Rostam, Lowassa hawafukuziki

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
picture-4.jpg

Na Saed Kubenea - Imechapwa 05 October 2011

ROSTAM Aziz, mwanasiasa, mfanyabiashara na mmoja wa maswahiba wa karibu wa Rais Jakaya Kikwete, hafukuziki ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa ndani ya serikali na CCM zinasema, pamoja na chama chake kumuona kuwa ni "gamba" linalopaswa kuvuliwa; bado Rostam ni nguzo muhimu ya Rais Kikwete na chama chake.

Vilevile pamoja na Rostam kutamka kuwa kuna siasa uchwara ndani ya chama chake na hatimaye kujiuzulu ubunge na ujumbe wa halmashauri kuu ya chama chake, mwenyekiti wa chama hicho na hata viongozi wastaafu, bado wanamhitaji – ni mwenzao.


MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake kwamba Rostam ndiye aliyefadhili helkopta iliyotumiwa na CCM katika siku za mwisho za kampeni jimboni Igunga.

Imeelzwa pia kuwa ndiye aliyekuwa kinara wa mkakati wa ushindi na ndiye alitumika kurejesha kundini baadhi ya viongozi wa chama hicho waliogoma kushiriki kampeni. Kazi yote hiyo aliifanya kwa mtandao akiwa nje ya nchi.

Aidha, Rostam anatajwa kuwa ndiye aliyeshinikiza uongozi wa CCM taifa, kumzuia katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kushiriki kampeni za uchaguzi jimboni humo.


Taarifa zinasema ni Rostam aliyeonya kuwa hatua yeyote ya kumpeleka Nape katika uchaguzi wa Igunga, ingesukuma wafuasi wake kutokukipigia kura chama hicho.


Wakati Rostam akijiuzulu wadhifa wake, alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuchoshwa na kile alichoita, "Siasa uchwara ndani ya CCM."


Helkopta iliyotumiwa na CCM katika kampeni za Igunga, taarifa zinasema, imelipiwa na Rostam. Iliondoka jijini Dar es Salaam kwenda Igunga, Jumanne, tarehe 27 Septemba ikiwa na Hussen Bashe na January Makamba.


Bashe ni mtendaji mkuu wa kampuni ya Rostam, New Habari Corporation inayochapisha magazeti ya Rai, Mtanzania, Bingwa, Dimba na The African.


Naye Makamba anatajwa kuwa ni mmoja wa kambi ya Rostam katika harakati za kumtafuta mrithi wa Kikwete katika uchaguzi wa ndani ya chama mwaka 2010.

Inaelezwa pia kwamba Makamba alikuwapo nyumbani kwa Rostam, siku moja kabla ya mwanasiasa huyo kwenda Igunga kutangaza kujiondoa katika uongozi. Juhudi za kumpata Makamba kwa simu hazikuzaa matunda.

"Ndugu yangu, kwa jinsi tulivyohenya kwenye kampeni za Igunga, kuondokana na ufisadi na kufukuza ndani ya chama watuhumiwa wakuu wa ufisadi chini ya kauli mbiu ya kujivua gamba, ni jambo ambalo haliwezekani tena. Kila mmoja sasa anaona…kwa jinsi wapinzani walivyotuhenyesha, hakuna wa kuleta tena hoja hii," ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM kwa sharti la kutotajwa gazetini.


Viongozi na wanachama wanaotakiwa kuondolewa CCM kwa tuhuma za ufisadi, ni pamoja na Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz. Tayari Rostam amekuwa nje ya vikao vya maamuzi, lakini amebaki kama silaha kubwa ya Kikwete.


Taarifa zinasema, pamoja na Rostam kuachia nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama chake, amebaki kuwa tegemeo na nguzo muhimu ya Rais Kikwete katika mikakati ya ushindi wa CCM.


