleo tena ambayo inajengwa kwa kodi zetu na kusimamiwa na wataalamu wetu ambao tumewasomesha kwa fedha nyingi na kuwapa dhamana ya kubuni na kuisimamia miradi yetu wamekuwa wakitenda kana kwamba hawana utaalamu wowote!!!


Katika tafakuri yangu, ninaweza kuwatupia lawama wananchi kwa upande mmoja na hata watendaji kwa upande wa pili.


Wananchi ni wadau muhimu sana katika mapambano dhidi ya rushwa. lakini baadhi yetu sisi wananchi tumekuwa tukichangia sana katika kuwafanya watumishi wetu kujiingiza katika vitendo viovu vya wizi, ubadhirifu na hata matumizi mabaya ya mamlaka walizokabidhiwa watendaji wa serikali na hata taasisi binafsi.


Wiki mbili zilizopita nilikuwa katika kijiwe fulani cha kahawa. Kama inavyofahamika, katika vijiwe vya kahawa, mada mbalimbali huwa zinajadiliwa. Siku hiyo alikuwepo mzee mmoja mwenye umri wa makamo ya takribani miaka sabini na ushee hivi. Mzee huyo alikuwa ni muongeaji sana na kila aliloongea alikuwa analishabihiisha kwa mifano dhahiri kabisa.


Kimuonekano alikuwa ni mzee wa kipato cha chini lakini kimuono na kiakili alikuwa anaonekana ni msomi wa kiwango cha wastani, inawezekana akawa darasa la nane la mkoloni na mzoefu wa mambo mbalimbali yanayoendelea katika nchi yetu na hata katika nchi mbalimbali za Afrika.


Nilivutiwa sana na maongezi ya mzee wangu huyu na kwa bahati mbaya, tangu siku hiyo sikuwahi kumuona hapa mjini.
Baada ya kumaliza kahawa yake, niliwauliza wana kijiwe wenzangu, ni nani hasa Yule mzee.


Majibu ya swali langu hili kutoka kwa wanakijiwe ndio hasa kiini cha makala yangu haya. Wapo waliomuita ni limbuleni, wengine waliuita amechanganyikiwa na maisha na kila aina ya kebehi zilitupwa kwake. Na mwingine alithubutu kunionya kuwa, lile ni “funzo kwa wale wote ambao wamepata bahati ya kuwa waajiriwa wa serkali na kwa ujinga wao wakachezea bahati hizo”


Walinieleza kuwa mzee Yule alikuwa ni mkuu katika idara moja ya serikali ambayo waliisifia kwamba ilikuwa “inalipa sana”. Walieleza kuwa mzee Yule alikuwa mjinga sana kwa kujidai kuwa eti mwadilifu kwa kuzitunza mali za umma.


Tukio hili lilinikumbusha tukio katika riwaya maarufu ya A beautyful Ones Are Not Yet Born iliyotungwa na Ayi Kwei Armah mtunzi maarufu wariwaya raia wa Ghana. Ambapo wananchi walikuwa wanamsifia sana kiongozi mla rushwa (Koomson) na kumdhihaki bwana mmoja aliyekuwa akikataa kushiriki katika vitendo vya rushwa na kumuita Chichidodo(ndege anayejinasibu kuwa mstaarabu na hawezi kula kinyesi lakini maisha yake yote anaishi kwa kula funza wanaokula kinyesi). Sasa hapa ndipo tulipo kama jamii. Binafsi nilitegemea kiongozi Yule mstaafu aenziwe na kuchukuliwa kama mfano bora kwa kile alichokuwa akikifanya kwa maslahi ya jamii yake na bila kutanguliza maslahi binafsi.


Matokeo yake, wanajamii ambao ndo walikuwa wampa dhamana naye akaitekeleza kwa uadilifu wake wote ndo wamekuwa wa kwanza kumcheka na kumdhihaki kana kwamba uadilifu wake ni jinai. Wananchi siku zote humsifia sana kiongozi anayefuja dhamana aliyokabidhiwa na kumuona kuwa ni shujaa na mfano wa kuigwa.


Mfano huo nilioutoa unafanana sana na maoni waliyoyatoa watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii mara baada ya kigogo mmoja wa serikali kuachiwa huru katika kesi iliyokuwa inavuta hisia za watu wengi na mahakama kwa tuhuma za vitendo vya rushwa zilizokuwa zikimkabili.


