Rufaa ya Sosteni wa Kata ya Ulenje kwa Tume | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Rufaa ya Sosteni wa Kata ya Ulenje kwa Tume

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Lunyungu, Jan 2, 2009.

 1. Lunyungu

  Lunyungu JF-Expert Member

  #1
  Jan 2, 2009
  Joined: Aug 7, 2006
  Messages: 8,836
  Likes Received: 75
  Trophy Points: 145
  30 Disemba, 2008

  MSIMAMIZI MSAIDIZI WA UCHAGUZI
  KATA YA ULENJE
  JIMBO LA MBEYA VIJIJINI

  Ndugu:

  YAH: MAELEZO DHIDI YA PINGAMIZI JUU YA UTEUZI WANGU WA UGOMBEA UDIWANI KWA TIKETI YA CHADEMA KATIKA KATA YA ULENJE

  Rejea fomu ya pingamizi na barua toka kwa Mchona Musa Sapyanila(mgombea udiwani wa CUF) ya tarehe 28 Disemba 2008 isiyokuwa na nambari ya kumbukumbu yahusu “Pingamizi dhidi ya uteuzi wa mgombea udiwani wa CHADEMA kata ya Ulenje Sosteni Kanjanja Mwajojo’’.

  Maelezo yangu na majibu yangu kuhusu pingamizi hilo ni kama ifuatavyo:

  UTANGULIZI:

  Awali ya yote ieleweke kwamba ofisi yako ilitangaza ratiba ya kuchukua fomu na kurejesha fomu za kugombea udiwani kuwa ni kuanzia Disemba 17 mpaka Disemba 27 mwaka 2008. Ofisi yako ilitangaza hivyo ikielewa kwamba kwa tangazo hilo ni haki ya raia yoyote mwenye sifa ya kugombea udiwani kuweza kuchukua fomu na kurudisha katika tarehe zozote kati ya hizo. Ofisi yako ilikuwa ikitambua kabisa kuwa tarehe 25 na 26 Disemba ni siku za sikukuu ya Noeli/Chrismas na tarehe 27 Disemba ilikuwa ni siku ya jumamosi. Ofisi yako kwa kuzingatia tarehe ambayo imetangaza ilikuwa imeruhusu na kutoa haki ya wananchi kuweza kuchukua na kurudisha fomu katika siku hizo kwa mchakato wa uchaguzi kuwa huru na haki. Lakini ofisi yako inaelewa pia kuwa chombo kingine cha mhimili wa dola-MAHAKAMA; kwa kawaida hazifunguliwi katika siku za sikukuu na mapumziko ya mwisho wa wiki. Hatahivyo naamini kuwa ofisi yako ilielewa kabisa kuwa zipo fursa nyingine za wachukua fomu na warudisha fomu kuweza kutumia njia nyingine zilizotolewa kisheria kuweza kutimiza masharti mbalimbali yanayohitajika kisheria kuhusu viapo na masuala mengine kama nitavyoeleza zaidi katika barua hii.

  1. KUHUSU MADAI YA MLETA PINGAMIZI KWAMBA FOMU YANGU NI BATILI KWA KUWA HAINA KIAPO KWA MUJIBU WA SHERIA YA UCHAGUZI

  Sheria ya Uchaguzi na. 1/1985 pamoja na marekebisho yake inaeleza kuwa mgombea udiwani anatakiwa aape mbele ya hakimu, “magistrate” kwa kiingereza. Maelekezo kwa vyama vya siasa yanafuata na/ama kufafanua kile kilichoelezwa na sheria ya uchaguzi.

  Kinachotakiwa kueleweka ni kwamba sheria hii haisomwi na wala haipaswi kusomwa peke yake. Na pia ni lazima kiini cha kuapishwa na “magistrate” kieleweke.

  Kimsingi ni kwamba “magistrate” au hakimu anapata uwezo wa kuapisha kisheria kutokana na sheria ya ‘Oaths (Judicial Proceedings) and Statutory Declarations Act 1966) katika kifungu cha 11 ikisomwa pamoja na sheria ya Notaries Public and Commissiner for Oaths kifungu cha 10 kinachotaja nani wanaruhusiwa kuapisha.

  Kabla ya kuelezea kifungu hicho, sheria hii inamtaja mtu wa kwanza kuhusika na viapo katika kifungu cha 3(a) kuwa ni Wakili na (b) mtu mwingine yoyote aliyetajwa kufanya kazi hiyo.

  Kimsingi ni kwamba kiapo kinachosimamiwa na wakili ni halali kisheria na si batili hata kidogo.

  Kwa maana hiyo, wakili au hakimu wakati anaapisha anakuwa na wadhifa wa Notary Public and Commissioner for Oaths. Kutajwa kwa hakimu pekee kwenye sheria ya uchaguzi hakuzuii wala kuharamisha sheria hii wala viapo mbele ya Notaries Public and Commissioner for Oaths wengine. Kisheria wako sahihi na wana uwezo wa kuapisha labda kama sheria itasema wasiapishe tena.