MwanaHALISI lilipowasiliana na Bashe kufahamu iwapo helikopta hiyo ilikodishwa na Rostam, kwanza alishutuka na kisha akasema, "Hapana…Ninachojua mimi imekodishwa na CCM, nje ya hapo sijui."


Alipong'ng'anizwa kwamba taarifa zilizopo zinaonyesha helikopta hiyo ilikodishwa na Rostam, Bashe alisema, "Kwanza, sina uhakika kama imekodishwa na Rostam. Jambo hili ukimuuliza Mukama (Wilson, katibu mkuu wa CCM) atakuwa na majibu mazuri.


"Pili, hata kama imekodishwa na Rostam, kuna ubaya gani? Rostam ni mwanachama wa CCM ambaye hana budi kukichangia chama chake. Ni kweli amejiweka kando kwa nyadhifa zake, lakini bado mwanachama na mchango wake unahitajika," alieleza.

Alisema, iwapo mwanasiasa huyo ndiye ametoa ndege hiyo basi ni jambo jema, kwa kuwa wale waliokuwa wanaeneza taarifa kwamba Rostam ana fedha chafu na kwamba "CCM inajitenga na watu wenye fedha chafu, watakuwa wameaibika."

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa gazeti hili, Nape alizuiwa kwenda Igunga ili "kumfurahisha" Rostam kwa kile kilichoelezwa, alichochea kujiuzulu kwake.


Nape alitekeleza sharti hilo kwa shingo upande. Katika kipindi chote cha kampeni hakukanyanga Igunga. Alisikika akiwa pembezoni mwa jimbo hilo ikiwamo mikoa ya Sigida, Mara na Mwanza.


"Haijawahi kutokea katika historia ya chama chetu, katibu mwenezi kutengwa katika kampeni. Kwa kweli, Rostam bado ana nguvu ndani ya CCM; nguvu ambazo zinasababishwa na Kikwete mwenyewe kuwa mara baridi, mara vuguvugu," ameeleza mjumbe mmoja wa NEC.


Alipoulizwa Nape, kwamba kutoshiriki kwake kwenye kampeni za Igunga, ni chachu ya kumdhoofisha kisiasa alisema, "Sijui kama nimedhoofishwa."


Akiongea kwa sauti ya upole, Nape alisema, "Kaka, sina la kusema. Sijafanya utafiti. Sijui kama nimedhoofishwa."


Mtoa taarifa anasema, Rostam aliweka sharti pia kwa viongozi wake wa mkoa na taifa, kutoshirikisha Samwel Sitta, mbunge wa Urambo Mashariki na waziri wa Afrika Mashariki kwenye kampeni za Igunga.


Sharti hilo lilitekelezwa na viongozi wa juu wa CCM. Katika muda wote wa kampeni, Sitta hakukanyaga hata mara moja Igunga.


Gazeti hili lilipowasiliana na Sitta kufahamu kilichosababisha kutotia mguu Igunga, spika huyo wa zamani wa Bunge alisema, "Ni kweli sikwenda Igunga, lakini ni kwa sababu ya majukumu niliyonayo."


Alisema, "…unajua haka kawizara kangu, kana kazi nyingi sana. Dosari yake ni kwamba kama waziri husika hakushiriki vikao vyake na shughuli zake, basi ujue nchi imekosa mwakilishi."


Alisema, "Kabla ya kampeni tayari kulikuwa na programu mbalimbali zilizonilazimu mimi kusafiri hadi Kigali, nchini Rwanda. Hivyo ilikuwa si rahisi kushiriki kampeni kwa muda mfupi na kurudi Kigali.


"Isitoshe CCM ina timu nzuri ya kampeni. Imefanya kazi nzuri. Sisi wengine ambao hatukushiriki tulihitajika kutoa michango yetu kwa utaratibu tuliojiwekea na nadhani michango yetu imefanya kazi maana matunda tumeyaona."


Sitta ndiye kamanda wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) mkoa wa Tabora; kutoonekana kwake katika kampeni za Igunga kulionekana waziwazia kulizua shaka.