Mara baada ya kushinda kesi yake, takribaani 80% ya wachangiaji katika mitandao hiyo, walimsifu sana kwamba alionewa na walithubutu hata kuibeza serikali kwamba ilikuwa na hila katika kesi hiyo. Waliobeza si tu walikuwa wananchi wa kawaida bali hata watumishi katika idara mbalimbali za serikali na za binafsi.


Katika kutimiza malengo ya millennia, hasa lengo namna moja (1) ambalo ni kuondoa umasikini uliokithiri na njaa pindi ifikapo mwaka 2020, serikali ya Tanzania ilianzisha mpango wa kugawa pembejeo kwa wakulima wadogo kwa njia ya ruzuku. Mpango huu endapo ungefanyika kwa uadilifu na umakini makengo ya serikali ambayo ni kuhakikisha kunakuwa na usalama wa chakula, kujiongezea kipato na kutoa elimu ya kilimo cha kisasa yangefanikiwa sana.

Wadau wakubwa katika mpango huu ambao ni wakulima/wananchi na mawakala wamekuwa wakikwamisha jitihada hizi za serikali. Wakulima kwa upande wao wamekuwa wakirubuniwa na mawakala na kuwauzia vocha zao kwa bei ya chee. Katika hili. Ni wazi kabisa kuwa hapa wananchi wanakuwa chanzo cha kuendeleza vitendo vya rushwa kwa kuwasaidia mawakala wasio na nia ya dhati ya kutenda uadilifu katika kazi walizokabidhiwa na serikali.


Tunaweza kupambana na rushwa kwa kujenga uwazi (transparency). Kazi hii inaweza kufanywa na kila raia. Katika serikali zetu za vijiji na mitaa, tujenge utamaduni waa kudai na kuhoji pesa zinazotolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Pia viongozi wa serikali za vijiji na mitaa wajenge tabia ya kuweka hadharani katika mbao za matangazo, mapato yote ya fedha zinazoingia katika serikali za vijiji.


Wananchi tuwe wapiga mbinja/wapuliza zumari (whistleblowers). Wananchi tuwe wepesi katika kupaza sauti pale tunapoona mambo yanakwenda segemnege (ndivyo sivyo). Hii itawezesha watawala wetu kuwa makini kwa kuwa watafahamu kuwa kumbe hatujalala.


Kwa viongozi wetu ni vema wakawa waadilifu na wa kweli kwa kuishi kwa uadilifu na ukweli (integrity circle). Wanaweza wakawajulisha wananchi juu ya kutokutoa rushwa. Baadhi ya ofisi huandikwa “Hatupokei rushwa” kwa kimombo Corruption free zone na wengine huandika “Tunalipwa na mwajiri kwa lengo la kukuhudumia wewe”/we are paid by our employer to serve you. Hii inamuwezesha mwananchi kuwa huru na pia kutokuwa na mawazo ya rushwa.


Nimalizie makala haya kwa kutoa angalizo. Ni makosa makubwa kuilaumu serikali kuwa inashindwa kupambana na rushwa, wakati ni sisi wenyewe ambao tumekuwa tukishiriki katika kuipamba rushwa na kuwadhihaki wote ambao wamekuwa wanaonesha uadilifu katika ofisi walizokabidhiwa. Kila mmoja wetu ana nafasi na wajibu mkubwa wa kuipinga rushwa popote pale anapokuwa na anapobaini kuwa kuna vitendo vya rushwa vinafanyika.


Mwaka 2014 ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka 2015 ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa Rais, madiwani na wabunge. Umejiandaa vipi kutokomeza rushwa katika uchaguzi?


JIULIZE!! Je, mimi ni mla/mtoa rushwa? Na je, rushwa ikija upande wangu, nitaweza kujizuia? Ikanye na uionye nafsi yako juu ya rushwa. Hakikisha unakuwa mfano. Tukijenga hisia kuwa rushwa ni sehemu ya ushamba na kila mla rushwa ni mshamba na jamii kumpuuza, nina imani rushwa itapungua katika jamii zetu
 

Forum statistics

Threads 1,272,606
Members 490,036
Posts 30,455,044