  Kwa ajili ya ufafunuzi zaidi ni kwamba Hakimu ametajwa kuwakilisha waapishaji wengine kwa ajili ya urahisi wa kupatikana(tena siku za kazi) tu na kuepusha gharama za mawakili ama kutokapatikana kwa mawakili katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu.

  Nasisitiza kwamba Sheria ya Uchaguzi haijasema kwamba viapo mbele ya makamishina wengine ni haramu ama haviruhusiwi na haijafanya marekebisho ya sheria husika ya Notaries Public and Commissioners for Oaths.

  Orodha ya waapishaji kwa mujibu wa sheria hii ya viapo, zaidi ya kumtaja wakili kwenye kifungu cha 3 cha sheria hiyo, ipo kwenye kifungu cha 10 ambacho kinasema, miongoni mwa wengine kwamba:

  “Every officer to whom this section applies shall have the powers and duties of the Notary Public in the respect of administering Oaths, taking affidavits, attesting signatures and certifying documents and shall have the powers and duties of a commissioner for Oaths under this Act

  2(a)………..
  (b)………...
  (c) the registrar of the High Court and every deputy registrar
  (d) a Magistrate
  (e)………...

  Kwa maana hiyo katika ngazi ya uapishaji wakili hutajwa kwanza na hakimu huangukia katika kundi la ‘watu wengine’, hii haina maana kwamba wakili ni bora kuliko hakimu; la hasha, bali watu hawa kwa nyadhifa zao wana wajibu na uwezo wa kisheria wa kuapisha na kuthibitisha.

  Kusema kwamba kiapo cha wakili ni batili kama inavyodaiwa na mgombea aliyeleta pingamizi ni kutokujua sheria na upotoshaji wa makusudi ambao kwa namna moja au nyingine tume ya uchaguzi iangalie kwa umakini ama kumwajibisha ikiwezekana. Kwa suala hilo nawasilisha kwako kwamba kiapo cha wakili ni halali na kizito kisheria.

  Suala la kujazwa na kusaniniwa, kusainiwa na kupigwa na muhuri na Evarist Mashiba Advocates, Notary Public and Commissiner for Oaths badala ya Hakimu ni suala la kutokujua sheria inayowapa watu hawa uwezo wa kuapisha. Maelezo ya suala hili yapo hapo juu na nina hakika yanajitosheleza.

  Kwa nyongeza, suala la mgombea wa CUF Jimbo la Bunda kula kiapo cha wakili na msimamizi wa jimbo kumwondoa nitalitolea maelezo yafuatayo:
  a) Kwanza msimamizi wa uchaguzi wa jimbo moja hafungwi na maamuzi ya msimamizi wa jimbo lingine kutokana na mazingira ya suala husika.
  b) Pili maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la uchaguzi Bunda kama ilivyoelezwa na mleta pingamizi hayaeleweki yaliambatana na malalamiko gani mengine ili kujua ni suala lipi hasa lilipelekea maamuzi hayo.
  c) Tatu, maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Bunda hayajawa “precedent” au kufuli kwa waamuzi wengine kuamua vinginevyo kwa hiyo hawafungwi na maelezo au maamuzi yake.
  d) Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi wa Kata ya Ulenje anapaswa kuliangalia suala hili kwa mazingira halisi yaliyopo na kwa mustakabali wa usalama na maendeleo ya kata ya ULENJE na wapiga kura wake.

  2. KUHUSU SABABU KWAMBA MGOMBEA AWE ANAWEZA KUSOMA NA KUANDIKA KISWAHILI AU KIINGEREZA SHARTI AMBALO MLETA PINGAMIZI ANASEMA SIJALITIMIZA

  Huu ni uzushi wenye kulenga kuipotosha ofisi yako na kunikashifu; mleta pingamizi alipaswa alete ushahidi ni kwa vipi sijui kusoma na kuandika. Kama mleta pingamizi angekuwa mtu makini angeweza kubaini haraka katika fomu yangu maeneo ambayo nimejaza na alipaswa kubaini saini/sahihi yangu. Mtu asiyejua kusoma na kuandika Kiswahili au kiingereza hawezi kujaza fomu ya kugombea na hawezi kuweka sahihi/saini ya kuandika badala yake mara nyingi huweka saini/sahihi ya dola gumba.

  Uzushi kama huu na kushindwa kubaini ukweli wa kawaida unaacha maswali mengi kuhusu uwezo na maadili ya kiuongozi ya mgombea udiwani wa CUF aliyeweka pingamizi. Badala ya ofisi yako kuchunguza fomu zangu, nashauri mleta pingamizi achunguzwe ‘credibility’ yake kama kweli anafaa kuongoza umma wa wananchi wa ULENJE.
  3. KUHUSU MADAI KUWA MGOMBEA AMEJAZA FOMU KWA HERUFI NDOGO KINYUME NA SHERIA NA MAELEKEZO YA TUME

  Kwa kifupi ni kwamba mgombea wa CUF anatafuta upenyo usio na msingi wowote. Ni muhimu kwa mgombea kuelewa kwa suala la kugombea katika uchaguzi ni haki ya Kikatiba na kisheria ambayo haiwezi kunyimwa kwa sababu ndogo ndogo za kiufundi. Ieleweke kwamba hitaji la kujaza fomu kwa herufi kubwa halipo katika sifa za kikatiba na kisheria za mtanzania kuweza kukidhi matakwa ya kuwaongoza na kuwatumikia watanzania wenzake katika nafasi ya udiwani.