Sitta alikuwa spika wa Bunge la Tisa lililoongoza harakati za uchunguzi wa mkataba feki wa Richmond, ambao ulimuondoa swahiba mwingine wa Rostam, Edward Lowassa katika wadhifa wake wa waziri mkuu.


Katika uchunguzi huo ulioongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, Rostam alitajwa kuwa ndiye kinara wa mkataba tata wa Richmond na baadaye Dowans, ambao kwa pamoja umeiweka serikali ya Kikwete kitanzini.


Naye Dk. Mwakyembe, hakukanyaga Igunga. Taarifa zinasema ni sehemu ya matakwa ya Rostam.


Hata hivyo, Mwakyembe aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu, kwamba kutokuwapo kwake Igunga kulitokana na yeye kuwa nje ya nchi kikazi.


Kwa mujibu wa taarifa, hata uamuzi wa rais mstaafu Benjamin Mkapa kukubali kwenda Igunga kwa shughuli za kufunga na kufungua kampeni, kulikuja baada ya Rostam kukubali kuongozana naye ili kuweka sura ya kuwa na mshikamano naye.


Mkapa na Rostam walikuwa wote Igunga, tarehe 10 Septemba 2011, siku ambayo CCM ilizindua kampeni zake. Walirejea pamoja jijini Dar es Salaam ambapo katika safari hiyo walipitia Zanzibar walikokaa kwa muda mrefu wakisubiri ndege ya kuwafikisha Dar es Salaam.


Mtoa taarifa anasema siku ambayo Mkapa na Rostam walikuwa wanarejea jijini, ilitokea hitilafu ya umeme katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, jambo ambalo liliwafanya kutua Zanzibar kwa dharula.


Rostam ndiye anatajwa kuwa mpanga mkakati wa kumuingiza Kikwete madarakani katika uchaguzi wa ndani ya chama na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.


Inaelezwa kwamba alikuwa Rostam aliyefanya kazi kubwa ya kuunganisha makundi ya Lowassa na Kikwete.


Taarifa nyingine zinasema alikuwa Rostam aliyesababisha Sitta kugombea uspika badala ya nafasi aliyokuwa ameahidiwa awali na Kikwete ya waziri mkuu.


Mwingine ambaye ametajwa kutopendwa na Rostam kuingia Igunga hata kama hakumtaja kwa viongozi wake, ni Anne Kilango Malecela. Katika karibu siku 30 za kampeni, Kilango aliishia katika Kata ya Masakelo kwenye manispaa ya Shinyanga, alikoshiriki ufunguzi wa kampeni za udiwani wa chama chake.


Kwenye uchaguzi huo, mgombea wa CHADEMA, Zacharia Mfuko amembwaga mgombea wa CCM, Rashida Mahenga.




 
"hatua ya kumpeleka nape igunga itasababisha wafuasi wa R.A Kutoichagua ccm" Jamani, ni mwaka wangu wa 7 nipo igunga, nje na utumiaji wa hela ulio kithiri RA hakuwa ushawishi wala wafuasi wa kuiathiri ccm!. Ccm walisha amua tu kuongozwa na wawazo ya mtu 1 pasipo kuruhusu udadisi jambo linalo wagarim maana wameamua watu wachache kufikiria na kuamua kwa niaba yao
 
Si ni huyo huyo Rostam aliyekuwa akipita kwa siri siri kupiga kampeni CCM isichaguliwe ili wadai sera ya kuvua magamba ndiyo imeigharimu? Ghafla wakakimbia ku-claim responsibility.
 
Si ni huyo huyo Rostam aliyekuwa akipita kwa siri siri kupiga kampeni CCM isichaguliwe ili wadai sera ya kuvua magamba ndiyo imeigharimu? Ghafla wakakimbia ku-claim responsibility.

Mbopo bwana !!!
Good morning mkuu wangu
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom