RPC Mtwara kupandishwa kizimbani ...............

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
215,419
2,000
RPC Mtwara kupandishwa kizimbani
Friday, 03 December 2010 20:23 0diggsdigg

Leon Bahati, aliyekuwa Tandahimba
WAKATI kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi zikiendelea, mgombea ubunge wa Jimbo la Tandahimba ana mpango wa kufungua kesi tofauti; kumshtaki kamanda wa polisi wa mkoa kutokana na askari wake kumshambulia na kumsababishia majeraha.
Ahmed Katani, ambaye aligombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF na kushindwa na mgombea wa CCM katika mazingira anayoelezea kuwa tata, anasema kesi hiyo ataifungua wakati wowote kuanzia wiki hii, hatua ambayo itamfanya kamanda huyo, Stephen Buyuya kuwa wa kwanza, kusimamishwa kizimbani kwa makosa ya ubabe wa polisi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31.

"Polisi walinipiga na nikapata maumivu makali, lakini kadri muda ulivyokuwa unaenda, mwili ulikufa ganzi na nikawa sisikii tena maumivu ya virungu walivyokuwa wananipiga,” alisema Katani wakati akiongea na Mwananchi kuhusu uamuzi wake wa kumshtaki kamanda wa polisi wa mkoa na kigogo mwingine ambaye jina lake limehifadhiwa.
Mwanachama huyo wa CUF hakuweka bayana kiwango cha fidia ambacho atakidai mahakamani, lakini alisema ataiomba mahakama iliamujuru Jeshi la Polisi limlipe mamilioni ya fedha baada ya kipigo cha polisi hao kumsababishia majeraha makubwa, ikiwa ni pamoja na kuvunjika mifupa inayounganisha kiwiko na kiganja.
"Nasubiri ushauri kutoka kwa mwanasheria wangu ili kuona kama kuna haja ya kumuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa kesi hiyo inaihusu pia serikali," alisema Katani.

Katani aliliambia Mwananchi jana kwamba kipigo hicho alichokipata siku mbili baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, kilisababisha mfupa wa mkono wake wa kushoto kuvunjika mara mbili.
Katani pia amemrushia tuhuma nzito mkuu wa wilaya hiyo, Husna Mwilima kuwa alijaribu kumuandaa kuyapokea matokeo ya kushindwa kwa kumuahidi kuwa angeteuliwa na rais kushika madaraka mengine, lakini akamkatalia na ndipo mpango huo wa kumpiga ulipotekelezwa.

Katika uchaguzi huo, Juma Njwayo wa CCM alitangazwa kuwa mshindi, lakini wafuasi wa CUF walipinga ushindi huo wakidai kura zao ziliibiwa.
"Kusema kweli hali yangu tangu siku ile (Novemba 2) siyo nzuri na nimekuwa nikipata matibabu Hospitali ya Muhimbili. Jana (juzi) madaktari walibaini bado mfupa haujaunga na hivyo wakanifungia tena POP (plasta ngumu maarufu kama muhogo),” alilalamika Katani.
Mbali na Buyuya, kigogo mwingine (jina tunalo) alisema atamfikisha mahakamani kwa sababu ndiye aliyekuwa akiamuru askari polisi wampige.
Kuhusu Kamanda Buyuya, alisema atamfikisha mahakamani kwa sababu askari anaowasimamia ndio waliotekeleza kipigo hicho.

Mwananchi lilipowasiliana na Kamanda Buyuya alisema hana taarifa yoyote ya malalamiko ya kuumia kwa mgombea huyo wa CUF.
Kamanda huyo pia alipinga madai ya mlalamikaji kuwa askari wake walimpiga mgombea huyo wa ubunge na kubainisha kwamba hadi sasa hajaripoti popote kuhusu kupigwa kwake.
“Ninachojua ni kwamba askari walioenda Kitama (Kata anayoishi Katani) Novemba 2 (mwaka huu) walienda kupambana na wananchi waliokuwa wanafanya vurugu,” alisema Buyuya.
Wakati Buyuya akikanusha taarifa hizo, Katani aliihadithia Mwananchi jinsi askari walivyomkamata, kumpiga na kumtesa.

“Siku ya pili baada ya kupiga kura, lilifuata zoezi la kuhesabu kura,” alisema Katani.
"Kura zilihesabiwa katika mazingira makubwa ya mvutano kutokana na matokeo aliyokuwa nayo msimamizi wa uchaguzi kuwa tofauti na yale yaliyobandikwa vituoni.
"Kwakuwa CUF ilikuwa imejumlisha kura kulingana na zilivyopigwa vituoni, wafuasi wake walikuwa wanaamini wameshinda, hivyo kumiminika kwa wingi kujiandaa kumpongeza mara atakapotangazwa."
Kabla matokeo hayajatangazwa, Katani alidai, mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Husna Mwilima alimuita na kumuambia kuwa yeye bado ni kijana mdogo lakini ameonyesha nguvu kwa kupata kura nyingi.

Katani alidai Mwilima alimtaka awe na utulivu iwapo mgombea wa CCM atatangazwa mshindi na kwamba wingi wa kura alizopata zinaweza kumfanya Rais Jakaya Kikwete akamteua kwa nafasi nyingine, lakini alimkatalia akimweleza kuwa aliamua kugombea ili kutetea maslahi ya wakazi wa jimbo hilo.
Baada ya mbinu hiyo kushindikana, alipigiwa simu na kigogo mwingine (jina tunalihifadhi) akimtaka aelewe anachoambiwa na wakubwa zake.
Alidai kuwa baadaye jioni, mkurugenzi wa Manispaa ya Tandahimba ambaye alikuwa ni msimamizi wa jimbo, alimuita na kumwambia kuwa CCM imeonekana imeshinda na kumuomba asaini matokeo, lakini akawajibu kuwa hakuwa tayari kufanya hivyo kwa sababu hakubaliani nayo.
Ndipo askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walipowasili na kuanza kuwatawanya wafuasi wa CUFwaliokuwa wamerundikana nje ya ofisi za Halmashari ya Tandahimba kwa kuwavurumushia mabomu ya machozi.
Baadaye ndipo msimamizi huyo wa uchaguzi alimtangaza mgombea wa CCM kuwa mshindi.
Kitendo hicho, anadai, kilimsononesha na ndipo alipoanza kutafakari juu ya namna ya kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo hayo.

Alisema moja ya mambo yaliyowafanya wananchi kupandwa na hasira ni kitendo cha Tume ya Uchaguzi kushindwa kutangaza matokeo hayo mapema.
“Kura zilianza kuhesabiwa alfajiri na hadi mchana wangeweza kutangaza matokeo, lakini hawakutangaza hadi majira ya jioni. Matatizo yote yalikuwa ni ya kujitakia,” alisema.
Alisema alipofika nyumbani, usiku ule alipata taarifa kwamba polisi wametaarifiwa kuwepo kwa vurugu eneo la Kitama, lakini walipofika walikuta hali shwari na kurejea makwao.
Siku iliyofuata, yaani Novemba 2, anadai kuwa alikwenda nyumbani kwa baba yake anayeitwa Ahmed Katani ambako walishirikiana kuhesabu upya kura walizopata.