  Ni vyema mgombea wa CUF akaelewa kuwa sharti la kuandika kwa herufi kubwa halijaweka kama kipimo cha mgombea bali limewekwa kumrahisishia msimamizi wa uchaguzi na watendaji wenzake wa tume ya uchaguzi kuweza kusoma kwa urahisi kilichoandikwa kwenye fomu.

  Kwa ujumla, fomu yangu imekidhi matakwa yote ya kuweza kusomwa na kueleweka na msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya ULENJE pamoja na tume ya uchaguzi kwani katika maeneo yote kuanzia ukurasa wa kwanza wa fomu ambayo ndio tume inatumia kuchukua taarifa za msingi za mgombea nimejaza kwa HERUFI KUBWA. Na sehemu moja ndogo, katika ukurasa ambao mtoa pingamizi ameutaja inasomeka kwa ufasaha na hivyo kutimiza mahitaji ya kisheria yanayopaswa.

  Hivyo nawasilisha kwamba mapingamizi yote yaliyoletwa na mgombea MCHONA MUSA SAPYANILA wa CUF ni ya kipuuzi, hayana msingi, ya uzushi na uoga wa kupambana kwa wapiga kura; hivyo, yatupiliwe mbali.


  HITIMISHO:

  Kwa hitimisho, naeleza kwamba kwa sababu ya mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu kuendelea mpaka kipindi cha sikukuu ya Noeli na mapumziko ya mwisho wa wiki, na kwa kuwa sheria za nchi yetu zimetoa fursa ya viapo kwa namna mbalimbali; hakuna kipengele cha sheria kilichokiukwa kwenye fomu zangu za kugombea udiwani na kwamba fomu zangu ni halali kwa kuwa na tamko/kiapo, zimejazwa kwa misingi ya sheria za nchi, na kwamba kiapo changu si batili.

  Malalamiko na mapingamizi ya mgombea wa CUF yachukuliwe kuwa ni ya ubababishaji, yasiyotambua sheria. Kitu ambacho ni udhaifu mkubwa na hatari kwa mtu anayeomba kiti cha kuwa mmoja wa watunga sheria ndogo ndogo(Baraza la Madiwani/Halmashauri); kwa ujumla ni uzushi na kutojua anachodai na kuzua asioyajua. Hivyo, madai na pingamizi lake litupiliwe mbali kwani halina msingi.

  Mgombea mwenye hoja nyepesi za namna hii, hawezi kuwatetea kikamilifu wananchi wanaonyanyaswa kwa michango wala kuweza kuibana serikali ya CCM kuweza kutekeleza wajibu wake kikamilifu kwa wananchi wa kata yetu wa kuweka mazingira ya upatikanaji kwa huduma za msingi zikiwemo pembejeo/mbolea, maji, umeme nk.

  Mimi naamini kwamba wananchi wa Kata ya ULENJE hawahitaji kiongozi anayezusha ili apewe ushindi wa mezani. Mimi niko tayari kupambana kwa kura na si mbinu za kiufundi(technicalities) za kubuni. Huu ni wakati wa tumaini jipya la mabadiliko katika taifa letu lenye kuhitaji siasa safi na uongozi bora. Hivyo, pingamizi hili halipaswi kuwa kikwazo kwa dhamira yangu ya kuwatumikia wananchi na nia ya wananchi ya kuchagua diwani mwenye msimamo wa kupambana na aina zote za ufisadi na kutetea rasilimali za za Taifa katika kata yetu ya ULENJE.

  Wako katika demokrasia na maendeleo,

  Sosteni Kanjanja Mwajojo
  Mgombea Udiwani Mteule(CHADEMA)
  Kata ya ULENJE
  Jimbo la Mbeya Vijijini
   
 2. M

  Mtanzania JF-Expert Member

  #2
  Jan 2, 2009
  Joined: May 4, 2006
  Messages: 4,818
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 145
  Lunyungu,

  Kwahiyo hata huyu mheshimiwa naye katupwa nje?

  Hapo wamedanganywa na huyo mwanasheria mgombea ubunge. Kujua kwingi huleta matatizo.
   
 3. I

  Ilongo JF-Expert Member

  #3
  Jan 2, 2009
  Joined: Feb 25, 2007
  Messages: 292
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Duh!! Makubwa haya ...
   
 4. I

  Ilongo JF-Expert Member

  #4
  Jan 2, 2009
  Joined: Feb 25, 2007
  Messages: 292
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0


  Hadi maelezo waliyoyatoa katika rufaa zao yanafanana ... copy and paste ...
   
 5. Kibunango

  Kibunango JF-Expert Member

  #5
  Jan 2, 2009
  Joined: Aug 29, 2006
  Messages: 7,639
  Likes Received: 185
  Trophy Points: 160
  Na yote haya yamefanyika katika chama mbadala.... Kazi ipo
   
Loading...