Lakini ilipofika jioni, walisikia milio ya risasi pamoja na milipuko ya mabomu katika barabara kuu ya Newala-Mtwara ambayo imepita kwenye kata hiyo.
“Hali hiyo iliwafanya baadhi ya watu kukimbia nyumba zao na wengine kujificha ndani ya nyumba zao. Sisi tuliendelea na kuhesabu kura,” alisema.
Punde askari wawili waliingia kwenye nyumba hiyo, alisema Katani, na kuwataka wawe watulivu akidai kuwa kazi waliyokuwa wakiifanya ni ya kukamata vijana wahalifu.
Wakati wakiendelea na operesheni hiyo, alisema baadhi ya vijana wenye hasira walifunga kwa magogo barabara kuu iendayo mji mdogo wa Tandahimba kwa magogo.
Kitendo hicho anasema kiliwafanya askari hao wa FFU kuongeza kasi ya kupiga mabomu ya machozi na ya moto ambayo alidai yalisababisha baadhi ya nyumba kuungua.

Hata hivyo, Kamanda Buyuya alikana kutumia mabomu ya moto na kwamba nyumba zilizoungua zilichomwa na vijana waliokuwa wakifanya vurugu.
Katani alisema askari watatu walifika nyumbani kwake na kumlazimisha kufuatana nao ili awatangazie vijana waliokuwa wanafanya vurugu waache mpango huo.
“Nilikubali nikaenda nao, lakini cha ajabu nilipofika barabarani, alifika kiongozi wao… (jina tunalihifandhi) akafoka:
“Yaani kijitu hiki ndicho kinachotufanya hatulali tangu jana? Akanipiga kwa kirungu mgongoni. Nikawauliza mbona sielewi sababu za kunipiga," alisema Katani huku akimkariri bosi huyo wa polisi.

Baadae akadai walimpeleka sehemu wanayokusanya watu waliowakamata na hapo wakamuamuru alale kifudifidi na kuanza kumcharaza kwa virungu mgongoni na kwenye mikono.
“Nilipata maumivu makali lakini kwa jinsi muda ulivyokuwa unaenda, mwili ulikufa ganzi na nikawa sisikii tena maumivu ya virungu walivyokuwa wananipiga,” alisema Katani.
“Baadae walinipeleka hadi kituo cha polisi cha Tandahimba lakini huko hali yangu ilibadilika nikajikuta nimepoteza fahamu.

“Nilisikia baadae OCD (mkuu wa polisi wa wilaya) alipofika na kuniona, akataharuki na kuamuru nipelekwe hospitali haraka.
“Wakati mimi nazinduka nilijikuta niko Hospitali ya Tandahimba. Mmoja wa madakaktari alikataa kunipokea baada ya kubaini kwamba nilipigwa."
Katani alisema daktari huyo alitaka apatiwe hati ya matibabu ya polisi (PF3) ili aweze kumtibu na kusababisha mvutano mkubwa hadi polisi walikubali na kwenda kuiandika.
Usiku huo, alisema Mwilima alifika kumpa pole na akaonekana kusikitika huku akilaumu polisi kwa kumpiga.
Katani alisema katika kumtibu ilibidi madaktari wampeleke hospitali ya wilaya ya Newala kwa ajili ya kupigwa picha ya mionzi (X-ray).

Inadaiwa kuwa mkuu huyo wa wilaya alimtaka Katani achague hospitali ambayo angependa kutibiwa kati ya Newala au ya Mkoa wa Mtwara, lakini anadai kuwa alikataa 'ofa' hiyo na kueleza kuwa ameamua kwenda kutibiwa Dar es Salaam, kwa gharama zake.
Alikiri kwamba gari ya Halmashauri lilitumika kumbeba hadi Hospitali ya Mtwara ambako walimpiga tena picha ya x-rays.
Mgombea huyo wa ubunge anadai kuwa katika uchunguzi iligundulika kuwa mkono wake wa kushoto umevunjika mara mbili mifupa inayounganisha kiwiko na bega.
Alisema baadaye alisafiri kwa ndege hadi Dar es Salaam na kuanza matibabu.
Wakati akiwa Dar es Salaam, anasema polisi walifika Kitama Novemba 4 na kufanya kikao cha maridhiano kati yao na wananchi.
Katika kikao hicho pia, waliwataka wananchi kuepuka mikusanyiko ya kisiasa ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom